Kushirikiana na Mtu Ambaye Mali zak...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kushirikiana na Mtu Ambaye Mali zake Nyingi ni za Haramu.

Question

Katika eneo la biashara ya vyakula pamoja na vyombo vya majumbani, kuna mtu anaishi hapo hapo na ambaye anafahamika kwa ubaya na kujipatia mali kwa njia zisizo za halali, lakini pia mtu huyu huko nyuma ana matukio ya uhalifu kama wizi, uporaji pamoja na kufanya biashara za uuzaji mihadarati, pembezoni mwa kazi hizi pia anafanya kazi zengine ambazo ni halali kisheria, lakini hata hivyo inaonekana faida aipatayo ni ndogo kwenye kazi zake za halali, je inafaa kumwuzia yule mtu kile anachotaka kununua kwa wafanya biashara wakati ambapo mimi sifahamu pesa atakayonilipa kwenye biashara yangu ameipata kwa njia halali au haramu? 

Answer

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Sala na Salamu zimwendee Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, pamoja na jamaa zake na Masahaba wake na wale wote waliomfuata. Ama baada ya hayo ...
Suala la kuchuma mali kwa njia zisizo halali linazingatiwa ni kula mali za watu kwa njia za udanganyifu ambazo ni batili. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi mlioamini! Msiliane mali yenu kwa dhuluma, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe} [AN NISAA, 29] .. {Wala msiliane mali zenu kwa nyia batili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua} [AL-BAQARAH, 188].
Ukweli wa mambo ni kuwa, mali ambayo mwanadamu anaweka mkono wake au nguvu zake hiyo ni mali inayomilikiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini hupewa uangalizi mwanadamu kwa njia ya kufaa kupewa uangalizi huo, huyu mwanadamu hakuwa isipokuwa ni mja tu wa Mwenyezi Mungu ambapo Mola Mtukufu Amempa dhamana ya kusimamia na kuendesha hizo mali kwa njia ya kumjaribu na kumfanyia mtihani. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Kisha tukakufanyeni nyiye ndio wenye kushika mahala pao baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyo tenda} [YUNUUS, 14]. Na Akasema tena: {Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu Aliyokupeni} [AN NUUR, 33]. Na Akasema: {Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika alivyo kufanyeni nyinyi kuwa ni waangalizi wake} [AL HADID, 7].
Anasema Imamu Al-Qurtwubiy katika kufasiri kwake Aya inayosema: {katika alivyo kufanyeni nyinyi kuwa ni waangalizi wake} ni dalili ya kuwa asili ya umiliki ni wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ama kwa upande wa mja hana ruhusa ya kutumia isipokuwa kwa utaratibu unaoridhiwa na Mwenyezi Mungu”. [17/238, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Masriya].
Na anasema Al-Abdariy Al-Maliky katika kitabu chake 1/132, chapa ya Dar Al-Turath: “Ikiwa mwanadamu ana haki ya kutumia chochote katika mali zake, basi matumizi yake si yenye kukamilika kwani ndani yake amezuiliwa, kwa sababu mwanadamu hana umiliki kamili, isipokuwa amepewa uhalali wa kutumia kwenye maeneo haya na amezuiliwa kutumia kwenye maeneo mengine, mali - kwa kweli - si mali yake lakini ipo kwenye mikono yake kwa njia ya kuazimwa azitumie katika mambo haya na wala asizitumie kwenye mambo yale, na hili limeelezwa kwa uwazi ndani ya Qur`ani na Hadithi”.
Kutokana na maelezo haya: Matumizi ya mwanadamu katika mali yake kwa namna yoyote ile, kiuhalisia ni matumizi ya mali isiyo kwenye miliki yake, na kutumia mali inayomilikiwa na mwengine kunaendana na ruhusa ya mwenye mali. Mwenyezi Mungu Ametoa ruhusa kwa mwanadamu kutafuta mali na kunufaika nayo lakini pia kuitoa kwenye njia ya halali na iliyopangiliwa, mali anayoipata kutoka kwa mtu mwengine haiwi miliki yake na wala hana haki ya kuitumia hata katika matumizi ya mambo mema, kama mtu ametoa sadaka mali aliyoipora kwa njia ya dhuluma pamoja na kuwa na uwezekano wa kuirejesha mali hiyo, basi anapata dhambi kwa uporaji wa dhuluma na matumizi yake na wala hataandikiwa thawabu za hiyo sadaka yake.
Amesema Imamu Al-Qurtwubiy katika ufupisho wa kitabu cha Imamu Muslim, [3/59, chapa ya Dar Ibn Kathir na Dar Al-Kalim Al-Twayyib] “Haikubaliki kwetu sadaka inayotokana na mali ya haramu, kwa sababu si yenye kumilikiwa na mwenye kutoa sadaka, nayo inazuiliwa kutumiwa, kama itakubalika hiyo sadaka basi lazima iwe ni yenye kuamrishwa na yenye kukatazwa kwa upande mmoja, nalo ni jambo lisilowezekana”.
Na ikiwa mali iliyopo mkononi mwa mwanadamu hakuichuma kwa njia ya halali haiwi miliki yake, na wala haifai kwa mwenye kujua hali hii kushirikiana naye na kupokea katika mali hiyo, isipokuwa ikiwa ni kwa lengo la kuirejesha kwa mwenyewe ikiwa anafahamika au kutolewa sadaka kwa niaba yake, kinyume na hivyo ni kushirikiana kwenye mambo ya dhambi na uadui pamoja na kula mali za watu kwa njia batili. Anasema Ibn Rajab Al-Hanbaliy katika kitabu cha: [Jamii Al-Ulum wa Al-Hikam, 1/210, chapa ya Dar es Salaam]: “Wakati wowote mtu atakapofahamu kuwa mali yenyewe ni ya haramu, imepatikana kwa njia haramu, basi inakuwa ni haramu kwake kuwa nayo. Limeelezwa hili kwa pamoja na Ibn Abdulbar na wengine”.
Anasema Al-Dusuqiy, katika wafuasi wa madhehebu ya Imamu Malik katika kitabu chake cha: [Sharh Al-Kabir 3/277, chapa ya Dar Ihyaa Al-Kutub Al-Arabiya] “Ama mtu mwenye mali ambayo yote ni ya haramu nayo ndiyo inayokusudiwa kutumika, basi inazuiliwa kushirikiana na mtu huyo, na anazuiliwa kutumia mali na vitu vyengine vinavyotokana na hii mali”.
Na anasema Imamu Al-Nawawiy katika kitabu cha: [Raudhat Al-Talibeen 7/337, chapa ya Al-Maktaba Al-Islamia] “Dua ya mwenye mali nyingi za haramu, inachukiza kupokelewa kama vile inavyochukiza kushirikiana naye. Ikiwa imefahamika kuwa chakula chake ni haramu basi ni haramu kujibiwa maombi yake”.
Anasema Ibn Qudama Al-Hanbaliy katika kitabu cha: [Al-Mughniy 4/180, chapa ya Dar Ihyaa Al-Turath Al-Araby]: “Pindi mtu akinunua kwa mtu ambaye mali yake ni haramu na halali: Kama vile mfalme dhalimu na mla riba, ikiwa inafahamika kuwa mauzo yake yanatokana na mali ya halali, basi hiyo itakuwa ni halali, na ikiwa itafahamika kuwa ni haramu basi hiyo itakuwa ni haramu”.
Ama ikiwa amepata baadhi ya mali kwa njia halali na baadhi yake kwa njia haramu, basi ikiwa itawezekana kwake kutenganisha mali ya halali na ile ya haramu, inafaa kushirikiana naye kwenye mali ya halali, na ni haramu kushirikiana naye kwenye mali ya haramu. Hii ndiyo asili kwenye mzunguko wa mali.
Ama ikiwa amechanganya mali halali na haramu na wala hakuna uwezekana wa kutenganisha kati ya mali hizo, basi kwa kawaida kiwango cha mali haramu kitakuwa kikubwa au kichache au sawa na mali ya haramu, au kutofahamika asilimia kati ya mali hizo za aina mbili, basi mali ambayo kwa kawaida kiwango chake cha haramu hakitakuwa kikubwa, inafaa kushirikiana naye, kwa sababu uwazi wa umiliki wa mwanadamu ni kile kilichopo mkononi mwake, na wala haubadilishwi uwazi huo isipokuwa kwa uelewa au dhana ya kweli, wala hakuna kinachopatikana katika hili isipokuwa kwa kupambanua mali ya haramu au kuwa kawaida yake ya kuwa na mali ya halali, ama kwa kuleta shaka tu au kuhisi hilo halipewi nguvu ya kuondoa uwazi wenye kauli yenye nguvu, kama vile kuingiza shaka katika mambo kama haya kutawaingiza watu kwenye matatizo na ubaya na kuenea ubaya wao, basi hakuna ubaya kushirikiana naye, kwa sababu kanuni inasema kuwa: Mwenye kuenea tatizo lake hupungua kadhia yake, na jambo likiwa kero kwa watu hupanuka hukumu yake.[Kitabu: Al-Ash-bah wa Nadhair cha Ibn Najm uk. 84, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya, na kitabu cha Fat-h Al-Qadir cha Ibn Al-Maham, 9/310, chapa ya Al-Kutub Al-Elmiya].
Ama ikiwa haramu ndiyo ina nafasi kubwa, asili hapo ni kuwa kushirikiana kunafaa pamoja na kuwa ndani yake kunachukiza, lakini ikiwa kuacha kushirikiana katika hali hii kutapelekea upande mmoja kuingia kwenye ubaya au kuwepo hali ya dharura, au kuenea ubaya wa watu kwa hilo, basi inafaa kushirikiana bila ya kuchukiza, kwa sababu kushirikiana kwenye mali ya haramu wakati huo kuna kuwa katika sehemu ya dhana, wakati ambapo kuwepo kwa ubaya kuna kuwa ni sehemu ya ukweli, na ukweli unatangulizwa dhidi ya dhana, kama vile ilivyokuwa kwenye kanuni ya Fiqhi ya Uislamu kuwa: Ikiwa kuna mgongano wa madhara mawili moja ni lenye madhara zaidi basi huchukuliwa dogo lake [Kitabu: Al-Ashbah wa Nadhair cha Imamu Suyutiy uk. 87, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Na madhara ya kuchukua mali isiyojulikana ukweli wa uharamu wake, ni afadhali zaidi kuliko kutokea madhara na kuenea matatizo, katika hali kama hii kauli inayopewa nguvu ni kufaa moja kwa moja pasi na kuwepo chukizo.
Mtume S.A.W., pamoja na Masahaba wake walikuwa wanashirikiana katika mashirikiano mbalimbali, walikuwa wanaingia makubaliano ya kibiashara na Mayahudi pamoja na Washirikina hali ya kuwa Mayahudi na Washirikina mikono yao haikuacha kuwa karibu na mali za haramu kama vile mali za riba, fedha za mauzo ya vilevi, ufasiki, masanamu na visivyokuwa hivyo katika vile vinavyokatazwa, pamoja na yote hayo inafaa kushirikiana nao kwa sababu ya kuenea matatizo, na kuchanganyika mali zao za haramu na zile za halali, na kutotenganisha mali haramu, wala haijapokewa kuwa Mtume S.A.W, alikuwa kawaida yake kumuuliza anayeshirikiana naye miongoni mwa wale wasiokuwa Waislamu au kuwataka maelezo ya kina kuhusu njia wanazozitumia kujipatia mali zao, wala haya hayajafanyika kwa Masahaba wala Mtume kuwaamrisha kufanya hivyo, pamoja na kufahamika wengi wasio kuwa Waislamu kuwa mali zao wanazichuma kwa njia za haramu kisheria, na uwezekano mkubwa wa mali hizo kuwafikia Waislamu kupitia mashirikiano mbalimbali, kanuni ya kisheria yaani ya kifiqhi iliyokubaliwa na Imamu Shafi R.A, na kukubaliwa pia na jopo la wanachuoni inasema: “Kuacha kuulizia undani wa mambo pamoja na kuwezekana huchukua sehemu ya kuenea yanayosemwa” [Kitabu: Al-Bahr Al-Muhit cha Zamakhashary, 4/201 – 203, chapa ya Dar Al-Kutub, na sherehe ya Al-jalaali al-mahally alaajam’hil-jawaami’I 2/24 chapa ya Dar Al-kutub Al-Elmiy, na utafiti unasema: Kanuni ya kuacha kuuliza undani wa mambo ni somo la vitendo uk.113, Dkt. Abdulrahman Al-Qarniy, chapisho la Chuo Kikuu cha Umm Al-Qura].
Mtume pamoja na Masahaba wake walishirikiana na wasio kuwa Waislamu pasi na kujua kwa kina kuhusu njia za mapato yao, na hii inachukua nafasi ya jumla ya ruhusa katika kushirikiana nao ni sawa sawa mali zao zimekuwa halali kutumika au zimechanganyika pasi na kuwezekana kutenganisha zilizo haramu katika zile za halali, - japo dhana kubwa itakuwa mapato yao mengi yanapatikana kwa njia za haramu – madamu mzunguko wa fedha unafanyika kati yao na Waislamu kwa sura ya makubaliano yaliyo halali, ama kunapokuwepo uhakika kuwa mali zilizopo mikononi mwao ni mali za haramu kutumika, basi hili ni lenye kukatazwa na ni haramu kushirikiana nao kwa mali hizo, au kuzungushwa kama zilivyo mali zengine zilizo haramu zinazokatazwa kuzungushwa au kuzunguka thamani yake. Imamu Bukhari na Imamu Muslim wamepokea kwenye vitabu vyao Sahihi, kutoka kwa Aby Masuud Al-Ansari R.A. amesema kuwa: “Hakika ya Mtume S.A.W. amekataza thamani ya mbwa, mali ya uzinifu na kumpa mali kuhani” na katika tamko la Abu Daud: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W: “Si halali thamani ya mbwa, wala kumpa mali kuhani na mali ya uzinifu” na imepokelewa na Abu Daud katika kitabu chake kutoka kwa Abu Huraira R.A. amesema: Hakika Mtume S.A.W. amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu ameharamisha pombe na thamani yake, akaharamisha mzoga na thamani yake, akaharamisha nguruwe na thamani yake”. Na imepokelewa na Abu Daud katika Hadithi ya Ibn Abbas R.A. kuwa: “Hakika Mwenyezi Mungu pindi anapowaharamishia watu kula kitu basi uharamishaji huo pia huwa ni kwa thamani yake”.
Kushirikiana kupitia mali ambayo ndani yake imechanganyika halali na haramu pasi na kufahamika moja wapo dhidi ya nyengine, kunazingatiwa ni katika dhana ambayo inapendeza kujitenga nayo kwa lengo la kuiweka mbali Dini na heshima, na inachukiza kuisogelea pasi na kuwepo haja ya msingi inayopelekea kuisogelea mali hiyo, kuepusha dhana mbaya na kuhofia kuingia kwenye haramu, kutokana na Hadithi iliyopokelewa na Bukhari na Muslim Hadithi ya Al-Na’man Ibn Bashir R.A. amesema: Nimemsikia Mtume S.A.W, anasema: “Hakika halali ipo wazi, na haramu ipo wazi, kati ya halali na haramu kuna vinavyofanana watu wengi hawafahamu hukumu zake, basi yeyote mwenye kujiepusha na hivi vyenye kufanana atakuwa ameiweka mbali dini yake na heshima, na mwenye kuingia kwenye hivi vyenye kufanana atakuwa ameingia kwenye haramu, ni kama mchungaji anayechunga pembezoni mwa eneo linalokatazwa, anaweza kulisha humo, fahamu kuwa kila mmiliki ana eneo alilokatazwa, fahamu kuwa makatazo ya Mwenyezi Mungu ni yale aliyoyaharamisha, fahamu kuwa ndani ya kila mwili kuna kipande kidogo cha nyama, pindi kipande hiko kinapokuwa salama basi mwili wote unakuwa salama, na kinapo haribika, huharibika mwili mzima, fahamu kuwa kipande hiko ni moyo”.
Na madhehebu ya wanachuoni wanasema kuwa, kushirikiana na mtu ambaye mali zake nyingi ni za haramu haziharamishwi lakini inachukiza kwa kuhofia kuingia kwenye haramu. Anasema Al-Hamawiy katika wafuasi wa Imamu Abu Hanifa katika kitabu cha: [Ghamzi U’yuunil-baswaairi 1/192, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya] “Kushirikiana na mtu ambaye mali zake nyingi ni za haramu lakini haijathibitika uharamu wa mali yake hiyo, basi si haramu kukubaliana naye kwa sababu kuna uwezekano wa mali kuwa halali na kutoharamishwa, lakini inachukiza kwa kuhofia kuingia kwenye haramu. Pia maelezo haya yapo kwenye kitabu cha: [Fat’hul-qadiir].
Na anasema Al-Dusuqiy katika kitabu chake cha: [Sharhul-Kabiir 3/277, chapa ya Dar Ihyaa Al-Kutub Al-Arabiya] “Fahamu kuwa mwenye kumiliki mali nyingi ambazo ni za halali na sehemu ndogo ni mali ya haramu, kauli iliyopitishwa ni kuwa inafaa kushirikiana naye na kula katika mali yake, kama alivyosema Ibn Qaasim tofauti na wanaoeneza kauli ya uharamu kufanya hivyo. Ama yule mwenye mali nyingi za haramu na sehemu ndogo ya mali yake ni ya halali, madhehebu ya Ibn Qaasim yanasema: Inachukiza kushrikiana naye na kula katika mali yake hiyo, ni kauli iliyopitishwa tofauti na wanaoeneza kauli ya uharamu kufanya hivyo”.
Anasema Imamu Al-Nawawiy miongoni mwa watu wa Imamu Shafi kwenye kitabu cha: [Rawdhwatul-Twaalibeen 7/337)] “Maombi ya mwenye mali nyingi za haramu, inachukiza kujibiwa kwake kama vile inavyochukiza kushirikiana naye”.
Na anasema Al-Suyutiy miongoni wa watu wa Imamu Shafi katika kitabu cha Al-Ash-bah wa Nadhair uk. 107 “Kushirikiana na mwenye mali nyingi za haramu ikiwa halifahamiki hilo basi si haramu kwa kauli iliyosahihi, lakini inachukiza, na vile vile kuchukua zawadi kwa Mfalme ikiwa sehemu kubwa ya haramu imo mikononi mwake, kama alivyosema kwenye kitabu cha Sharh Al-Muhadhab: Kilichokuwa kinafahamika ni kuchukiza na wala sio haramu”.
Na anasema Ibn Qudama Al-Hanbaliy katika kitabu cha: [Al-Mughniy 4/180]: “Ikiwa atanunua yule ambaye katika mali yake zipo za haramu na halali kama vile Sultani mwenye kudhulumu na mla riba, ikiwa itafahamika kuwa mauzo yanatokana na mali yake ya halali basi hiyo ni halali, na ikifahamika kuwa ni ya haramu basi hiyo ni haramu, kwa sababu uwazi ni kuwa kile kilichokuwa mikononi mwa mwanadamu ni miliki yake, ikiwa hafahamu mali ipi tumeifaanya kuwa inachukiza kwa uwezekano wa kuwa ndani yake kuna haramu, basi haibatilishi kuuza, kwa sababu ya uwezekano wa kuwa ni mali ya halali. Ikiwa haramu ni ndogo au nyingi, hii ndiyo dhana, na kiwango cha haramu kuwa kichache na kingi ndicho kinachoujenga wingi wa dhana na uchache wake”.
Na anasisitiza Al-Ruhaibany Al-Hanbaliy kuwa, kilichopitishwa katika madhehebu ya Imamu Hanbal ni kuchukiza ni sawa sawa haramu hiyo ni chache au ni nyingi. Anasema kwenye kitabu cha: [Matwaalibu Uli-nnuhaa 5/233, chapa ya Al-Maktab Al-Islamiy] “Inachukiza kuitikiwa yule ambaye katika mali yake kuna halali na haramu, kama vile inavyochukiza kula katika mali hiyo na kushirikiana na mtu mwenye mali hiyo na kupokea zawadi yake na kupokea anachojitolea, pia kukubali sadaka yake iwe haramu ni ndogo au nyingi, na amesema Uqailu katika kitabu cha: [Al-Fusul] na vitabu vyengine, nayo ndiyo madhehebu na yanaungwa mkono na Hadithi inayosema: “Mwenye kuacha yenye kufanana hakika atakuwa ameiweka mbali dini yake na heshima yake” hupewa nguvu hukumu ya kuchukiza na kudhoofishwa kwa mujibu wa wingi wa mali haramu na uchache wake”.
Na katika madhehebu mengine yanayokwenda kinyume na kauli za jopo la wanachuoni, lipo kundi la waja wema waliotangulia kama vile Al-Hassan, Mak’hul, Al-Fadhil Ibn Ayadh, ambao wameruhusu kuwa naye mtu huyu mwenye kuchanganya mali yake na haramu pamoja na kukubalika zawadi yake na kula naye iwapo haijafahamika kwa uwazi kuwa mali yake hiyo ni ya haramu. Imepokewa na Ibn Mas’uud R.A. kuwa aliulizwa kuhusu yule jirani anayekula mali za riba bila kificho wala haoni ubaya kutumia mali chafu na kulisha watu, akasema: muitikieni, kwa sababu kinachotolewa ni chenu na dhambi ni zake. Imepokewa kama hivi kutoka kwa Salman Al-Farisy R.A. na pia kutoka kwa Said Ibn Jubair na Is-haqa Ibn Raahuwih pamoja na Muuraq Al-Ajaly na Ibrahim Al-Nakhiy na wengineo, na katika mapokezi ya Ibn Mas’uud yanasema muulizaji alimuuliza: Sifahamu kitu kwake isipokuwa ni ubaya na haramu, akasema: Muitikie. Haya yamesahihishwa na Imamu Ahmad kutoka kwa Ibn Mas’uud, lakini hata hivyo yamepingana na yale yaliyopokewa kutoka kwake pale aliposema: Dhambi ni miliki ya moyo.
Na imepokewa kutoka kwa Ibn Syreen kuhusiana na mtu anayetumia mali ya riba, akasema: Hakuna ubaya kwake, na kuhusu mtu anayetumia mali itokanayo na mchezo wa kamari, akasema: Hakuna ubaya kwake. Na imepokewa tofauti na hivi na Al-Hassan, naye amesema: Hakika uchumaji huu ni mbaya basi chukueni katika mali hiyo kama vile mtu aliyetenzwa nguvu, miongoni mwa wale waliokuwa hawakubali hilo ni Ibn Musayyib na Qaasim Ibn Muhammad, Bashir Ibn Said, Al-Thauriy, Muhammad Ibn Waasii, Ibn Mubaaraka na Ahmad Ibn Hanbal katika mapokezi yao, radhi za Mwenyezi Mungu ziwaendee wote. [Kitabu: Al-Majmuu, 9/432, chapa ya Al-Muniriya. Na kitabu: Jamii Al-Ulum wa Al-Hikam cha Ibn Rajab Al-Hanbaliy 1/208 – 210, chapa ya Dar es Salaam].
Kuna kundi lengine la wanachuoni ambalo limekubaliana juu ya uharamu katika kushirikiana kifedha na yule ambaye pato lake kubwa ni mali ya haramu, kama ambavyo hayo pia yamesemwa na Imamu Al-Ghazali mfuasi wa Imamu Shafi, na vile vile yamesemwa hayo na Al-Izz Ibn Abdulsalaam, pindi haramu inapokuwa nyingi kiasi ambapo halali ni chache, na amesema kwa upande wa haramu pia kundi la watu wa Imamu Malik, wametofautiana watu wa Imamu Hanbal lipo kundi kama vile Shirazy na Al-Azjiy wamesema kuwa ni haramu kufanya mashirikiano ya kifedha hata kama mali haramu itakuwa ni ndogo, kundi lengine miongoni mwao kama vile Al-Kharqy na Ibn Juziy wanaona ni haramu kushirikiana kifedha ikiwa mali ya haramu ni nyingi, kundi lengine pia ambalo miongoni mwao kuna kama vile yule mwenye kitabu cha: [Al-Ria’ayat] amesema kuwa, ikiwa mali ya haramu imezidi zaidi ya theluthi moja, basi ni haramu kushirikiana na mwenye mali hiyo, na kama ni chini ya hapo hakuna ubaya wa kushirikiana naye. Lakini kauli yenye nguvu kwenye madhehebu ni ile kauli ya kuchukiza moja kwa moja kama ilivyotangulia kuelezwa. [Kitabu: Matwaalivu Uli nnuhaa 5/233. Na kitabu: Al-Insaf cha Mardawiy 8/322 – 323, chapa ya Dar Ihyaa Al-Turath Al-Araby].
Aliulizwa mwanachuoni Ibn Hajar Al-Haitimy mfuasi wa Imamu Shafi kuhusu kushirikiana na Mayahudi na Wakristo hali ya kuwa wao hawana hofu kwa kile walichonacho ikiwa ni pamoja na kufanya biashara za pombe, utoaji riba na mengineyo, je ni halali kushirikiana nao katika miamala ya kifedha na kukubali zawadi zao? na je ni haramu kushirikiana kifedha na yule ambaye sehemu kubwa ya mali yake ni ya haramu au hapana? Akajibu kwa kauli yake, “Muda wa kuwa haujabainika uharamu kwenye hiyo mali basi inafaa kushirikiana kifedha na kuchukua zawadi zao, kwani Mtume S.A.W, aliwahi kupokea zawadi kutoka kwao, lakini ikibainika kama vile mtu kafiri anayeishi kwa makubaliana na Waislamu anauza pombe na akapata pesa kwa uuzaji huo kisha akampa Mwislamu ima kwa njia ya mkopo au vinginevyo, basi kwa Mwislamu si halali kupokea fedha hizo, kama vile walivyosema Masheikh wawili (Bukhari na Muslim).
Na imenukuliwa kutoka kwa Al-Zarkhashiy na Ibn Al-Imad tamko linalokubaliana na kauli hii, vile vile inasemwa katika kula mali ya dhuluma na mwenye kumiliki mali nyingi ya haramu inachukiza ikiwa haijafahamika mali ya haramu au imechanganyika, na mwenye mali anaweza kufahamu kama ilivyokuja kwenye kitabu cha Al-Majmuu, lakini ikiwa haiwezekani kufahamika basi inakuwa ni katika mali za kuingizwa kwenye mfuko mkuu wa pato la Taifa. [Kitabu: Al-Fatawa Al-Fiqhiya Al-Kubra, 2/233, chapa ya Al-Maktaba Al-Islamiya]. Na Hadithi ya Al-Baihaqiy na wengine: “Mtu asiyetaka kujua chakula chake kinatoka wapi, wala kinywaji chake kinatoka wapi, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu wala haujali mlango wowote ule wa moto wa Jahannam atakaomuingizia”. Ni wazi kwa yule anayejichumia kwa mkono wake kile kilicho halali, na ikiwa anajua pia kilicho haramu. Ama kwa yule asiyejua hakubaliki katika hilo, na ikiwa atafanya zuri huachwa. Na amesema Al-Ghazaliy katika kitabu cha: [Ghairil-Basiitw] kuwa ni haramu kushirikiana naye kifedha yule ambaye mali yake nyingi ni ya haramu, amesema kwenye kitabu cha Al-Majmuu katika kulijibu hilo: “Si katika madhehebu yetu isipokuwa wameiga watu wetu kutoka kwa Al-Abhary Mtu wa Imamu Malik kuwa, lau mtu atafahamu mali nyingi aliyonayo ni ya haramu si lazima kuuliza, tofauti na kauli ya Al-Ghazali, na kukubalika na Ibn Abdulssalaam katika hilo, kama atakiri kuwa Dinar elfu moja iliyopo mkononi mwake ni ya haramu lakini Dinar moja ni ya halali, kama vile wakichanganyika njiwa elfu moja wa jangwani na wale wa kijijini, tofauti ni kuwa hii ni asili inayozingatiwa, nayo ni mkono unaochuma halali na tofauti yake katika masuala ya njiwa, na kutokana na hilo hawakuwa mbali na kauli mbili katika uchafu na usafi, kwa sababu asili hapa ni halali na hupewa nguvu halali iliyopo mkononi na wala hakuna mfano mwingine wa kupewa nguvu kama huu. Na ikaibua tofauti pia kwamba ikiwa kutachanganyika vyenye akili na wafu hivyo wafu wenyewe ni haramu tu. Na wala hakuna uwiano unaoonesha tofauti na halali, mkononi mwa mwenye mali nyingi iliyo ya haramu”.
Maelezo ambayo tunayapa nguvu zaidi ni yale yaliyoelezwa na jopo la wanachuoni na kupitishwa na wanachuoni wa madhehebu manne nayo ni kauli ya kuchukiza kushirikiana kifedha isipokuwa pale patakapo kuwa na haja au dharura ya kufanya hivyo, kutokana na yale tuliyotangulia kuyaeleza na kuyatolea dalili na kanuni, kwa sababu kauli ya uharamu ndani yake ina uzito na ubaya, kama ambavyo ndani yake pia inafungua mlango wa kutiliana shaka na pengine hata magonvi yakatokea pamoja na watu kutuhumiana. Ama kauli ya kufaa moja kwa moja inapingana na maandiko ambayo yanahimiza kujitenga na yale yenye kuleta shaka. Na Mwislamu kuieweka mbali dini yake na heshima yake katika hilo, kama vile kujitoa kwenye tofauti za wanachuoni katika mambo kama haya ni jambo lenye kupendeza.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia na kwa msingi wa swali ni kuwa: Inafaa pamoja na kuchukiza kushirikiana kifedha na jirani yake ambaye anashukiwa kuwa mali yake imechanganyika ya halali na ya haramu, iwapo dhana kubwa ya muulizaji katika mali hiyo itakuwa haramu ni nyingi zaidi, basi inapendeza kwake kujitenga na kutoshirikiana naye, na kushirikiana na yule asiye na shaka shaka kwenye mali yake. Na hili ikiwa hali yenyewe inapelekea kushirikiana huko kunatokana na uwepo wa dharura na haja, basi kwa wakati huo inafaa kushirikiana naye kifedha bila ya kuchukiza.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.


 

Share this:

Related Fatwas