Swala ya Wanaotubia.

Egypt's Dar Al-Ifta

Swala ya Wanaotubia.

Question

Ni ipi Swala ya Wanaotubia? Na huswaliwa vipi? Ina idadi ngapi ya rakaa zake? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Swala asili yake kwa upande wa lugha ni: dua, kwa kauli yake Mola Mtukufu: {Na uwaombee rehema} [AT-TAWBAH, 103]. Kwa maana ya waombee dua.
Na katika istilahi: wanachuoni wamesema: ni kauli na vitendo ambapo hufunguliwa kwa takbira na hukamilishwa kwa kutolewa salamu pamoja na nia, kwa masharti maalumu.
Amesema Imamu Abu Hanifa: ni jina la vitendo hivi vinavyofahamika kuanzia kisimamo kurukuu hadi kusujudu.
Na neno Al-Awaben (Wanaotubia): ni wingi wa neno (Awab), nalo lina maana ya mtiifu, na pakasemwa kuwa: ni mwenye kurudi kwenye utiifu [sharhu ya An-Nawawiy kwenye sahihi ya Muslim, 6/30, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy], au kwa maana nyengine ni mwenye kufanya wingi wa kurejea na kurudi kwa Mwenyezi Mungu kwa kutubia [Kitabu Faidh Al-Qadir, 1/408, Maktabat At-Tujariya].
Wanachuoni hawapo mbali katika kulitumia neno hili kwa maana hii, nayo ni Swala ya Sunna, na hutekelezwa kama vile Swala zengine zote, kwa uwingi ina rakaa ishirini na kwa uchache wake ni rakaa mbili.
Wafuasi wa madhehebu ya Imamu Shafiy wameelezea kuwa yenyewe huitwa kwa kushirikishwa na Swala ya Adhuha na Swala ya Sunna anayoiswali mtu baada ya Swala ya Magharibi kuelekea Swala ya Isha [Kitabu Asnaa Al-Matwalib, 1/206, chapa ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy].
Na Swala hii huitwa pia kuwa ni Swala ya kusahaulika, hii ni kutokana na watu wengi kuwa wameisahau na kushuhulishwa kwao na Swala zingine za Sunna kulala na mambo mengine [Kitab Al-Iqnaa cha Sherbeniy pamoja na Hashiyat Al-Bujairimy, 1/427, chapa ya Dar Al-Fikr, Hashiyat Al-Jamal sherehe ya Al-Minhaj, 1/478, chapa ya Dar Al-Fikr].
Na imeitwa Swala ya Sunna ambayo huswaliwa baada ya Magharibi kuwa Swala ya Wanaotubia, kwa sababu mwenye kuisawli anakuwa ni mwenye kurejea kwa Mola Mtukufu pamoja na kutubia kwa yale aliyoyafanya ndani ya mchana wake, pindi anaporudia kufanya hivyo inajulisha juu ya kurudi kwake kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hata kama haikuzingatiwa maana hiyo [Hashiyat Al-Jamal sherehe ya Al-Minhaj, 1/478].
Na amesema Imamu Shafiy: kwa uwingi wake ni rakaa ishirini na inakuwa ni kati ya wakati wa Magharibi na Isha, na kwa uchache wake ni rakaa mbili. [Kitabu Al-Iqnaa cha Sherbeniy na Hashiyat Al-Bajairamiy, 1/427], na Sunna ya Magharibi yawezekana kuingizwa kwenye Swala hii [Kitab Tuhfat Al-Ahwadhiy, 2/421, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Na katika yaliyopokelewa kuhusiana na Swala ya Wanaotubia kuwa yenyewe ni Swala ya Adhuha, ni yale yaliyokuja kwenye Hadithi ya Zeid Ibn Arqam R.A. amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.: “Swala ya Awwaabeena huswaliwa muda ule anapoungua jua mtoto wa ngamia” Hadithi imetokana na Muslim.
Kwani wakati wa Adhuha pindi jua linapopanda ndani ya kipindi cha kiangazi huwa linakuwa na miyale mikali yenye joto kali sana ambalo linaunguza. [Sharhu ya Anawawiy kwenye kitabu cha sahihi Muslim, 6/30, na kitabu Nail Al-Awtar, 3/80, chapa ya Dar Al-Hadith).
Na katika yaliyokuja ni Hadithi itokanayo na Abu Huraira R.A. amesema, “Ameniusia kipenzi change S.A.W. mambo matatu: kufunga siku tatu kila mwezi, kuswali rakaa mbili za Adhuha, na kuswali Swala ya Witri kabla ya kulala” Hadithi hii imekubaliwa na maimamu wote.
Na katika mapokezi: “Na wala nisiache kusali rakaa mbili za Adhuha kwani zenyewe ni Sala ya Wanaotubia” ni mapokezi yanayotokana na Imamu Ahmad.
Kutoka kwa Abu Huraira R.A. hakika ya Mtume S.A.W. amesema: (Hakuna anayeswali Sala ya Adhuha isipokuwa ni mtu Awab “Mwenye kutubu kwa Mola wake”. Akasema: “hiyo ni Swala ya Wanaotubia”. Imepokelewa na Hakim katika kitabu cha: [Mustadrak, 1/422,] na akasema: Hadithi hii ni sahihi kwa sharti ya Imamu Muslim.
Na katika yaliyopokelewa kuhusiana na Swala hii ya Wanaotubia na yenyewe kuwa ni Swala ya Sunna ambayo hutekelezwa baada ya Magharibi, ni yale yaliyopokelewa na Muhammad Ibn Al-Munkadir kuwa hakika ya Mtume S.A.W. amesema: “Mwenye kuswali kati ya magharibi na Isha basi hiyo ni swala ya Wanaotubia”. [Kitab Az-Zuhud cha Ibn Al-Mubarak, uk. 445, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Na akasema Imamu Shaukaniy katika kitab Nail Al-Autar, 3/67: “Na Hadithi hii ijapokuwa ni Hadithi Mursal lakini haipingani na yale yaliyomo katika sahihi miongoni mwa kauli yake Mtume S.A.W.: “Swala ya Wanaotubia ni pale jua linapomuunguza mtoto wa ngamia” yenyewe hakuna kiziwizi cha kuwa Swala zote hizi mbili ni Swala za Wanaotubia. Na kutokana na Abdillah Ibn Umar R.A. amesema: “Swala ya Wanaotubia husaliwa kati ya kugeuka watu kwenye Sala ya Magharibi kuelekea Swala ya Isha” [yamepokelewa na Ibn Abi Shaiba katika kitabu chake, 2/103, Maktabat Ar-Rushd].
Na kutoka kwa Abdillah Ibn Amr Ibn Al-As R.A. amesema: “Sala ya Wanaotubia: ni Swala ya chemba kati ya Magharibi na Isha”. [maelezo yamepokelewa na Ibn Al-Mubarak katika kitabu cha Az-Zuhud uk. 445].
Na kutokana na Abi Uqail Zahra Ibn Maabad amesema: nimemsikia Ibn Al-Munkidar na Aba Hazim wanasema katika kauli ya Mola Mtukufu: {Mbavu zao zinaachana na vitanda}[AS-SAJDAH, 16]. Ni wakati kati ya Magharibi na Swala ya Isha, ni Swala ya Wanaotubia. Imepokelewa na Al-Baihaqiy.
Na kumepokelewa uhimizo kwa ujumla juu ya Swala hii kuswaliwa kati ya muda wa Magharibi na Isha ndani ya baadhi ya Hadithi za Mtume S.A.W., miongoni mwa Hadithi hizo ni pamoja na ile iliyopokelewa kutoka kwa Abu Huraira R.A. kuwa Mtume S.A.W. amesema: (Yeyote mwenye kuswali rakaa sita baada ya Swala ya Magharibi kisha hakuzungumza ndani ya wakati huo jambo baya, basi hulinganishwa sawa na amefanya ibada kwa miaka kumi na miwili) [imepokelewa na At-Tirmdhiy na Ibn Maja].
Na Hadithi inayotokana na Bi. Aisha R.A. amesema kuwa Mtume S.A.W. amesema: :Mwenye kuswali rakaa ishirini kati ya Magharibi na Isha, basi Mwenyezi Mungu Atamjengea mtu huyo jumba Peponi”. Imepokelewa na Ibn Maja.
Na hadithi inayotokana na Ibn Omar RA kuwa Mtume S.A.W., amesema: (Mwenye kuswali rakaa sita baada ya Magharibi kabla ya kuzungumza lolote, basi Mwenyezi Mungu humsamehe kwa ibada hiyo dhambi za miaka hamsini). Imepokelewa na Muhammad Ibn Nasr Al-Muruziy, kama vile ilivyo pia kwenye kitabu cha Mukhtasar Qiyam Al-Lail, uk. 87, na katika isnadi yake Muhammad Ibn Ghazwan Ad-Demashqiy, amesema Abu Zara’: akipinga Hadithi. Rejea: Kitab Al-Jarh’ wa At-Ta’adil, 8/54, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy.
Kutoka kwa Amar Ibn Yasir kuwa, alimwona Mtume S.A.W. anaswali baada ya Magharibi rakaa sita, na akasema: “Mwenye kuswali rakaa sita baada ya Magharibi husamehewa dhambi zake hata kama zitakuwa nyingi mfano wa mapovu ya bahari”. Imepokelewa na At-Tabraniy ndani ya kitab Ausat wa Saghir.
Na kutokana na Ubeid mtumishi wa Mtume S.A.W. amesema: aliulizwa kama Mtume S.A.W. alikuwa akiamrisha kusali baada ya Swala za Lazima au Swala za Faradhi au zisizo za faradhi? Akasema: “Ndyio ni kati ya Magharibi na Isha”. Imepokelewa na Ahmad.
Na vile vile imepokelewa kuwa waja wema waliotangulia Mola Awe radhi nao walikuwa wanafanya juhudi kubwa katika kuhuhisha wakati huu kati ya Magharibi na Isha kwa kufanya ibada na kusali na kuwa na shime kubwa katika hayo, kutoka kwa Abdulrahaman Ibn Al-Asad kutoka kwa baba yake amesema: sikuwa nakwenda kwa Abdillah Ibn Masud ndani ya wakati huo – kwa maana ya kati ya Magharibi na Isha – isipokuwa nilimkuta akiwa anaswali, nikamuuliza kuhusu hilo, akasema: ndiyo ni wakati wa kujisahau kwa watu wengi – yaani ni kati ya Magharibi na Isha. [Kitab Az-Zuhd cha Ibn Al-Mubarak, uk. 445].
Na kutokana na Ibn Umar R.A. amesema: Mwenye kuingia kwenye ibada ya rakaa nne baada ya Magharibi, basi anakuwa ni kama aliyeendelea kupigana vita moja baada ya nyengine. [Kitab Az-Zuhd cha Ibn Al-Mubarak, uk. 445].
Na kutoka kwa Anas Ibn Malik R.A. alikuwa anaswali kati ya Magharibi na Isha na anasema: huko ndiko kuhuhisha usiku. [Kitabu cha Musanaf Ibn Abi Shaiba, 2/102].
Na kutokana na tafsiri ya kauli yake Mola Mtukufu: {Mbavu zao zinaachana na vitanda} [AS-SAJDAH, 16], amesema: wanaswali kati ya Magharibi na Isha. (ameinasibisha As-Shaukaniy katika kitabu cha: ]Nail Al-Autar, 3/67, cha Ibn Mardawiy] katika tafsiri yake, na kunukuliwa kuwa Al-Iraqiy ameisemea hivyo kwenye kitabu chake).
Na kutoka kwake pia katika tafsiri ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Walikuwa wakilala kidogo tu usiku} [Adh-dhariyat, 17]. Amesema: Aya hii imeteremka kwa wale wenye kuswali kati ya Magharibi na Isha. [amesahihisha Al-Iraqiy kama ilivyokuja kwenye kitabu Naili Al-Autar, 3/67].
Na kutokana na Abi As-sha’athaa amesema: amani iwe kwenu kwa kuswali kati ya Isha mbili - kati ya Magharibi na Isha - kwani wakati huo hupunguziwa mmoja wenu na mambo ya kawaida ayafanyayo na kukesho mwanzoni mwa usiku kunaondoa uwezo wa kuamka usiku kwa ajili ya ibada. [Kitab Musanaf Ibn Abi Shaiba, 2/102].
Na kutokana na Said Ibn Jubeir alikuwa anaswali kati ya Magharibi na Isha na anasema: huko ndiyo kuhuhisha usiku. [Kitabu Musanaf Ibn Abi Shaiba, 2/102].
Na kutokana na Mansour Ibn Al-Mu’utar katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu pale Aliposema: {Miongoni mwa Watu wa Kitabu wamo watu walio simama baraabara, wanasoma Aya za Mwenyezi Mungu nyakati za usiku, na pia wanasujudu} [Aal-Imran, 113], amesema: nimepata habari kuwa walikuwa wanasali kati ya muda wa Magharibi na Isha. [Kitab Mukhtasar Qiyaam Al-lail, uk.78].
Amesema Shaukaniy: “amesema Hafidh Zainulddin Al-Iraqiy: miongoni mwa waliokuwa wanasali kati ya Magharibi na Isha katika Masahaba ni: Abdillah Ibn Mas’ud, Abdillah Ibn Amr, Salman Al-Farisy, Ibn Umar, Anas Ibn Malik, hao ni katika watu wa asili ya Madina. Katika watu waliofuata baada yao kwa maana ya taabin ni pamoja na: Al-Usud Ibn Yazeed. Abu Uthman An-Nahdiy, Ibn Abi Malik, Said Ibn Jubeir. Muhammad Ibn Al-Munkadir, Abu Hatim, Abdillah Ibn Sakhbara, Aly Ibn Al-Hussein, Abu Abdulrahmaan Al-Hably, Sharih Al-Qadhy. Abdillah Ibn Mughfel na wengineo. Na katika Maimamu: Sufyan Al-Thauriy.
Aya na Hadithi zilizotajwa kwenye mlango huu zinaonesha juu ya uhalali wa kufanya wingi wa kuswali kati ya magharibi na Isha, na Hadithi hata kama zitakuwa nyingi zake ni dhaifu zenyewe kwa ujumla wake ni zenye kuendeleza na kukuza hasa matendo mema. (Kitabu Naili Al-Autar cha Shaukaniy, 3/68).
Kuzifanyia kazi hadithi dhaifu katika matendo mema ni jambo linalofaa, hasa wameyafanyia kazi kwa nguvu zote Maimamu waliotangulia, maudhui hii imetujia kwa namna ya pakee - kwa maana ya kuzifanyia kazi hadithi dhaifu - kwa Fatwa inayojitegemea.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia, yanatubainishia wazi ufahamu na uelewa wa Swala ya Wanaotubia, namna yake na uhalali wake, na kutokana na hilo, basi hakuna kiziuizi chochote katika kuendeleza Swala hii, kwa sababu ni katika Swala za Sunna.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas