Hukumu ya mwenye kuhitaji kuwepo kw...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya mwenye kuhitaji kuwepo kwa mbwa nyumbani kwake:

Question

Mimi ni mzee, ninateseka na kupooza upande mmoja, natumia kiti cha magurudumu, na ninaishi peke yangu bila mke wala mtoto. Je, inajuzu kwangu kufuga mbwa nyumbani ili nijisaidie katika mahitaji yangu na nijiburudishe katika upweke wangu? Na hukumu ya najisi yake ni ipi kuhusu mimi na anayenitembelea?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:

Asili katika kufuga mbwa ni katazo, na kinachotolewa ruhusa ni hali za dharura na mahitaji; kwa sababu mahitaji huwekwa katika nafasi ya dharura, iwe ni mahitaji ya jumla au ya mtu binafsi. Dharura ni hali ambayo mtu mwenye jukumu la kidini anahitaji kufanya jambo lililokatazwa, la sivyo ataangamia au karibu na maangamio; kama kupoteza kiungo au kupata ulemavu. Na haja ni hali ambayo mtu anahitaji kufanya lililokatazwa, la sivyo ataingia katika mashaka makubwa au dhiki kubwa katika ibada au miamala yake; kama vile maradhi kuzidi au kuwa na uzito zaidi. Haya yote ni kwa sababu Mwenyezi Mungu hakuweka uzito wowote juu yetu katika dini.

Na Mtume (Rehma na amani zimshukie) hakuwa akipewa kuchagua kati ya mambo mawili ila huchagua lililo rahisi zaidi iwapo halina dhambi. Na kwa sababu hiyo, sharia yetu tukufu inaitwa dini iliyo nyooka na iliyo rahisi.

Kwa hiyo, sharia imeruhusu kufuga mbwa pale mtu anapomhitaji kwa ajili ya maisha na kazi yake. Mtume (Rehma na amani zimshukie) amesema, kama alivyosimulia Abu Huraira (radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) "Mwenye kumshika mbwa, hupungukiwa kila siku katika matendo yake mema kwa kiasi cha qirat moja, isipokuwa mbwa wa mifugo, au wa kulinda mashamba au wa kuwinda."

Imehadithiwa na Bukhari na Muslim, na wametaja Hadithi yenye maana karibu na hiyo kutoka kwa Ibn Umar (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie).

Na unajisi wa mbwa ni suala lenye tofauti kati ya Wanazuoni wenye kujitahidi wa Kiislamu: Jumuia ya Wanazuoni (Jamhuri) wanaona mbwa ni najisi, na Madhehebu ya Imamu Maliki wanaona kuwa mbwa ni twahara, na kila upande una dalili na msingi wake.

Hivyo kutokana na swali: Ikiwa uko katika haja kubwa ya mwenye kukusaidia, anzia kwa kutafuta watu wa kawaida kama jamaa, marafiki, majirani au wengineo, hata kama itakuwa kwa kumkodisha mtumishi ikiwa unaweza, na si halali kwako kugeukia mbwa ilhali una uwezo wa kupata hayo. Ikiwa utashindwa kabisa na mambo yakakubana na ukahitaji msaidizi na hukupata ila mbwa, basi hapo inakubalika kufuga mbwa kwa haja hiyo. Na katika hali hiyo, unaweza kufuata rai ya Madhehebu ya Imamu Malik kuwa mwili wa mbwa si najisi, lakini tahadhari na utakase vyombo ambavyo mbwa amelamba (yaani aliyekunywa ndani yake) kwa kuvisafisha mara saba, miongoni mwa hizo mara moja kwa udongo.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

Share this:

Related Fatwas