Mkusanyiko wa Maswali ya Kimatibabu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mkusanyiko wa Maswali ya Kimatibabu.

Question

Mtaalamu mmoja wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi nchini Uingereza anaulizia Masuala yafuatayo:
Suala la Kwanza: Hukumu ya kuharibu mimba katika hali mbili za ubakaji na kuzini na ndugu wa karibu.
Suala la pili: Hukumu ya kutumia mbinu ya mfuko mwingine wa uzazi katika hali ya kuwa mwanamke mwenye mfuko wa uzazi mbadala ambaye hubeba mimba kwa niaba ya mwingine ni mke mwingine wa mume mwenye yai la uzazi lililorutubishwa.
Suala la tatu: Hukumu za Sheria zinazohusiana na upasuaji wa mfuko wa uzazi mbadala iliyotajwa kama ikitokea.
Suala la Nne: Hukumu ya upasuaji wa kuhamisha mfuko wa uzazi.
Suala la Tano: Hukumu ya upasuaji wa kupima jeni ya kiinitete cha mke mzee kabla ya kuingizwa, ili kuepusha kasoro za kiinitete.
Suala la Sita: Hukumu ya upasuaji wa kupima jeni kwa ajili ya kuchagua jinsia ya kiinitete kabla ya kuingizwa, kwa sababu za kijamii.
Suala la Saba: Hukumu ya upasuaji wa kupima jeni ya kiinitete ili kujua kufanana kwake na mtoto mgonjwa ambaye anahitaji kupandikiziwa ute wa mifupa au kiungo cha mwili.
Suala la Nane: Hukumu ya kutumia uhandisi wa jeni kwa madhumuni ya kuboresha tabia ya kiinitete.
Suala la Tisa: Hukumu ya kutumia teknolojia ya seli za shina katika matibabu.
Suala la Kumi: Je! Inawezekana kufanya utafiti na majaribio juu ya tiba ya seli ya shina katika kesi ya kiinitete kilichoondolewa moja kwa moja au kiinitete kisichohitajika katika kesi za kurutubisha kwa matibabu, au viinitete vilivyopachishwa au viinitete vilivyorutubishwa katika maabara?
Suala la Kumi na Mmoja: Hukumu ya kisheria katika upachishaji kwa wanadamu, au kwa madhumuni ya matibabu kama vile upachizaji wa tishu (mkusanyiko wa seli za aina moja zenye shuguli maalumu mwilini) au viungu vya mwili.
 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni zake Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Suala la kwanza: Kuhusu suala la utoaji wa mimba katika kesi ya mwanamke aliyebakwa, imeelezewa kuwa misingi ya kisheria haizuii hili kwa kuwa ujauzito haujakamilika na kufikia siku mia na ishirini; na kuzingatia idhini ya wanavyuoni wa fiqhi kutoka kwa madhehebu ya Hanafiy, Shafiy na wengine kwa hiyo. Kama suala hili likiruhusiwa kwao katika ujauzito uliotokea kwa njia ya kisheria, basi inaruhusiwa kufanyika kupitia ndugu wa karibu na itakuwa bora zaidi, pamoja na kupunguza madhara kwa yule mwanamke aliyebakwa. Lakini ikiwa siku mia na ishirini zimepita tangu mimba kwenye tumbo la mama yake, basi hairuhusiwi kuharibu mimba kwa hali yoyote;
Vivyo hivyo katika hukumu hii pia kesi ya kujamiiana kwa ndugu wa karibu; kufuatana na maoni yaliyotajwa hapo juu, na kuzuia madhara yaliyo makubwa zaidi.
Suala la pili: kutumia mfuko wa uzazi katika ujauzito kwa faida ya wengine ni marufuku kwa mujibu wa maoni ya wengi wa wanavyuoni wa kisasa, na hakuna maoni yoyote muhimu yaliyoruhusu hivyo, isipokuwa yale yaliyosemwa na baadhi ya wanavyuoni na mabaraza ya kifiqhi isipokuwa hali moja tu, ambayo ni: ikiwa mama mbadala anayebeba mimba kwa ajili ya mwingine ni mke mwingine, kwa mume ambaye ni mwenye yai la uzazi lililorutubishwa, waliruhusu kubeba ujauzito huo kwa yule mke mwingine kwa kuwepo haja, kama vile kuwa tumbo la mwenye yai la uzazi limeharibika au kuondolewa, lakini yai la uzazi la mama mbadala ni salama.
Maoni ambayo ni sahihi ni kusema kuwa ni marufuku na haramu wakati wote katika hali hii na nyingine; kwa sababu ya matatizo ya ugomvi ambao hutokea kati ya wake wawili, ni nani anayestahiki zaidi mtoto, na ugomvi ambao hutokea kati ya wanawake wawili kuhusu mtoto baadaye, masuala ya urithi kati ya tawi na asili na ulazima wa matumizi kwa tawi juu ya asili na mengine.
Suala la tatu: Kuhusu hukumu zinazohusika na wahusika wa operesheni ya mfuko wa uzazi mbadala ikitokea kwa hali iliyotajwa hapo juu -tunasema kwamba ni haramu- maneno hapa yanahusu mwenye yai, na mwenye mfuko wa uzazi mbadala, mume na daktari.
Tunasema kuwa: maoni ya wanavyuoni wa kisasa yametofautiana kuhusu nasaba ya mtoto inathibitishwa kwa mwenye yai la uzazi lililorutubishwa au kwa mwenye mfuko wa uzazi mbadala? Ni kweli kwamba linathibitishwa kwa mwenye mfuko wa uzazi mbadala, na inajumuisha hukumu zote za mtoto kwa mama yake, na ana mahitaji yote ya mama kwa mtoto wake kwa mujibu wa urithi, wajibu wa matumizi, malezi, na upanuzi wa uhalali na uharamu kwa asili yake, matawi yake na maelezo yake.
Na dalili ya hayo: Aya za Qur'ani Tukufu zinazoonesha wazi wazi kuwa mama ndiye anayebeba mimba na kuzaa, na kwamba ukuaji wa mimba ni ndani ya tumbo lake mama, kama Mwenyezi Mungu Mtukufu asemavyo: {Na Mwenyezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu, hali ya kuwa hamjui kitu...}. [AN NAHL: 78]. Inaonesha kuwa aliyezaa na akatoka mtoto huitwa mama, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu...} [LUQMAAN: 14] Basi anayebeba mimba ndiye huitwa mama kwa uhakika, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema pia: {Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu} [AL AHQAAF: 15]. Mwenyezi Mungu Mtukufu alionesha kuwa yule anayebeba mimba yake kwa taabu na kumzaa kwa taabu ndiye mama yake.
Pia Qur`ani imethibitisha hadhi ya umama kwa wale ambao wamebeba mimba na kuzaa, kwa njia inayoonesha uhusika wake kwa hadhi hii, kama ilivyo kwenye Aya hii: {Wale miongoni mwenu wanao watenga wake zao, hao si mama zao. Hawakuwa mama zao ila wale walio wazaa} [AL MUJADALAH: 2], Mwenyezi Mungu ameeleza kuwa mama ndiye aliyezaa, na kufuata njia zenye nguvu za uthibitisho, ambazo ni: kukanusha na uthibitisho, akakanusha kuwa mama kutoka kwa yule ambaye hakuzaa mtoto, na kuthibitisha kwa wale waliozaa.
Hii inaungwa mkono na Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Al-Bukhariy na Muslim kutoka kwa Hadithi ya Ibn Mas'ud R.A. kwamba Mtume S.A.W. alisema: "Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu. Kisha huwa donge la damu kwa muda kama huo. Kisha huwa pande la nyama kwa muda kama huo". Mtume S.A.W. alisema katika Hadithi hii kuwa ambaye umbo hukusanywa ndani ya tumbo lake ndiye ni mama, na kwa hivyo mtoto ni haki ya mama yake ambaye alibeba mimba na kumzaa, sio haki ya mwenye yai la uzazi.
Ama mwanamke aliye na yai la uzazi lililorutubishwa, kazi yake inachukuliwa kuwa ni bure, na haina hukumu, naye hana ukaribu kwa mtoto aliyetokana na chanjo hiyo, na wala hakuna uhusiano kati yao, na hii pia inathibitishwa na mtazamo wa wanavyuoni wa Fiqhi kwamba sababu za uharamu wa ndoa kwa wanawake ikiwa ni ya nasaba au kuoleana au kunyonyesha.
Ama kwa upande wa mume katika hali hii, hakuna shida katika kuthibitisha nasaba ya mtoto mchanga kwa upande wake, ndiye baba halali wa mtoto mchanga bila shaka; manii yaliyotumiwa katika chanjo hiyo ni manii yake, na kila mmoja wa wake wawili ni mke wake, mtoto ni wake, naye ndiye mwenye kitanda ambamo mtoto alizaliwa, na imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhariy na Muslim Kutoka kwa Hadithi ya mama wa Waumini Aisha R.A. kwamba Mtume S.A.W. alisema: "Mtoto ni wa mwenye kitanda alicho zaliwa".
Lakini inabaki kusema: kwamba daktari ambaye hufanya operesheni hii, na mume ambaye amemhimiza mkewe kuitekeleza au kuiidhinisha wamepata dhambi, na wamesaidia kufanya haramu, na Mwenyezi Mungu amesema: {Na saidianeni katika wema na uchamungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui} [AL MAIDAH: 2].
Suala la nne: Upasuaji wa kupandikiza mfuko wa uzazi una aina mbili: Ya kwanza ni: kwamba mfuko wa uzazi hupandikizwa kutoka kwa mwanamke aliye hai kupitia mchango, na aina hii ni haramu, kwa sababu ya uharibifu wa mfadhili mwenyewe kuondoa faida isiyoweza kutengwa kwa kuondoa kiungo cha mwili kilichotajwa, na kuletwa kwa uharibifu ni haramu. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Majah na Ahmad kutoka kwa Hadithi ya Ibn Abbas R.A. kwamba Mtume S.A.W. alisema: "Hakuna madhara wala kudhuriana", na mwanamke aliyechangia, ingawa kwa kufanya hivyo huondoa uharibifu kutoka kwa mwingine, lakini uharibifu bado ni uharibifu, kama ilivyo katika misingi ya Sheria. Imepokelewa kutoka kwa Al-Sananiy katika kitabu cha: [Subul As-Salaam 2/160, Ch. Dar Al-Hadith] Wanavyuoni walikubaliana juu ya uharamu wa kukatwa uume na kuhasiwa, vile vile kukatwa mfuko wa uzazi ni sawa katika hukumu ya kukatwa uume na kuhasiwa.
Aina ya pili ni: Ni kuwa mchango kuwa baada ya kifo chake, ameusia hivyo, na katika aina hii inawezekana kusema kuwa inaruhusiwa, kwa sharti la kuthibitishwa kisayansi kwamba mfuko wa uzazi mara moja hauna tabia ya jeni ya mfadhili, ikiwa imethibitishwa kinyume na hivyo, basi aina hii inafuata aina ya kwanza katika kukataza na kuharimisha.
Suala la tano: Kuhusu hukumu ya upasuaji wa kupima jeni ya kiinitete cha mke mzee kabla ya kuingizwa, ili kuepusha kasoro za jeni, hali hii inaruhusiwa kama haitasababisha uharibifu au uwezekano wa kuumizwa kwa mama au kiinitete baadaye. Hali ya kufuatilia kasoro za jeni katika hatua za mwanzo, inawapa wazazi nafasi ya kuamua kuendelea au kumalizia ujauzito, zaidi ya hivyo Madaktari wawatahadharishe juu ya umuhimu wa kufuata kiinitete kwa uangalifu hata kabla ya kuzaliwa.
Suala la sita: Kuhusu hukumu ya upasuaji wa kupima jeni kwa ajili ya kuchagua jinsia ya kiinitete kabla ya kuingizwa, kwa sababu za kijamii, tunaeleza kwamba hali ya kuainisha jinsia ya kiinitete kwa kiwango cha mtu binafsi inaruhusiwa, kwa sababu hakuna kikwazo cha kisheria kwa hali hii, na hii inasaidiwa na umiliki wa asili.
Inasisitizwa kuruhusiwa kwake ikiwa madhumuni ya kuainisha jinsia ya kiinitete ni kukidhi hitaji kubwa katika wanandoa, kama vile kuwa wana wasichana na wanatamani kuwa na mwanaume, au kinyume chake, au ikiwa hali ya kuzaa haikupatikana kwao kwa urahisi, nao -au mmoja wao- anatamani awe na kiume, au mfano wa hivyo.
Lakini katika kiwango cha kundi, hairuhusiwi, kwa sababu haitaelekea katika usawa wa asili kati ya jinsia mbili, na itasababisha usumbufu wa usawa wao wa idadi, ambao ni sababu ya kuendelea kwa kizazi cha mwanadamu.
Kwa hivyo, kuna tofauti kati ya hukumu kati ya kuainisha jinsia ya kiinitete kwa kiwango cha kibinafsi na kuainisha jinsia ya kiinitete kwa kiwango cha kundi kulingana na hukumu ya kisheria kwa kila aina, na tofauti ya Fatwa, kwa mujibu wa tofauti ya hali kwa wanavyuoni wa dini.
Suala la saba: Kuhusu Hukumu ya upasuaji wa kupima jeni kwa kiinitete ili kujua kufanana kwake na mtoto mwingine mgonjwa ambaye anahitaji kupandikiza mfupa wa uboho au kupandikiza kiungo cha mwili. Tunasema kwamba asili ya suala hili ni kwamba ikiwa kiinitete kikiendelea kuwa hai, basi suala la matibabu linapaswa kuelekezwa kuhifadhi maisha yake, sio kuwekeza kwa ajili ya kupandikiza viungo vya mwili. Lakini kama kiinitete hakitaendelea kuwa hai, hairuhusiwi kufaidika hadi baada ya kifo chake, kwa sharti la kuidhinishwa na walezi wake tu, kwamba faida ya matibabu ni ya yakini au itakuwa kwa kiwango kikubwa, na kwamba hakuna njia nyingine ya matibabu inayoruhusiwa.
Kusudi la utoaji wa mimba ili kutumia kiinitete kwa ajili ya kupandikiza viungo vyake katika mtu mwingine hali hii hairuhusiwi, lakini inaruhusiwa kwa hali ya utoaji wa mimba bila ya kukusudia, na utoaji wa mimba kwa udhuru wa kisheria.
Suala la nane: Kuhusiana na utumiaji wa uhandisi wa jeni kwa madhumuni ya kuboresha tabia ya kiinitete, kama vile kuzaliwa kwa mtoto mwenye nywele za shaba au mwenye macho buluu au mrefu, inayoonesha - na Mwenyezi Mungu anajua zaidi - inakatazwa hivyo; kwani kiinitete kitakuwa katika majaribio ambayo matokeo yake yanawezekana kutokea, hali hii inasababisha madhara kwa kiinitete na ulemavu kisaikolojia na kimwili pia. Kama suala hili likiweza kufanikiwa kwa baadhi ya wanyama, basi halihitaji kutokea kwa wanadamu kwa sababu hakuna kipimo cha kutosha. Akiwa mtu anaweza kujaribu aina fulani za dawa au matibabu, basi mtu huyu anapaswa kuwa na akili timamu kwa ajili ya kuchagua, pamoja na kujua kwa kiwango kikubwa kwamba chaguo hili halina madhara kwake, na hali hii haipatikani kwetu kwa kila njia, matokeo hayafikiriwi kwa uhakika, mpaka tunahitaji uwezeshaji wake.
Licha ya hivyo ni kinyume na Sunna ya utofauti ambayo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu, matokeo ya kijamii na kukataliwa kwa yasiyokubalika kimaadili; hivi sasa kuna mwelekeo wa kitabia unaokatazwa kisheria ambao tayari umeanza duniani, siku hizi kuna mwelekeo katika nchi za magharibi unaoita kuboresha kwa vizazi kufuatana na mwelekeo wa ubaguzi wa rangi kwa ajili ya kuwepo kwa watu wenye ustaarabu na kulinda jamii na kabila, na kwamba jamii masikini na dhaifu sio muhimu kuipa kipaumbele juu ya hatima yao, kuwepo kwao sio lazima kwa ubinadamu. Maana ya matokeo ya jambo hili siyo salama.
Suala la tisa: na kumi: Kuhusu matumizi ya teknolojia ya seli ya shina katika matibabu na tafiti za kisayansi, tunasema: seli za shina ni seli ambazo zina uwezo wa kugawanyika na kuzidisha kutoa aina tofauti za seli maalumu na kuunda tishu tofauti za mwili, na wanasayansi hivi karibuni wameweza kutambua seli hizi na kuzitenga na kuzikuza kwa ajili ya utumiaji wake katika matibabu ya magonjwa fulani. Seli hizi zinaweza kupatikana kwa kiinitete katika mchakato wa kijidudu, au kiinitete kinachoanguka wakati wowote wa ujauzito, au kwa kondo au kwa uzi wa kitovu, au kwa watoto au watu wazima, au kwa upachishaji kwa kuweka seli kutoka kwa seli ya ndani.
Na kupata, kukuza na kutumia seli hizi kwa madhumuni ya matibabu, au kufanya tafiti zinazofaa za kisayansi ikiwa hazimdhuru mtu ambaye amechukuliwa seli hii, basi inaruhusiwa kisheria, ikiwa imepatikana kutoka kwa mtu mzima kwa ruhusa yake, na pia inaweza kuchukuliwa kutoka kwa kondo au uzi wa kitovu, au katika hali ya kiinitete ambayo imetolewa moja kwa moja au kwa sababu ya kisheria kama wazazi wakikubali. Pia katika hali ya chanjo ya ziada kutoka miradi ya watoto ambao wapo katika mbolea (IVF) ikiwa imepatikana na imetolewa na wazazi.
Hairuhusiwi kupata seli za shina kwa njia ya haramu, kama vile kutoa mimba kwa makusudi bila ya sababu ya kisheria, au kwa kuingiza kwa makusudi kati ya yai la mwanamke na manii kutoka kwa mgeni, au kwa kuichukua kutoka kwa mtoto hata kwa idhini ya mlezi wake; kwani mlezi hawezi kufanya kitu chochote kwa mtoto ambaye ni chini ya ulezi wake, isipokuwa kwa faida ya mtoto tu.
Suala la kumi na moja: Kuhusiana na hukumu ya kisheria ya upachishaji kwa wanadamu, au kwa madhumuni ya matibabu kama vile kuzaliana kwa tishu au viungo, tunasema kwamba upachishaji unawezekana katika aina tatu za viumbe: mwanadamu, mnyama na mmea.
Kuhusu mmea uzalishaji wake umekuwepo tangu zamani, kwa kile kinachoitwa "ukuwaji wa mimea"; aina hii ina njia nyingi zikiwemo: kuchukua sehemu yoyote ya mmea na kuipanda, mmea kamili unatoka nje unaofanana na mmea wa asili bila ya kutumia chavua, au kuhamisha sehemu ya mmea uliotaka kuzaliwa kwa hivyo iwe na tumba moja na kuwekwa kwenye sehemu ya mmea mwingine ili kuzunguka kati ya sehemu hizi mbili kuunda mmea mpya wa kujitegemea kwa njia inayojulikana kwa wale wanaohusika katika mambo haya.
Upachishaji katika aina hii ni halali na inaweza kuhitajika kwa sababu ya faida zake kama vile kuboresha mifugo ya mimea na kuokoa aina zilizo hatarini na duni.
Katika uwanja wa wanyama, majaribio yalifanikiwa kwa hiyo, ambapo yai lisilo na mbolea lilichukuliwa kutoka kwa kondoo wa kike na kutengwa kutoka kiini chake, na kuimeingizwa mahali pa kiini kilichoondolewa kiini cha seli ya mwili iliyochukuliwa kutoka kwa kiwele cha kondoo wa kike mwingine ambaye ana mimba. Kiini hiki kimeingizwa ndani ya yai kwa umeme unaochochea, kisha kikawekwa ndani ya tumbo la kondoo wa tatu wa kike, kiini kilianza kugawanyika katika seli, hadi kikawa kiinitete kamili, kikatoka ndani ya mwangaza baada ya hivyo kiumbe hai.
Aina hii ya upachishaji pia inaruhusiwa, kwa sharti tu la kutokuwepo uharibifu na kupata manufaa ya kweli, kama vile uboreshaji wa mifugo, au utafiti halali wa kisayansi, na haileti madhara au kuteseka kwa mnyama mwenyewe bila ya sababu ya kisheria.
Na maana hii inasisitizwa kwa maneno ya Mwenyezi Mungu: (Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi) [Al-Baqarah: 29], na akisema pia: (Na nyama hoa amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya kutia joto na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala) [An-Nahl: 5].
Kuhusu upachishaji wa wanadamu, kama kusudi lake ni kupachisha mwanadamu kamili, umezuiliwa na kongamano la wanavyuoni wa kisasa. Baraza la Utafiti wa Kiislamu na mabaraza mengine ya kifiqhi, kama vile Baraza la Fiqhi la kiislamu la Kimataifa na Baraza la Kifiqhi lililopo Makka, mabaraza haya yametoa maazimio ya kuiharimisha aina hii, na kwamba lazima kuizuia kwa njia zote; kwani aina hii inamfanya mwanadamu ambaye ameheshimiwa na Mwenyezi Mungu kuwa kitu cha mchezo na majaribio, ambapo inaweza kutokea aina potofu na ya ajabu ya viumbe, pamoja na usumbufu unaofuatia katika maswala ya watu wa karibu, urithi, nasaba na haki zingine.
Kama upachishaji ukiwa ni sehemu ya tishu za viungo muhimu, kama vile tishu za moyo katika kesi ya shambulio la moyo kwa mfano, katika hali hii seli zilizopachishwa zinachanjwa kwenye misuli ya moyo iliyojeruhiwa ili kukua na kuchukua nafasi ya zilizoharibika, kufanya kazi zake na kurudisha maisha ya moyo wa mgonjwa, au kama upachishaji ukiwa kwa viungo vyote kama vile moyo, ini, figo, au viungo vengine. Ambavyo ni muhimu; kwa nia ya kufaidika katika matibabu, basi jambo hili linaruhusiwa, kama halikuleta madhara kwa mtu yeyote, au kushambulia utakatifu wake.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas