Ukiritimba wa Wakala Kwenye Mikatab...

Egypt's Dar Al-Ifta

Ukiritimba wa Wakala Kwenye Mikataba ya Uletaji Bidhaa

Question

Je, inafaa kwa wakala kulazimisha kampuni inayoleta bidhaa kumwuzia yeye tu, na mteja kutonunua isipokuwa kwake? Je, hii si katika ukiritimba ulioharamishwa? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Uwakala una maana ya kuhifadhi, na ni neno lenye maana pia ya uwakilishi, kwa maana ya usimamizi wa uwakilishi wa kitu kwa mtu mwengine, na imeitwa wakala kwa sababu ya aliyemwakilisha amempa ruhusa ya kusimamia jambo lake kwa amri yake, hivyo anakuwa ni amewakilishiwa jambo [Angalia kamusi ya lisan Al-Arab, 11/736, chapa ya Dar Sadir].
Kwa upande wa Sharia: Ni kusimamia mtu mwengine nafasi ya mwenyewe katika uendeshaji na utumiaji unaofaa wenye kufahamika.[Kitabu Hashiyat Ibn Abideen, 4/400, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath].
Kusudio la kampuni: Ni wakala kuuza bidhaa ya kampuni ndani ya nchi fulani kwa bei anayolipa wakala ili apate kuiuza hiyo bidhaa kwa bei ya juu ndani ya hiyo nchi, na kuchukua ongezeko la bei pasi na kubadilisha bidhaa ya kampuni au kuiga, ikiwa wakala atakiuka hayo mtakaba unavunjwa kwa kulipa gharama ambayo pande mbili zimekubaliana. Hivyo uwakala kwa msingi huu ni makubaliano ya uwakala anayolazimika wakala kuyafuata na vitu ambavyo ni haki ya kampuni au shirika.
Au kwa maana nyengine makusudio ya wakala: Ni kwa mwenye kununua bidhaa kutoka kwenye kampuni ili apate kuuza ndani ya nchi fulani na kampuni kulazimika kutomwuzia mtu mwengine ndani ya hiyo nchi, pia kampuni itamlazimisha kutobadilishwa bidhaa yake kwa kuharibu au kuiga ili isije kuharibu jina la kampuni mama. Hivyo kwa msingi huu ni makubaliano ya uuzaji na kampuni mama kwa sharti zilizokubalika na pande mbili ambazo watawajibika nazo pande zote mbili.
Katika sura ya kwanza kampuni inazingatia kuwa ni makubaliano ya uwakala, na uwakala unafaa kisharia kwa mujibu wa Qurani na Sunna pamoja na makubalinao ya wanachuoni. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu aende mjini, akatazame chakula kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote} [AL KAHF, 19].
Hiyo ilikuwa ni uwakala. Mwenyezi Mungu Amehadithia kisa cha watu wa pangoni, katika Sunna ni Hadithi inayotokana na Bukhari: Kutoka kwa Urwa Ibn Abi Al-Jaad Al-Bariqiy R.A., amesema: Hakika Mtume S.A.W.. alimpa dinari moja ili anunue mbuzi, yeye akanunua mbuzi wawili, akamwuza mmoja kwa dinari moja, akarudi akiwa na danari moja pamoja na mbuzi, Mtume akamwombea dua ya baraka katika uuzaji wake, ilikuwa hata kama angenunua udongo basi angepata faida. Hadithi hii inaonesha uhalali wa uwakala katika kuuza na kununua.
Na Hadithi nyengine inayotokana na Abu Dawud kutoka kwa Jabir Ibn Abdillah R.A. amesema: Nilitaka kutoka kuelekea Khaibar, nikapitia kwa Mtume S.A.W. na kumsalimia, nikamwambia mimi ninataka kwenda Khaibar, Mtume S.A.W. akasema: “Pindi ukipita kwa wakala wangu, basi chukua kwake pishi kumi na tano za tende, ikiwa atakutaka ushahidi basi weka mkono wako sehemu ya juu ya kifua chake”. Hadithi hii inaonesha pia uhalali wa uwakala. Na wanachuoni wamekubaliana kufaa kwa uwakala na uhalali wake.
Ama wakala kununua uwakala ni kununua mali yenye thamani, nayo ni alama (nembo) ya biashara ya kutangazwa katika masoko, hivyo kununua alama (nembo) hii inafaa kisharia, ama sharti la makubaliano ya uwakala na kampuni ni kutompa uwakala mtu mwengine ndani ya hiyo nchi, na kampuni inaweka sharti la kutobadilishwa bidhaa yake kwa kuharibiwa au kuiga, masharti haya ni katika masharti yanayofaa kisharia katika makubaliano ya uwakala ambayo hayapingani na muktadha wa makubaliano.
Amesema Al-Kasaniy mmoja wa wafuasi wa Abu Hanifa: “Uwakala wa kuuza ukiwa una sharti, basi sharti hizo zinachungwa kwa makubaliano ya wanachuoni, ikiwa atapinga sharti zake, basi hazitekelezwi kwa wakala lakini zitafanya kazi kwa kupitisha kwake, isipokuwa ikiwa tofauti yake ni katika uzuri na manufaa kwa sababu wakala anasimamia kwa mamlaka aliyopewa na kunufaika na mwenye kutoa uwakala, na kusimamia kiasi cha mamlaka aliyopewa, ikiwa tofauti ni yenye manufaa, basi sharti zitatekelezwa, kwa sababu ikiwa tofauti ni sura ya nje lakini yenyewe ni yenye kukubaliana kwenye maana, kwa sababu kupewa amri kwake ni dalili na anakuwa ni mwenye kusimamia kwa mamlaka ya mwenye kutoa amri ya uwakala” ]Kitabu Badaii Al-Sanaii cha Al-Kasaniy, 6/26, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Na sharti la kutopewa uwakala mtu mwengine ndani ya nchi fulani si miongoni mwa sura za ukiritimba ulio haramu, kwa sababu ukiritimba wa soko ni kusubiri kupanda kwa bei na kuwabana watu pamoja na kuwasababishia madhara, lakini ukiritimba huu wa uwakala si wa sura hiyo.
Ama sura ya pili, makubaliano haya ni makubaliano ya uuzaji na sharti za makubaliano haya zinafaa madamu tu sharti ni sahihi hazipingani na muktadha wa makubaliano wala kupingana na Sharia, na kwa hivyo basi sura hii inafaa kisharia, Anasema Mwenyezi Mungu: {Enyi mlio amini! Timizeni ahadi [AL MAIDAH, 01]. Na kauli yake Mola Mtukufu: {Enyi mlioamini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe} [AN NISAA, 29].
Na Hadithi inayotokana na Tirmidhiy kutoka kwa Amr Ibn Auf Al-Muziniy amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.: “Waislamu wana sharti zao, isipokuwa sharti iliyoharamisha halali au kuhalalisha haramu”.
Na imepokelewa na Bukhari kutoka kwa Bi. Aisha R.A. amesema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.: “Jambo lenye sharti isiyokuwepo ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi sharti hiyo ni batili”, kwa maana katika yale aliyoyaandika Mwenyezi Mungu na kuyalazimisha ndani ya Sharia zake ambazo ameziweka.
Ama Hadithi ya At-Twabraniy kutoka kwa Amr Ibn Shuaib kutoka kwa baba yake pia kutoka kwa babu yake kutoka kwa Mtume S.A.W.: “Kuwa amekataza kuuza na kuweka sharti” inakusudia sharti hapa ni lile linalopingana na mwenendo wa makubaliano au zile shuruti zisizokubalika ambazo hakuna mwenye haki hata mmoja kati ya pande mbili za makubaliano kuziweka katika makubaliano yao kwa kuwafanya zinakwenda kinyume na makusudio, au kwenda kinyume na kanuni halali, au kugongana makusudio katika makusudio ya Sharia, ama shuruti zengine ni halali kwa pande mbili zenye kufanya makubaliano, wanapeana hiyari vile watakavyo ili kuwajibika nazo katika makubaliano yao.
Amesema Al-Haskafiy katika kitabu cha: [Ad-Durr Al-Mukhtar]: “Na katika mauzo yasiyofaa ni uuzaji wa sharti isiyokubaliana na mkataba wala kwenda sawa, na ndani yake kuna manufaa kwa upande mmoja, na wala masharti hayo si yenye kufahamika wala hayajapokelewa ndani ya Sharia juu kufaa kwake, ama lau yamekuwa ni yenye kufahamika kama vile kuuza kiatu pamoja na sharti ya kuwepo mwenzake, au imepokelewa na Sharia kama vile hiyari ya sharti hakuna uharibifu, kama sharti ya muuzaji kukikata na kukishona au kikutumia kwa muda wa mwezi” (Kitabu cha: Ad-Durr Al-Mukhtar, 4/121, chapa ya Ihayaa At-Turath].
Amesema Al-Kharshiy mfusi wa Imamu Malik: “Miongoni mwa mauzo mabaya ni kuuza na kuweka sharti, kwani “Mtume S.A.W. amekataza kuuza na kuweka sharti”, watu wa madhehebu wamechukulia katazo la sharti linalopingana, au kuharibu thamani. [Sharhu ya Mukhtasar Khalil ya Al-Kharshiy, 5/80, chapa ya Dar Sadir].
Na sharti ya kutouza kwa mtu mwengine ndani ya nchi si katika mlango wa ukiritimba ulio haramu, kwa sababu ukiritimba ulio haramu ni kuifungia bidhaa na kuchunga soko ikiwa lengo ni kusubiri kupanda kwa bei ili kuwakamua watu na kupandishi bei lengo ndani ya nchi kusiwe na mwengine anayeuza bidhaa hii kwa sifa zake zote na aina zake isipokuwa yeye tu, ama kwa upande wa hii alama ya biashara yenyewe ni aina katika aina za bidhaa, yeye anachukua uwakala wa kuuza chombo fulani cha aina fulani, anakusudia kukinunua kutokana na ubora na jina lililobora na zuri kuliko alama zengine zilizosalia za biashara ili apate faida zaidi, hii ni halali na inazingatiwa ni katika juhudi za kutafuta kipato halali, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri} [AL BAQARAH, 168].
Na anasema Mtume S.A.W., katika Hadithi iliyopokelewa na Imamu Muslim kutoka kwa Abi Huraira amesema: Amesema Mtume S.A.W.: “Enyi watu, Hakika Mwenyezi Mungu ni nzuri na hakubali isipokuwa kilicho kizuri, na Mwenyezi Mungu amewaamrisha Waumini yale aliyo waamuru Mitume. Mungu Mtukufu anasema: {Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda} [AL MUMINUUN, 51]. Mola Akasema tena: {Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyokuruzukuni} [AL-BAQARAH, 172].
Na mwenye kutaka kununua kitu, basi anapaswa kununua aina nyengine, na kwa sura hii hufanya kazi pia kwenye bidhaa zengine.
Ikiwa makubalino haya yatafanyika katika bidhaa muhimu na kufanyka ukiritimba kwenye aina zake zote za bidhaa hizo, basi katika hali hii ni lazima kiongozi kuingilia kati ili kuepusha kukamuliwa watu, ima atalazimisha kuuzwa kwa bei ya kawaida ya sokoni au yeye kiongozi aweke bei.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia: Makubaliano haya hayazingatiwi kuwa ni ukiritimba ulio haramu, nayo ni makubaliano yanayofaa na hakuna ubaya wowote ndani yake, isipokuwa ikiwa utafanyika ukiritimba huu kwenye bidhaa muhimu, au kuwasababishia watu shida na tabu badala ya kuwepo pande nyingi za usambazaji na uuzaji.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas