Hukumu ya Ukeketaji wa wasichana

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya Ukeketaji wa wasichana

Question

Ni ipi hukumu ya ukeketaji wa wasichana, kwani kuna wanaosema kuwa ukeketaji wa wasichana ni wajibu?

Answer

Suala la ukeketaji wa wanawake si suala la kidini la kiibada katika asili yake, bali ni suala linalorejea kwenye mila, desturi, urithi wa kijamii na wa kitiba. Madaktari wamethibitisha kwa yakini kuwa ukeketaji wa wanawake unasababisha madhara ya kitiba na kisaikolojia; na kutokana na hilo, pamoja na kutokuwepo kwa maandiko ya kisharia yaliyo sahihi yanayoweza kutumika kama hoja ya kuwakeketa, basi hukumu yake imekuwa ni haramu.

Maelezo

«Ukeketaji wa wasichana» ni mchakato unaopelekea madhara makubwa kwa afya na usalama wa mwanamke katika upande wa kimwili na kisaikolojia. Hii ni miongoni mwa mila zilizorithiwa ambazo zimeenea nchini Misri kutoka kizazi kimoja hadi kingine; ambapo kulipatikana michoro na maandishi ya Kifarao yanayoonesha mchakato wa ukeketaji, hivyo ukeketaji wa wanawake si miongoni mwa ibada za Kiislamu kama ambavyo baadhi ya watu wanavyopigia upatu jambo hilo.

Ama kutahiri wavulana[1], hiyo ni miongoni mwa Sunna za kimaumbile[2] na ni wajibu kisharia ikiwa hakuna kizuizi cha kufanya hivyo[3].

Baadhi ya Wanazuoni wa Fiqhi walielekea kwenye kuruhusiwa kwa ukeketaji wa wanawake, na wakatoa ushahidi wa jambo hilo kwa baadhi ya Hadithi zilizopokelewa katika Sunna, miongoni mwazo ni:

Hadithi ya Abu Huraira (R.A.) aliyesema: “Nilimsikia Mtume (S.A.W.) akisema: asili ya maumbile (fitra) ni mambo matano: Kutahiri, kunyoa nywele sehemu za siri, kupunguza masharubu, kukata kucha, na kung`oa nywele za kwapani” [Imepokelewa na Al-Bukhari].

Na Hadithi ya Umm Atiyya Al-Ansariyyah (R.A.), kwamba mwanamke mmoja alikuwa akikeketa mjini Madina, Mtume (S.A.W.) akamwambia: “Usikate kupita kiasi kwani hilo ni bora zaidi kwa mwanamke, na linapendelewa zaidi kwa mume” [Imepokelewa na Abu Dawood].

Majibu dhidi ya kauli hii inayoona kuruhusiwa kwa ukeketaji wa wanawake yanatokana na mitazamo kadhaa:

Kwanza: Hadithi hizi walizozitumia kama ushahidi hazimaanishi kuruhusiwa kwa ukeketaji wa wanawake, na ufafanuzi wa jambo hilo ni kama ifuatavyo:

Hadithi ya Abu Huraira (R.A.) imetaja Sunna tano za kimaumbile, miongoni mwazo kuna ambazo ni maalumu kwa wanaume kama kupunguza masharubu na kutahiri, na miongoni mwazo kuna zinazoshirikiana kati ya wanaume na wanawake nazo ni kunyoa nywele za siri, kukata kucha, na kung`oa kwapa. Hivi ndivyo walivyobainisha kundi la Wanazuoni wa Fiqhi. Kutoka kwa Abu Huraira (R.A.) amesema: Mtume (S.A.W.) amesema: “Ibrahim (A.S.) alitahiriwa akiwa na umri wa miaka themanini kwa kutumia shoka[4]»[5]. Hadithi hii inaonesha kuwa kutahiri ni maalumui kwa wanaume na si wanawake.

Ama Hadithi ya Umm Atiyya (R.A.), Wanazuoni wa Hadithi wameiona kuwa ni dhaifu, bali hata Imamu Abu Dawood aliitolea maelezo kwa kusema: «Na Hadithi hii ni dhaifu».

Pili: Imethibitika kutokana na upande wa kitiba kuwa mchakato wa ukeketaji wa wanawake una madhara makubwa kwa afya na usalama wa mwanamke kimwili na kisaikolojia. Na kanuni iliyothibiti kwa Wanachuoni wa Fiqhi ni kwamba «hakuna kudhuru wala kudhuriwa», hivyo imekuwa ni lazima kutoa kauli ya kuharamisha ukeketaji wa wanawake.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Na baada ya ufafanuzi huu, yale yaliyofikiwa na Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri ni uharamu wa ukeketaji wa wanawake, na hiyo ni kwa sababu zifuatazo:

1- Imethibitika kwa madaktari kuwa mchakato wa ukeketaji wa wanawake unapelekea kutokea kwa madhara makubwa juu ya afya na usalama wa mwanamke.

2- Ukeketaji wa wanawake si miongoni mwa ibada za Kiislamu, bali ni miongoni mwa mila zilizorithiwa tangu kale ambazo zimeenea katika baadhi ya nchi kutoka kizazi kimoja hadi kingine, na ziko mbioni kutoweka na kuisha.

Yale yaliyothibiti kwa walio wengi miongoni mwa Wanachuoni wa Fiqhi ni uwajibikaji wa kutahiri kwa upande wa wanaume na si kwa wanawake.

 

[1] «Kutahiri wanaume»: Ni kukata ngozi inayofunika kichwa cha uume (gozi), ili kichwa chote cha uume kionekane. Na «kichwa cha uume»: Ni ncha ya duara ya kiungo cha uzazi cha mwanamume.

[2] «Sunna za Fitra»: Ni desturi ambazo inampasa Muislamu azihifadhi kwa ajili ya usafi wake binafsi, kama kukata kucha na mfano wake.

[3] «Al-Majmu'» cha Al-Nawawi (1/284).

[4] «Al-Qaddum»: Ni chombo kinachotumiwa na seremala.

[5] Imepokelewa na Al-Bukhari.

Share this:

Related Fatwas