Mjadala wa Muswada wa Sheria Kuhusu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mjadala wa Muswada wa Sheria Kuhusu “Kuwalinda Wanawake na kuwaepusha na Unyanyasaji wa Kifamilia”

Question

Kutokana na barua iliyotufikia kutoka kwenu yenye nambari 918 ya tarehe 19/05/2010, iliyo na pendekezo la muswada wa sheria kuhusu “Kuwalinda wanawake na kuwaepushia Unyanyasaji wa kifamilia” ambapo ndani yake barua imependekeza baadhi ya sheria ambazo zinalenga kusimamisha vitendo vya Unyanyasaji dhidi ya mwanamke na kumlinda na aina zote za Unyanyasaji wa kifamilia dhidi yake na kulinda haki yake ya kuishi maisha bora, Mnauonaje muswada huu? 

Answer

Sifa zote ni za Mwenyezi Mungu, sala na salamu zimwendee Mtume wa mwisho naye ni Mtume Muhammad pamoja na jamaa zake na Masahaba zake na mwenye kumfuata kwa wema mpaka siku ya mwisho, na baada ya utangulizi huo:
Uislamu ni Dini ya huruma, Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuelezea kipenzi chake Mustafa S.A.W, kuwa ni rehema kwa walimwengu wote, na akasema: {Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote} [AL ANBIYAA: 107] na Sharia imesisitiza juu ya haki ya mtu mnyonge kuhurumiwa, na kumfanya mwanamke kuwa ni mmoja wa watu dhaifu, Mtume akasema: “Ewe Mwenyezi Mungu ninapata taabu kwenye haki za wanyonge wawili: Yatima na mwanamke” imepokelewa na An-Nasaai na Ibn Majah kwa mapokezi mazuri kama alivyosema Imamu An-Nawawy katika kitabu cha: [Riyadh Saliheen], na mwanamke ana haki zaidi ya kuhurumuwa kuliko mtu mwengine yoyote, kutokana na udhaifu wa mwili wake na mara nyingi ni mwenye kuhitaji mtu atakayesimamia mambo yake, hivyo basi Mtume S.A.W. aliwafananisha wanawake na kioo kwa wepesi na nguvu pamoja na udhaifu wa umbile, alimwambia Anjashah: “Kuwa makini ewe Anjashah, pole pole kwenye hivyo vioo”.
Wanachuoni Waislamu wamefahamu hilo na wakalitekeleza kwa utekelezaji wa hali ya juu mpaka zikawa ibara zao ambazo zimetengeneza mfumo wa kufikiri kwao kifiqhi: “Uke daima ni kushindwa hivyo kunahitaji usimamizi wa kudumu”.
Uislamu umemtaka mume kuifanyia wema familia ya mke wake, na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema kuwa maisha ya ndoa yanajengeka kwa msingi wa utulivu upendo na huruma. Anasema Mola Mtukufu: {Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri} [AR RUUM, 21].
Na Mtume S.A.W. akafanya vipimo vya kheri kwa waume vinasimama kwa ushirikiano wao mwema kwa wake zao, akasema Mtume S.A.W.: “Mbora wenu ni yule aliyebora kwa familia yake, na mimi ni mbora wenu kwa familia yangu” Hadithi hii imepokelewa na Tirmidhy kutoka kwa Bibi Aisha R.A.
Sharia imehimiza upole katika kurekebisha makosa, na Mtume S.A.W. akatoa wito wa kumtendea upole mwanamke katika mambo yote, akasema: “Hakika ya upole hauwi kwenye kitu isipokuwa hupendezesha na wala hauondolewi kwenye kitu isipokuwa huwa ni ubaya kwenye nafsi” Imepokelewa na Muslim Hadithi ya Bibi Aisha R.A.
Mtume S.A.W. hajawahi kumpiga mke wake hata mmoja, kutoka kwa Mama wa Waumini Bibi Aisha R.A. amesema: “Mtume S.A.W. hajawahi kupiga kitu kwa mkono wake hata siku moja, wala mwanamke wala mfanya kazi, isipokuwa katika kupigana jihadi kwenye njia ya Mwenyezi Mungu na wala hajawahi kulipiza kisasi hata siku moja isipokuwa kwa mwenye kukiuka kitu alichokiharamisha Mwenyezi Mungu, hapo hulipiza kisasi” Ni Hadithi iliyopokelewa na Imamu Muslim, na Mtume S.A.W. ni kigezo chema ambacho wanaume wanapaswa kuuiga mwenendo wake katika mtangamano na wake zake, kama Alivyosema Mola Mukufu: {Hakika nyinyi muna kigezo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana} [AL AHZAAB, 21].
Kupigwa mwanamke ndani ya Qur`ani kumetajwa sehemu moja tu kwenye kauli yake Mola Mtukufu: {Na ambao wanachelea kutoka katika utiifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikutiini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu} [AN NISAA 34], kutoka kwenye utiifu: Ni ukiukaji wa kijamii na kimaadili, unaomzuia mwanamke kutekeleza wajibu wake, na huo wajibu ni haki ya mume, kama ambavyo, wajibu wa mume unazingatiwa ni haki juu ya mke, katika ukiukaji huo wa kijamii na kimaadili Mwenyezi Mungu ametoa miongozo kwa wanaume yenye mbadala wa aina mbalimbali katika kuwanyoosha wake zao kwa mujibu wa mazingira kwa upande mmoja na kwa mujibu wa mazoea yaliyopo na utamaduni wa kimazingira ambao amekulia mwanamke na ambayo kwa mazingira hayo anakuwa ni mwenye kuathirika zaidi katika kumrekebisha kwa upande mwingine, kwa maana njia hizi mbadala haziainishwi kwa utaratibu, hivyo mwanamume anapaswa kushirikiana na mke wake kwa mawaidha, nayo ni maneno laini na kumkumbusha Mungu na haki zake ambazo Mwenyezi Mungu amezitaka kutoka kwake mwanamke, kama vile Sharia imehalalisha kwa mume kumuhama mke wake kwenye kitanda katika jaribio la mume la kumshinikiza ili asimame kwenye wajibu wake pasi na kumdhulumu wala kumfanyia uadui, kwa sharti la kutofikia kiwango cha kuidhuru nafsi ya mwanamke.
Ama hatua ya kupiga iliyotajwa katika Aya: Wanachuoni wamekubaliana kuwa sio kusudio hapa kumfanyia kero mke wala kumdharau, lakini hatua imekuja kuhalalisha baadhi ya hali pasi na ulazima na katika baadhi ya mazingira ambayo hayazingatiwi mfano wa kitendo hiki kuwa ni dharau kwa mke na kinyume na hivyo ni kero kwake, na hilo ni kuonesha kutoridhia mume na kuchukia kwake kuendelea mke kuacha wajibu wake, na hilo ni kwa kumpiga kipigo chepesi kwa njia ya kumkanya na kumpinga ambapo kipigo hiko kisiache athari, na inakuwa kwa kumpiga na mswaki wa mti na ule wa plastiki na mfano wa hivyo miongoni mwa vitu ambavyo kwa kawaida si vya kupigia. Maelezo haya yametoka na Ibn Jarir kutoka kwa Atwaa amesema: Nilimuuliza Ibn Abbas R.A: Ni aina gani ya kipigo kisicho jeruhi? Akasema: “Kwa mswaki na mfano wake”.
Kuna tofauti kubwa kati ya kupiga huku kwa mswaki pasi na kumletea maumivu na kati ya kutumia nguvu au kumchampa kwa fimbo au kumletea maumivu au dharau, wanachuoni wamesema kuwa kupiga huku – pamoja na kuwa kwepesi kusiko umiza – kunapaswa kuwa hatua ya mwisho inayoweza kufuatwa na mume, na kuwa haifai kumuondoka kitandani wala kumpiga kwa kudhania tu amehusika na ukiukaji kabla ya kutokea, ni haramu kipigo hiki kisichoumiza ikiwa atafahamu kuwa mke anaweza kujirekebisha kwa maelekezo, bali wameelezea uharamu pia ikiwa mume atafahamu kuwa kipigo hakitakuwa na faida katika kumrekebisha, au kinaweza kumletea madhara au kumuacha na alama, amesema Imamu Al-Khattab Al-Maliky katika kitabu cha: [Mawahib Al-Jalil, 4/14 – 16]: “Ikiwa anauhakika kuwa kipigo hakina faida basi haifai kumpiga, na katika kitabu Al-Jawahir: Ikiwa atakuwa na uhakika kuwa hatoacha tabia yake hiyo ovu isipokuwa ni kwa kipigo chenye kuogopesha basi haifai kumuadhiri, maelezo haya yamekubaliwa pia na Ibn Arafah”.
Bali wameelezea kuwa mume anapigwa na kutiwa adabu vilevile pindi anapokosea kwenye haki ya mke, Kama vile mume akamtoa bikira mke wake kwa kidole, amesema Imamu Dardeer katika kitabu sharh Saghir maelezo ya pembeni ya Sheikh Saawiy 4/392 chapa ya Dar Al-Maarif: “Kuondoa bikra kwa kutumia kidole ni haramu, hutiwa adabu mume kwa kitendo hicho”.
Wanachuoni wameelezea maana hii, miongoni mwao wamesema kuwa kumpiga mke haifai kwa kutumia fimbo na mfano wake, bali kunakuwa ni kwa mkono au mswaki tu ikiwa ni kumlaumu na kuonesha makemeo, kama ilivyotangulia kuelezwa na Ibn Abbas R.A., na imepokelewa na Abi Hatim katika tafasiri yake kutoka kwa Hassan Al-Basariy kuwa amefasiri kupiga huko kusiko jeruhi wala kuacha alama, na wala haifai kupiga huko kwa kusudio la kulipiza kisasi isipokuwa ni kwa lengo la kumuadabisha, wakasema kuwa inapaswa mpigaji kujiepusha kumpiga maeneo yenye hisia kali na sehemu muhimu ambazo kwa kuzipiga zinaonesha dharau, kama vile sehemu za usoni kichwani shingoni na sehemu za siri kwa kauli ya Mtume S.A.W.: “Pindi mmoja wenu anapopiga basi na ajiepushe kupiga sehemu za usoni” ni Hadithi iliyokubalika inatokana na Abi Hurairah R.A. wala haifai kupiga kunako sababisha kujeruhi wala kuleta maudhi kwa hali yoyote ile.
Na kwa maelezo hayo, kupiga kulikoelezwa kwenye Qur`ani na Hadithi, ukweli ni kuwa ni aina ya kuonesha makemeo kulaumu na kutoridhishwa na kitendo kilichotendeka, na kutajwa huko kwenye Qur`ani na Hadithi maana yake sio ndiyo ruhusa ya kupiga kwa kutumia fimbo au kumuadhibu kimwili, bali kuja kwake ni katika aina ya kupiga kwa kutumia mswaki ambao ukweli haukusudiwi kupigia kwa kiwango kinachokusudiwa kuonesha makemeo na kumlaumu.
Kupiga huku kumehalalishwa na Sharia kwa vigezo kwa baadhi ya mazingira ya kitamaduni ambayo mwanamke anahitaji hivyo na kuona yeye mwenyewe dalili za uwanaume wa mume wake, na mazingira haya ya kitamaduni watu wa Magharibi hawayafahamu wala kuyaangalia, na Qur`ani imekuja kwa wanadamu wote kwa zama zote na sehemu yote na kwa kila mtu mpaka siku ya mwisho, ikakusanya misingi yake aina zote za kimazingira na tamaduni mbalimbali ambazo pindi zisipochungwa kutapelekea kuyumba kwa uwiano wa utulivu ndani ya familia na kutishia kuharibika na kuporomoka, likawa hili kwa lengo la kunyoosha na kurekebisha.
Miongoni mwa yanayoonesha usahihi wa uelewa wa Aya na kuwa uhalali wa kumpiga mke sio upigaji tu katika hali zote ndani ya nyakati zote na mazingira yote ni kuwa imethibi kwa Mtume S.A.W, kuwa amekataza kupiga wanawake kwa kauli yake: “Musiwapige waja wa Mwenyezi Mungu”, alikuja Umar R.A. kwa Mtume S.A.W. akimlalamikia juu ya wanawake kuwaasi waume zao, basi Mtume S.A.W. akaruhusu kupiga ambako ni kwa sura ya makemeo. Baadhi ya Masahaba wakafahamu kimakosa kuwa hiyo ni ruhusa ya moja kwa moja ya kupiga, wake zao wakampelekea malalamiko yao Mtume S.A.W. katika hali hiyo Mtume aliwafokea Masahaba wake na kuwakasirikia na kuwaambia: “Watu wa nyumbani kwa Muhammad wamefikiwa na wanawake wengi wakiwalalamikia waume zao hayo sio kheri kwenu”. Impokelewa na Abu Dawud katika kitabu chake.
Hii inaonesha kuwa kupiga sio halali tu moja kwa moja, bali kumezuiliwa ikiwa kupiga huko ni kwa njia ya dharau au kumfanyia ubaya au kero, ndiyo sababu kubwa ya kuzuia Mtume S.A.W. mwanzoni kabisa, kisha akaruhusu kwa njia ya kukemea na kuonesha kukasirishwa kwa kutumia kitu cha kupigia kama vile mswaki na mfano wake, kisha mwisho Mtume S.A.W. alikasirishwa na vitendo vya baadhi ya Masahaba vya kuwakera na kuwatendea ubaya wake zao, na huondosha kheri kwa mwenye kufanya hivyo kwa mke wake, kwanza imeonesha katazo pili ruhusa tatu kukemea kitendo hicho kwa kuwa sehemu iliyohalalishwa na Sharia kwake mume ni kile kinachozingatiwa kwa mazoea ya kawaida kuwa ni kemeo na kuonesha kutoridhika, sehemu ya uharamu ni pale kunapokuwa na kero na ubaya kwa mke, na hili huenda likawa katika mazingira ambayo vitendo hivi havizingatiwi ni dharau wala ubaya, pamoja na hayo vitendo hivi havifanywi na watu wakarimu.
Amesema Twahir Ibn Ashuur katika tafasiri yake ndani ya kitabu cha: [At-Tahrir wa Tanweer 5-41 – 42 chapa ya Dar Sahanuun – Tunisia]: “Mtazamo wangu mimi ni kuwa athari hizo na habari hizo zenye kubeba uhalali ni kuwa zimesambazwa na mazoea ya baadhi ya matabaka ya watu au baadhi ya makabila, kwani watu ni wenye kutofautiana katika hilo, watu wa mashambani miongoni mwao hawazingatii kumpiga mwanamke ni unyanyasaji, wala kuzingatia kuwa ni unyanyasaji kwa mwanamke…hakuna ubaya ni ruhusa kwa watu wasiozingatia kupiga wake ni sehemu ya madhara wala si jambo la aibu wala uzushi katika maisha ya kifamilia, wala wanawake hawahisi kiwango cha kukasirishwa kwa waume zao kuwa ni sehemu katika hayo”.
Kama vile inafaa kwa kiongozi kuweka vigezo kwenye halali hii na kuwazuia waume kupiga wake wakati wa kutumika vibaya pamoja na kuwepo na adhabu kwa mwenye kutenda (Sharia imeruhusu kwa kiongozi, halali kuiwekea vigezo kwa masilahi) ambapo baadhi ya waume wanachukua ni kiegemeo cha kupiga kwa kujeruhi, au kushushia hasira zao na ulipizaji wao kisasi na wala sio kwa lengo la kurekebisha, mwisho wake hutokea mambo yasiyo mazuri ikiwa ni pamoja na kuenea kwa roho za uadui katika maisha ya kifamilia, kwa sababu hiyo kiongozi anapaswa kuzuia ili kukinga madhara ya baadaye, au kutoruhusu kabisa ikiwa ni kama njia ya kurekebisha kama ilivyo hivi sasa kwenye mazingira mengi ambapo kupiga mara nyingi kumekuwa ni njia ya kuadhibu mwili bali wakati mwengine ni kulipiza kisasi, na hili ni haramu bila tofauti yoyote kwa wanachuoni.
Amesema Twahir Ibn Ashuur kwenye kitabu hiko hiko 5/44: “Ama kupiga ni jambo hatari na kuainisha kwake ni jambo gumu…. Ambapo Jopo la wanachuoni wameliwekea vigezo vya usalama kutokana na madhara, na kufanyika kitendo hicho cha kupiga kwa watu wasiozingatia kupiga ni dharau na madhara kwao, hivyo tunasema: Inafaa kwa viongozi pindi wanapojua kuwa wanaume hawafanyi vizuri kuweka adhabu za kisharia sehemu hizo, bila ya kuwa na kikomo adhabu hiyo, na kuwatangazia kuwa mwenye kumpiga mke wake ataadhibiwa, lengo ni kutoongezeka mambo ya madhara kati ya wanandoa na hasa kwa kuwepo udhaifu mkubwa”.
Hii ndiyo maana iliyoelezwa na wanachuoni ya kuzuia kupiga, kama alivyosema mfasiri mkubwa Atwaa Ibn Aby Ribaha – katika yale yaliyonukuliwa na Kadhi Ibn Al-Araby Al-Malikiy katika kitabu cha: [Ahkam Al-Qur`an 1/536 chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah] – ambapo amesema: “Asimpige hata ikiwa amemuamrisha na kumkataza bila ya kumsikiliza, lakini atamkasirikia” wakaitolea maelezo Aya kwa maana ya kuonesha kutoridhishwa, na kukubalika hilo kwa wanachuoni wote, amesema Ibn Al-Faras: Wamepinga Hadithi iliyopokelewa na amri ya kupiga, imenukuliwa kutoka kwa Twahir Ibn Ashuur katika tafasiri yake 5/43.
Hakuna shaka kuwa kupiga kwa kujeruhi au kutumia fimbo au kuadhibu kimwili (Ambako kunafahamika kama utumiaji nguvu kifamilia) ni haramu kwa kauli moja ya wanachuoni, ni lazima kwa watu wote kusimama dhidi ya vitendo hivyo, na kuendeleza matumizi ya nguvu dhidi ya mke hakuna uhusiano na Uislamu, isipokuwa vyanzo vya Sharia kwa Waislamu vinahimiza huruma na upendo katika maisha ya ndoa wala havilinganii kwa hali yoyote ile kupiga wanawake na kuwadhulumu. Mwenyezi Mungu Anasema: {Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri} [AR RUUM: 21], na wanachuoni Waislamu wanasimama dhidi ya vitendo hivi vya kupiga na kutumia nguvu, na Mtume S.A.W. anabainisha kuwa uhusiano kati ya mwanamume na mwanamke unasimama kwa msingi wa upendo na huruma, na msingi huu unapingana kabisa na kitendo cha kupiga na kuleta kero na adha, kwa sababu hiyo Mtume S.A.W. anapinga vikali na anasema: “Hivi mmoja wenu atampiga mke wake kama vile anavyompiga mtumwa kisha usiku anamuingilia?” ni Hadithi imetokana na Bukhary katika sahihi yake na Baihaqy katika sunani yake kubwa na tamko lake hilo, katika hilo kuna jibu kwa mwenye kudhania kuwa Uislamu umemdharau mwanamke na mwanamume kuhalalishiwa kumpiga.
Asili katika Sharia ni haramu kuleta maudhi ya aina yote, Amesema Mola Mtukufu: {Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake pasi na wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhuluma kubwa na dhambi zilio wazi} [AL AHZAAB 58], na amesema Mtume S.A.W. katika hija ya kuaga: “Je nikufahamisheni nani Muumini? Ni yule watu wanakuwa na amani naye kwenye mali zao na nafsi zao, na Mwislamu ni yule mwenye kuwasalimisha watu kutokana na ulimi wake na mkono wake” imetokana na Imamu Ahmad katika kitabu chake, na Ibn Habban katika sahihi yake, na wengineo. Na amesema Mtume S.A.W.: “Mgongo wa Muumini ni wenye kulindwa isipokuwa kwa njia za haki” imepokelewa na Twabrany katika Muujab Al-Kabiir ni Hadithi inayotokana na Ismah Ibn Malik Al-Khatmiy, na kuiweka Imamu Bukhariy kwenye kitabu chake kwenye mlango wa Mgongo wa Muumini ni wenye kulindwa isipokuwa katika adhabu au haki.
Amesema Al-Hafidh Ibn Hajar katika kitabu cha: [Fat-h Al-Bariy 12/85 chapa ya Dar Al-Maarifa]: “Kulindwa, maana yake ni kulindwa na kuzuiliwa kutofanyiwa maudhi, na kuali yake: Isipokuwa katika adhabu au haki, kwa maana hapigwi wala kudhalilishwa isipokuwa kwa njia ya utekelezaji wa adhabu kuadhirishwa na kutiwa adabu”. Na katika yanayofahamika ni kuwa haya yanasimamiwa na mamlaka zinazosimamia sheria na mfumo na wala si watu wa kawaida.
Na yale yanayotokea kwa baadhi ya jamii za Kiislamu katika mambo hayo ni matokeo ya kutowajibika kwa waume na mafunzo ya Dini yao, wala haifai kunasabishwa matendo yao hayo na Uislamu wala hakuna uhusiano na mafundisho ya Uislamu kwa ukaribu wala kwa umbali, na sheria za maisha ya ndoa zinazofanya kazi ndani ya nchi za ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa na zinazotokana na Sharia ya Kiislamu, zinatia hatiani vitendo vya matumizi ya nguvu dhidi ya mke, na kufanya hilo ni madhara na kumpa mke haki ya kutaka fidia ya uhalifu na kinafsi na anapewa haki katika kutaka talaka pamoja na kuchukua haki zake kamili pasi na upungufu.
Imekuja katika makubaliano ya familia katika Uislamu, ambayo yamefikiwa na kamati ya Kiislamu ya kimataifa kwa ajili ya mwanamke na mtoto na kuandaliwa na kamati inayoundwa na wanachuoni wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu miongoni mwao akiwemo Mufti wa Misri uk. 50: “Haifai – kwa tofauti yoyote ile kati ya wanandoa wawili – kukimbilia kutumika nguvu ikiwa ni kukiuka vigezo vya Sharia vilivyowekwa, na mwenye kwenda kinyume na zuio hili anakuwa ni mwenye kuhusika na adhabu za kiraia na za kijinai”.
Na imekuja katika kipengele cha 6 cha sheria nambari 25 ya mwaka 1929 iliyofanyiwa marekebisho na sheria nambari 100 ya mwaka 1985: “Ikiwa mke atadai kufanyiwa madhara na mume kwa kiasi ambacho uhusiano wao hauwezi kudumu basi inafaa kwake mwanamke kutaka kwa kadhi kutenganisha ndoa yao”.
Na mfano wa kisheria kwenye madhara haya ambayo yanaruhusu kuachana: Ni pamoja na mume kufanya uadui kwa mke wake kwa kumpiga au kumtukana:
Imekuja hukumu ya mahakama ya rufaa ya Misri: “Ikiwa utiifu ni haki ya mume kwa mke wake basi ni kwa sharti ya mume kuwa muaminifu kwa mke na mali za mke, hakuna utiifu kwa mume ikiwa mume amekusudia kumdhuru mwanamke, kwa kumfanyia ubaya wa kauli au kitendo au ameshikilia mali za mke wake kinyume na haki”.
Rufaa nambari 116 ya mwaka 55 katika Sharia za ndoa, kesi ya tarehe 24/6/1986.
Ama kuhusu muswada wa sheria inayopendekezwa: Tunaona kuna haja ya kurudia tena kuandaliwa kwake – sura yake na maudhui – ili iende sambamba na jamii ya Kimisri na asili ya uhusiano wake wa kifamilia, ambapo asili ya uhusiano wa kifamilia katika jamii yetu unatofauti sana na ile ya Magharibi, kama vile ndani yake kuna muingiliano wa misingi kati ya mamlaka za mahakama na serikali ya utendaji, na kutenganishwa kati ya mamlaka hizo na kuondolewa muingiliano wa misingi hiyo ni katika nukta muhimu ambazo ni lazima kuangaliwa wakati wa kutengeneza sheria.
Na yafuatayo ni baadhi ya maelezo kwenye pendekezo hili:
1- Imekuja kwenye kipengele kinachopenedekezwa nambari 6: Katika kuelezea ufafanuzi wa uhalifu wa matumizi ya nguvu wa kifamilia kuwa: “Ni kitendo cha kutumia nguvu kinachofanywa kwa msingi wa kijinsia, na kupelekea kero au matatizo ya kimwili au nafasi kwa mwanamke, ikiwa ni pamoja na kitisho kwa kitendo kama hiki, au kutenza nguvu au kuzuiwa kwa nguvu uhuru na mmoja wa wanafamilia kutokana na mamlaka au uongozi au uhusiano na mwenye kufanyiwa uadui”.
- Uelewa huu hauainishi “kitendo cha utumiaji nguvu” kwa undani ambapo itawezekana kurejea uelewa huo wakati wa kutekeleza, kama vile katika ufahamu na uelewa wa “matumizi ya nguvu kifamilia” kwa kitendo cha kutumia nguvu ni tafasiri ya kitu hicho hicho, hii ni nafasi inapaswa kuachwa kwenye muundo wa sheria, na yawezekana kuacha hilo kwa kusema kwa mfano: “Uadui wowote ule”.
- Kigezo cha matumizi ya nguvu kwa msingi wa jinsia hakina maana, bali kunahitajika kuachwa kwa yeyote.
- Pamoja na kuweka wazi juu ya uhusiano kati ya wanandoa wawili pindi unapokuwa umeimarika, basi haizingatiwi kila uhusiano wa kindoa pasi na utashi wa mke ni uporaji wa kindoa au matumizi ya nguvu dhidi ya mwanamke, hii ni katika sifa ya ndani yenye mgongano, na wala sio katika sifa za wazi ambazo inawezekana kuchukulia dalili.
- Vilevile kwa upande wa msamiati “uhuru” katika kipengele hiki, hakija ainisha uelewa wake na wala hakuna vigezo vinavyoweka wazi sura yake.
2- Imekuja kwenye kipengele pendekezwa nambari 8 katika maelezo juu ya hatua ambazo zinafanywa na tume husika ya kupokea maoni kuwa miongoni mwa hatua hizi: “kuwawezesha watoto kutoa kauli zao”.
Inafahamika kuwa ugonvi wa wazazi wawili ni hatari sana kwa watoto kimalezi kinafsi na kijamii, kama inavyokubalika kisharia kuwa watoto ushahidi wao hauchukuliwi kama haujaunganishwa na dalili inayomridhisha hakimu, ambapo pendekezo la sheria linataka kuifanya hii tume husika kama vile mamlaka ya kimahakama kwa kusimamia hatua za kiutendaji ambazo wanazijengea kwenye uchunguzi wake.
Asili ya kutokubalika ushahidi wa watoto ni kauli ya Mola Mtukufu: {Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu} [AL BAQARAH, 282], na imekuja kwenye Hadithi iliyopokelewa na Abu Daud katika suna yake kutoka kwa Bibi Aisha R.A. kuwa Mtume S.A.W. amesema: “Imeondoshwa peni kwa watu wa aina tatu: Mtu aliyelala mpaka atakapo amka, mwendawazimu mpaka apone na mtoto mdogo mpaka atakapokuwa”.
Mtoto mdogo kwa asili pamoja ni mkweli isipokuwa yeye ni bado hajakuwa mtu wa kubeba amri za Mungu, huenda akamezeshwa maneno na akameza, na anaweza kuelemea upande mmoja, lakini pia anaweza kuwa na upendeleo huu kwa kupewa kitu chenye kuonekana au kisichoonekana.
Wanachuoni waliokataa ushahidi wa mtoto ni pamoja na – watu wa Imamu Malik na baadhi ya watu wa Imamu Hanbal – wameweka sharti ya kuwa katika uhalifu wa kujeruhi au kuua, na watoe ushahidi kabla ya kuondoka sehemu ya tukio, na wala asiingie kati yao mtu mzima, angalia: [Sharhu ya Al-Kharshiy kwenye Fiqhi ya Malik, 7/196, pia kitabu Al-Insaf cha Mardawy katika Fiqhi ya Imamu Hanbal 12/37, kanuni za kifiqhi cha Ibn Juzay, 1/264, chapa ya Dar Al-Fikr]
Na kwa maelezo hayo kuyatumia maneno ya mtoto mdogo katika hali kama hizi inakuwa ni kwa upande wa udhibiti na wala sio upande wa ushahidi.
3- Imekuja kwenye kifungu kinachopendekezwa nambari 8 kuwa miongoni mwa hatua ambazo zinachukuliwa na tume iliyotajwa: “Kuchukua mazingatio yanayohitajika ili kumuweka mbali mtuhumiwa wa nyumba ikiwa itathibiti kuwa uwepo wake umekuwa ni hatari kwa aliyefanyiwa jinai….nk”.
Kipengele hiki kinahitaji maelezo ya kina na vigezo maalumu ili kutodhuru upande wowote, kwa sababu kutouzingatia upande wa mmiliki wa nyumba huenda kukawa ni msukumo kwa mwanamke kuwa na madai batili kwa mwanamume kwa lengo la kumtoa kwenye nyumba, na huenda ikaibua hisia mbaya kwa sababu ya kuingia kwenye makosa kutokana na matokeo hayo, na kuna hali nyengine inayokubalika kwa upande wa vitendo inawezekana kutengenezwa ikawa inakubaliana na zama pamoja na wakati, pasi na kupelekea uadui kwenye miliki ya yeyote.
4- Imekuja kwenye kipengele cha 10: “Kuzuiwa mtuhumiwa kuwa na mawasiliano na mtendewa uhalifu ni sawa sawa nyumbani au sehemu ya kazi”.
Ni lazima kuwa na vigezo vya kuzuia mawasiliano haya kwa sababu ya kuzuia madhara, ama mawasiliano ya moja kwa moja kwa lengo la kutaka jambo zuri haizuiliwi, wakati mwingine huwa mawasiliano si ya moja kwa moja kupitia kati kati ya hukumu mbili zilizotajwa kwenye kauli yake Mola Mtukufu: {Na mkichelea kutakuwepo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutoka jamaa za mume, na muamuzi kutoka jamaa za mke. Wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu atawawezesha. Hakika MwenyeziMungu ni Mjuzi Mwenye habari} [AN NISAA, 35], jambo hilo pia halijazuiwa.
5- Imekuja kwenye kipengele pendekezwa nambari 12 kuwa upande wa utawala unalazimika kutoa huduma, na miongoni mwa huduma hizo ni: Kuongozea idadi ya sharti ambazo zitamlinda mwanamke kwenye hati ya ndoa, ikiwa ni pamoja na: Haki ya kujifunza, haki ya kufanya kazi, na haki yake kutoolewa mwanamke mwingine isipokuwa kwa kukubali kwake mke huyo kimaandishi.
Masharti haya pamoja na kuwa ni haki ya mwanamke kumwekea mumewe wakati wa kufunga ndoa, isipokuwa masharti hayo yenyewe hayana uhusiano wowote na vitendo vya kutumia nguvu dhidi ya mwanamke muhusika, yametajwa kwenye sheria ya kwamba hayana umuhimu.
Mwisho: Ofisi ya Mufti wa Misri inatoa wito kwa watungaji wa sheria wakati wa kutekeleza jukumu hilo kuwaangalia walio wengi ndani ya jamii na wala sio kuwaangalia wachache, na pia wayachunge mambo mengi yenye masilahi kwa familia pindipo yanapokuwa hayakujumuishwa na mfano wake, na kufahamu ambayo yanaweza kuzalika kutokana na sheria hizi ikiwa ni pamoja na athari za pembeni zitakazoidhuru jamii mpaka kuondoshwa kwake kutakapokamilika.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.


 

Share this:

Related Fatwas