Kufanya Upasuaji wa Kujihasi.
Question
Je inafaa kisharia kwa mwanamume kujitokeza na kuchukua hatua za kufanya upasuaji wa kujihasi yeye mwenyewe ikiwa hana uwezo wa kifedha wa kuoa na akawa anajihofia yeye mwenyewe kuingia kwenye mambo ya haramu, ambapo inasikika kwenye ndimi za watu kuwa baadhi ya wanachuoni wamepitisha hilo, na wanasema kuwa Mtume S.A.W. alilipitisha hilo kwa baadhi ya Masahaba?
Answer
Shukrani za Mwenyezi Mungu peke yake, Swala na salamu ziwe kwa Mtume wa mwisho naye ni Mtume Muhammad S.A.W. pamoja na Watu wake na Masahaba zake na kila mwenye kumfuata kwa wema mpaka siku ya malipo, na baada ya utangulizi huo:
Neno hili la kuhasi: Maana yake ni mtu kutaka kuziondoa Korodani zake mbili ambazo ni sehemu ya viungo vya uzazi kwa wanaume.
Kitendo cha kuondoa Korodani mbili za mwanadamu kisharia ni haramu, kumekuwa na dalili za kisharia juu ya hilo:
Kutoka ndani ya Qur`ani Tukufu: Kuna kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: {Wao hawawaombi badala yake Yeye ila wanawake, wala hawamuombi ila Shetani aliye asi. Mwenyezi Mungu Amemlaani. Naye Shetani alisema: Kwa yakini nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili aliyo umba Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shetani kuwa ni mlinzi wake badala ya Mwenyezi Mungu, basi huyo amepata hasara ya wazi} [AN-NISAA: 117 – 119]. Aya hizi zinaonesha kuwa kubadilisha maumbile aliyoyatengeneza Mwenyezi Mungu ni jambo la haramu, kwa sababu ni kufuata amri za shetani na wafuasi wake kinyume na Mwenyezi Mungu na ni hasara kubwa, kitendo cha kujihasi kwa maana ya kuondoa korodani ni kubadilisha maumbile ya Mwenyezi Mungu na kwenda kinyume na maumbile yake ambayo amewaumbia watu basi hilo linakuwa ni haramu. Ama kuwa kwake kubadilisha maumbile yaliyoumbwa na Mwenyezi Mungu ni wazi, kwa sababu kuna uharibifu wa sehemu ya maumbile ya mwili bila ya muundo wa kisharia.
Imekuja katika tafsiri ya Aya Tukufu kuwa “Kubadilisha maumbile ya Mwenyezi Mungu” ni kuhasi, vilevile yamesemwa na zaidi ya mmoja katika wanachuoni waliotangulia wakiwamo miongoni mwao Masahaba na Taabiina waliokuja baada yao kama vile Ibn Abbas na Anas Ibn Malik R.A. pia Rabii Ibn Anas na Shahar Ibn Haushab. [Angalia tafasiri ya Imamu Tabariy, Jaamii Al-Bayan, 9/215 – 216 Ch. ya Taasisi ya Ar-Risala].
Amesema Imamu Nuru ya umma As-Sarghasy katika kitabu cha: [Al-Mabsout, 15/135 Ch. ya Dar Al-Maarifa]: “Kumhasi mwanadamu ni jambo linalokatazwa, nalo ni katika jumla ya mambo yanayo amriwa na shetani. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Nitawaamrisha, basi watabadili aliyoumba Mwenyezi Mungu} [AN-NISAA, 119].
Ama dalili katika Sunna takatifu: Ni Hadithi iliyopokelewa na Bukhari na Muslim katika vitabu vyao, kutoka kwa Ibn Masoud R.A. amesema: “Tulikuwa vitani pamoja na Mtume S.A.W. tulikuwa hatuna wanawake, tukauliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je tunaweza kujihasi? Mtume akatukataza kufanya hivyo”.
Amesema Al-Hafidh Ibn Hajar katika kitabu cha: [Fat-h Al-Bariy, 9/119, Ch. ya Dar Al-Maarifa]: “Ni katazo la kuharamisha kumhasi Mwanadamu bila uwepo wa tofauti yoyote baina ya Wanachuoni”.
Na imepokelewa pia kutoka kwa Saad Ibn Abiy Waqas R.A. amesema: “Mtume S.A.W. alimjibu Uthman Ibn Madhuun kuhusu kukata Korodani, lau angemruhusu basi tungejihasi”.
Amesema Imamu An-Nawawiy katika kitabu cha: [Sharhu ya Muslim 9/177 Ch. ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy]: “Kauli yake: Lau angemruhusu tungejihasi” maana yake: Lau angemruhusu kuwa mbali na wanawake na mengineyo katika ladha za dunia basi tungefanya kitendo cha kujihasi, ili kuondoa matamanio ya kutaka wanawake..... na hili linachukuliwa kuwa wao walikuwa wakidhani kwamba inafaa kujihasi kwa jitihada zao, lakini dhana yao hii haikuwa ya wote kukubaliana, kwani kitendo cha kuhasi mtu ni haramu, iwe ni kwa mtoto mdogo au mtu mkubwa.
Amepokea Imamu Ahmad katika kitabu chake Hadithi inayotokana na Jabir Ibn Abdillah R.A. amesema: Kuna kijana mmoja alikuja kwa Mtume S.A.W. akamuuliza: Je unaniruhusu nijihasi? Mtume S.A.W. akasema: “Funga na muombe Mwenyezi Mungu fadhila zake”.
Na amepokea Tabraniy katika kitabu chake cha Muujam Al-Babeer pia Baihaqiy katika kitabu cha Shuab al-Iman, na Abu Naeem katika kitabu Maarifat As-Sahabah kutoka kwa Uthman Ibn Madhuun R.A. amesema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi ni mtu ninayepata tabu na hali hii ya kutokuwa na mke nipe ruhusa ya kujihasi, je nijihasi? Mtume S.A.W. akasema: “Hapana, bali funga”.
Katika mapokezi mengine kutoka kwake pia kuwa Uthman R.A. alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, niruhusu nijihasi, Mtume S.A.W. akasema: “Ewe Uthman, hakika Mwenyezi Mungu ametubadilishia kwa utawa wa kati na kati wa usamehevu, na kutoa takbira katika kila jambo tukufu – kwa maana lenye nafasi ya juu – ikiwa wewe ni katika sisi basi fanya kama tunavyofanya”.
Imepokelewa pia na Ibn Abbas R.A. amesema: Kuna mtu mmoja alilalamika kwa Mtume S.A.W. kuhusu kutokuwa na mke, akasema: Je ninaweza kujihasi? Mtume S.A.W. akasema: “Hapana, si katika sisi mwenye kujihasi au kuwahasi wengine”.
Hadithi hizi kwa ujumla wake zimeonesha zuio la kufanya kitendo cha kuhasi na kuonesha uharamu wa kitendo hicho, kisha Mtume S.A.W. akatoa muongozo katika Hadithi nyingine ya kuhasi ambako ni halali kunakokubalika kisharia, na muongozo huo ni katika Hadithi iliyopokelewa na Ahmad katika musnadi yake kutoka kwa Abdillah Ibn Amru R.A. kuwa Mtume S.A.W. amesema: “Kuhasi kwa umma wangu: ni Kufunga na Kuswali Swala ya Kisimamo cha usiku”.
Na yanayopelekea uharamu pia ni kama ilivyo katika kumhasi binadamu ambako ni uhalifu na ni haramu, ni kulipiza kisasi kama vile kuua, kung’oa pua na viungo vyengine ambavyo vinapelekea hukumu ya kisasi. Amepokea An-Nasaaiy na Abu Dawud kutoka kwa Samrah Ibn Jundab R.A. kuwa Mtume S.A.W. amesema: “Mwenye kumhasi mtumwa wake basi na yeye tutamhasi, na mwenye kumng’oa kiungo chochote mtumwa wake nasi tunamng’oa”. Kufanya uhalifu ni jambo la haramu kwa kauli za wanachuoni wote ni sawa sawa uhalifu huo dhidi ya haki ya mtu yeye mwenyewe au mtu mwengine, na kwa ajili hiyo hivyo basi kujiua kumeharamishwa, vilevile mwanadamu kuharibu viungo vyake pasi na dharura kubwa ni kitendo kinachukiza na Sharia Takatifu.
Na mtazamo sahihi unaonesha hivyo pia. Anasema Imamu Ibn Bat-tal katika kusherehesha kwake kitabu cha: [Sahihi Al-Bukhari 7/169 Ch. ya Maktabat Al-Rashad – Riyadh]: “Kuondoa korodani ni jambo lililokatazwa, na hakuna uhalifu wa nafsi tofauti na kuizuia kwenye kitu kilicho halali kwake, kuizuia kwa kile kinachopelekea uhalifu ndani yake kwa kujiadhibu kwa kukata baadhi ya viungo vyengine vilivyo katazwa kufanya hivyo, hivyo ikathibiti kwa hili kuwa kukata sehemu ya viungo vya mwanadamu pasi na dharura kubwa inayopelekea kufanya hivyo ni haramu”.
Kauli ya kuruhusu kuhasi inagongana na makusudio ya kulinda kizazi ambayo ni sehemu ya makusudio matano ya Sharia ambapo Sharia ya mbinguni imekuja ili kulilinda kusudio hilo. Ameyasema hayo mwanachuoni Shihaab Ramly katika fatwa zake 4/220 chapa ya Al-Maktaba Al-Islamiya: “Mambo matano muhimu... lazima kuyalinda katika mila zote”. Ikiwa ni pamoja kulinda kizazi, ni Makusudio muhimu na ya msingi katika Makusudio Makuu ya Sharia, na ikiwa kuhalalisha kitendo cha uhasi ndani yake kunapalekea kupoteza kusudio hili, basi hilo linakuwa ni haramu.
Kama vile kuuhasi ambako ndani yake kuna madhara kwa mtu mwenyewe, na kanuni ya kisharia inayokubalika ni kuwa: “Madhara huondolewa” angalia kitabu cha: [Al-Ashbah wa An-Nadhair cha Imamu As-Suyutiy, uk. 86, Ch. ya Dar Al-Elmiya – Beirut], kwa kauli yake Mtume S.A.W.: “Hakuna kudhuru wala kujidhuru” Imepokelewa na Ibn Majah na Ahmad kwenye Musnadi yake kutoka kwa Ubadah Ibn Saamit na Ibn Abbas R.A.
Na hili ni tamko la wanachuoni wa mambo ya mila na Maimamu wa Dini, wameliweka wazi pamoja na tofauti za madhehebu yao, na kunukuliwa na wanachuoni wengi.
Amesema mwanachuoni Al-Zailai katika wasomi wa Abu Hanifah kwenye kitabu cha: [Tabyeen Al-Haqaiq 6/31 Ch. Dar Al-Kutub Al-Islaamy]: “Watu kufanya kitendo cha kujihasi...ni kama ushoga, ni wazi kuwa Mtume S.A.W. amekataza hilo, na kwa hivyo ni haramu”.
Na amesema Al-Hafidh Ibn Abdul Barr Al-Malikiy katika kitabu cha: [Al-Istidhkar, 8/433 Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya]: “Jopo la wanachuoni wa Hijaz na Kufah limeufanya kuwa Haramu ununuzi wa watumwa walio hisiwa na wasio kuwa hao, na wakasema: Lau wasingewanunua baadhi yao wasinge hasiwa, na wala hawajatafautiana kuwa kuhasiwa mwanadamu si halali na wala haifai na kufanya hivyo ni kama kuwafanya wanawake na kuwabadilisha maumbo aliyoyaumba Mwenyezi Mungu Mtukufu, vilevile baki ya viungo vyao vyingine na maeneo mengine ya mwili kinyume na utekelezaji wa adhabu”.
Amesema Imamu Al-Qurtwubiy Al-Malikiy katika kitabu cha: [Tafsiri ya Al Qutwubiy 5/391 Ch. ya Dar Al-Shaab]: “Ama kumuhasi mwanadamu ni tatizo, kwani pindi anapo hasiwa hufa moyo wake na nguvu zake kumwishia, kinyume na wanyama, na kumkata kizazi chake alichopewa amri ya kuoa na kuzaa kutokana nacho, kwenye kauli ya Mtume S.A.W.: “Oaneni mzaane, kwani mimi nitajifaharisha kwa wingi wenu kwa uma zengine Siku ya Kiama”. Kisha kitendo hiko kina maumivu makali huenda yakapelekea Umauti kwa mwenye kufanyiwa hivyo, na inakuwa ni kupoteza mali na kuondoa nafsi, na yote hayo ni mambo yaliyokatazwa, kisha katika hili ni kama kujifananisha na wanawake, na Mtume S.A.W. amekataza vitendo vya kujifananisha na wanawake, na kuhasi ni moja ya vitendo hivyo na ni mfanano huo.
Amesema Imamu Abu Al-Waleed Al-Baj Al-Malikiy katika kitabu cha: [Al-Muntakiy sherehe ya kitabu cha Al-Muwataa, 7/268 chapa ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy]: “Kumhasi mwanadamu ni haramu kama vile kumkata viungo vyake”.
Amesema Imamu Muhyiddeen An-Nawawy As-Shafiy katika kusherehesha kitabu cha sahihi Muslim 9/177: “Kumhasi mwanadamu ni haramu akiwa ni mtoto mdogo au mtu mzima”.
Amesema mwanachuoni Al-Buhutiy Al-Hanbaliy katika kitabu cha: [Kas-shaf Al-Qinaai, 5/495 Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya]: “Ni haramu kuhasi wanadamu kinyume na kisasi hata kama ni mtumwa”.
Amesema Imamu Ibn Hazm Al-Dhahiry katika kitabu cha: [Maraatibu Al-Ijmaa, uk. 157, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya]: “Wanachuoni wamekubaliana kuwa kuwahasi watu wa vita, watumwa na wengineo kinyume na kisasi na kuwafanya kama wanawake ni haramu”.
Ama madai kuwa Mtume S.A.W. aliwaruhusu kuhasi baadhi ya Masahaba, hayo ni madai ya uongo na uzushi hayana ukweli wowote kwake Mtume S.A.W. Na Hadithi iliyopokelewa na Imamu Bukhari kutoka kwa Abu Huraira R.A. kuwa amesema: nilimuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi ni kijana, na ninahofia nafsi yangu kuingia kwenye mambo ya haramu, wala sina mwanamke wa kumuoa, akaninyamazia, kisha nikarudia tena, akaninyimazia, kisha nikasema tena kama nilivyosema mara ya kwanza, akaninyimazia, kisha nikasema tena, Mtume S.A.W. akasema: “Ewe Abu Hurairah, wino umeshakauka kwa hayo unayokutana nayo, kwa hali hiyo jihasi au acha”. Katika mapokezi ya An-Nasaai ruhusa ya kutaka kujihasi, imekuja katika kauli yake: Nikasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni kijana ninaogopa kuingia kwenye uzinifu na sina uwezo wa kuoa mwanamke, je nijihasi? Mtume S.A.W. akampuuza, mpaka akarudia kuuliza mara tatu, akasema Mtume S.A.W.: “Ewe Abu Huraira, wino umeshakauka kwa hilo ambalo wewe unalo, kwa hali hiyo jihasi au acha”.
Hadithi hii Takatifu pamoja na usahihi wake kwa upande wa mapokezi, lakini si dalili kabisa kuwa Mtume S.A.W. alimruhusu Abu Huraira kujihasi, na hiyo ni kwa mambo yafuatayo:
Jambo la Kwanza: Mtume S.A.W. alimpuuza Abu Huraira wala hakumjibu mpaka akasisitiza kuulizia mara tatu, na pindi alipojibiwa kwa sura ya kukemea Mtume akasema kumwambia Abu Huraira: “kwa hali hiyo jihasi au acha” hiyari hii haiwezi chukuliwa kuwa ni sehemu ya uhalalishaji wa kuhasi au kujihasi, bali kusudio ni kutishia na kutoa ahadi mbaya, kama vile kauli yake Mola Mtukufu: {Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona munayo yatenda} [FUSWELAT: 40], na kauli yake: {Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae} [Al-Kahf, 29]
Amesema Al-Qadhiy Al-Baidhawiy: “Maana ya kuwa imehusisha yaliyokadiriwa na kujisalimisha kwake na kumwacha na kumpuuza ni sawa, kwani kile ulichokadiriwa kiwe cha heri au shari basi ni lazima kikufike, na kile kisichoandikwa basi hakina njia kwako ya kukipata. Na amesema At-Tibbiy: Ni uhusishaji gani niliutaja kwake na ridhika na makadirio ya Mwenyezi Mungu Mtukufu au acha niliyoyasema na uendelee na hali yako na ujihasi, inakuwa ni kitisho”.
Amesema Imamu Badruddeen katika kitabu Umdatul Qaariy 20/104: Kauli yake: “Jihasi” sura yake ni sura ya amri ya kuhasi, lakini hili ni mfano wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae} [AL-KAHF, 29], siyo amri ya kutaka kitendo, bali ni kitisho, na maana jumla: Ikiwa utafanya au hautafanya basi ni lazima kutekeleza makadirio.
Amesema Haafidh Ibn Hajar katika kitabu cha: [Fathul baary 9/119]: “Sio amri ya kutaka kitendo, bali ni kitisho, nayo ni kauli ya Mola Mtukufu: {Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae} [AL-KAHF, 29], na maana: Ikiwa utafanya au kutofanya ni lazima kuyatekeleza kadari, na wala hakuna ndani yake kupingana na hukumu ya kuhasi, na jibu ni kuwa: Mambo yote ni kwa kadari ya Mwenyezi Mungu tokea hapo kale, kuhasi na kuacha kuhasi ni sawa sawa, kwani ambayo yamekadiriwa ni lazima yatokee. Na kauli yake “Juu ya hilo” ni kuwa inafungamana na kadari, kwa maana: Jihasi hali ya kufahamu kwako kuwa kila kitu ni kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu na kadari yake, na wala sio ruhusa ya kuhasi, bali ndani yake kuna ishara ya kukatazwa hilo, kana kwamba amesema: Ikiwa utafahamu kuwa kila kitu ni kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu basi hakuna faida katika kujihasi.
Anasema Sandy katika kitabu cha: [Haaashiya yake ya Sunna ya An-Nasaaiy 6/59 Ch. ya Maktaba ya Uchapishaji Vitabu vya Kiislamu – Halabu]: “Wino umekauka” maana yake: Wino umekauka kwa kuandika hayo yaliyo upande wako, kwa maana: Imeandikwa kwako na kuamuliwa unayokutana nayo katika maisha yako, na yaliyokadiriwa hayabadilishwi kwa sababu, wala haipaswi kujibebesha sababu zilizo haramu kwa sababu hiyo. Ndipo Mwenyezi Mungu Anapoweka sababu au amelazimisha kwa kitu chingine, kwa kauli yake: “Jihasi kwa hali hiyo au acha” sio katika hali ya kupewa hiyari, bali ukemeaji kama vile kauli yake Mola Mtukufu: {Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae}[AL-KAHF, 29], kwa maana ikiwa utataka kukata kiungo chako bila ya faida na ukiwa utataka kiache. Na kauli yake: “Juu ya hilo hakuna kudhuru wala kujidhuru” kwa maana: Pamoja na kukutana na yaliyokadiriwa kwako.
Jambo la Pili: Ni kuwa Abu Huraira R.A. yeye mwenyewe hakufahamu jibu la Mtume S.A.W. kuwa kujihasi ni halali kwake, hakuwahi kufanya hivyo pamoja na kuwa alikuwa anasisitiza kwenye kutaka ruhusa ya kitendo hiko, bali ameishi mpaka akaja kumuoa Bibi Busrah binti Ghazawani dada wa Sahaba Attabah Ibn Ghazawani Al-Mazniy kiongozi wa Basrah. Angalia kitabu: [Al-Isabat fi Tamyeez Sahaba, 7/537 Ch. ya Dar Al-Jeel- Beirut].
Jambo la Tatu: Ni kuwa ufahamu huu ni kinyume na yaliyoelezwa na Sharrah Hadithi ya Qatiba, imenukuliwa huko nyuma mara nyingi maandiko yake na sherehe zake.
Jambo la Nne: Ikiwa tutakubali kuwa uwazi wa Hadithi unaonesha kufaa kitendo cha kuhasi, basi uwazi huu unakuwa ni wenye kugongana na Sharia na ujumla wake ambao unaonesha uharamu wa uhalifu huu, na kubainishwa maelezo yake, kama yalivyoelezwa sehemu yake katika elimu ya misingi ya Sharia.
Kisha baada ya hapo kitendo cha kuhasi sio kukata matamanio kama inavyodhaniwa, kwa sababu matamanio huzalika kwenye ubongo, pindi unapotokea msukumo wa kijinsia unaofasiriwa na ubongo na kupelekea ishara maalumu hapo mwanadamu anahisi kuibuka kwa hisia na utashi wa kutenda kitendo cha ngono.
Anasema Imamu Sarkhasiy katika kitabu Al-Mabsout, 10/158: “Kuhasi katika hukumu za ushahidi na mirathi ni kama mnyama dume, na kukata kiungo hicho ni kama vile kukata kiungo chingine chochote, na maana ya fitina haiondoki, mwenye kuhasiwa huenda akawa na uwezo wa kuingilia, na imesemwa: Ni mtu mkali zaidi kwenye kuingilia, kwa sababu kifaa chake hakikosi uwezo wa kuteremsha manii.
Anasema mwanachuoni Al-Kasaniy katika kitabu cha: [Badaai Sanaai 5/122 chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya – Beirut]: Utumwa na uhasi havikati matamanio, vilevile hali ya kushindwa kuingilia na kuwa na tupu mbili ya kiume na ya kike, ama utumwa ni wazi kabisa, ama kuhasi kwetu mwenye kuhasiwa ni mwanamume isipokuwa anafananishwa na mwanamke”.
Na amesema mwanachuoni Zailay katika kitabu cha" ]Tabyeen Al-Hakaik 6/20]: “Mtu aliyehisiwa ni mwanamume mwenye matamanio na anaingilia, ikasemwa: Ni mtu mwenye uwezo mkubwa sana wa kuingilia, kwa sababu ni kwamba uume wake haukuharibika kwa kuhasiwa na anakuwa ni kama mnyama dume”.
Pindi Sheikh Abu Salim Al-Ayyaashy Al-Malikiy alipotokewa kwenye safari yake ya kuzungumzia juu ya watu waliokuwa wanapatikana kwenye miji ya Makkah na Madinah – nao ni watu waliohasiwa miongoni mwao walizaliwa na hali hiyo na wengine walifanyiwa hivyo, akakaribia karibu na moja ya miji hiyo kwa lengo la kuhudumia sehemu pamoja na wanaotembelea mji huo – aliwaambia [1/462 Ch. ya Dar Sweden Abu Dhab]: “Bali baadhi yao ni wanaume wamefanya hivyo ili kujipa ladha zaidi kinyume na kuinglia. Sheikh mwingine alisema miongoni mwao walikuwa na wake watatu na wanne, angalia kitabu cha taarighiya hadhaariya, [uk. 24, Ch. ya Chuo Kikuu cha Umm Al-Quraa].
Anasema Al-Hafidh Ibn Jauzy, katika kitabu chake cha: [Kashf Al-Mushkil] miongoni mwa Hadithi zilizomo kwenye kitabu cha: [Al Bukhariy na Muslim, 1/1005 Ch. ya Dar Al-Watan – Riyadh], ni Hadithi hii: “Tumeona baadhi ya wajinga wa matukio ambao hukufanya kuipa nyongo Dunia katika ujana wao pindi hali ya kutokuwa na mke inapokuwa ngumu hujirudi wenyewe, na tulikuwa tumesikia baadhi ya watu wa zamani kuwa kuna mtu alijirudi mwenyewe kwa kumuonea haya Mwenyezi Mungu Mtukufu, angalia anachofanya mtu mjinga kwa watu wake, kitu cha kwanza kitakachosemwa kwenye hili: Hauna uwezo wa kufanya lolote isipokuwa ni ruhusa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na jambo hili wala halisemwi kwa kile alichoruhusu bali Mola amekiharamisha, kisha inapaswa kufahamika kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameliweka jambo hili kwa hekima zake nayo ni kupata kizazi, basi mwenye kusababisha kukatika kizazi basi anakuwa kinyume na Hekima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kisha miongoni mwa neema kwa mwanamume ni kuumbwa kwake kuwa mwanamume na wala hakufanywa mwanamke, ikiwa atajisababishia yeye mwenyewe basi atakuwa amechagua upungufu kwenye ukamilifu, kisha anakuwa anafanya kile kilichokatazwa, ikiwa atafariki katika hali hiyo basi atastahiki kuingia motoni, kisha anajiingiza kwenye shida isiyoelezeka kisha anaizuia nafsi yake na ladha ya haraka na kupata mtoto atakaye mkumbuka na kumtaja au kujipatia thawabu kwa mtoto huyo, kisha nasaba yake itaendelea kuungana kutoka kwa Adamu mpaka kwake ambapo atasababisha kukatika kwa nasaba hiyo, kisha atakuwa ameidhulumu nafsi yake na kuwa mbali na mategemeo yake, ikiwa uume wake utakatika basi matamanio yaliyopo kwenye moyo hayataondoka, kwani matamanio kwenye moyo yapo kama yalivyo na kufikiria matamanio hakukatiki, jambo la ajabu katika hilo ni kwamba mwenye zuhudi ya kijinga ambaye amesikia haya kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kile alichomwekea, lau Mwenyezi Mungu angetaka asingekiweka kitu hiki kwenye nafsi, Mwenyezi Mungu atukinge na ujinga kwani ujinga ni giza juu ya giza”.
Kwa maelezo yaliyotangulia yanaonesha wazi kuwa kitendo cha mtu kujihasi ni uhalifu ulio Haramu moja kwa moja kwa kuharamishwa ndani ya Sharia ya Kiislamu, kama vile si ufumbuzi wa kweli wa kukata matamanio, lakini ni matatizo makubwa kusikika mtu miongoni mwetu mwenye kudai vitendo hivyo vichafu ndani ya nchi za Waislamu na kuutangaza ubatili huu kati ya Waislamu, miito hii sio tu inagongana na Sharia ya Kiislamu bali ni mgongano pia na maumbile ya mwanadamu, na hilo lipo wazi ambapo hatukuwa tunafikiria kuwa hili linahitaji dalili, wala hatukuwa wenye kuingia kwenye kelele hizi lau kama maneno juu ya masuala haya yasingesemwa hadharani kwenye masikio ya watu na kuripotiwa na vyombo vya habari pamoja na kuenezwa na kutajwa sana kwenye ndimi za watu wasio na werevu ikiwa ni jaribio la kubandika ubatili wake na Sharia Takatifu pamoja na maneno ya wanachuoni, ndio ukaletwa uwazi wa majibu na ubainifu, kama alivyosema Mola Mutukufu: {Bali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na mara ukatoweka. Na ole wenu kwa munayo yazua} [Al-Anbiyaa, 18].
Tunatoa wito kwa Waislamu kujiletea uelewa wa kijamii wao kwa wao ambao utapelekea kurahisisha ndoa na kupunguza mahari pamoja na kuheshimu maisha ya ndoa.
Vilevile tunatoa wito kwa Taasisi na watu wenye uwezo kufanya juhudi kadiri ya uwezo wao katika mali za Mwenyezi Mungu ambazo amewamilikisha kutoa msaada kwa yule asiyepata uwezo wa gharama za kuoa, katika hilo kuna thawabu nyingi kwenye kufariji matatizo ya viumbe, na kueneza sababu za kuwawepesishia watu, na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wanao toa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishii simulizi wala udhia kwa walichokitoa, wana malipo yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika} [AL BAQARAH, 262].
Ama mwenye kutaka wepesi na upungufu ni juu yake kumtaka msaada Mwenyezi Mungu Mtukufu na kusubiri pamoja na kufanya kazi na kujitahidi katika kazi yake, aishughulishe nafsi yake kwa ibada na kupata uwezo mpya na kujifunza elimu yenye manufaa, ili Mwenyezi Mungu Amfanyie wepesi. Anasema Mola Mtukufu: {Na anaye mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea. Na humruzuku pasi na kutegemea. Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake} [AT TALAAQ, 2: 3].
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.