Israa

Egypt's Dar Al-Ifta

Israa

Question

Matni ya Qur`ani

Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuoneshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona} [ISRAA: 01].

Nini amesema mjenga hoja?

Answer

Amesema Imamu Baidhawi: Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu siku moja alikuwa amelala baada ya Sala ya Isha nyumbani kwa Mama Hani, ndipo akapelekwa usiku na kurudishwa usiku huo huo, akaelezea kisa na akasema: Nililetewa Manabii Amani ya Mungu iwe kwao nikawasalisha kisha nikarudi Msikiti wa Makka na nikawaelezea Makuraishi walishangazwa kwa kutowezekana kwake, ndipo kuna watu waliacha Uislamu miongoni mwa wale walioamini.

Watu wakaenda kwa Abu Bakri R.A na akawaambia: Ikiwa amesema basi ni kweli, wale watu wakamuuliza: Je unaamini hilo? Akasema: Mimi ninaamini zaidi ya hivyo, ndipo alipoitwa As-Siddik, na hilo lilikuwa kabla ya kuhama Mtume kwa mwaka mmoja, kumekuwa na tofauti je ilikuwa ndani ya njozi au akiwa macho na ufahamu kamili? Je ilikuwa ni kwa roho au kwa mwili? Kauli za wengi ni kuwa alipelekwa kwa mwili mpaka Baitul-Maqdas, kisha akapandishwa mpaka mbinguni na kufika mpaka eneo la Sidratul-Muntaha, kwa sababu hiyo Makuraishi walishangazwa na kuona ni jambo lisilowezekana, na hali ya kutowezekana inasukumwa na uthibiti wa kiuhandisi kuwa kati ya pande mbili za duara la jua ni zaidi ya pande mbili za duara la ardhi kwa zaidi ya mara mia moja na sitini, kisha upande wake wa chini unafikia upande wake wa juu chini ya sekunde moja, na Mwenyezi Mungu ni Mweza wa kila chenye kuwezekana hukadiria kuumba mfano wa hatua hii ya haraka kwa Mtume S.A.W.

Sisi tunauliza: Nani hao walioshuhudia muujiza wa Muhammad kupelekwa usiku? Miongoni mwa masharti ya muujiza ni kufanyika mbele ya mashahidi na uwe wenye faida, na hili halipo kwenye kisa hiki cha Israa na Miiraj, kama vile Msikiti wa Al-Aqsaa haukuwepo wakati wa Muhammad bali ulijengwa baada ya kufa kwake kwa kiasi cha miaka mia, hivyo ni vipi alisali ndani ya Msikiti huo na kuelezea milango yake na madirisha yake?([1]).

Maeneo ya Shaka:

  1. Ubora wa muujiza haukamiliki isipokuwa kwa kuonekana na mashahidi, lakini muujiza wa Israa na Miiraji haukushuhudiwa na yeyote.
  2. Miongoni mwa masharti ya muujiza ni kuwa wenye faida na katika muujiza wa Israa na Miiraji hakuna faida yoyote.
  3. Vipi Mtume anakwenda Msikiti wa Al-Aqsaa ndani ya kipindi hiki ambacho bado hakuwa Mtume? Na namna gani anaelezea milango yake na madirisha yake?

Kuondoa Shaka:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Ubora wa muujiza sio kama alivyosema kuonekana na mashahidi wake tu lakini ubora mwingine ni kuuthibitisha moyo wa Mtume ambao umetokewa na huu muujiza.

Kama vile ubora wa muujiza ambao haukuonekana bali umepatikana kwa maelezo na kukubalika na wanaoambiwa habari na kuikubali habari kwa dalili zinazokubaliana na ukweli kama vile Mtume S.A.W. alivyouelezea Msikiti wa Al-Aqsaa kwa Masahaba Radhi za Mungu ziwe kwao bali na kwa makafiri wa Makka ambao waliotaka kupinga hilo.

Na kwa hili muujiza wa Israa na Miiraji umethibiti faida nyingi.

Hadithi inayotokana na Jabir Ibn Abdillah R.A.: Kuwa amemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: “Pindi Makuraishi waliponipinga nilisimama kwenye jiwe Mwenyezi Mungu akanifungulia Baitul-Maqdis na nikaanza kuwaelezea alama zake huku nikiwa naiangalia”([2])

Kutoka kwa Anas Ibn Malik Ibn Saasaah R.A: Mtume S.A.W. aliwazungumzisha kuhusu usiku aliopelekwa Msikiti wa Aqsaa: “Wakati nikiwa nimelala mara akanijia aliyenijia - Nikasikia akisema akapasua – kati ya eneo hili na hili – nikamuuliza Jarud akiwa pembezoni mwangu ana maanisha nini? Akasema kuanzia sehemu ya juu ya mfupa wa kifua chake mpaka chini – akauotoa moyo wangu kisha akaja na jagi la dhahabu limejaa imani akauosha moyo wangu kisha akaziba na kuurudisha, hapo akaletwa mnyama mweupe mwenye ukubwa chini ya nyumbu zaidi ya punda – ndipo Jarud akauliza huyo ndiyo Burak Ewe baba wa Hamza? Anasi akasema ndiyo – anaweka hatua yake umbali wa peo ya macho yake, ndipo alipombeba na kuanza safari akiwa na Malaika Jibril mpaka alipofika mbingu ya dunia akaomba ruhusa ya kufunguliwa ndipo wakauliza ni nani? Akajibu mimi ni Jibril, akaulizwa upo nani? Akajibu nipo na Muhammad, akaulizwa je ameshapewa Utume? Jibril akajibu ndiyo, wakaambiwa karibu sana kwani neema ya mwenye kuja imekuja hivyo wakafunguliwa mlango, walipoingia wakamkuta Nabii Adam A.S. Mtume S.A.W. akatambulishwa huyu ndiyo Baba yako Adam hivyo akamsalimia na akajibiwa salamu kisha akamwambia karibu sana ewe kijana mwema na Mtume mwema, kisha Jibril akapanda nami mpaka mbingu ya pili akaomba kufunguliwa mlango akaulizwa ni nani? Akajibu mimi ni Jibril, akaulizwa upo na nani? Akajibu nipo na Muhammad, akaulizwa je ameshapewa Utume? Akajibu ndiyo, akaambiwa karibu sana kwani neema ya mwenye kuja imekuja wakafunguliwa mlango walipoingia wakakutana na Nabii Yahya pamoja na Nabii Isa ambao ni ndugu, ndipo akatambulishwa huyu ni Nabii Yahya na Nabii Isa A.S. akawasalimia nao wakajibu salamu, kisha wakasema karibu sana ndugu mwema na Nabii mwema. Kisha akapanda na mimi mpaka mbingu ya tatu akaomba ruhusa ya kufunguliwa mlango akaulizwa ni nani? Akajibu ni Jibril, akaulizwa upo na nani? Akajibu nipo na Muhammad, je ameshapewa Utume? Akajibu ndiyo, akaambiwa karibu sana kwani neema ya mwenye kuja imekuja ndipo wakafunguliwa mlango, walipoingia wakakutana na Nabii Yusuf A.S. hivyo Mtume akatambulishwa huyu ni Nabii Yusuf, akamsalimia na akajibiwa salamu na kuambiwa karibu sana ndugu mwema na Nabii mwema. Kisha Jibril akapanda pamoja nami mpaka mbingu ya nne akaomba ruhusa ya kuingia akaulizwa ni nani? Akajibu mimi ni Jibril, akaulizwa upo na nani? Akajibu nipo na Muhammad, akaulizwa je ameshapewa Utume? Akajibu ndiyo, akaambiwa karibu sana kwani neema ya mwenye kuja imekuja ndipo ukafunguliwa mlango walipoingia wakakutana na Nabii Idris akatambulishwa huyu ni Nabii Idrisa hivyo akamsalimia na akajibiwa salamu, kisha akaambiwa karibu sana ndugu mwema na Nabii mwema. Kisha Jibril akapanda nami mpaka mbingu ya tano na akaomba kufunguliwa mlango akaulizwa ni nani? Akasema ni Jibril, akaulizwa upo na nani? Akajibu nipo na Muhammad, akaulizwa je ameshapewa Utume? Akajibu ndiyo, akaambiwa karibu sana kwani neema ya mwenye kuja imekuja, walipoingia wakamkuta Nabii Harun akatambulishwa huyu ndiyo Nabii Harun hivyo akamsalimia na akajibiwa salamu kisha akamwambia karibu sana ndugu mwema na Nabii mwema. Kisha jibril akapanda nami mbingu ya sita akaomba ruhusa ya kuingia akaulizwa ni nani? Akasema ni Jibril, akaulizwa upo na nani? Akasema nipo na Muhammad, akaulizwa je ameshapewa Utume? Akajibu ndiyo, akaambiwa karibu sana kwani neema ya mwenye kuja imekuja, alipoingia wakamkuta Nabii Musa akatambulishwa huyu ndiyo Nabii Musa akamsalimia na akajibiwa salamu, kisha akaambiwa karibu sana ndugu mwema na Nabii mwema, baada ya kuondoka Nabii Musa alilia, alipoulizwa nini kinamliza? Akasema ninalia kwa sababu kijana amepewa Utume baada yangu anaingia Peponi yeye na umma wake kwa wingi kuliko watakavyoingia umma wangu. Kisha Jibril akapanda na mimi mpaka mbingu ya saba, akaomba ruhusa kuingia akaulizwa ni nani? Akajibu ni Jibril, akaulizwa upo na nani? Akasema nipo na Muhammad, akaulizwa ameshapewa Utume? Akajibu ndiyo, akaambiwa karibu sana kwani neema ya mwenye kuja imekuja, alipoingia akakutana na Nabii Ibrahim, akatambulishwa huyu Baba yako hivyo akamsalimia na akajibiwa salamu, akaambiwa karibu sana mtoto mwema na Nabii mwema. Kisha nikapandishwa Sidratul-Muntaha tahamaki matunda yake ni kama kimtungi kidogo, na jani lake ni kama sikio la tembo akasema huu ndio mti wa mkunazi “Sidratul-Muntaha” eneo hilo likiwa na mito minne, miwili ipo ndani na miwili ipo kwa nje, nikauliza ni mito gani hii Ewe Jibril? Akasema, mito miwili ya ndani ni mito ya peponi ama mito miwili ya nje ni mto wa Naili na Furati, kisha nikapelekwa Baitul-Maamur sehemu ambayo kila siku wanaingia Malaika elfu sabini, kisha kikaletwa chombo kimejaa mvinyo na chombo kingine kimejaa maziwa na kingine kimejaa asali, hivyo nikachukua chombo cha maziwa, akasema haya ndiyo maumbile wewe uliyonayo na watu wako, kisha nikapewa ibada ya Sala hamsini za kila siku, hivyo nikarudi nikapita kwa Nabii Musa akaniuliza umepewa amri gani? Nikasema nimepewa Sala hamsini za kila siku, akasema umma wako hautaweza kutekeleza Sala hamsini kwa kila siku kwani mimi ninaapa kwa Mwenyezi Mungu nimewajaribu watu kabla yako hivyo rudi kwa Mola wako na umwombe awapunguzie watu wako, ndipo nikarudi na nikapunguziwa Sala kumi kisha nikarudi tena kwa Musa akasema mfano wa alivyosema nikarudi tena nikaondolewa tena Sala kumi kisha nikarudi kwa Musa akasema kama alivyosema, nikarudi tena nikapunguziwa Sala kumi nikarudi tena kwa Musa akasema kama alivyosema nikarudi tena nikapunguziwa mpaka zikafika Sala tano kwa kila siku, nikarudi kwa Musa akaniuliza umepewa amri gani? Nikasema nimepewa Sala tano kwa kila siku, akasema Nabii Musa umma wako hautaweza kutekeleza Sala tano kwa siku kwani mimi nimewahi kuwajaribu watu kabla yako hivyo rudi tena kwa Mola wako na mwombe awapunguzie watu wako, akasema Mtume nimeshamwomba Mola wangu mpaka sasa naona haya lakini naridhia na nazipokea, alipoondoka Mtume akaita mwenye kuita “Nimepitisha ibada zangu na nimeshawapunguzia waja wangu”([3]).

Kisa cha Israa kimeenea kwa watu, kwani Waislamu wameamini na washirikina wakapinga, na katika kisa hicho kimekusanya nafasi ya Muhammad na kuthibitisha kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na amepewa dalili za ukweli wa Ujumbe wake, kupelekwa kwake usiku kulikuwa ni kuona mambo mengi yasioonekana ardhini.

Asili ya Muujiza unapingana na kufuatana na faida yake hufikiwa bila ya huko kufuatana:

Swali la washirikina wasifu wa Msikiti inathibitisha uwepo wake wakati wa kutokea muujiza ambapo kama usingekuwepo wakati huo basi washirikina wasingemuuliza Mtume wasifu wake bali walikuwa wakipinga habari ya Mtume S.A.W. na kumtaka kuelezea wasifu wa Msikiti ni dalili ya kuwepo kwake ndani ya kipindi hiki.

  1. Israa na Miiraji ni Muujiza Maalumu

Muujiza wa Israa ulikuwa ni maalumu kwa Mtume S.A.W. ikiwa ni sehemu ya kumliwaza baada ya kumpoteza mke wake Bi Khadija na baba yake Mzee Abi Talib nao wote wawili walikuwa nguzo katika kazi za ulinganiaji wake kwani walimpa nguvu na kumlinda na kero mbalimbali za watu, pindi sababu hiyo imara ilipokatika ambapo makafiri watadhani kuwa Mtume S.A.W. kwa kupoteza watu hao sasa atakuwa mpweke katika kuwakabili makafiri kwenye kazi za ulinganiaji, hivyo Mwenyezi Mungu Akamkaribisha kwenye safari tukufu ili apelekwe na kuelimishwa kuwa yeye yupo pamoja na Mwenyezi Mungu na yupo chini ya uangalizi wake na usimamizi wake na ili makafiri na washirikina wafahamu kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kumwacha Mtume wake kwa waovu wake na wabaya wake na vyovyote vile sababu zitakavyokatika lakini Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wake msimamizi wake na mtetezi wake na pia kumfundisha Mtume wake S.A.W. kuwa yeye si amezuka tu katika Mitume bali ni mwenendo wa ndugu zake miongoni mwa Manabii, lengo kuu la safari hiyo ni yeye mwenyewe Mtume S.A.W. hivyo hakukuwa na faida yoyote ya kuwepo mashahidi miongoni mwa watu wa ardhi kwenye hiyo safari, kwa sababu lau angefuatana na mtu miongoni mwa watu ili kushuhudia yaliyomo kwenye safari basi ingekataliwa safari hiyo kuwa muujiza maalumu kwa Mtume kwa sababu ya kushiriki mtu mwingine kwenye hiyo safari, pindi ilipozuilika kwa mwingine yeyote asiyekuwa Mtume S.A.W. kufika hizo sehemu za juu kabisa basi ni jambo lisilowezekana kuwepo mashahidi wa kushudia muujiza huo.

  1. Miongoni mwa hukumu za muujiza huu

Vilevile miongoni mwa hukumu muhimu za huo muujiza ni kutahiniwa imani za Waumini ili kufahamika imani ya kina miongoni mwa wale walio na imani dhaifu, na makafiri kupewa mtihani ili kuongezeka upingaji wao baada ya kufunuliwa haki na ukweli mbele yao kwa Mtume S.A.W. kuwaelezea wasifu wa Msikiti na vinavyozunguka Msikiti bali na kuwapa habari kuhusu msafara utafika kwao siku fulani na fulani hivyo hawakuwa na sababu yoyote ya kutomwamini Mtume S.A.W. katika yale anayowapa habari.

  1. Msikiti wa Al-Aqsaa ulijengwa kabla ya kuzaliwa Mtume kwa karne nyingi

Ama kauli kuwa Msikiti wa Al-Aqsaa ulijengwa baada ya miaka mia moja tokea kufariki kwa Mtume S.A.W. kauli hii si sahihi, na historia inashuhudia kuwa Nabii Ibrahim A.S. aliujenga kiasi cha miaka 1800 kabla ya kuzaliwa kwa Nabii Isa A.S. na baada yake Isaka na Yakobo A.S. na ulikuwa ndio Kibla yao, kisha ukajengwa tena na Nabii Suleiman A.S. kiasi cha miaka 1000 kabla ya kuzaliwa kwa Nabii Isa A.S. na athari zake ziliendelea kubakia zikifahamika mpaka zama za Mtume S.A.W. ambapo ulikuwa ndio Kibla ya Wayahudi na ukawa pia Kibla ya Waislamu kwa muda mrefu, pindi Mtume S.A.W. alipoutembelea kwenye safari hiyo sehemu hiyo haikuwa na kitu bali ilikuwa na mabaki ya ujenzi yanayo onesha, nayo ndiyo yaliyopelekea Mtume S.A.W. kusali hapo na kuuelezea pale alipotakiwa na washirikina kutoa wasifu wake.

Wakati wa ukombozi wa Uislamu wa Jerusalem mwaka 636 sawa na mwaka wa 15 Hijria, ndipo Umar Ibn Al-Khattab alirudia kujenga upya sehemu ya mbele ya kusalia, na ujenzi huu ulimchukua kiasi cha miaka 30 kutoka mwaka 66 Hijria sawa na mwaka 685 mpaka mwaka 96 Hijria sawa na mwaka 715 AB, muda huu wote ni hatua ya uboreshaji wa ujenzi ili baadaye kukamilika Msikiti wa Al-Aqsaa kwa sura yake na umbile lake la hivi sasa, ama msingi wenyewe upo tokea kale hivyo swali limekuwa batili kutokana na matukio ya kihistoria.

Kutokana na hayo safari ya Israa na Miiraji ni muujiza mkubwa kwa Mtume S.A.W. na ni safari yenye faida nyingi na hukumu kubwa nayo ni safari isiyoshindikana kwenye uwezo wa Mwenyezi Mungu kwani kuamini kwake wala hakufungamani na jambo lisilowezekana kiakili hivyo ni lazima kuamini ukweli wa kutokea kwake.

Maana inayokusudiwa kwenye Israa

Ni ishara kuwa Mwenyezi Mungu Ameifanya safari hii ya Israa ni alama kuwa Uislamu umekusanya yote yaliyokuja kwenye Sharia ya Tawheed kutoka zama za Nabii Ibrahim A.S. zilizokuja kutoka Msikiti Mtakatifu wa Makka kuzaliwa kutokana na Sharia hizo Sharia ambazo makao yake makuu yalikuwa Baitul-Maqdis kisha kufika mwisho wake ambao ulionekana pia hapo Makka, kwani Sharia zilitoka Makka na kufika Msikiti wa Al-Aqsaa kisha zikarudi tena Makka kama ilivyorudi Makka safari ya Israa kwa sababu kupelekwa safari ya usiku hufuatiwa na karipio na kwa sababu hiyo likapatikana jibu la kushindwa kwenye kifua.

Na kutokana na hilo kunapatikana mnasaba wa kuteremka Sharia katika Sura hii ndani ya Aya zilizoanza na kauli yake Mola:  {Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu} na Aya nyingine: {Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipokuwa kwa haki} na kauli nyingine:{Wala msiikaribie mali ya yatima, isipokuwa kwa njia iliyo bora} na Aya nyingine:  {Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa} Israa: 23 – 35. Ishara kuwa dini hii itakuwa ni dini yenye hukumu kwa watu na kutekelezwa hukumu zake.

Yaliyopokelewa kwa Mtume S.A.W. katika ujenzi wa Msikiti:

Msikiti wa Al-Aqsaa ni Msikiti wa pili uliojengwa na Nabii Ibrahim A.S. kama yalivyopokelewa hayo kutoka kwa Mtume S.A.W. kwani katika vitabu viwili vya Sahihi Muslim na Sahihi Bukhari kutoka kwa Abi Dhari amesema: Nilimuuliza Mtume S.A.W. ni Msikiti gani wa kwanza kujengwa? Akasema: Msikiti Mtakatifu wa Makka, nikamuuliza: Kisha upi? Akasema: Msikiti wa Al-Aqsaa, nikamuuliza ni muda gani imepishana? Akasema: Miaka Arobaini.

Hadithi hii imebainisha kuwa Msikiti wa Al-Aqsaa ni katika majengo aliyoyajenga Nabii Ibrahim kwa sababu umeainishwa muda nao ni muda alioishi Nabii Ibrahim A.S. na umekutanishwa kutajwa kwake na utajo wa Msikiti wa Makka.

Haya ni katika yasiyoelezewa na Watu wa Kitabu

Nayo ni katika mambo maalumu Mwenyezi Mungu ameyahusisha kwa Mtume wake S.A.W. kuyafahamu, na Taurati inashuhudia hilo kwani imekuja katika Kitabu cha Mwanzo sura ya kumi na mbili: Ibrahim alipoingia nchi ya Kanaani akajenga hema lake kwenye mlima ulio upande wa Mashariki wa Betheli “Betheli ni mji ulioumbali wa maili kumi na moja kutoka Arusheleem kwenda kaskazini nao ni mji ulikuwa unaitwa na Wapalestina (Luza) Yakobo akauita Betheli, kama ilivyokuja kwenye sura ya ishirini na nane Kitabu cha Mwanzo: Magharibi mwa nchi ya Ai “Mji wa Ibrania hivi sasa unafahamika kama Tibah” na huko kumejengwa machinjio ya mungu.

Na wao wanaita machinjio kwa jina la msikiti kwa sababu wanachinja kwa ajili ya matambiko ndani ya misikiti yao.

Hakuna shaka kuwa Msikiti wa Nabii Ibrahim ndio sehemu ambayo Nabii Daudi alikusudia kuweka hema na kujenga Mihirabu yake au alishushiwa ufunuo na Mwenyezi Mungu kufanya hilo, nao ndio ambao Nabii Suleiman alimuusia mtoto wake kujenga Msikiti, kwa maana ya Hekalu, wanahistoria wa Kiibrania wamesema miongoni mwao Josephus kuwa mlima ambao aliishi Nabii Ibrahim kwenye mji wa Kanaan jina lake ni “Nabu” nao ni mlima ambao Suleiman alijenga Hekalu nalo ni Msikiti ambao wa mwamba au jiwe.

Kisa cha Suleiman kujenga kimeelezwa kwa ufafanuzi ndani ya kitabu cha Wafalme wa kwanza kwenye Taurati. Na uliharibiwa ndani ya awamu tatu:

Awamu ya Kwanza: Uliharibiwa na Bakhtnasr mfalme wa Babeli mwaka 578 kabla ya Masihi kisha Mayahudi wakaufanyia marekebisho wakati wa utawala wa Fursi.

Awamu ya Pili: Uliharibiwa na utawala wa Warumi kipindi cha titus baada ya vita vya muda mrefu kati yake na Mayahudi hivyo ukajengwa tena, akakamilisha uharibifu huo Adrianos mwaka 135 na kuondoa athari zake hakuna kilichobakia isipokuwa magofu.

Awamu ya Tatu: Pindi mfalme wa Hailana au mtawala wa Constantine, mfalme wa Roma alipoingia kwenye Ukristo na moyo wake ulijaa chuki kwa baadhi ya Mayahudi kwa inavyoaminika kuwa wamemuua Masihi, ilikuwa imezoeleka kwake pindi anapotembelea Yerusalem kuamrisha kuondoa magofu ya hekalu ya Suleiman na kuhamisha mabaki na kujenga Kanisa kwenye kaburi la Masihi wanalodhani ndio sehemu ya kaburi lake, “Wanahistoria wa Kikristo wamekuwa na shaka juu ya hiyo sehemu inayodaiwa kuwa Masihi amezikwa” na liitwe Kanisa la ufufuo, na akaamrisha Msikiti wa Al-Aqsaa kufanywa sehemu ya kutupia takataka za mji mzima na mifuko ya plastiki na kupelekea eneo la mwamba au jiwe kufunikwa takataka na ngazi zake kubomoka.

Waislamu walipoikomboa ardhi ya Shamu katika zama za Umar Ibn Al-Khattab na kushuhudiwa kufunguliwa mji wa Elia nao ulifahamika hapo nyuma “Yerusalem” na ukawa unaitwa Elia, vilevile jina lake lilikuwa linafahamika kwa Waarabu wakati Waislamu walipoikomboa Palestina, na jina la Elia ni jina la Nabii miongoni mwa Manabii wa Waisrael alikuwa mwanzoni mwa karne ya tisa kabla ya kuzaliwa kwa Masihi.

Siku moja Umar Ibn Al-Khattab alimuuliza Pangwini wao jina lake ni Sophronius: Nioneshe Msikiti wa Nabii Daud, akaenda naye mpaka mwisho wa sehemu ya mlango samadi ikiwa imeshuka mpaka kwenye ngazi za mlango ndipo Umar alipopiga kelele akaingia na kuangalia akasema: Allahu Akbar “Mungu Mkubwa” ninaapa kwa yule nafsi yangu ipo mikononi mwake huu ndio Msikiti wa Nabii Daud ambao Mtume S.A.W. alituambia kuwa alipelekwa safari ya usiku kwenye Msikiti huu, kisha Umar pamoja na Waislamu wakaanza kazi za kuondoa samadi kwenye jiwe au mwamba mpaka likaonekana lote, ndipo Umar alipoelekea upande wa Mihraab ya Nabii Daud akasali eneo hilo, kisha akaondoka mji wa Jerusalem na kueleka Palestina.

Wala haikubainika kuwa kuna Msikiti mpaka ndani ya zama za Abdulmalik Ibn Marwan alitoa amri ya kuanza kujengwa Kubba juu ya mwamba au jiwe na kujenga Msikiti wa Al-Aqsaa, na alimpa kazi za kumwakilisha kwenye ujenzi wake Raja Ibn Haywa Al-Kindi mmoja wa Wanachuoni wa Uislamu, hivyo kazi hiyo ya ujenzi ilianza mwaka wa 66 na kumaliza kazi hiyo ilikuwa ndani ya mwaka wa sabini na tatu.

Umar alikuwa ndio Mwislamu wa kwanza kusali hapo na kuwa Msikiti Mtakatifu, na kwa maelezo haya kuitwa sehemu hiyo kwa jina la Msikiti wa Al-Aqsaa ndani ya Qur`ani uitaji wa Qur`ani umezingatia yale yaliyokuwa hapo mwanzo, kwa sababu hukumu ya Msikiti haikatiki kwenye ardhi ya Msikiti, hivyo kuitwa kwa kuzingatia yaliyokuwepo ni ishara iliyojificha kuwa utakuwa Msikiti kwa sifa kamilifu ya Msikiti.

Waislamu waliuelekea kwenye ibada ya Sala baada ya kuwajibishwa kwa ibada ya Sala ndani ya usiku wa Israa mpaka baada ya kuhama kwa kipindi cha miezi kumi na sita, kisha kukaondolewa kuuelekea na ikawa Kaaba ndiyo Kibla ya Kiislamu.

Nilipata kumwona mtalii wa Kikristo jina lake “Arcolv” alitembelea Jerusalem mwaka 670, kwa maana baada ya utawala wa Umar kwa miaka thelathini na nne, na akasema kuwa ameuona Msikiti uliojengwa na Umar ukiwa wa umbo la pembe nne wenye ukubwa wa kuchukua watu elfu tatu.

Uwazi ni kuwa kunasibishwa Msikiti wa Al-Aqsa na Umar Ibn Al-Khattab ni dhana katika dhana za Wakristo wamechanganya Umar kuligundua eneo la Msikiti wakadhania amejenga, ikiwa Arcolv atakuwa amesema kweli kuwa aliona sehemu ya pembe nne basi kilikuwa ni kitu kilichoanzishwa na Waislamu wa mji huo ili kulinda sehemu hiyo na hali ya kutoheshimika.

 

 

 

([1]) Ukurasa wa 159, 189 kitabu cha Je Qurani haina makosa?

([2]) Sahihi Bukhari, kitabu cha ubora wa Masahaba, mlango wa Hadithi ya Israa. Hadithi nambari 3673 – 3/1409.

([3]) Sahihi Bukhari, kitabu cha ubora wa Masahaba, mlango wa Miiraj. Hadithi nambari 3674 – 3/ 1410.

Share this:

Related Fatwas