Kuzitilia Shaka Rai za Wanazuoni.
Question
Siku hizi tunawaona vijana wengi wenye msimamo mkali wa dini, katika misikiti, televisheni, na vikao vya elimu, wanatoa Fatwa nyingi za masuala ya kisheria, na wanakosoa rai za wanazuoni na kuwasahihisha, na huenda jambo hili linafikia hadi kutia shaka rai za wanazuoni wa zamani na wa sasa, na kutia shaka mifumo yao na nia zao. Ni ipi hukumu yao?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na Sifa njema za Mwenyezi Mungu, na Rehema na Amani zimshukie Bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, Aali zake na Masahaba zake, na waliomfuata, na baada ya hayo:
Hakika Mwenyezi Mungu amewasifu wenye elimu, na amewafanya kuwa bora katika Kitabu chake Kitukufu, Amesema: {Mwenyezi Mungu ameshuhudia ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye tu. Na Malaika na wenye ilimu, (wote wameshuhudia hayo); (Yeye) ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu}. [AALI IMRAAN: 18], basi tazama vipi kwanza alivyoanza nafsi yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, na pili Malaika, kisha tatu wenye elimu, na huu ni upeo wa heshima, fadhila, uwazi na Utukufu.
Na Mwenyezi Mungu Amesema: {Sema: “Je, wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua?”}. [ AZ ZUMAR: 9], na ulizo hapa ni kwa ajili ya kutanabahisha kuwa walio mwanzo ni wanazuoni wapo katika ngazi ya juu ya heri, na walio mwisho wapo katika ngazi ya chini ya shari, na hali hii iko wazi ambapo haifichiki kwa muadilifu wala kwa mwenye kiburi. [Tafsiir Roh Al-Maa’aniy: 23/246, Ch. ya Dar Ihiyaa’ At-Turarh Al-Arabiy, Bairut]
Na Mwenyezi Mungu amewapandisha daraja sana wanazuoni kuliko waumini, na akawapandisha sana waumini kuliko wengine, Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenyezi Mungu atawainua wale walioamini miongoni mwenu; na waliopewa ilimu watapata daraja zaidi}. [AL MUJADILAH: 11]. Na Ibn Abbas R.A., anasema: wanazuoni wana daraja ya juu zaidi kuliko waumini kwa kadiri ya daraja mia saba, kati ya daraja hizi mbili kadiri ya safari ya muda wa miaka mia tano.
Na Mwenyezi Mungu Amesema: {kwa hakika wanaomwogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja Wake ni wale wataalamu (wanavyuoni}. [FATWER: 28], na At-Twahir Ibn A’ashuur anasema: “ikijulikana hivyo, basi kuna dalili ya lazima kuwa wasio wanazuoni hawamuogopi Mwenyezi Mungu, na hii inaonesha kuwa wanadamu wanatofautiana kuhusu hali za nyoyo zao na uelewa wao”. [Tafsiir At-Tahriir wat-Tanwiir: 22/304, Ch. ya Dar Sahnuun, Tunisia]
Na Mwenyezi Mungu alimuamuru Bwana wetu Muhammad S.A.W., amuombe elimu zaidi, amesema Mwenyezi Mungu: {Na (uombe) useme: “Mola wangu, nizidishie elimu”. [TWAHA: 114]; yaani Ewe Muhammad sema: Mola wangu nizidishie elimu zaidi ya hiyo uliyonielimisha, basi alimuamuru amuombe kutokana na faida za elimu ambazo hajazifahamu kabla ya hapo.
Na Bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu Amesema: “Mtu ambaye Mwenyezi Mungu anamtakia heri, basi humuelimisha katika dini”. [Muttafaq]
Imamu Al-Ajuriy anasema: “Mwenyezi Mungu anapowatakia heri huwaelimisha katika dini, na kuwafundisha Kitabu na hekima, kwa hiyo wakawa taa kwa watu, na mwangaza kwa nchi”. [Akhlaq Al-Ulamaa: uk. 28, Ch. ya Riasat Idarat Al Buhuuth Al Elmiyah wal Iftaa wa Ad Daa’wah wal Irshad, Saudia].
Na kutoka kwa Abu Umamah Al-Bahiliy R.A., amesema: “Watu wawili walitajwa mbele ya Mtume S.A.W., mmoja wao ni mwenye ibada na mwingine ni mwanazuoni, na mtume S.A.W., Amesema: “Ubora wa wanachuoni juu ya mfanya ibada, ni kama ubora wangu juu ya mwenye daraja ya chini miongoni mwenu”, kisha Mtume S.A.W. akasema: Hakika Allah, Malaika Wake, walio mbinguni na ardhini, hata wadudu chungu waliomo katika mashimo yao na hata samaki, wanawatakia rehema wanaowafundisha watu heri”. [At-Tirmidhiy ameipokea]
Na Mtume S.A.W. Amesema: “Wanazuoni ni warithi wa Manabii”. [Imepokelewa na Abu Dawud, At-Tirmidhiy, Ibn Majah , na Ibn Hibban].
Inajulikana kuwa hakuna daraja la juu zaidi kuliko la Unabii, na hakuna heshima ya juu zaidi kuliko ya urithi wa daraja hili.
Na Mtume S.A.W., amesema pia: “Sifa mbili hazikusanyiki kwa mnafiki; heshima na ufahamu wa dini”. [At-Tirmidhiy]
Na akasema pia: “Si katika Umma wangu asiyemheshimu mkubwa wetu, asiyemhurumia mdogo wetu, na asiyefahamu haki za Wanachuoni wetu”. [Ameipokea Ahmad].
Na Imamu Ahmad anasema: “Watu wanahitajia sana elimu kuliko kula na kunywa; kwa sababu kula na kunywa kunahitajika kila siku mara mbili au tatu, lakini elimu inahitajika kila wakati”. [Ii’laam Al-Muwaqii’in: 2/257, Ch. ya Dar Aj-Jiil, Bairut]
Na ilivyopokelewa kutoka kwa Abdullahi Ibn Ahmad Ibn Hanbal, kutoka kwa baba yake, kuwa alimuuliza: “ Imamu Shafiy ni nani, kwa kuwa nilikusikia unaomba dua nyingi kwa ajili yake? Akasema: Ewe mwanangu, alikuwa kama Jua kwa dunia, na kama afya kwa watu; Je, vitu hivi viwili viwe na mfano au mbadala?”. [Siyar Aa’laam An-Nubalaa’, na Adh-Dhahabiy: 10/45, Ch. ya Muassasat Ar-Risalah, Bairut].
Ni afadhali kutofautisha kati ya mwanazuoni, mhubiri, na mlinganiaji, kwa sababu baadhi ya watu akili zao huvutwa kwa majina maalumu ya watu wasio na uhusiano na elimu, na mvuto wa akili kwa majina unaathiri sana kuhusu kufuata na kupenda; na hali hii inajitokeza kutokana na uwezo wao wa kuhutubu, wakadhani kuwa hiyoni dalili ya elimu; kwa hivyo utanaona watu wa kawaida, wasio wasomi, wanakwenda mbio sana kwa mhubiri na mwenye kuhutubu kuliko kwenda mbio kwa mwanazuoni.
Na Ibn Masu’ud anasema: “Hakika nyinyi mpo katika zama ambayo wanazuoni wake ni wengi, na wenye kuhutubu ni wachache… na baada yenu itakuja zama wanazuoni wake ni wachache na wenye kuhutubu ni wengi”. [Bukhariy katika kitabu cha Al-Adab Al-Mufrad]
Na Ibn Al-Jawziy anasema: “zamani wahubiri walikuwa ni wenye elimu na wenye Fiqhi, na Abdullahi Ibn Omar R.A, alikuwa akihudhuria kikao cha Ubaid Ibn Umair, vile vile Omar Ibn Abdulaziz alihudhuria kikao cha Al-Qaas, kisha kazi hiyo ikapungua, na wajinga walishughulika na kazi nayo, na wakuu wa watu walijiepusha kuhudhuria kwao, na watu wa kawaida na wanawake wakaambatana nao, kwa hiyo hawakuishughulikia elimu, na badala yake walielekea katika visa na yaliyowapendeza wajinga”. [Talbiisu Ibliis: Uk. 151, Ch. ya Dar Al-Kitab Al-Arabiy, Bairut]
Na wahubiri hawa wangekubali kuelezwa hivyo, pamoja na upungufu wao wa elimu ingekuwa bora, lakini walidai kuwa ni wenye elimu, wakatoa Fatwa na kufundisha, kwa hivyo walisababisha fitina kwa watu, kuwaepusha haki na njia ya sawa, na hao walistahiki kuelezwa kwa kauli ya Imamu Adh-Dhahabiy:
“Hawa ni watu ambao wameielekea elimu juu juu tu, lakini hawakuipata isipokuwa chache, na walijidanganya kuwa wao ni wanazuoni wakubwa, na hawakuzingatia kamwe kuwa ni jikurubisha kwa Allah, kwa sababu hawakuona Sheikh ambaye hufuatwa katika elimu, basi wakawa ni makundi ya watu wasio na nidhamu, na upeo wa msomi kati yao ni mwenye kupata baadhi ya vitabu vya marejeo, na kuvihifadhi, na kuvitazama siku moja miongoni mwa masiku, kisha kunukulu kimakosa na bila ya kuhakikisha; na sisi tumuombe Mwenyezi Mungu nusura na msamaha”. [Siyar Aa’laam An-Nubalaa’: 7/ 153].
Na Al-Khatwib Al-Baghdadiy pia anasema kuhusu watu kama hao: “Niliwaona watu miongoni mwa watu wa zama hizi wanajiunga kwenye elimu ya Hadithi, na wanajizingatia kuwa wao ni miongoni mwa wataalamu waliobobea katika usikilizaji wake na kuinukulu, na kwa hakika wao wako mbali sana na wanayoyadai pamoja na maarifa machache ya elimu hii, na mmoja kati yao anaona wakati anapoandika sehemu chache, na kusikia kwa muda mfupi, kuwa yeye ni mtu wa Hadithi kwa uwazi, na hali ya kuwa bado hajafanya bidii wala hajapata tabu katika kujifunza, na wala hajapata ugumu wa kuzihifadhi aina zake wala milango yake…
na wao pamoja na upungufu wa kuandika kwao katika elimu hii na kutoelewa kwake, wakawa ni wenye kiburi sana kuliko wengine na wenye kujiona na kujivuna, na hawazingatii heshima ya Mashekhe, na wala hawawajibiki na haki ya mwanafunzi, na wanawalaumu wapokezi wa Hadithi, na wanawatendea wanafunzi ujeuri, kinyume cha maamrisho ya elimu waliyoisikia na dhidi ya wajibu wanaowajibika kuufanya”. [Al-Jamii’ Li Akhlaq Ar-Rawiy Wasamii’: 1/ 75-77, Ch. ya Dar Al-Kitaab Al-Arabiy, Bairut]
Na kutoweka wazi tofauti kati ya wanazuoni na wengineo katika uelewa wa watu wengi, ni sababu ya kuwepo kwa wasiobobea wenye elimu, kwa hivyo wakaingia katika fatwa, na wakatoa maoni yao katika masuala ya Fiqhi ya ulinganishi, mpaka mchanganyiko mkubwa ukapatikana, katika wakati wetu huu, kati ya anayetoa Fatwa na mhubiri, na hiyo ndiyo iliyopelekea usumbufu mkubwa ambao sisi sote tunauona na kuuhisi.
Kwa hiyo haisihi kuingia katika kutoa Fatwa na masuala ya Fiqhi ya ulinganishi, isipokuwa kwa aliyebobea kitaaluma katika mambo haya: kusoma sana Fiqhi, Uswuli, Misingi ya Fiqhi; kuwa na mazoezi ya kushughulikia masuala ya kitaaluma na majadiliano ya kifiqhi; kuwa na uelewa na uzoefu wa Elimu ya Hadithi kwa ujumla, na hasa Elimu ya kupambanua daraja za wapokezi wa Hadithi (Al-Jarh wat-Taa’diil); vile vile kusoma sana Elimu za Kiarabu: Lugha, Sarufi, Elimu tatu za Balagha; na uelewa mzuri wa mazingira ya maisha; na katika wakati huu inapendeza mtu awe amepata masomo ya juu kwenye Vyuo Vikuu vyenye ubobezi huu.
Hayo yote kwa ajili ya kuzuia mchanganyiko wa Fatwa unaotokea huku na kule kutoka kwa wale wsiobobea katika Elimu ya Fiqhi na Usuuli, na anaonywa kujadili kuhusu fatwa, wakati hakusoma vyanzo vyake vya Fiqhi wala usuuli wake. Na wanazuoni wa zamani walizungumzia umuhimu wa ubobeji wa Fiqhi.
Zamani walisema kuwa: “Aliyeshughulikia elimu kabla hajasoma, ni mfano wa mmea bila ya mizizi”.
Na Mwanafasihi Ali Ibn Zaid Al-Baihaqiy ana Risala yenye jina la: (Tanbiih Al-U’lamaa’ Ala Tamwiih Al-Mutashabihiin Bil U’lamaa’).
Kwa hivyo hawa wanaojidai kuiwa na elimu wanaposhughulikia yale yasiyokuwa yao, inazingatiwa ni sababu kuu ya kutia shaka na kuwashutumu wanazuoni, kwa sababu kushidwa kwao kushughulikia masuala ya Fiqhi Linganishi na Fatwa, pamoja na upungufu wa elimu yao, na kuwa na haraka ya kufikia ngazi hii ya juu, na hayo yanakwenda sambamba na kuwakosoa wanaowapinga na kuwadharau, na kuwaelezea kuwa wajinga, hayo yote yanapelekea baadhi ya watu wa kawaida kurahisisha kuwakosoa wanazuoni na kuwashutumu kwa yasiyofaa.
Na hakuna kosa kuwa mtu anayehitilafiana na mwanazuoni au mlinganiaji kuhusu rai au jitihada, sharti awe na elimu ya hayo, lakini kosa la uhakika ni kugeuza hitilafu hii kuwa jembe la kuivunja hadhi ya mwanazuoni huyu, kupunguza daraja yake, kumdharau, na kumtendea yasiyostahiki.
Na kati ya watu yupo anayekanusha rai ya mwanazuoni kwa sababu ya ujinga wake kwa Fatwa iliyotolewa na mwanazuoni huyu; basi anasikia jambo linalowezekana au linalojumlisha, na hajui jambo la kuelezea ujumlisho huu, na haulizi mwanazuoni juu yake, lakini analichukua jambo hili analolisikia kisha akalieneza kuwa ni kosa kubwa. Na Mshairi anasema:
Wanasema hilo halijuzu kwa maoni yetu
Na nyinyi ni nani hata mkawa na maoni?
Na huanza kutoa shutuma nyingi kama vile: kurahisisha, kufanya bidaa, kufuata serikali, na mengi yasiyo sahihi na hayana asili isipokuwa katika akili ya mpingaji tu, na mtu kama huyu hawi ila ni miongoni mwa wanaojidai kuwa wana elimu, ambao wengi wao wamekuwa ni mtihani kwa wakati wetu huu, kwa sababu kama angelikuwa mwanazuoni yasingetoka kwake mambo kama hayo, na mwanazuoni wa kweli anaijua haki ya mwenzake, na anajua namna ya kujibu hitilafu ya suala la kitaaluma, na namna ya kujadili kwake.
Imamu Adh-Dhahabiy katika wasifu wake kwa Muhammad Ibn Nasr Al-Maruziy anasema: “Lau kila Imamu alipofanya kosa dogo katika jitihada yake ya suala moja, na sisi tungelimpinga kuwa ni bidaa na tukamwepuka, basi asingelisalimika Ibn Nasr wala Ibn Mundhir wala walio wakubwa kuliko wao, na Mwenyezi Mungu ndiye ni Mwongozi wa watu kwa haki, na Yeye ndiye Mwingi wa Rehema kabisa, na tunajikinga kwa Mwenyezi Mungu na matamanio na jeuri. [Siyar Aa’laam An-Nubalaa’: 14/39-40].
Na Imamu Adh-Dhahabiy pia alitaja kuwa: Abu Kamil Al-Basriy alisema: nilisikia baadhi ya Mashekhe wetu walisema: “Tulikuwa katika kikao cha Abu Khanb, na yeye alitoa sifa kuhusu fadhila za Ali R.A, baada ya kutoa kuhusu watu Watatu waliotangulia, hapo Abul Fadhl As-Sulaimaniy alisimama, na akalia: Enyi watu! Huyu ni muongo, msiandike, na akatoka kwenye kikao; kwa sababu yeye hakusikia fadhila za Watatu; na Imamu Adh-Dhahabiy alielezea kisa hicho akisema: “hii inaonesha ubaya wa As-Suleimani na uchokozi wake, na Mwenyezi Mungu amsamehe”. [Siyar Aa’laam An-Nubalaa’: 15/524].
Hivyo wanazuoni walikubali kuwa mtu wa kawaida, na mwanazuoni ambaye alijifunza baadhi ya taaluma za jitihada, lakini bado hajafikia ngazi ya jitihada, hao wanawajibika kumfuata Imamu, na haisihi kwa wafuasi kuwakanusha wengine, hali ya kuwa wao pia ni wafuasi kauli ya Imamu anayefuatwa, basi vipi inasihi kukanushwa wanazuoni wenyewe na hao wanofuata na kujidai kuwa na elimu?!
Hatuwezi kusema isipokuwa ilivyosemwa na Imamu Adh-Dhahabiy kuhusu kumtetea kwake Imamu Ahmad, wakati baadhi ya wajinga walimuelezea kuwa ni mjuzi wa Hadithi na siyo mjuzi wa Fiqhi akisema: “Hakika mjinga hajui daraja yake mwenyewe, basi vipi atajua daraja la mwingine?!” [Siyar Aa’laam An-Nubalaa’: 11/321].
Ni lazima kusemwa kwa hao wanaojidai kuwa na elimu: ijue nafsi yako, na usiiweke mahali pasipofaa, kwa sababu mtu akijua kadiri ya nafsi yake hiyo itakuwa ni sehemu ya elimu, na jiepushe na kiburi ambacho ni kuikataza haki na kuwadharau watu, kutosema kauli ambayo mtu haifahamu vizuri, hayo yote huleta majadiliano yasiyo ya taaluma yanayokuwepo katika uwanja wa kiislamu. Na Imamu Al-Ghazaliy alisema kweli aliposema: “Mtu asiyeijua haki anaponyamaza, basi hitilafu hupungua”.
Tunahitimu maneno haya kwa kauli ya Imamu miongoni mwa Maimamu wakubwa, akitutahadharisha na matokeo ya hali ya kuwatilia shaka wanazuoni na kupunguza heshima zao, naye ni Imamu Al-hafidh Abul Qasim Ibn A’asakir, Mwenyezi Mungu amrehemu, katika utangulizi wa kitabu chake [Tabyiin Kadhib Al-Muftariy Fima Nusiba Ila Al-Imaam Al-Asha’ariy: Uk. 29, Ch. ya Matbaa’at At-Tawfiiq, Damascus] anasema: “Fahamu ewe ndugu yangu! Mwenyezi Mungu atuongoze kwa njia ya radhi zake, atujaalie tuwe miongoni mwa wanaomuogopa na kumcha ipasavyo, jua kuwa nyama za wanazuoni ni zina sumu, na njia ya Mwenyezi Mungu ya kuwafedhehesha wapingaji wao inajulikana, na kuwa aliyetoa ulimi wake kuwashutumu, Mwenyezi Mungu atamuadhibu kwa kuufisha moyo wake, kabla hajafa yeye mwenyewe”.
Na kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia: Hakika kuwatilia shaka wanazuoni ni Jambo linalokatazwa kiasili, na limeharamishwa kabisa kwa watu wa kawaida kwa uwazi. Lakini kwa wenye elimu inajuzu kwao kuwakosoa wanazuoni, kuwapinga, na kuwajadili, kwa masharti maalumu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.