Kuvikufurisha Vikundi vya Kidini Vinavyobeba Silaha
Question
Baadhi ya watu wanaeneza habari za kukufurisha kwa vikundi vya kidini vinavyotuhumiwa kubeba silaha na kuzitumia katika maandamano dhidi ya jeshi na polisi; na dalili yao ni Hadithi inayosema: "Yeyote anayeshika silaha dhidi yetu sio miongoni mwetu," Wanasema kwamba silaha hizi zinabebwa kwa ukweli sio kwa majazi. Kwa kukosekana kwa dalili ya moja kwa moja, na asili ya maneno ni ukweli, na kisichohitaji tafsiri huchukua nafasi ya kwanza kuliko kile kinachohitaji tafsiri, kwa hivyo, je, ufahamu na maagizo haya ni sahihi na ni sawa?
Answer
Sifa zote njema ni za Allah pekee, na Sala na Salamu ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu, na pia juu ya jamaa zake na maswahaba zake, na juu ya wale wanaowafuata kwa mpaka Siku ya Malipo.
Kukufuru ni kukana au kukataa mojawapo ya misingi ya kidini, au kufanya kitendo kilicho kinyume na mafunzo ya Uislamu; Imamu Ibn Hazm anasema katika kitabu cha: [Al-Ihkam fi Usul Al-Ahkam, 1/49, 50, Dar Al-Afaaq Al-Jadidah]: “Kukufuru maana yake katika lugha ni: kufunika ... nayo katika dini ni: sifa ya mtu anayekataa kitu ambacho Mwenyezi Mungu ameamuru kukiamini, baada ya kutoa hoja juu yake, kwa kumfikia ukweli, kwa moyo wake bila ulimi wake, au kwa ulimi wake bila moyo wake, au kwa vyote viwili. Au alifanya kitendo, ambacho matini ilitaja kwamba kitendo hicho kinasababisha kukufuru, na haijafichwa kwamba hukumu juu ya watu haijaambatanishwa na kitu chochote isipokuwa juu ya sura yao ya nje. Ama mtu aliyekataa kwa moyo ambaye anaonesha Uislamu, inatosha kutoka kwake mambo yanayodhihirika tu, na hatafuti siri yake, na ukafiri wake uko tu kati yake na Mwenyezi Mungu. Imamu Taqi Al-Din Al-Subkiy anasema katika Fatwa zake (2/586, Dar Al-Maaref]: “Kukufurisha ni hukumu ya kisheria, ambayo sababu yake ni: kuukana Ubwana, au Upweke, au Ujumbe, au neno au kitendo, ambacho Mwenyezi Mungu amekihukumu kuwa ni kukufuru, hata akiwa mtu huyo sio mwenye kukataa.”
Hukumu ya ukafiri kwa Mwislamu mmoja inajumuisha athari ambazo ni hatari sana. Zikiwemo: kwamba mahakama inaweza kumpitishia adhabu ya kifo, na kwamba hairuhusiwi kwake kuoa mwanamke mwislamu au kumuweka kama mke wake, badala yake analazimika kutenganishwa kati yao, na kwamba hana uangalizi juu ya Mwislamu, na kwamba kama akifa, haoshwi au kuswaliwa na Waislamu na hazikwi katika makaburi ya Waislamu, na kwamba hakuna urithi kati yake na jamaa zake ambao ni Waislamu, na kwamba anastahili ghadhabu na laana ya Mwenyezi Mungu na adhabu ya milele ya moto wa Jehanamu.
Kwa kuwa hukumu ya ukafiri kwa mtu aliyepewa ni hatari sana, Sheria imeonya dhidi ya kujihusisha nayo bila dalili au uthibitisho wa wazi; Kwa sababu ukafiri ni hukumu ya kisheria, basi hairuhusiwi kuupitisha kwa mtu isipokuwa kwa dalili ya kisheria. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Sema: Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya dhaahiri na ya siri, na dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asicho kiletea uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua.” [AL A'RAAF: 33]; kumkufurisha yule ambaye hastahili kukufurishwa ni miongoni mwa udhalimu; Kwa sababu dhuluma ni kuvuka kikomo, na aina hii ya kukufurisha huenda ikawa inavuka kikomo.
Na Mwenyezi Mungu alisema: “wala msimwambie anaye kutoleeni salamu: Wewe si Muumini;” [AN NISAA: 94] Imamu Al-Qurtubi alisema katika tafsir yake [5/338, Dar Al-Kutub Al-Masriyah]: “Hiyo ni, usimwambie yule ambaye alijisalimisha kwenu na kudhihirisha wito wenu: Wewe sio muumini. Ikasemwa: Amani. Msemo wake: Amani iwe juu yako, na inahusu wa kwanza; Kwa sababu salamu yake na salamu ya Uislamu ni ishara ya utii na unyenyekevu wake.
Na imepokelewa kutoka kwa Maimamu wawili - na maneno hayo ni ya Imamu Muslim – kutoka kwa Abdullah Ibn Omar, R.A., kwamba Mtume, S.A.W., alisema: “Yeyote anayemwambia ndugu yake: Ewe kafiri, basi mmoja wao atakuwa ameupata ukafiri huo, ikiwa ni kama alivyosema, au utarudishwa kwake.”
Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhariy kutoka kwa Abu Dharr, R.A., kwamba alimsikia Mtume, S.A.W. anasema: "Mtu hamshtaki mtu kwa uasherati, wala hamshutumu kwa ukafiri, isipokuwa unamrudia yeye mwenyewe, ikiwa mwenzake siyo kama alivyodaiwa.”
Imam Al-Nawawiy alisema katika kuelezea Hadithi ya Imamu Muslim [2/49, 50, Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabi]: “Katika tafsiri ya Hadithi kuna maana zaidi ya moja: ya kwanza ni kwamba imeelezewa juu ya hali ambayo haiwezekani kufanywa, na katika hali hii mmoja wao atapata ukafiri. Na ya pili: maana yake ni: tuhuma yake kwa ndugu yake na dhambi ya ukafiri wake inarudishwa kwake. Ya tatu ni: kwamba inaelezea Khawarij ambao wanawakufurisha waumini, na maoni haya yalipitishwa na Kadhi Iyadh, Mwenyezi Mungu amrehemu, kutoka kwa Imamu Malik Ibn Anas, na mapokezo hayo ni dhaifu, kwa sababu madhehebu sahihi iliyochaguliwa ambayo wengi na wachunguzi walisema: kwamba Khawarij hawakufuru, kama watu wote wenye uzushi. Maana yake ni kwamba hii inasababisha ukafiri, na hiyo ni kwa sababu dhambi - kama walivyosema - zinasababisha ukafiri, na inaogopwa kwa mwenye madhambi mengi kwamba atapata ukafiri, na maana ya tano: Inamaanisha kuwa ukufurishaji wake umerejeshwa kwake, kwani siyo iliyochaguliwa ni ukweli wa ukafiri, bali ni kukufurisha tu, kwa sababu mtu yule amemtuhumu ndugu yake ambaye ni muumini kwa ukafiri, hali hii ni kana kwamba amejikufurisha mwenyewe, labda kwa sababu alimkufurisha mtu kama yeye, au kwa sababu alimkufurisha mtu ambaye ni kafiri na anayeamini ubatilifu wa dini ya Uislamu, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi”.
Haiwezekani kumweleza mtu maalumu kuwa ni kafiri isipokuwa baada ya kuwapo kwa masharti na kutokuwepo kwa vizuizi, kwani jambo linaweza kuwa lenyewe ni ukafiri, lakini haiwezekani kumwelezea mtu mwingine kwamba ni kafiri kwa sababu ya kupoteza kwa baadhi ya masharti hayo - kama kukalifisha kwa mfano - au uwepo wa kizuizi kinachozingatiwa - kama ujinga na tafsiri kwa baadhi ya hali-.
Kuhusu suala hilo, Sheikh Ibn Taymiyyah anasema katika kitabu cha: [Majmuu 'Al-Fatawa, 7/619, Mujamaa al-Malik Fahd]: “Pengine kauli ni ya ukafiri kama kauli ya Jahmiyyah wanaosema kwamba: Hakika Mwenyezi Mungu hasemi wala haoni katika Akherah; Lakini anaweza kuwaficha baadhi ya watu kuwa ni makafiri, basi atamkufurisha yule aliyemtuhuma mwenzake kwa ukafiri, kama walivyosema Watu wema waliotangulia kwamba yeyote aliyesema: Qur'ani imeumbwa ni kafiri, na anayesema kuwa Mwenyezi Mungu hasemi wala haoni katika Akherah, basi yeye ni kafiri, na hairuhusiwi kumkufurisha mtu maalumu mpaka hoja itakapothibitishwa dhidi yake ... Kama yule anayekataa uwajibu wa Sala na Zaka na aliyehalilisha pombe na uzinzi na kufasiri maana yake kwa maana isiyokusudiwa. Kuibuka kwa hukumu hizi miongoni mwa Waislamu ni jambo kubwa kuliko kuonekana hizi. Kama aliyekosea kufasiri katika mambo hayo, hahukumiwi kuwa kafiri mpaka baada ya kupewa taarifa na baada ya toba yake; kama walivyofanya Maswahaba kwa watu waliohalalisha pombe, vinginevyo ni bora na inafaa zaidi.”
Na Sheikh Ibn Taymiyyah akasema katika kitabu cha: [Al-Masa’il Al-Mardiniya, uk. 155, Dar Al-Falah]: “Maneno ambayo anayeyasema atakuwa ni kafiri, inawezekana kuwa mtu hajajulishwa na matini ambazo zinalazimisha ujuzi wa ukweli, na inawezekana mtu yule akawa anazijua matini hizi lakini hazijathibitishwa kwake, au hakuweza kuzielewa vizuri, na labda mashaka yametolewa kwake na kwa hivyo Mwenyezi Mungu atamsamehe, basi yeyote kati ya waumini anaefanya bidii ya kumtafutia ukweli na akakosea, basi Mwenyezi Mungu atamsamehe makosa yake hata kama yatakuwa mengi, ikiwa katika masuala ya kinadharia au ya vitendo. Hivyo ndivyo vilivyochaguliwa na masahaba wa Mtume, S.A.W., na maimamu wa Uislamu, kisha Sheikh Ibn Taymiyyah akasema: “Madhehebu ya maimamu yanategemea hivyo”.
Vivyo hivyo, ikiwa kitendo cha Muisilamu au msemo wake unazunguka baina ya maana nzuri na ambayo ni mbali na maana mbaya ambayo ni karibu, hufahamika maana nzuri hata ikiwa iko mbali, kwa mujibu wa uhakika wa uislamu wake, na kwa kumfikiria kuwa nia yake ni njema, na ili kuepukana na kuingia kwenye utata wa kuwakufursha wengine bila ya haki.
Imamu Abu Hamid Al-Ghazaliy anasema katika kitabu cha [Al-Iqtisad fi Al-‘Etiqad, uk. 135, Dar Al-Kutub Al-Elmiyya]: “Inayopaswa kutegemewa ni: Jihadhari na kufuru kadiri inavyowezekana, kwani kuhalalisha umwagaji damu na kuwaibia pesa wanaosali kwa kuelekea kibla wanaokiri wazi kuwa: (Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu tu, na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu) ni kosa, na kukosea kwa kuwaacha makafiri elfu maishani ni jambo dogo zaidi kuliko kukosea kwa kumwaga damu ya Mwislamu.”
Ibn Nujaim alisema katika kitabu cha [Al-Bahr Al-Ra’iq, 5/134, Dar Al-Kitab Al-Islami]: “Katika muhtasari: ikiwa suala lina maana nyingi zinazolazimisha ukafiri, na maana moja inakataza ukafiri, basi mufti anapaswa kuegemea maana inayozuia ukafiri, ili kuboresha dhana kwa Mwislamu.”
Imethibitishwa katika itikadi ya Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah kwamba yule anayetenda dhambi hatakuwa kafiri kwa kuitenda tu; Imamu Al-Tahawi alisema kwa itikadi yake ambayo dola liliipokea kwa kukubalika kwake [uk. 102 - na Sharhu Al-Babarti - Wizara ya Awqaf ya Kuwaiti]: “Wala hatumkufurishi mtu yeyote miongoni mwa watu wa kibla kwa dhambi isipokuwa yeye anapoihalalisha.”
Mwanachuoni Al-Babarti alisema: “Alisema haya kujibu Khawarij ambao walisema kwamba ikiwa Muislamu atafanya dhambi kubwa, anakuwa ameachana na imani na kuuingia ukafiri, na kwa Mu'tazila ambao walisema: Anajitenga na imani na hataingia katika ukafiri, na yuko kati ya viwango hivi viwili.”
Kumekuwa na dalili nyingi kwamba mja anayeamini hatakuwa kafiri kwa kutenda tu dhambi, hata ikiwa dhambi hiyo ni kubwa. Kama vile:
Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Enyi mlio amini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yake” [AT TAHRIM: 8]; Allah aliwaita wenye dhambi kuwa waumini, na hii inaonesha kwamba hali ya kutenda dhambi peke yake haimtoi mja kutoka imani.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika walio uwawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakaye vuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu” AL BAQARAH: 178]; Kuua ni dhambi kubwa, lakini Mungu Mwenyezi alimwita muuaji huyo ndugu, na inayooneshwa kutokana na kuelezea undugu kwamba ni kizuizi chake cha imani - kama ilivyoelezwa mwanzoni mwa aya hizi -.
Imepokelewa kutoka kwa Masheikh wawili kutoka kwa Abu Dharr, R.A, alisema: Mtume wa Allah, S.A.W., alisema: “Alinijia mtu mmoja kutoka kwa Mola wangu, akaniambia – Au alisema: akanibashiri kwamba – mtu yeyote atakayekufa miongoni mwa Umma wangu hali ya kuwa hajamshirikisha Mwenyezi Mungu, basi ataingia Peponi, nikamwuliza: Hata kama mtu huyo aliiba na alizini? Akasema, ndio, hata kama mtu huyo aliiba na alizini”. Hadithi hii inadhihirisha kwamba hali ya kutenda dhambi kubwa haikuzuii kuingia Peponi maadamu utakufa katika hali ya Kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Imepokelewa kutoka kwa Al-Tirmidhiy kutoka kwa Anas Ibn Malik, R.A., alisema: Nilimsikia Mtume wa Allah, S.A.W., akisema: “Mwenyezi Mungu, atukuzwe na ametukuka. Akasema: Ewe Mwanadamu utakaponiomba na kuweka matumaini kwangu, basi nitakusamehe makosa uliyoyafanya na sitojali. Ewe Mwanadamu kama dhambi zako zingefika mawinguni na wewe ukaniomba msamaha, Ningekusamehe. Ewe Mwanadamu kama ungelinijia na dhambi kubwa kama Dunia na ukanikabili bila ya kunishirikisha Nitakupa maghfira”. Hadithi hii inaonesha kwamba dhambi ambazo hazifikii kushirikisha hazimzuii mtu yule kupata maghfira, na maghfira hayo siyo kwa makafiri.
Imepokelewa kutoka kwa Abu Dawud kutoka kwa Anas Ibn Malik, R.A., kwamba Mtume, S.A.W., alisema: “Uombezi wangu ni kwa watu wenye dhambi kubwa katika Umma wangu.” Hadithi hii iliwathibitishia Uislamu wao ingawa dhambi zao ni kubwa.
Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhariy kutoka kwa ‘Ubada Ibn As-Samit, R.A., kwamba Mtume wa Allah S.A.W., amesema wakati akizungukwa na kundi la maswahaba: “Nipeni kiapo cha Uaminifu cha: Kutomshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote katika ibada. Kutoiba. Kutofanya zinaa. Kutoua watoto wenu. Kutomtuhumu asiye na hatia (kusambaza shutuma kwa watu). Kutodharau/tii (mnapoamrishwa) kufanya jambo jema”. Nabii S.A.W., akaongeza: “yeyote miongoni mwenu mwenye kutimiza kiapo chake cha Uaminifu atalipwa (thawabu) na Mwenyezi Mungu. Na yeyote mwenye kufanya lolote katika hayo (isipokuwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu) na akaadhibiwa duniani, adhabu hiyo itakuwa ni kama kafara ya dhambi hiyo. Na endapo atafanya lolote katika hayo, na Mwenyezi Mungu akamfichia dhambi yake, ni juu Yake kumsamehe au kumuadhibu (akhera).” ‘Ubada Ibn As-Samit akaongezea: “Kwa hiyo tukala kiapo cha Utiifu kwa hayo mambo” (mambo kwa Mtume wa Allah S.A.W)”
Imamu Al-Mazari alisema katika kitabu cha [Al-Muallem Bi Fawaid Al- Muslim, 2/398, Ad-Dar At-Tunisia Lil-Nashr]: “Hadithi hii ni jibu kwa wale wanaokufurisha watu kwa dhambi; nao ni Khawarij, na ni jibu kwa wale wanaosema: Mwenye tabia mbaya lazima aadhibiwe ikiwa atakufa kwa dhambi kubwa na hajatubu dhambi hiyo, nao ni Mu’tazila, kwa sababu Mtume, S.A.W., alitaja dhambi hizi na akasema kwamba hali ya anayefanya dhambi hizi ni juu ya Mwenyezi Mungu, akipenda atamsamehe, na akipenda atamwadhibu, na hakusema: Lazima kumwadhibu.”
Ama yale yaliyotajwa katika matini kadhaa za kisheria juu ya kuikana imani ya mtenda dhambi fulani, au kumwita kafiri, au kwamba “Siyo kutoka kwetu”, basi inatafsiriwa kwa kukaripia na kuepusha dhambi, sio kwa ukweli wa ukafiri ambao unamlazimisha mtu kujitenga na Uislamu; Huu ni mchanganyiko wa dalili.
Mfano wa haya ni Hadithi ile iliyopokelewa kutoka kwa masheikh wawili kutoka kwa Abu Hurairah, R.A., kwamba Mtume, S.A.W., alisema: “Hazini mzinifu anapozini hali ya kuwa ni Muumini, wala hanywi pombe anapokunywa hali ya kuwa ni Muumini, wala haibi mwizi anapoiba hali ya kuwa ni Muumini.”
Imamu Al-Nawawi alisema katika kitabu cha [Sharh Sahih Muslim 2/41, 42, Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabi]: “Hadithi hii ni moja wapo ya mambo ambayo wanazuoni walitofautiana katika maana yake. Basi usemi sahihi ambao wachunguzi wameusema: Hiyo inamaanisha kwamba: Mtu hafanyi dhambi hizi katika hali ya kuwa na imani kamili. Hii ni moja ya kauli zinazohusu kukataliwa kwa kitu na imekusudiwa kupuuza ukamilifu wake na chaguo. Kama inavyosemwa: Hakuna elimu isipokuwa yenye faida, wala hapana mali ila ngamia, wala hapana uhai ila maisha ya Akhera. Badala yake, tulitafsiri kulingana na yale tuliyoyataja; Kulingana na Hadithi ya Abu Dharr na wengineo: “Yeyote anayesema: Hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu, ataingia Peponi, ingawa amefanya uzinzi, na ingawa ameiba.” Na Hadithi inayojulikana sana ya Ubadah Ibn As-Samit kwamba Walimwahidi Mtume, S.A.W, kutoiba, kutozini, na kutoasi na kadhalika. Kisha Mtume S.A.W. akawaambia: yeyote miongoni mwenu atakayetimiza kiapo chake atalipwa (thawabu) na Mwenyezi Mungu. Na yeyote mwenye kufanya lolote katika dhambi hizi na akaadhibiwa duniani, adhabu hiyo itakuwa ni kama kafara ya dhambi hiyo. Na endapo atafanya lolote katika hayo, na Allah akamfichia dhambi yake, ni juu yake kumsamehe ama kumuadhibu (akhera).” Hadithi hizi mbili ziko pamoja na mifano yao katika Sahih pamoja na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye.” [AN NISAA: 48], pamoja na makubaliano ya watu wa haki kwamba mtu ni mzinifu, mwizi, mwenye dhambi, na muuaji na wengine ambao hufanya dhambi kubwa isipokuwa ushirikina hawakuwa makafiri kwa dhambi hizi, bali wao ni waumini ambao Imani yao ina kasoro. Wakitubu hawataadhibiwa, wakifa hali yao wakisisitiza juu ya dhambi kubwa, basi hali yao ni juu ya Mwenyezi Mungu, akipenda atawasamehe na kuwaingiza Peponi kwanza, na akipenda atawaadhibu kisha awaingize Peponi. Na dalili hizi zote hutulazimishi kutafsiri Hadithi hii na mifano yake, basi tafsiri hii ni dhahiri, inaaminika kwa lugha hiyo, na inatumika sana. Na ikiwa Hadithi mbili maana zake ni tofauti, lazima ziunganishwe, na zimetajwa hapa, kwa hivyo lazima ziunganishwe. Baadhi ya Wanachuoni walitafsiri Hadithi hii juu ya yule aliyefanya dhambi hizo na akiona kuwa dhambi hizi ni halali, ingawa alikuwa anajua kuwa Sheria imezikataza dhambi hizi zote. Al-Hasan na Abu Jaafar Muhammad Ibn Jarir Al-Tabari walisema: Maana yake: Jina la sifa ambalo vipenzi vya Mwenyezi Mungu wameitwa linafutwa, na mwenye kutenda dhambi anastahili jina baya; Itasemwa: mwizi, mzinifu, na mwasherati. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas, R.A., kwamba maana yake ni: Ni kwamba mtu huyu anaondolewa Nuru ya imani ndani yake. Al-Muhallab alisema: Ufahamu wake kwa kumtii Mungu Mwenyezi unaondolewa kutoka kwake. Al-Zuhriy alisema kuwa Hadithi hii na zinazofanana nayo zinaaminiwa kwake, na zimepitishwa kulingana na zilivyokuja, na hakizungumzwi chochote katika maana yake, na sisi hatujui maana yake, na akasema: zipitishwe Hadithi hizo kama walivyofanya waliotangulia. Na ilisemwa juu ya maana ya Hadithi hiyo isipokuwa ile niliyoitaja, ambayo haionekani katika matini ya Hadithi, lakini baadhi ya tafsiri hizi zilikosea, kwa hivyo niliziacha, na maneno haya niliyoyataja katika tafsiri ya Hadithi hii yanawezekana, na ambayo ni sahihi kwa maana ya Hadithi hiyo ndio tuliyowasilisha kwanza, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi.”
Al-Hafiz Ibn Hajar alisema katika kitabu cha: [Fath Al-Bariy, 10/34, Dar Al-Maarifa]: “Na Khawarij wameambatanishwa na Hadithi hiyo, basi wakamkufurisha mwenye kutenda dhambi kubwa kwa makusudi akijua kwamba ni marufuku, na watu wa Sunnah walibeba imani hapa kwa ukamilifu; Kwa sababu anayetenda dhambi ana upungufu wa imani yake zaidi kuliko yule ambaye asiyetenda dhambi, na inawezekana kwamba inayokusudiwa ni: yule mtendaji hivyo hali yake inarudia kupoteza imani.
Mfano mwingine ni ile ambayo imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari kutoka kwa Abu Hurairah, R.A., kwamba Mtume, S.A.W., alisema: “Msikane Wazazi wenu; mwenye kumkana baba yake amekufuru.”
Imamu Ibn Battal alisema katika Sharh Al-Bukhari: [8/383, 384, Ar-Rushd]: “Ilisemwa: Haimaanishi kufuru ambayo inastahili kuendelezwa katika Moto wa Jehanamu, bali ni kufuru kwa haki ya baba yake na haki ya mabwana wake, kama alivyosema Mtume S.A.W., juu ya wanawake: “Wanakufuru (Wanakana) neema za waume”.
Mfano mwingine ni Hadithi ambayo imetajwa kama dalili katika swali hilo, ambayo imepokelewa kutoka kwa masheikh wawili kutoka kwa Ibn Umar, R.A., kwamba Mtume, S.A.W., alisema: “Anayebeba silaha dhidi yetu sio katika sisi.” Kusema juu yake ni kama kusema juu ya mifano yake iliyotajwa hapo awali, inakusudiwa kukemea vikali kitendo hicho.
Imamu Al-Tahawiy alitaja katika kitabu cha: [Sharh Mushkil Al-Athar, 3/378, Muasastur Risalah] Hadithi hii na Hadithi zingine kadhaa zinazofanana; kama vile: ile ambayo imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslim kutoka kwa Abu Hurairah, R.A.: kwamba Mtume wa Allah, S.A.W., alisema: "Mwenye kubeba silaha dhidi yetu si katika sisi, na yule anayetudanganya sio katika sisi.” Na ile iliyopokelewa kutoka kwa Abu Dawud kutoka kwa Abdullah Ibn Buraidah, kutoka kwa baba yake, R.A., alisema: Nilimsikia Mtume wa Allah, S.A.W., akisema: “Sala ya Witri ni kweli, kwa hivyo yule ambaye hasali sala hiyo basi sio katika Sisi.” Na ile iliyopokelewa kutoka kwa Al-Tirmidhi kutoka kwa Zaid Ibn Arqam, R.A., kwamba Mtume wa Allah, S.A.W., alisema: “Yeyote ambaye hatachukua kutoka kwa vyanzo vyake sio katika sisi.” Vile vile Hadithi ile iliyopokelewa kutoka kwa Al-Hakim katika Al-Mustadrak kutoka kwa Ubadah Ibn As-Samit, R.A, kwamba Mtume wa Allah, S.A.W., alisema: “Yeyote asiyewaheshimu wazee wetu, asiyewahurumia wadogo zetu, na asiyeujua uzito na hadhi ya mwanchuoni wetu, basi sio katika sisi.” Halafu At-Tahawi akasema: “Basi haya ndiyo mambo ambayo Mtume wa Allah, S.A,W., aliyakana, kwa hivyo Mwenyezi Mungu alimchagulia Mtume wake, S.A.W., mambo ya kusifiwa, na alimwepushia mambo ya yeye kulaumiwa, kwa hivyo aliyefanya mambo mazuri ya kusifiwa atakuwa miongoni mwa Umma wake Mtume S.A.W., na yule asiyefanya mambo ya kusifiwa hatakuwa miongoni mwa Umma wake Mtume S.A.W., kama Mwenyezi Mungu alivyosema juu ya Nabii Ibrahimu kwa kauli yake juu ya kizazi chake: “Basi aliye nifuata mimi huyo ni wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu” [IBRAHIM: 36]. Na kama vile Mwenyezi alivyosema, akiwajulisha waja wake katika hadithi ya Nabii wake Daudi, S.A.W.: “Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa mto. Atakaye kunywa humo si pamoja nami, na asiye kunywa atakuwa pamoja nami” [AL BAQARAH: 249] Inaonyesha kwamba kila mtendaji anayetenda kitendo kilicho katika sheria ya Mtume wake, ambaye wafuasi wake wanawajibika kumfuata, basi watakuwa pamoja naye, na kwamba kila mtendaji anayetenda kitendo ambacho ni marufuku na sheria ya Mtume wake, ambaye wafuasi wake wanawajibika kumfuata, basi hawatakuwa pamoja naye; Kwa sababu watakuwa wamejitoa katika wito wake, na watakuwa kinyume na Mtume wao.
Na Imamu Al-Mazari anasema katika kitabu cha [Al-Mu'allim, 1/306]: “Hakuna hoja ndani yake kwa yule anayesema: mwenye dhambi ameacha imani, kwa sababu inawezekana kwamba alitaka kufanya hivyo ilhali aliona kuwa ni halali, au (yeye sio pamoja nasi) kwa maana: hafuati mwongozo wetu au Sunnah zetu; Kama yule anayemwambia mwanawe: Wewe sio pamoja nami ikiwa ana tabia nyingine isipokuwa tabia yake.
Ama kusema kuwa Hadithi hii inafahamika kwa ukweli na sio kwa majazi; Kwa kukosekana kwa dhana ya moja kwa moja, sio sahihi kwa sababu hali ya kulinganisha ushahidi wa kisheria kutoka katika Qur'ani na Sunnah huelekeza Hadithi hiyo kutokana na maana yake ambayo ni dhahiri. Kwa Qur'ani Tukufu: Mwenyezi Mungu anasema: “Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalo dhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu.” [AL HUJURAAT: 9], Mwenyezi Mungu Mtukufu anayaelezea makundi haya mawili kwa imani, licha ya mapigano yao. Kwa upande wa Sunnah: Tayari zimetajwa Hadithi nyingi katika maneno ya Imamu Al-Nawawi yaliyonukuliwa hapo awali.
Vikundi hivyo vya kidini ambavyo hubeba silaha dhidi ya ndugu zao katika jeshi na polisi havibebi isipokuwa kwa tafsiri mbaya, kwa hivyo vinakuwa kama Khawarij ambao walimwasi Kamanda wa Ali R.A, na wakabeba silaha dhidi ya Waislamu, pamoja na hivyo, hawakuwahukumu kama ni wenye kukufuru; Imepokelewa kutoka kwa Abd Al-Razzaq katika kitabu chake kutoka kwa Al-Hassan kwamba alisema: Wakati Ali, R.A., alipowaua Al-Harouriyyeh (kikundi cha kwanza cha Khawarij), walisema: Ni akina nani hawa, Ewe Amiri wa Waamini, Je, ni makafiri? Akasema: “Waliukimbia ukafiri.” Ikasemwa: Je! Wao ni wanafiki? Akasema: Hakika Wanafiki hawamkumbuki Mwenyezi Mungu isipokuwa kidogo tu, na hawa wanamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.” Ikasemwa: Ni akina nani? Akasema: “Ni watu ambao wamekumbwa na jaribio, basi wakawa vipofu na viziwi.”
Imamu Ibn Battal alisema katika kitabu cha: [Sharh Al-Bukhariy, 10/16] - wakati akielezea Hadithi hii: “Anayebeba silaha dhidi yetu sio katika sisi”: “Kauli yake Mtume S.A.W., “Sio katika sisi” inamaanisha: Hafuati Sunnah zetu wala hafuati njia yetu. Kama alivyosema Mtume S.A..: “Sio katika sisi mtu ambaye hugawanya mifuko yake na kuomba dua mbaya ya ujinga.” Kwa sababu ni haki ya Muislamu juu ya Muislamu mwenzake kumnusuru na kutomwacha kwa adui, na kwamba Muumini kwa Muumini mwenziwe ni kama jengo, baadhi yake hutilia nguvu baadhi nyingine, Yeyote atakayebeba silaha dhidi yao kwa tafsiri mbovu aliyoiona, basi amekiuka Sunna yake Mtume, S.A.W., ambayo ni pamoja na kuwanusuru waumini na kushirikiana nao, na wanavyuoni walikubaliana kwa kauli moja kuwa Khawarij ni miongoni mwa waumini; Kwa sababu wote wamekubaliana kwa kauli moja kwamba imani inaweza kuondolewa tu kwa ushirikina na kutomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na kwamba dhambi mbali na kufuru hazimkufurishi yule anayezitenda.
Yeyote anayebeba silaha dhidi ya Waislamu kutokana na vikundi vilivyotajwa ni mharibifu ambaye amepotea njia iliyonyooka, lakini kusema kwamba yeye ni kafiri kwa sababu tu amebeba silaha ni kosa na ni uwongo na kunapingana na ushahidi wa kisheria, maadamu hakusema kuwa dhambi hizi ni halali, au ana tafsiri yake hata ikiwa tafsiri yake hiyo ni mbovu.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Zaidi.
Amanat Al-Fatwa