Kuziondosha Nywele Kikamilifu.
Question
Je, inajuzu kuziondosha nywele za kinenani na za kwapani kikamilifu kwa kutumia dawa za kisasa?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba zake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu na kumpendelea zaidi kuliko viumbe vyote. Na Mwenyezi Mungu anasema: {Bila shaka Tumemuumba mwanadamu kwa umbo lililo bora kabisa}. [AT TEYN: 4], na amemuhalalishia mapambo kwa vigezo vyake vya Sheria. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Sema: “Ni nani aliyeharamisha mapambo ya Mwenyezi Mungu ambayo amewatolea waja wake. Na (nani aliyeharamisha) vitu vizuri katika vyakula?” Sema; “Vitu hivyo vimewahalalikia Waislamu (hapa) katika maisha ya dunia; (na) vitakuwa vyao peke yao siku ya Kiyama.” Namna hivi tunazieleza Aya kwa watu wajuao}. [AL AARAF: 32].
Na katika Sunna ya Mtume S.A.W., iliyotwaharika tunaona hivyo kwa uwazi jinsi Mtume S.A.W., anavyoyapenda kujipamba. Na alipoulizwa na mtu kuwa: “Hakika mtu huyo anapenda mavazi yake yawe mazuri, na viatu vyake viwe vizuri, akasema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Mzuri na anapenda uzuri”. [Ameipokea Imamu Muslim]
Na kama alivyobainisha Mtume S.A.W., kuwa katika maumbile ambayo Mwenyezi Mungu aliwaumbia watu, na Manabii A.S., walikuwa nayo ni mambo ambayo watu wanapaswa kuyachukua. Na kutoka kwa Abu Huraira, kutoka kwa Mtume S.A.W., amesema: “Mambo matano ni katika Maumbile: kutahiriwa, kunyoa nywele za kinena, kukata kucha, kunyonyoa nywele za kwapani, na kukata masharubu”. [Muttafaq], na Imamu Bukhari ameitoa kama ilivyo hivyo, kutoka kwa Ibn Omar.
Na Imamu Muslim ameitoa, kutoka kwa Aisha R.A., amesema: Mtume S.A.W., amesema: “Mambo kumi ni katika Maumbile: Kukata masharubu, kufuga ndevu, kupiga mswaki, kuvuta maji puani, kukata kucha, kuosha maungio ya vidole, kunyonyoa nywele za kwapani, kunyoa nywele za kinena, na kustanji kwa maji”. Na Zakariya alisema: Musa’ab alisema: jambo la kumi nimelisahau, nadhani kuwa ni kusukutua.
Al-Khattabiy anasema: Kauli yake S.A.W., (Mambo kiumi ni katika Umbile), wanachuoni wengi walifafanua Umbile katika Hadithi hii kuwa ni Sunna, na maana yake ni: Mambo haya ni katika Sunna ya Manabii, ambao tumeamrishwa kuwafuata wao, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi fuata uongozi wao}. [AL ANA'AM: 90]. Na mtu wa kwanza aliyeamriwa kwa mambo haya ni Ibrahimu A.S., na hii kwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na (kumbukeni khabari hii): Mola wake alipomfanyia mtihani (Nabii) Ibrahim kwa amri nyingine; naye akazitimiza}. [AL BAQARAH: 124].
Na Ibn Abbas amesema: “Alimwamuru amri kumi, kisha akazihesabu, na Ibrahimu alipozitimiza, Mwenyezi Mungu {Akamwambia: “Hakika mimi nitakufanya kiongozi wa watu (wote)”}, yaani watakufuata katika Sunna yako, na umma huu uliamriwa kumfuata ilivyo, kama ilivyobanisha kauli yake mtukufu: {Kisha tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibrahimu (aliyekuwa) mtii kamili}. [AN NAHAL: 123], na inasemekana kuwa amri hizi zilikuwa faradhi kwa Ibrahimu, lakini ni Sunna kwetu”. [Maa’alim As-Sunan: 1/31, Ch. ya Al-Matbaa’ah Al-Ilimiyah, Halab]
Na bila shaka kuzitekeleza Sunna hizi kuna uzuri na kujitenga mbali na mambo yasiyo ya kibinadamu, na kuna athari njema katika dini na dunia. Imamu Al-Qurtubiy katika kitabu cha: [Al-Mufhim: 1/511-512, Ch. ya Dar Ibn Kathiir, na Dar Al-kalim At-Taiyb] anasema: “mambo haya kwa ujumla yanapelekea kuhifadhi sura nzuri na usafi, na hiya yanasaidia kuwepo ukamilifu wa uumbaji ambao Mwenyezi Mungu alimuumbia mwanadamu, na kwa kuongeza kuwa kutoyaondosha mambo haya kunapelekea uharibifu wa umbo la mwanadamu na kumfanyia ubaya, hata akawa mchafu na mwenye kuchukiwa na watu, na hali hii inamfanya awe mbali na uumbaji wa kwanza, na kwa hiyo mambo haya yameitwa Umbile kutokana na maana hii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi”. [Mwisho]
Al-Manawiy anasema; “Tanbihi: Yanayoambatana na mambo haya ni masilahi ya dini na dunia ambayo yanajulikana kwa uhalisi, miongoni mwake: Kuboresha umbo, kusafisha mwili kwa ujumla, kutekeleza usafi, kufanya hisani kwa wengine wasije wakasumbuliwa kwa harufu mbaya, kutofautiana na makafiri kama vile Majusi, Mayahudi, Manasara, kufuata amri ya Mwenye Sharia, na kuhifadhi aliyoyaashiria Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kauli yake: {kisha sura zenu (hizo) akazifanya nzuri}, ni kama kwamba yeye amesema: Nilizifanya sura zenu nzuri, basi msiziharibu kwa kuzifanya vibaya. Na kuzihifadhi sura hizi ndio kuhifadhi ungwana na upendo; kwa sababu mtu akiwa na muonekano mzuri basi watu watampenda, kwa hiyo kauli yake itakubalika, na maoni yake yatasifika, na kinyume kwa kinyume” [Fadhul Qadiir: 4/316, Ch. ya Al-Maktabah At-Tijariyah].
Na hapa inabainika kuwa: Alivyouliza mwenye swali, nayo ni kuziondosha nywele za kinena na za kwapani ni jambo linalotakiwa kisheria, na kuhusu mabaki ya swali nayo ni: Je, unaweza kuziondosha nywele kwa kutumia dawa za kisasa? Jibu ni kujuzu, na ilivyopokelewa katika Hadithi kuhusu kuainisha njia ya kuziondosha nywele si njia pekee ya kufanya hivyo, bali ni njia iliyokuwa ukitumiwa kwa jumla, au ni mfano mmoja wa kufanya hivyo, au kuwa mfano huu ni bora zaidi kuliko mwingine, na sio mwingine haujuzu. Kwa hiyo walitoa mfano wa kutumia (Nurah) yaani unga wa madawa, ambapo tunaona katika baadhi ya mapokezi ya Hadithi kuhusu tendo la Mtume S.A.W., hapo imepokelewa kutoka kwa Umm Salamah kuwa: “Mtume S.A.W., alikuwa akitaka kuziondosha nywele zake, alianza kuiweka (Nurah) katika tupu zake, kisha mwili wote”. [Ibn Majah ameipokea]
Na vile vile imepokelewa kutoka kwa baadhi ya Manabii; kutoka kwa Abu Musa, kutoka kwa Mtume S.A.W., alisema: “Mtu wa kwanza kutengenezewa (Nuurah) maada intengenezwayo kwa chokaa kwa ajili ya kukatia nywele za kwapani, na akaingia kwenye maji ya kuoga yenye maada hiyo, ni Nabii Suleiman Ibn Dawud, na alipoingia katika maji ya kuoga yaliyotiwa maada hiyo na akapata joto na dhiki yake, akasema: Ninaumia! Najikinga na adhabu ya Allah! Ninaumia! Ninaumia!, aliumia sana kabla hajafaidika!”. [At-Twabaraniy ameipokea katika kitabu cha Al-Awsat]
Na katika kitabu cha [Lisaan Al-A’arab: 5/244, Ch. ya Dar Saadir]: “Nurah ni jiwe la chokaa ambalo inatengenezwa kwa ajili ya kuziondosha nywele za kinena”.
Na katika kitabu cha [Al-Misbaah Al-Muniir; 2/629, Ch. ya Al-Maktabah Al-Ilmiyah]: “Nurah ni jiwe la chokaa, pamoja na mada zingine ambazo zinaongezwa, na kutumiwa kwa kuziondosha nywele”.
Na kueleza kwa wanachuoni kuhusu ilivyopokelewa katika Hadithi kuwa ni bora, kwa msingi wa kudhooofisha mizizi ya nywele kulingana na kunyonyoa nywele za kwapani, au kuwa ni nyepesi kwa mtu kama vile kunyoa nywele za kinena, maelezo haya yanatuongoza kwa makusudi katika umuhimu wa swali, nayo ni kuziondosha nywele kikamilifu kunaambatana na yote yaliyotajwa kwa sababu na hekima, ambapo njia hizi zinaondosha mizizi ya nywele pamoja na wepesi katika kuondosha huko.
Ibn Daqiiq Al-I’id katika kitabu cha: [Ihkaam Al-Ahkaam: 1/124-125, Ch. ya Matba’at As-Sunnah Al-Muhammadiyah] anasema: “(Istihdaad) neno limechukuliwa katika (chuma) yaani ala ya chuma inayotumika katika kuziondosha nywele za kinena, na inajuzu kuziondosha kwa njia nyingine kama vile kunyonyoa au kutumia (Nurah) ambapo maada hiyo huyafikia makusudio, lakini Sunna na ubora zaidi ni kama ilivyotaja Hadithi… na kunyonyoa nywele za kwapani ni kuziondosha nywele zake kwa njia ya kunyonyoa, au kwa njia nyingine, lakini kutumia njia iliyotajwa katika Sunna ni bora zaidi.
Tamko la Hadithi limetofautisha kati ya kuziondosha nywele za kinena na nywele za kwapani, kuhusu ya kwanza ilitajwa (Istihdaad), na ya pili kunyonyoa, na hii inaonesha kuangalia njia hizi maalumu kwa kila moja, na sababu ya hii kuwa kuzinyoa nywele huimarisha mizizi yake, na kuzifanya ziwe na nguvu, na kwa sababu hii madaktari wanaagiza kuzinyoa nywele mara nyingi, hali ya kuzitaka ziwe na nguvu, lakini nywele za kwapani zikiwa na nguvu na kuwa nyingi zitanuka na kutoa harufu mbaya kwa walio karibu, kwa hivyo inafaa kuziondosha kwa njia ya kunyonyoa ambayo inadhoofisha mizizi yake, pamoja na kupunguza harufu mbaya, kinyume cha nywele za kinena: ambapo haidhihiriki harufu mbaya ukilinganisha na za kwapani, kwa hiyo sababu ya kunyonyoa haipatikani, basi inafaa kuzinyoa (Istihdaad); na kwa sababu njia hii ni nyepesi na rahisi bila ya upinzani”. [Mwisho]
Al-A’ainiy katika [Sharh Abu Dawud: 1/165-166, Ch. ya Maktabat Ar-Rushd, Riyadh] anasema: “Kauli yake: (kunyonyoa kwapani) ni afadhali kuzinyonyoa kwa aliyeweza kulifanya, au kuzinyoa au kutumia (Nurah). Na Yunus Ibn Abdel Aa’laa anasema: Niliingia kwa Shafi wakati wa kinyozi anaponyoa kwapani yake, na Shafiy akasema: nilijua Sunna ni kuzinyonyoa, lakini siwezi kustahimili maumivu… na kauli yake (kunyoa nywele za kinena) nazo ni nywele zilizo juu ya uume wa mwanamume na pembezoni mwake, na pia nywele zilizo pembezoni mwa utupu wa mwanamke.
Na imenukuliwa na Abul A’abbas Ibn Suraij kuwa: Ni nywele zilizopo pembezoni mwa utupu, na inafahamika kuwa: Inatakiwa kuzinyoa nywele zote za mbele na nyuma na zilizo pembezoni, na ni bora zaidi kuzinyoa, na inajuzu kuzikata, kuzinyonyoa, na kutumia (Nurah). [Mwisho]
Al-Manawiy katika kitabu cha: [At-Taysiir Bisharh Al-Jamii’ As-Saghiir: 1/346, Ch. ya Maktabat Al-Imam Ash-Shafiy, Riyadh] anasema: “(kunyonyoa kwapani) yaani kuziondosha nywele zake kwa kunyonyoa, akiweza kufanya hivyo, na asipoweza kufanya, aziondoshe kwa kunyoa au njia nyingine, na (Istihdaad) yaani kuzinyoa nywele za kinena kwa ala ya chuma, nayo ni wembe, yaani kuziondosha nywele zake kwa chuma au kinginecho, na kuainisha chuma hapa, kwa sababu ni ala ya kuziondosha nywele kwa jumla”. [Mwisho]
Ibn Qudamah katika kitabu cha: [Al-Mughniy: 1/64, Ch. ya Maktabat Al-Qahirah] anasema: “(Istihdaad) yaani kuzinyoa nywele za kinena, nayo inatakiwa; kwa sababu ni miongoni mwa umbile, na kuacha ni vibaya, kwa hiyo inatakiwa kuziondosha, na kwa njia yoyote iwayo ya kuziondosha basi haidhuru, kwa sababu kuziondosha ni makusudio. Imesemwa kwa Abu Abdillahi: Unaonaje kuhusu mtu kuzikata nywele za chini kwa mkasi bila ya kuziondosha zote? akasema: Natarajia kuwa ni inatosheleza Inshaallah. Imesemwa: Ewe Abu Abdillahi, unasema nini kuhusu mtu anayenyonyoa nywele za kinena? Akasema: Je, kuna anayeweza kufanya hivyo?! Na kama akizipaka kwa (Nurah) basi haidhuru, lakini asimwache mwingine kuiona tupu yake, isipokuwa mwenye ruhusa kuiona kama vile mke na mjakazi.
Abul Abbas An-Nasaiy anasema: Nilimtengenezea Abu Abdillahi (Nurah), nikampaka, nilipofikia mahali pa utupu akaipaka yeye mwenyewe. Na Al-Khallal amepokea kwa Isnad yake, kutoka kwa Nafii’ alisema: Nilikuwa nikimpaka Ibn Umar, na kama alipofika kwenye tupu alipaka yeye mwenyewe. Na hivyo hivyo imepokelewa kutoka kwa Mtume S.A.W, Al-Maruudhiy anasema: Abu Abdillahi alikuwa haingii bafu la maji ya maada ya Nurah, na kama alipoihitaji kutumia (Nurah) aliifanya nyumbani, na mara nyingi nilimtengenezea (Nurah) akampaka kwayo, nikanunua glavu kwa ajili yake ili kuitumia wakati wa kuipaka (Nurah).
Na kuzinyoa nywele za kinena ni afadhali, kutokana na mapokezi, na Ibn Umar alisema: Hiki ni miongoni mwa kitu kizuri kilichoanzishwa na watu, yaani (Nurah)”. [Mwisho]
Kuna maoni mazuri yanayothibitisha rai tuliyoielekea, nayo waliyoitaja baadhi ya wanachuoni kuhusu sifa kuu za Mtume S.A.W, kuwa: Kwapani yake hayakuwa na nywele, kwa hiyo tamko la (weupe wa kwapani yake) limepokelewa mara nyingi katika mapokezi. Na inajulikana sana kuwa Yeye S.A.W., ni mkamilifu wa kuumbwa na tabia, na Mwenyezi Mungu hakumuumba isipokuwa katika hali ya ukamilifu wa kibinadamu. Na hii huonesha kuwa kuziondosha nywele kama hizi kwa mwanadamu ni jambo la kisheria kama iwezekanavyo.
As-Sayutiy katika kitabu cha: [Al-Khasais Al-Kubra; 1/107, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah] anasema: “Mlango wa Alama ya Kwapani yake Sharifu S.A.W.; Maimamu Bukhari na Muslim walipokea kutoka Anas alisema: “Nilimwona Mtume S.A.W., akiinua mikono yake miwili wakati wa dua, hata weupe wa kwapani yake ulionekena.
Na Ibn Saad amepokea kutoka kwa Jabir alisema: “Mtume S.A.W., alikuwa akisujudu weupe wa kwapani yake ulionekana”. Hivyo weupe wa kwapani yake S.A.W., umetajwa mara nyingi katika Hadithi za kundi la Masahaba. Na Al-Muhib At-Tabariy anasema: miongoni mwa sifa zake kuu S.A.W., kwapani yake hayalingani na watu wengine, na Al-Qurtwubiy alitaja maneno kama haya, na akaongeza kuwa: Hayana nywele”. [Mwisho]
Wanazuoni walipotaja suala la kazi ya mwenye bafu la maji ya Nurah, naye ni kibarua wa usafishaji na urembo katika bafu la maji ya Nurah, ambapo baadhi ya wanazuoni walitaja kuwa: Inajuzu kwa kibarua huyu kuziondosha nywele za kinena kwa mtu anayesafishwa katika hali ya dharura. Na bila shaka kuwa kufichua tupu mara moja kwa ajili ya kuziondosha nywele kikamilifu, ni bora zaidi kuliko kufichua mbele ya kibarua huyu mara kwa mara, na huenda mtu yeyote akipatwa na maradhi, udhaifu, au uzee na kwa hivyo atahitaji msaada wa mwingine mara nyingi.
Al-Haskafiy anasema: “Kutoka kwa Abu Hanifa: Inajuzu kwa mwenye bafu la maji ya Nurah aione tupu, na dalili yake ni twahara”. [Ad-Durul Mukhtar, na Hashiyat Ibn A’abidiin: 6/382].
Na At-Turiy mfuasi wa madhehebu ya Hanafiy: “Katika kitabu cha At-Tatimah wal Ibanah: Abu Hanifa alikuwa haoni vibaya kuwa mwenye bafu la maji ya Nurah aione tupu ya mwingine.
Na katika kitabu cha Al-Kafiy: … Muhammad Ibn Muqatil anasema: hakuna ubaya kuwa mwenye bafu la maji ya Nurah aiguse tupu ya mwingine kwa mkono wake, wakati wa kuiweka (Nurah), akiinamisha macho yake. Na Mwanazuoni Abul Laith anasema: Hii ni katika hali ya dharura na siyo vinginevyo…”. [Mwisho] [Takmilat Al-Bahr Ar-Raiq, na At-Turiy: 8/219, Ch. ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy].
Na Muhtasari wa maelezo hayo ni kuwa: Hakuna ubaya wowote wa kuziondosha nywele zilizoruhusiwa kisheria kuondoshwa, kwa njia yoyote iliyo halali na isiyo na madhara, hata ikiwa ni kuondosha mara kwa mara, kwa sharti la kuangalia jinsia kwa jinsia, yaani mwanamume na mwanamume, na mwanamke na mwanamke.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.