Umma- Sababu za Maangamizo katika Q...

Egypt's Dar Al-Ifta

Umma- Sababu za Maangamizo katika Qura’ni Tukufu

Question

Je, Qur’ani Tukufu ilitaja sababu za maangamizo ya Umma na ufisadi wake? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Hakika Uislamu una msimamo wake mtukufu kuhusu ufisadi wa Umma na maangamizo yake, na umbali wake kutoka katika njia nyoofo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama yafuatayo:
1- Majivuno ya mtawala, ujeuri wake na kuwadhalilisha watu wake: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi}. [AL QASAS 4]
2- Ari ya uongo ya kujenga na kutengeneza, na kisingizio batili katika kuwalinda watu; Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na Firauni akasema: Niachieni nimuuwe Musa, naye amwite Mola wake Mlezi! Mimi nachelea asije kukubadilishieni dini yenu, au akatangaza uharibifu katika nchi}. [GHAFER 26]
3- Qur’ani Tukufu imewashambulia makuhani na watawa kwa mashambulizi makali kwa sababu ya uhalilishaji na uharamishaji wao wa uwongo juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na utashi wao wa usaliti. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Wamewafanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi bin Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayo mshirikisha nayo}. [ATAWABA 31]
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Enyi mlio amini! Hakika wengi katika makuhani watawa wanakula mali za watu kwa njia batili na wanazuia Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu}. [AT TAWABAH 34]
4- Qur’ani Tukufu inatutahadharisha na kumiliki mali, Mwnyezi Mungu Mtukufu anasema: {Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri. Akijiona katajirika}. [AL ALAQ 6-7] Na Qur’ani inakielezea kisa cha Mwenye Mali pamoja na uduni wa chanzo chake mpaka kuufikia udhalimu kutokana na mali yake. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na miongoni mwao wapo waliomwahidi Mwenyezi Mungu kwa kusema: Akitupa katika fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao mema. Alipowapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka, na huku wakipuuza. Basi akawalipa unafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watakapokutana naye, kwa sababu ya kuwa walimkhalifu Mwenyezi Mungu katika yale waliyomwahidi, na kwa sababu ya kusema kwao uwongo. Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong'ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua sana ya ghaibu?} [AT TAWBAH 75-78].
5- Qur’ani Tukufu inawatahadharisha watu kwa kuchelewa kwao kupambana na udhalimu, na kughafilika kwao kuitamka haki hadharani, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanaoonewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anayetoka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anayetoka kwako}. [AN NISAA 75]
6- Qur’ani Tukufu iliwapa watu jukumu la kuondosha unyonge wao na udhalili walionao, na hayo yamo katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, anaposema: {Na wanapohojiana huko Motoni, wanyonge watawaambia walio jitukuza: Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, hamtuondolei sehemu ya huu Moto? Watasema walio jitukuza: Hakika sisi sote tumo humo humo! Kwani Mwenyezi Mungu kesha hukumu baina ya waja!} [GHAFER 47-48]
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
Rejea: Dkt. Mohammad Said Ahmad Al Mosaiar; Al Mujtama’ Al Methali fi Fikr Al Fasafiy na Mawqef Al Islamu Minhu, Al Qaherah, Dar Al Maaref, Tw.2, 1989. (Uk. 112-113)


 

Share this:

Related Fatwas