Watu wa Dini na Kaaba
Question
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwingi wa kurehemu. “Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.” Mwenyezi Mungu amesema kweli.
Je, ni ipi hukumu ya kuwaruhusu watu wa dini nyinginezo kama vile Uyahudi na Ukristo kuzuru Al-Kaaba kwa sababu Mwenyezi Mungu alimuamuru bwana wetu Ibrahim awaalike watu wote?
Tafadhali ushauri juu ya jambo hili
Answer
Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu peke yake, rehema na amani zimwendee Mtume wa mwisho naye ni Mtume Muhammad S.A.W pamoja na watu wa nyumbani kwake na Masahaba zake na mwenye kumfuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.
Hijja ni miongoni mwa ibada za Dini safi ya Kiislamu, nayo ni miongoni mwa nguzo za dini ya Kiislamu pia, na Uislamu ndani yake umeafikiana na sheria ya bwana wetu Ibrahim, A.S.
Makusudio ya kuzuru Kaaba Tukufu ni kuhiji; lau Mayahudi na Wakristo hawa wangetaka kuhiji wangeruhusiwa kuzuru Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, na kizuizi baina ya watu hawa na kuhiji Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu ni kuingia kwao katika dini ya Kiislamu, basi waingie katika Uislamu na wahiji kwenye Nyumba Takatifu ya Mwenyezi Mungu kama wakitaka.
Ama kusema kwako kuwa usemi katika Aya umetajwa kwa tamko la watu, hivi ndivyo wanavyuoni wanavyoita Jambo la jumla linalotakiwa jambo linalohusika, na maana ya Aya ni, ewe Ibrahim, uwalinganie watu wote kuhiji kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu, ili wakuitikie wanaokufuata kutoka kwao; yaani aliyesilimu miongoni mwao tu.