Watu wa Mardin

Egypt's Dar Al-Ifta

Watu wa Mardin

Question

 Makundi mengi yenye misimamo mikali, katika zama hizi, yamechukua Fatwa ya Ibn Taimiyah kuhusu Watu wa Mardin, kama dalili inayohalalisha vitendo wanavyovifanya vya hujuma, uharibifu, na mauaji ya wanadamu, kwa jina la Uislamu. Je, ni upi uhakika wa Fatwa hii? Na je, inazingatiwa ni dalili ya kuhalilisha damu na mali za watu?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wafuasi, na baada ya utangulizi huu:
Fatwa ya Mardin ni mashuhuri kutoka kwa Ibn Taimiyah, Mwenyezi Mungu amrehemu, na Mardin ni Mji ulioko Kusini mwa Uturuki ya sasa, ambapo Ibn Taimiyah alizaliwa huko, na ndani yake kuna Mji wa Harran, na Watataari waliuteka mji huo wakati wa uhai wake, hali iliyosababisha yeye na Jamaa zake wauhame mji huo, wakati akiwa na umri wa miaka saba.
Wakazi wa Mardin walikuwa Waislamu, lakini Watataari waliwateka, na Watataari walikuwa wakichanganya ukafiri, ujeuri na uadui kwa mtazamo wa Ibn Taimiyah ambaye aliishi katika zama zao na akawaelewa.
Watataari waliziteka nyumba za Waislamu, wakafanya kiasi kikubwa cha dhuluma, jeuri, na machafu. hali ya kuwa wakazi wa mji huo ni Waislamu, lakini watekaji na watawala wao sio Waislamu.
Kwa hiyo Ibn Taimiyah alijiwa na swali hili kwa ajili ya kujua hali ya wakazi wa mji huu, na je, inasihi kuwaelezea kuwa wanafiki, na je, wanalazimika wahame? Na kama wanalazimika kuhama lakini hawakufanya hivyo, basi ni ipi hukumu yao, na je, mji wao unazingatiwa ni nchi ya Kiislamu?
Na matini ya Fatwa ni kama ifuatavyo:
Suala: Kuhusu mji wa Mardin, je, ni nchi ya vita au nchi ya amani? Na je, Mwislamu anayekaa ndani yake analazimika kuhama kwenda nchi ya Kiislamu, au hapana? Na kama analazimika kuhama lakini hakufanya hivyo na akawasaidia maadui wa Uislamu kwa nafsi au mali yake, je, atapata dhambi katika hayo? Na je, anayewaona kuwa ni wanafiki na kuwatukana kwa hayo atapata dhambi au hapana?
Jawabu:
“Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu , damu na mali za Waislamu ni haramu, wakiwa ndani ya mji wa Mardin au mji mwingine, na kuwasaidia walio nje ya Sharia ya Uislamu ni haramu, wakiwa ndani ya mji wa Mardin au mji mwingine, na mkazi wa mji wa Mardin asipoweza kusimamisha dini yake, analazimika kuhama, na vinginevyo itakuwa ni Sunna na siyo Faradhi, na kuwasaidia maadui wa Waislamu kwa nafsi na mali ni haramu kwao, na inawajibika wasifanye hivyo kwa njia yo yote iwezekanavyo, kama kutohudhuria, hila, au hadaa.
Na kama asipoweza kufanya hivyo isipokuwa kuhama, basi ni lazima kuhama, na haijuzu kwa ujumla kuwatukana na kuwaita wanafiki, kwa sababu kuwatukana na kuwaita wanafiki huambatana na sifa zilizotajwa katika Qu`rani na Sunna, na sifa hizi wataingia baadhi ya watu wa Mardin na wengineo.
Kuhusu mji wa Mardin ni nchi ya amani au ya vita, hakika kuna tofauti ya maana hizo mbili; siyo sio nchi ya amani ambayo hukumu za Uislamu zitekelezwe ndani yake, kwa sababu askari wake ni Waislamu, na wala hali yake si nchi ya vitana uadui ambapo wakazi wake ni makafiri, bali ni sehemu ya tatu, ambapo Muislamu ndani yake anatendewa haki yake anayostahihi, na aliye nje ya Sharia ya Uislamu anatendewa haki yake kama anavyostahiki”. [Al-Fatawa Al-Kubra: Juzuu 3, Uk. 533, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah].
Ipo kasoro ya kufahamu kwa baadhi ya wenye msimamo mkali, ambao waliichukua Fatwa hii, bila ya kurejea kwa wanazuoni na wenye taaluma ili wabainishiwe madhumuni ya Fatwa hii, maana yake, na muktadha ambao ilisemwa.
Na sababu ya kasoro hii ni kutojali kuitumia, licha ya uzoefu, matumizi ya njia ya taaluma kwa jinsi ya uhakiki wa matini na kuzifahamu kwa wanazuoni wa Uislamu.
Kwa hiyo vijana hawa wasio wa taaluma walichukua Fatwa ya Ibn Taymiyah kimakosa, basi wakabadilisha usemi wa (Aliye nje ya Sharia ya Uislamu anatendewa) kwa neno (Aliye nje ya Sharia ya Uislamu anapigwa vita), na kwa njia hii walihalalisha matendo ya mauaji, maonevu, uharibifu, na kuwatisha wenye amani, wakiwa Waislamu au wasio Waislamu.
Na usahihi wa usemi wa Ibn Taymiyah ni ule tuliouandika, kwa dalili zifuatazo:
A- Neno hili limeandikwa kama (anatendewa) katika nakala ya muswada ya pekee uliyopo katika Al-Maktabah Adh-Dhahiriyah, Namba ya (2757) katika Maktabat Al-Asad, Damascus.
B- Miongoni mwa ilivyonukuliwa na Ibn Muflih, naye ni mwanafunzi wa Ibn Taymiyah, na wakati wake ni karibu naye, kweli alilinukulu kwa njia sahihi liwe kama (anatendewa). [Al-Adaab Ash-Shari’yah: Juzuu 1, Uk. 212].
C- Fatwa hii imenukuliwa katika [Ad-Durar As-Saniyah Fi Al-Ajwibah An-Najdiyah: juzuu 12, Uk. 248] kwa njia sahihi.
D- Sheikh Rashid Redha katika Gazeti la Al-manar alilinukulu kwa njia sahihi.
Hakika kosa lililohusu neno hili lilikuwa mara ya kwanza kabla ya miaka mia kwenye chapisho la Al-Fatawa, lililotayarishwa na Farajullah Al-Kurdiy, Mwaka 1327 H., kisha amemfuata hivyo hivyo Sheikh Abdur-Rahman Al-Qasim katika Majmuu’ Al-Fatawa: Juzuu 28, Uk. 248, kwa hivyo matini hii ikawa mashuhuri na kuenezwa kwa mujibu wa umashuhuri wa chapisho la Majmuu’ Al-Fatawa na maenezi yake kati ya wanafunzi wa elimu.
Kutoandika kiusahihi Fatwa ya Ibn Taymiyah hakika kumepelekea kuibadili na kusababisha kupoteza damu nyingi za Waislamu na wengineo, licha ya hayo kumedhuru makusudio ya Sharia na malengo yake, na kumesababisha kuchafua sura ya Uislamu na Waislamu, na kuielezea kwa msimamo mkali, uonevu, na ugaidi, na hasa kufasiriwa Fatwa hii kwa Kiingereza na Kifaransa umetegemea maandishi yaliyobadilishwa.
Japo kuwa kanuni itumikayo kwa wanazuoni inayosema kuwa: madai ya fikra mbaya katika tafsiri ni mepesi zaidi kuliko madai ya kubadilishwa asili yake; isipokuwa waliotumia maandishi ya kubadilishwa ya Ibn Taymiyah walikuwa na makosa katika mambo hayo mawili; kwa sababu tafsiri imejengeka katika asili sahihi, na kwa upande huu, wao walikosea katika uandikaji sahihi wa matini na kusoma kwake, pia walikosea katika kuelewa neno lililobadilishwa kupitia muktadha, na maneno yaliyotangulia na yaliyofuata.
Na alama ya hivyo ni kiunganisho na kitenganisho ambavyo vimetajwa katika matini ya Fatwa kati ya kauli yake: (Aliye nje ya Sharia ya Uislamu anatendewa kwa haki yake), na kauli yake: (Mwislamu ndani yake anatendewa kwa haki yake). Na kama muradi wake, kama walivyofahamu, kuwa (Aliye nje anapigwa vita) basi hakuna haja ya kauli ya baada yake: (kwa haki yake), kwa sababu hitilafu siyo katika jinsi ya kupigwa vita, bali ni katika makubaliano ya vita na usharia wake, hili ni jambo moja.
Na jambo jingine ni: sababu ambayo wapiganiaji wametegemea Fatwa hii na kuichukua kama dalili kwao kuwa: ibara ya (Aliye nje ya Sharia anapigwa vita) inakusanya mambo mawili:
Kwanza: Kuweka usharia wa kumpiga vita aliye nje ya Sharia kwa kutumia kauli ya kutendewa humaanisha kuwa: Ni haki ya kila Mwislamu afanye hivyo, kwa hiyo makundi hayo wanadai kuwa wao wenyewe watatekeleza kazi hiyo ya kupigana vita na kuyapinga mataifa na jamii za kiislamu.
Pili: Tamko la (Aliye nje ya Sharia) ni tamko lenye maana pana, kwa sababu uhalifu wa Sharia ni maeneo mapana ambayo huanzia dhambi ndogo na huishia dhambi kubwa za ukafiri, na hali hii itakuwa maeneo mapana ya kupiga vita na kunyang’anya mali za watu.
Lakini kwa kusahihisha matini, kama tulivotaja, Fatwa haikuwa na hoja hii ya makundi ya msimamo mkali, na kwa kuongeza ni kuwa: Kuifahamu maana kamili ya Fatwa huondoa hoja hii, kwa sababu Ibn Taymiyah alitilia mkazo jumla ya misingi iliyo wazi kwa mwenye kuchunguza Fatwa, kama yafuatayo:
A- Uharamu wa damu na mali ya Watu wa Mardin, na kuwa kuwepo kwao chini ya utawala wa makafiri wanaowashinda, hali hii haipunguzi kitu cho chote cha haki zao, na haijuzu kuwashutumu wala kuwaita wanafiki, licha ya ukafiri.
B- Kutowajibika kuhama, wakati wakiweza kusimamisha dini yao.
C- Uharamu wa kuwasaidia maadui wa Waislamu, hata wakilazimika wafanye hadaa, hila, na kutokuwepo.
D- Mji wao siyo nchi ya Uislamu halisi; kwa sababu washindi katika nchi hiyo sio Waislamu, wala sio nchi ya ukafiri halisi; kwa sababu wakazi wake ni Waislamu, lakini ni nchi yenye hali hizi mbili; basi Mwislamu ndani yake anatendewa kwa haki yake, na aliye nje ya Sharia ya Uislamu anatendewa kwa haki yake.
Kwa hiyo haiwezekani kamwe kuwa Fatwa hii ya Ibn Taymiyah kuhusu Watu wa Mardin iwe sababu ya kuhalalisha damu na mali za Waislamu kwa dai la kuwa wanakaa katika Mji wao chini ya utawala wa makafiri wanaowashinda.
Na Ibn Taymiyah katika Fatwa hii anaelekea katika mtazamo halisi wa Uislamu, ambao ndani yake kuna hadhari mbele ya damu na mali, bali pia kukufurisha, kwa kiasi kikubwa sana.
Na kwa sababu Mwislamu anahukumiwa kuwa Mwislamu wakati alipokiri kuwa: Hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, atakaposema hivyo, atahifadhika damu yake na mali yake, isipokuwa kwa haki yake, na sifa ya Uislamu haiondoki kwake, isipokuwa kwa yakini.
Na miongoni mwa matini inayobainisha hivyo, ni hii ifuatayo:
Kauli yake Mtume S.A.W.: “Nimeamrishwa nipigane na watu mpaka washuhudie kuwa hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, watakaposema hivyo, watahifadhika damu zao na mali zao”. [Ameipokea Imamu Bukhariy; Mlango: Watakapotubu na kusimamisha swala, kutoka kwa Ibn Umar, Namba ya Hadithi: 25].
Na Hadithi iliyopokelewa na Usamah Ibn Zaid ambaye alimuua mtu akishuhudia kuwa hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mtume S.A.W, alimwambia: “Umemuua baada ya kuwa amesema: hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nikamwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: alikuwa akijikinga tu. Akakariri, akaendelea kukariri neno hili, mpaka nikatamani lau kama nisingelisilimu kabla ya siku hiyo”. [Ameipokea Imamu Bukhariy, Mlango wa: Jeshi la Usamah Ibn Zaid, Namba ya: 4269].
Na katika Hadithi: “Atatoka katika moto aliyesema: Hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu”. [Ameipokea Imamu Bukhariy, kutoka kwa Anas Ibn malik, Mlango: Kuzidi na kupungua Imani, Namba: 44].
Pia Mtume S.A.W, alisema: “Atakayekufa hali ya kuwa hakumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote, ataingia Peponi, na hata kama akizini na kuiba”. [Ameipokea Imamu Muslim, Mlango: atakayekufa hali ya kuwa hakumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote ataingia peponi, Namba: 282].
Na Umma wa Uislamu ulikubali pamoja kuwa matokeo ya kuzitamka Shahada mbili ni kumpa mwenye kutamka sifa ya Uislamu, na kuhifadhi damu na mali zake, pia matokeo ya katazo na ukanaji yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu ni kutoka katika imani, kwa sababu kitendo hicho ni kuzikataa Shahada na kuzikanusha kwake.
Na Mtume S.A.W, alitanabahisha mahali pa maovu na dhambi kwenye suala la imani katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Dawud, kutoka kwa Anas Ibn Malik, alisema: Mtume S.A.W, alisema: “Mambo matatu ni miongoni mwa asili ya Imani: Kuhifadhi aliyesema: Hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, hatumkufurishi kwa sababu ya dhambi, wala kumtoa nje ya Uislamu kwa sababu ya matendo yake mabaya”. [Sunan Abu Dawud, Mlango: kuwapiga vita Maimamu wenye dhuluma, Namba ya Hadithi: 2532].
Tunatilia mkazo umuhimu wa kazi njema ya kukamilisha Imani, na hatusahilishi maovu madogo au makubwa, lakini tunasema yalivyosemwa na wanazuoni, na tunazuia ndimi zetu dhidi ya watu waliosema: Hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Muhammad ni Mtume wake.
Na hakitakiwi kitu kingine pamoja na Shahada, na Mtume S.A.W, hakushurutisha kitu kwa ajili ya kuingia Uislamu isipokuwa Shahada mbili, na alikuwa akisema: “Semeni: Hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, mtafaulu”. [Ameipokea Imamu Ahmad katika Musnad yake, kutoka kwa Rabia’ah ibn Abbad Ad-Diliy, Namba: 16446].
Na kutoka kwa Al-Miqdad Ibn Al-Aswad, alisema:
“Nilisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Unaonaje nikimkuta mtu kafiri, akanipiga, akapiga mkono wangu kwa panga, akaukata, kisha akajikinga nyuma ya mti, na akasema: Nimesilimu kwa ajili ya Menyezi Mungu, basi nina ruhusa ya kumuua baada ya usemi wake huu? Mtume S.A.W., alisema: usimuue, nikasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Hakika yeye ameukata mkono wangu kisha akasema hivyo baada ya kuukata, basi nina ruhusa ya kumuua? Akasema: usimuue, na ukimuua, basi yeye ni mahali pako kabla ya kumuua, na wewe ni mahali pake kabla ya kusema usemi wake”. [Ameipokea Imamu muslim, Mlango: kuharamisha kumuua kafiri baada ya kusema: Hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu, Namba: 284].
Na Mtume S.A.W, amesema: “Aliyeswali Swala yetu, akaelekea Qibla yetu, akala mnyama wetu aliyechinjwa, basi huyo ni Mwislamu ambaye ana ahadi ya Mwenyezi Mungu na ahadi ya Mtume wake”. [Ameipokea Imamu Bukhariy, kutoka kwa Anas Ibn Malik, Mlango: kuelekea Qibla, Namba ya Hadithi; 391].
Ibn Hajar kwenye maelezo yake ya Hadithi hii alisema: “Inaonesha kuwa mambo ya watu yamechukuliwa kwa dhahiri, basi aliyedhihirisha ibada za dini atatendewa kwa mujibu wa hukumu za watu wa dini hii, isipokuwa akidhihirisha kinyume chake”. [Fat-h Al-Bariy: Juzuu 1, Uk. 497].
Kutegemea yaliyotangulia inabainika kuwa kuzitamka Shahada mbili, au mfano wake, ni asili ya kuthibitisha sifa ya Uislamu kwa uwazi kwa mwenye kutamka, na hii ni hukumu wazi ya Sharia, ambayo haihusu zamani wala mahali maalumu- Mji wa Mardin au mwingineo kama ilivyotajwa katika swali- na haihusu pia hali fulani bila hali fulani, isipokuwa ikiambatana na sifa maalumu inayowajibika kuvuliwa kwa hali ya jumla, na hapo itakuwa na hukumu maalumu, bila ya kupingana na kanuni ya jumla”. [Mabdaan Hadaman, na Umar Abdullahi Kaamil, Uk. 24; Qadiyat Takfiir Al-Muslim, na Salim Al-Bahnasawiy, Uk. 60].
Na Mwenyezi Mungu alitutahadharisha tuchukue mambo kwa dhahiri yake, akisema: {wala msimwambie yule anayekutoleeni salamu (ya kwamba): “Wewe si Mwislamu”}. [AN NISAA: 94], na maana hii ndiyo maneno ya wanazuoni waliionesha.
Mtaalamu Ibn Al-Humam, mfuasi wa madhehebu ya Hanafi anasema: “Hakuna shaka kwamba ni wajibu kuchukua tahadhari kwa kutomkufurisha Mwislamu, ambapo walisema: Suala hili kama lilikuwa na sura nyingi ambazo zinawajibika kukufurisha, lakini kuna sura moja tu, ambayo inakataza, Mufti analazimika kuielekea sura hiyo moja na kuijenga rai yake juu ya sura hii”. [Fat-h Al-Qadiir: Juzuu 5, Uk. 315].
Imamu Al-Ghazaliy anasema: “Kuzihalalisha damu na mali za wanaoswali kwenye Qibla, wanaodhihirisha kumpwekesha Mwenyezi Mungu ni kosa, na kosa la kuacha makafiri elfu katika maisha, ni bora kuliko kosa la kumwaga damu ya Mwislamu mmoja”. [Al-Manthuur Fil Qawqid, na Az-Zarkashiy, Juzuu 3, uk. 87].
Na Imamu Ash-Shawkaniy anasema: “Jua kuwa hukumu dhidi ya mtu Mwislamu atoke nje ya dini ya Uislamu, na kuingia dini ya Ukafiri, haijuzu kwa Mwislamu mwenye imani kwa Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kufanya hivyo, isipokuwa kwa dalili iliyo wazi zaidi kuliko Jua la Mchana”. [As-Sailu Al-Jarrar: Juzuu 4, Uk. 578].
Na Ibn Taymiyah, ambaye hawa waliochukua Fatwa yake iwe dalili ya kumwaga damu na kuhalalisha mali, yeye mwenyewe anasema: “Haijuzu kumkufurisha Mwislamu kwa sababu ya kuzifanya dhambi, wala kosa, hasa katika masuala wanayoyahitilafiana watu wa Qibla, kwa sababu Mwenyezi Mungu amesema: {Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi wake, na Waumini vile vile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake. Hatutafautishi baina yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghfira Mola Mlezi wetu! Na marejeo ni kwako}. [AL BAQARAH: 285].
Na imethibitika katika Hadithi Sahihi kuwa Mwenyezi Mungu ameikubali dua hii, na amewasamehe Waumini kosa lao”. [Majmuu’ Al-Fatawa: Juzuu 3, Uk. 282].
Na ajabu zote ni za hawa wanaohalalisha damu, mali, na heshima za Waislamu, si kitu tu ila ni ufafanuzi unaopita akilini mwao, pamoja na kughafilika mwelekeo wa wazi wa Uislamu ambao unatilia mkazo kuwa: “Kila Mwislamu juu ya Mwislamu Mwenzie ni haramu: damu yake, mali yake, na heshima yake”. [Ameipokea Imamu Muslim, Mlango: Kuharamisha kumdhulumu Mwislamu na kutosaidia kwake, Namba: 2564, na Abu Dawud, Mlango: katika Sengenyo, Namba: 4882].
Na alitanabahisha kuwa: “Si halali kwa Mwislamu kitu chochote cha mali ya Mwenziye isipokuwa kumpa kwa ridhaa zake”. [Ameipokea Al-Baihaqiy katika As-Sunan Al-Kubra, kutoka kwa Ibn Abbas, Namba: 11304].
Kwa kweli Mtume S.A.W, alitanabahisha uharamu wa damu na mali ya Mtu Mwenye Ahadi, ilhali yeye si Mwislamu, akisema: “Fahamu! Aliyemdhulumu Mtu Mwenye Ahadi, kumdharau, kumchosha zaidi ya uwezo wake, kuchukua kutoka kwake kitu chochote bila ya ridhaa zake, basi mimi ni hasimu wake Siku ya kiyama. Fahamu! Aliyemuua Mtu Mwenye Ahadi ambaye ana Ahadi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi Mwenyezi Mungu atamharamishia harufu ya Pepo, na harufu yake hunuswa kwa mwendo wa miaka sabini”. [Ameipokea Al-Baihaqiy katika As-Sunan].
Na hii ni hali ya kutendeana na asiye Mwislamu, basi uanonaje huyu anayesema: Hakuna Mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu, kusimamisha Swala, kutoa zaka, basi vipi inaweza kuhalalishwa heshima yake, damu yake, na mali yake bila ya hoja ya Sharia: “Haihalalishwi damu ya Mtu Mwislamu ambaye anashuhudia: Hakuna mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu; haihalalishwi isipokuwa katika jambo moja miongoni mwa mambo matatu; nafsi kwa nafsi, mzinifu mwenye kuoa, na mwanye kuacha dini yake na jamaa zake”. [Muttafaq].
Na masuala ya kukufurisha ni lazima kuchukua hadhari mbele yake, na hayatolewi ila kutoka kwa wanazuoni wenye taaluma, au kutoka kwa wenye wadhifa wa kutoa Fatwa, ambapo hutolewa uamuzi kutoka kwa kadhi mwenye sifa. Na Ibn Hajar anasema: “Ni lazima kwa Mufti kuchukua hadhari katika suala la kukufurisha awezekanavyo, kwa sababu jambo hili lina hatari kubwa, na huenda kutokusudiwa hasa kwa upande wa watu wa kawaida”. [Tuhfat Al-Muhtaj: Juzuu 9, Uk. 88].
Kwa mujibu wa Maelezo hayo: Haijuzu kuwa Fatwa ya Watu wa Mardin na Ibn Taymiyah ichukuliwe kama hoja ya kuzihalalisha damu na mali za watu. Na kuihalalisha damu au mali ya mtu maalumu ni miongoni mwa wadhifa wa Mufti na kadhi, kisha utawala unaohusika ni upande wa kutekeleza uamuzi huu. Na jambo hili haliachwi kwa watu wa kawaida au kundi miongoni mwa makundi, kinyume cha hayo mizani ya uadilifu na Sharia itaanguka.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas