Kukutana Kati ya Kuitekeleza Hija na Kumuozesha Mtoto.
Question
Nina kiasi cha fedha ambacho kinaniwezesha kuitekeleza fardhi ya Hija, na hakuna kisichonizuia kuitekeleza faradhi hiyo kwa kuitumia fedha hii isipokuwa mambo mawili: Ima naweza kuitekeleza faradhi ya Hija mwaka huu; au kulipia gharama za kumuozesha mtoto wangu, kwa ajili ya kujikinga na maasi na akamilishe nusu ya dini yake, kwa kujua kuwa yeye anastahiki msaada huu na anauhitajia, na kama nisipofanya hivyo, kuoa kwake kutachelewa muda mrefu.
Je, lipi linalopewa kipaumbele cha kuitumia fedha hii? Nipeni Fatwa, na Inshaallah mtapata thawabu, kwa sababu mimi nipo katika utata wa hali ya juu
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya hayo:
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Kitabu chake kitukufu: {Na Mwenyezi Mungu amewawajibishia watu wafanye Hija katika nyumba hiyo; yule awezaye kufunga safari kwenda huko}. [AALI IMRAAN: 97], Kwa hiyo Hija ni ibada inayowajibika kwa kila awezaye. Na katika Kitabu cha Imamu Muslim, kutoka kwa Abu Hurairah R.A., anasema: “Mtume S.A.W., alituhutubia akasema: Enyi watu, hakika Mwenyezi Mungu amekuwajibishieni Hija, basi hijini, na hapo mtu mmoja akasema: kila mwaka, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?, na Mtume akanyamaza, yule mtu akasema tena mara tatu, hapo Mtume S.A.W., akasema: Ningelisema ndiyo, basi ingeliwajibika, na nyinyi hamtaweza, kisha akasema: Niacheni ninapokuacheni, na hakika watu waliokuwa kabla yenu waliangamia kwa sababu ya maswali yao mengi, na hitilafu yao kwa Manabii wao, na mimi nikikuamuruni kitu kitekelezeni kadiri iwezekanavyo, na nikikutakazeni kitu basi kiacheni”.
Hadithi hii inamaanisha kuiambatanisha Hija na uwezekano, kwa sababu ya kutojibu Mtume S.A.W., kwa ile inayolazimu Hija kwa awezaye na asieiweza, na kwa yakini yake S.A.W., kuwa upole wake kwa umma wake ndiyo sababu ya kutotoa jibu, ili umma usije kukalifishwa kufanya usiyoyaweza. Kisha maelezo yake S.A.W., kuwa amri yake itekelezwe na wanaokalifishwa kadiri iwezekanavyo, kama anavyosema: “na mimi nikikuamuruni kitu kitekelezeni kadiri iwezekanavyo”, na umma umekubali kwa pamoja uwajibu wa Hija kwa awezaye mara moja tu katika maisha yake. Yaani ni ibada ya maisha. [Al-Mughniy, na Ibn Qudamah: 3/85, Ch. Ya Dar Ihiyaa At-Turaath Al-Arabiy].
Wanazuoni walikubali kwa pamoja masharti matano ambayo Hija inawajibika kwayo, nayo ni: (kusilimu), (kubaleghe), (akili), (uhuru), na (uwezekano), na haijulikani hitilafu kati ya wanazuoni juu ya hayo. [Mughniy Al-Muhtaj: 2/210, Ch. Ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah; Al-Mughniy na Ibn Qudamah].
Imamu Al-Bajiy, Mfuasi wa madhehebu ya Malik anaeleza (uwezekano) akisema katika [Al-Muntaqa Sharh Al-Muwatta’: 2/268- 269, Ch. Ya Dar Al-Kitaab Al-Islamiy]: “uwezekano wa kuifikia nyumba (Msikiti Mtukufu) bila ya kugeuza mazoea yo yote, na hii ina hitilafu kwa mujibu wa hitilafu ya hali za watu; mtu mwenye mazoea ya kusafiri kwa miguu, na akaweza kuifikia Hija kwa njia hii, basi analazimika kuhiji hata asipokuwa na kipando; na mwenye mazoea ya kuwaomba watu na akaweza kufikia Hija kwa njia hii, basi analazimika kuhiji hata asipokuwa na chakula; na mwenye kuzoea kupanda kipando, na hana haja ya watu, na akapata ugumu kufikia Hija kutokana na kutokuwepo vitu hivi, basi halazimiki kuhiji”. [Mwisho].
Wakati wa kupatikana sharti la uwezekano pamoja na masharti yote ya uwajibu wa Hija, basi analazimika Muislamu mwenye kubaleghe, mwenye akili, na mwenye uhuru aitekeleze Hija, nayo ni fardhi ya Uislamu, na asipoitekeleza fardhi hii wakati yeye anaweza kuitekeleza, na msimu wa Hija ukampita, hapa jukumu la faradhi litaendelea kuwepo juu yake, na dhima imo ndani yake, na itakuwa kama deni kwake, na hata kama uwezekano huo ungelipo au haupo; na jukumu lake la kuitekeleza ibada hii ya faradhi haliondoki kamwe mpaka aitekeleze au itekelezwe kwa niaba yake na mtu mwingine, kwa hali ya kushindwa au kufa, hapo sehemu ya mali yake itachukuliwa kwa ajili ya kuitekeleza kwa niaba yake, kama vile madeni yote ambayo hakuweza kuyalipa baada ya kuambatana na dhima yake. Na hii ni pamoja na uwepo wa hitilafu ya wanazuoni kuhusu uwajibu wa Hija: unalazimika kwa wakati huo au kwa kuchelewesha, na hakika mambo yalivyo ni kuwa kuiacha Hija wakati anaweza kuitekeleza, hapo fardhi hii inaambatana nae na kuwa dhima na deni juu yake.
Imamu An-Nawawiy katika kitabu cha: [Al-Majmuu’: 8/289, Ch. Ya Al-Muniiriyah] anasema: “Ikiwa Hija hii itawajibika ndani ya mwaka huu, na mtu akawa anaweza kuitekeleza mwaka huu na hakuweza mwaka uliopita, basi uwajibu unamlazimikia yeye kutokana na kuwa kwake na uwezo, na ni bora kuifanya ihramu ya Hija katika mwaka huo, na inajuzu kuiahirisha; kwa sababu Hija, kwa maoni yetu, ni wajibu unaochelewesheka”. [Mwisho].
An-Nawawiy anayafupisha madhehebu ya wanazuoni kuhusu suala la wakati huo au kuchelewesha akisema katika kitabu cha: [Al-Majmuu’: 7/86]: “Tawi la madhehebu ya wanazuoni kuhusu Hija iwe kwa wakati huo au kwa kuchelewesha: Tumetaja kuwa madhehebu yetu kuwa kuna kuchelewesha, na hii pia ni kauli ya Al-Awzaiy, Ath-Thawriy, na Muhammad Ibn Al-Hassan; na imenukuliwa na Al-Mawardiy kutoka kwa Ibn Abbas, Anas, Jabir, Attaa’, na Tawuus, Radhi za mwenyezi Mungu ziwashukie; na Malik na Abu Yusuf wanasema: ni kwa wakati huo, nayo ni kauli ya Al-Muzaniy, kama ilivyotangulia, na pia ni kauli ya wengi wa wanafunzi wa Abu Hanifa, lakini Abu Hanifa mwenyewe hana maandiko yoyote kuhusu hivyo”. [Mwisho].
Miongoni mwa dalili za wanaosema uwajibu wa Hija kwa njia ya kuchelewesha, ni kama ilivyotajwa na An-Nawawiy katika [Al-Majmuu’: 7/899] anasema: “Wanazuoni wenzetu wametoa dalili za Hadithi nyingi sahihi kuwa: Mtume S.A.W., katika Hija ya Kuaga aliwaamuru hawa ambao hawakuwa na Mnyama wa kumchinja waianze ihramu kwa Hija na waitekeleze Umra, na rai hii ni wazi kuhusu kuwa inajuzu kuiahirisha Hija hali ya kuwepo uwezekano. Na wanazuoni wenzetu pia walitoa dalili kuwa: mtu akiiahirisha mwaka hadi mwaka mwingine au zaidi kisha akaitekeleza, hapo ataitekeleza katika wakati wake, na sio kwa wakati mwingine, kwa kauli ya pamoja ya waislamu, na Kadhi Abu At Twayib na wengineo walinukulu kauli ya pamoja katika suala hili, na Kadhi Hussein na wengineo walinukulu makubaliano yao pia, lakini hali ya kuwa kwamba kuiahirisha ni haramu, akiitekeleza itakuwa vigumu kuifanya baada ya wakati wake na kwa wakati wake barabara”. [mwisho]. Na hii ni kauli yenye nguvu zaidi katika suala la wakati huo na wa kuchelewesha.
Na mtu akihofia kuiahirisha Hija kuwa kuna uwezekano wa kuipoteza na hawezi tena kuitekeleza kwa sababu ya maradhi, uzee, kupoteza mali n.k, basi kuna rai mbili za wanazuoni wa madhehebu ya Shafi kuhusu kosa lake la kuiahirisha; rai yenye usahihi zaidi ni kuwa haijuzu. An-Nawawiy katika [Al-Majmuu’: 7/86] anasema; “Yakipatikana masharti ya uwajibu wa Hija inajuzu kuichelewesha kwa mujibu wa matini ya Shafi, na wanazuoni walikubali hivyo isipokuwa Al-Muzaniy, naye anasema: ni kwa wakati huo. Kwa mujibu wa madhehebu: inajuzu kuiahirisha baada ya mwaka wa uwezekano, asipohofia kuipoteza, lakini akihofia hivyo kuna rai mbili mashuhuri katika vitabu vya wanazuoni wa Khurasan, ambazo zimepokelewa na Imamul Haramain, Al-Baghawiy, Al-Mutawaliy, Mtungaji wa Al-Uddah, na wengineo. Na Ar-Rafi’iy anasema: "Rai sahihi zaidi); ni kwamba haijuzu; kwa sababu wajibu mpana haujuzu kuuahirisha, isipokuwa kwa kuwepo sharti la dhana yenye nguvu kuwa ataishi mpaka autekeleze, na hili halikuwepo katika suala hili. Na (rai ya pili); ni kuwa inajuzu; kwa sababu msingi wa kuitekeleza Hija ni kwa kuchelewesha, na haubadilishwi kutokana na jambo la kukisia, na Al-Mutawalli anasema: Rai hizi mbili zinaambatana na anayehofia kuwa mali yake iatapotea, na Je, ana haki ya kuiahirisha Hija au la?”. [Mwisho].
Na hukumu hii akihofia uwezekano wa kuipoteza, lakini akawa na dhana yenye nguvu kuwa anaipoteza au anakufa au anaupoteza uwezekano kabla ya kuweza tena kuitekeleza, hapo kuiahirisha kunakatazwa; kwa sababu hakuna uhalali wa kuiahirisha wala kuipoteza.
Ash-Shirbiiniy Al-Khatwib katika kitabu cha: [Mughniy Al-Muhtaj: 2/207, Ch. Ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah] anasema: “Inajuzu kuiahirisha kwa sharti la kuazimia kuitekeleza katika siku zijazo, kama ilivyokwisha bainishwa katika Sala, na haishughulikiwi kwa nadhiri, kadha, au kuhofia kuipoteza. Na mwenye kuwajibika na Hija au Umra akihofia kuipoteza, basi anazuiwa yeye kuziahirisha, kwa sababu wajibu mpana haijuzu kuuahirisha, isipokuwa kwa kuwepo sharti la dhana yenye nguvu kuwa ataishi mpaka autekeleze wajibu huo”. [Mwisho]. Kwa hiyo, baba huyu mwenye uwezo wa kuitekeleza Hija akiwa na dhana yenye nguvu kuwa: akitumia mali yake katika kumuozesha mtoto wake hataweza tena kuitekeleza Hija, basi analazimika kuitumia katika Hija, na inaharamishwa kuitumia mali hiyo katika mambo mengine ambayo sio miongoni mwa dharura au mahitaji yanayofanana na dharura aliyonayo.
Miongoni mwa kauli inayohusu madhehebu ya Hanbal peke yake mbali na madhehebu mengine: kauli ya kuwa kuna wajibu wa kumkinga mtoto na maasi akiwa na haja ya ndoa, sharti la kuwa baba analazimika kwa matumizi ya fedha ya mwanawe. Al-Mardawiy katika kitabu cha: [Al-Insaaf; 9/404, Ch.ya Dar Ihiyaa At-Turaath Al-Arabiy] anasema: “Mtu analazimika kuwakinga na maasi wale anaowalea, kama vile: wazazi, babu, watoto na wajukuu, na wengineo, miongoni mwa anaolazimika kwa matumizi yao, na hii ni kauli sahihi ya madhehebu, miongoni mwa masuala pekee yanayogawika nayo”. [Mwisho].
Katika kumlazimu mtoto kumuozesha mama yake, Al-Bahutiy mfuasi wa madhehebu ya Hanbal katika kitabu cha: [Kashful- Kinaa’: 5/486, Ch. Ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah] anasema: “(Mtoto analazimika kumkinga mama yake na maasi, sawa sawa na anavyolazimika kumkinga baba yake. Kama mama akitaka hivyo, na anapoposwa na mtu anayemfaa), na Al-Kadhi anasema: ikiwa kauli hii ni sahihi, basi baba atapewa kipaumbele zaidi, kwa sababu haifikiriwi; kwani kumkinga mama ni kwa kumuozesha tu na matumizi yake yote yanamuhusu mume wake. Na katika kitabu cha: [Al-Furuu’] anasema: Inaelekewa kuwa baba analazimika kwa matumizi ya mwanawe ikiwemo uzito wa kumuozesha kama yeye hatafanya hivyo, na hii ni dhahiri kwa kauli ya kwanza”. [Mwisho].
Na inafahamika kuwa kama kuna ugumu wa kumuozesha mtoto anayechuma mali isiyomtosha kwa mahitaji yake ya ndoa, na kumkinga bila ya gharama zaidi kuliko anayeweza kuchuma mali yake inayomtosha, basi baba analazimika kwa matumizi ya mtoto huyo na kumuozesha.
Na iwapo baba atalazimika kwa matumizi ya kumuozesha mwanae ambapo hawezi kugharamia matumizi hayo pamoja na kuifanya Hija kwa wakati mmoja, hapo gharama za kumuozesha mtoto pamoja na Hija vitapewa kipaumbele, hali ya kuogopa kuwa mtoto atapata taabu; kwa sababu ya haja yake ya kufanya Hija ambayo ni sawa na haja yake ya kuoa, ambayo ni kipaumbele katika hali hii na Hija. Na baadhi ya wafuasi wa madhehebu ya Hanbal waliieleza taabu kuwa taabu na ugumu wa ukapera, na haja ya starehe, au utumishi kutokana na uzee au maradhi au nyinginezo; lakini Al-mardawiy anasema kuwa: rai sahihi ya madhehebu yao ni kuieleza kwa kuogopa kuifanya haramu yaani zinaa; na Al-Mardawiy katika [Al-Insaaf: 8/139-140] anasema: “Az-Zarkashiy anasema: Kadhi Abu Ya’laa, Abul Hussein, Ibn A’aqiil, Ash-Shiraziy, na Abu Muhammad waliieleza taabu na ugumu kuwa: ni zinaa. Vile vile mtungaji wa Al-Mustawi’ib. Aliieleza hivyo hivyo katika At-Targhiib na Al-Bulghah; akasema: akiweza kusubiri lakini subira hiyo ikapelekea maradhi, basi inajuzu kumwoa mjakazi. Na Al-majd katika Al-Muharar, Mtungaji wa vitabu vya: [Ar-Ria’ayatain, Al-Hawiy As-Saghiir, Al-Wajiiz, Al-Munawar, Tadhkirat Ibn Abduus,] na wengineo waliieleza kuwa: taabu na ugumu wa ukapera, ima kwa haja ya starehe, au kwa kuhitaji usaidizi wa mke kutokana na uzee au maradhi au sababu nyinginezo. Na wakasema: iliandikwa hivyo hivyo. Na hiyo ilitolewa katika kitabu cha: [Al-Furuu’] Na akasema mwandishi: baaadhi ya wanazuoni hawakutaja utumishi” [Mwisho]
Al-Mardawiy katika kitabu cha: [Al-Inswaf: 8/9] anasema: “Anayehofia taabu na ugumu, basi ndoa ni wajibu kwake, na hii ni kauli moja tu, lakini Ibn A’qiil alitaja mapokezi kuwa: si wajibu. Na maneno yake yanaambatana na kuzihesabu njia. Na Az-Zarkashiy anasema: huenda yeye alikusudia kwa kauli yake (kuhofia taabu): kuyahofia maradhi na shida, na si kuihofia zinaa, kwa sababu (taabu) inaweza kuelezwa kwa maana hizi zote.
Maangalizo: kwanza: taabu hapa ni zinaa kwa rai sahihi, na inasemekana ni kuangamia kwa zinaa, kama ilivyotajwa katika Al-Mustawi’ib. Pili: muradi wake kwa kauli ya (isipokuwa akihofia kukifanya kilichokatazwa), akijua kufanya hivyo kwa yakini au dhania, kama walivyosema wanazuoni wenzetu. Katika Al-Furuu’ anasema: inaelekewa hivyo akijua kuifanya tu. Tatu: sehemu hizi tatu ndizo njia sahihi zaidi; nayo ni njia ya mtungaji na mwenye maelezo, na wengineo. Na Az-Zarkashiy anasema: nayo ni njia mashuhuri”. [Mwisho]
Anasema pia katika marejeo yaliyotangulia [3/404]: “Akiopgopa taabu na ugumu yule anayeweza kuitekeleza Hija, aitangulize ndoa kwanza, kwa rai sahihi ya madhehebu. Nayo imeandikwa hivyo na wengi wa wanzuoni, na wengi wao pia waliitia nguvu kutokana na uwajibu wake” [Mwisho].
Na Ibn Qudamah katika [Al-Mughniy: 3/217, Ch. Ya Maktabat Al-Qahirah] anasema: “Akihitaji ndoa, na akahofia uzito na ugumu aitangulize ndoa kwanza, kwa sababu ni wajibu kwake, ambapo hawezi kuiacha, kwa hiyo ni kama matumizi yake, lakini asipohofia basi aitangulize Hija; kwa sababu ndoa ni mchango na haitangulizwi kwa Hija ya wajibu”. [Mwisho]
Kwa hiyo na kwa kauli ya baadhi ya wafuasi wa madhehebu ya Hanbal, nao walioeleza uzito na ugumu kuwa taabu ya ukapera ni kutanguliza kumuozesha mtoto badala ya Hija na kumkinga na maasi, hali ya kuwa mzazi ndiye mwenye jukumu la matumizi yake.
Wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy walizidisha sharti la ziada katika masharti ya Hija, nalo ni sharti la (wakati). Na maana yake ni kuwa masharti yote ya Hija yapatikane katika wakati wa kwenda watu wa mji wa mwenye kukalifishwa kwa Hija, kwani akimaliza kutekeleza masharti yote ya kuitekeleza Hija bila ya kufikia wakati wa kwenda, basi jukumu lake halitaendelea kuwepo, kwa hiyo Hija haiwajibiki kwake; vile vile haiwajibiki kwake kungoja kwa ajili ya kutimiza masharti ya uwajibu wa hija, hivyo ana hiari ya kutumia fedha kwa ajili ya kununua anavyovitaka, madam tu hiyo ni kabla ya kuja wakati wa kwenda Hija. Na katika hali hii inajuzu kwake kuitumia fedha katika kumuozesha mtoto wake kabla ya kufikia wakati huo; na mfano ni mtu anayemiliki kiasi cha mali ya uwajibu wa kutoa zaka lakini mwaka kamili haujapita bado, basi ana hiari kuitumia fedha hiyo jinsi anavyopenda au kuiwekea akiba ili atoe zaka yake.
Katika [Hashiyat Ibn Abidiin Ala Ad-durr Al-Mukhtar: 2/458, Ch. Ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah]: “Masharti ya uwajibu; yakipatikana yote Hija itawajibika, na pasipo nayo hakuna, ni masharti saba: Uislamu, kufahamu uwajibu kwa aliyekuwa ndani ya nyumba ya uadui, kubaleghe, uhuru, uwezekano, na wakati: yaani uwezekano katika muda wa miezi ya kuitekeleza Hija au katika wakati wa kwenda watu wa mji wake, kama itakavyokuja”. [Mwisho]
Ibn Abidiin katika kitabu cha: [Al-Hashiyah: 2/462] anasema: “Nilivyoiona katika Al-Khulasah ni kuwa: mtu huyo hakuwa na makazi na mengineyo, lakini ana mali inayomwezesha kuhiji, na inatosha kuajiri makazi, mtumishi, na vyakula, basi Hija inamlazimu, na kama akiitumia kinyume na hivyo basi atakuwa na dhambi. [Mwisho]
Lakini hukumu hii inaambatana na wakati wa watu wa mji wake kwenda kuhiji, kama ilivyoelezwa katika kitabu cha: [Al-Lubab] Ama kabla ya hayo, ana hiari ya kununua anavyovitaka; kwa sababu ni kabla ya uwajibu”. [Mwisho]
Al-Haskafiy katika kitabu cha: [Ad-Dur Al-Mukhtar; 2/461, na Hashiyat Ibn Abidiin, Ch. Ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah] anasema: “Baba akimpa mwanae zawadi ya mali asiyoitekelezea Hija, haiwajibiki kuichukua; kwa sababu mashrti ya uwajibu hayawajibiki kuyapata, na hii ni miongoni mwake, kwa makubaliano ya wanazuoni. Na katika Al-Ashbah: mtu ana elfu, lakini akahofia uakapera, ikiwa ni kabla ya kwenda watu wa mji wake kuhiji basi anaweza kuoa, ama kwa wakati wake basi Hija inamlazimu”. [Mwisho]
Mtaalamu Al-Kasaniy mfuasi wa madhehebu ya Hanafiy katika kitabu cha: [Badaiu’ As-Sanai’: 2/125, Ch. Ya dar Al-Kutub Al-Ilmiyah] anasema: “Tuliyoyataja miongoni mwa masharti ya uwajibu Hija ni kama vile: vyakula, kipando na mengineyo yazingatiwe wakati wa kwenda watu wa mji wake kuhiji, hata akimiliki vyakula na kipando mwanzoni mwa mwaka, kabla ya miezi ya Hija, na kabla watu wa mji wake hawajaanza kwenda Makkah; basi ana hiari ya kuitumia mali apendavyo; kwa sababu halazimiki kuwa tayari kwenda Hija kabla ya kwenda watu wa mji wake, kwani Hija haimlazimikii kabla ya hapo, na huyo asiyelazimikiwa na Hija halazimikiwi pia awe tayari kwa Hija, kwa hiyo ana hiari ya kuitumia mali yake kama apendavyo.
Na kama akitumia mali kisha watu wa mji wake wakaenda Hija, basi Hija hailazimiki kwake; lakini wakati ukifika na mali ipo mikononi mwake, basi hawezi kuitumia kwa kitu kingine isipokuwa Hija, kwa kauli ya anayeona uwepo wa uwajibu wa Hija katika wakati huo; kwa sababu wakati wa kwenda watu wa mji wake ukifika, basi Hija inamlazimu kwa kuwepo uwezekano, na analazimika kuwa tayari kwa safari ya kwenda Hija, hivyo haijuzu kwake kuitumia mali kwa kitu kingine; mfano wake; msafiri akiwa na maji ya kusafisha, kisha wakati wa Swala umefika, haijuzu kwake kuyatumia maji hayo kwa kitu kingine isipokuwa kwa kutawadhia, kwa hiyo akiyatumia mali hayo katika kitu kingine isipokuwa Hija atapata dhambi na Hija inamlazimu”. [Mwisho].
Kwa mujibu wa hayo na kwa uhalisia wa swali: inabainika kuwa ikiwa mwaka huu ni wa kwanza ambao unaweza kuitekeleza Hija kwa mara ya kwanza kutokana na kumiliki mali; basi inajuzu kuitumia mali katika kumuozesha mtoto wako, kwa mujibu wa madhehebu ya wafuasi wa Hanafi na Shafi, kama wakati ambao watu wa mji unamoishi kwenda Hija haujafika; lakini wakati ukifika basi Hija ni jukumu linaloendelea kuwepo na ni haramu kwako kuipoteza hija hiyo kwa kuitumia mali kwa kitu kingine kisichoambatana na dharura kwako au kwa wale unaolazimika kuwahudumia isipokuwa kama huna dhana ya nguvu kwamba utakuwa na uwezo tena wa kuitekeleza Hija, na ikiwa kuna dhana ya nguvu ya kupata uwezo, basi inajuzu kuitumia mali katika kumuozesha mtoto wako. Katika hali ya kuwa matumizi ya mtoto yanakulazimu, ambapo kuna shida ya kumuozesha bila ya msaada wako wa kifedha, na wakati wa kuhofia uzito na ugumu kwake kuyafanya maasi, hapo inajuzu kuitanguliza ndoa kwanza na kuichelewesha Hija, kwa mujibu wa madhdhebu ya Hanbal, na kama hakuna hofu yoyote ya uzito na ugumu kwa mtoto huyo, basi ndoa hapo ni Sunna na Hija ni fardhi, kwa hiyo Hija itangulizwe.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.