Hukumu ya kusafiri bila ya Mahramu

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kusafiri bila ya Mahramu

Question

Je, ni ipi hukumu ya wasichana wanaosafiri kwenda kwenye kambi za mafunzo ili kuwatayarisha kwa kazi ya utumishi, kama vile kufuta ujinga wa kutojua kusoma na kuandika, mbele ya wasimamizi na waandaaji na bila kuchanganywa?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:

Inaruhusiwa kwa mwanamke kusafiri bila mahramu kwa sharti ya kuwa na uhakika wa usalama katika safari yake, mahali pa kukaa, na kurudi kwake, na asikumbane na udhalilishaji wa aina yoyote, iwe ni wa kibinafsi au wa kidini. Hii ni kwa mujibu wa yale aliyosema Mtume (S.A.W) kama ilivyopokewa na Bukhari na wengine kutoka kwa Adi bin Hatim (R.A) ambapo alisema: "Ikiwa utaishi kwa muda mrefu, utamwona msafiri mwanamke akitoka Al-Hira mpaka atembee kuizunguka Kaaba bila ya kuogopa mtu yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu." Na katika riwaya ya Imamu Ahmad: "Naapa kwa yule ambaye roho yangu iko mikononi mwake, Mwenyezi Mungu atakamilisha hili jambo mpaka mwanamke atoke Al-Hira akizunguka nyumba ya Mweneyezi Mungu bila ya kuwa na hofu ya mtu yoyote."

Kutokana na Hadithi hii kwa riwaya zake, baadhi ya Wanazuoni wa Fiqhi wamekubali kwamba mwanamke anaruhusiwa kusafiri peke yake ikiwa anahakikishiwa usalama, na wamesema kwamba Hadithi nyingine zinazoharamisha kusafiri kwa mwanamke bila mahrimu zinahusiana na hali ya kukosekana kwa usalama ambayo ilikuwapo wakati wa zamani.

Vilevile, Wanazuoni wengi wa Fiqhi wanakubaliana kwamba mwanamke anaweza kusafiri kwa ajili ya Ibada ya Hijja ya faradhi bila mahrimu ikiwa atakuwa na wanawake waaminifu au wafuasi waliokubaliwa, na wanajenga hoja hiyo kwa mfano wa wanawake waaminifu waliokwenda Hijja baada ya kifo cha Mtume (S.A.W) katika utawala wa Omar (R.A), ambapo alikuwa ameenda nao Uthman bin Affan (R.A) ili awahifadhi.

Imamu Abu al-Hasan ibn Batal alisema: "Imam Malik, Al-Awzai, na Imamu Shafi walisema kuwa mwanamke anaweza kwenda Hajji ya faradhi akiwa na kundi la wanawake katika kundi la watu waliokwenda kwa usalama, hata kama hana mahrimu. Wengi wa maulamaa wanakubaliana na hilo, na Ibn Umar alikuwa akihiji na wanawake kutoka kwa majirani zake. Hii ni kauli ya Ataa, Sa'id ibn Jubayr, Ibn Sirin, na Al-Hasan al-Basri. Al-Hasan alisema: 'Muislamu ni mahrimu, na huenda baadhi ya wale wasio mahimu wakawa bora kuliko mahrimu[1].'"

Hukumu ya zama ni kwamba safari ya mwanamke peke yake kupitia njia za usafiri salama, kama vile njia zilizojazwa watu na mifumo ya usafiri wa umma kama vile bandari, viwanja vya ndege na mabasi, inaruhusiwa kisheria na hakuna kizuizi kwa hilo. Hii inahusu safari ya lazima, ya kupendeza, au ya kawaida. Hadithi zinazozuia mwanamke kusafiri bila mahrimu zinahusiana na hali ya kutokuwa na usalama ambayo ilikuwa inahusiana na safari za zamani. Lakini sasa, ikiwa kuna usalama, basi amri ya kuzuia haitumiki tena.

Imamu Al-Baji Al-Maliki alisema: "Labda kile kilichosemwa na baadhi ya wafuasi wetu kinahusu hali ya mtu mmoja au wachache tu, lakini kwa misafara mikubwa na njia za umma zilizo na watu na salama, basi mimi nadhani kuwa ni kama nchi zilizo na masoko na wafanyabiashara, kwani usalama huwepo bila ya mahitaji ya mahrimu au mwanamke. Hali hii imepokewa pia kutoka kwa al-Awzai.[2]"

Msomi Al-Khatab Al-Maliki alisema: "Alifanya hivyo Al-Baji akizingatia idadi ndogo, na maneno yake yalikuwa: Hii ni kwangu katika hali ya mtu mmoja au wachache tu, lakini kwa misafara mikubwa, mimi nadhani kuwa ni kama nchi, ambapo safari ya mwanamke inaruhusiwa bila wanawake wengine au mahramu." Hii imetajwa kutoka kwake katika "Al-Ikmāl" na alikubaliana nayo bila kueleza kupinga, na alisema Al-Zanati katika ufafanuzi wa "Al-Risāla" kama maoni ya muktadha, hivyo basi anachokisema msomi na wengine kinaambatana na maoni haya.

Maneno ya Al-Zanati ni: "Ikiwa yuko katika msafara salama wa watu wengi na wenye nguvu au jeshi lenye usalama dhidi ya mashambulizi na msafara mkubwa, hakuna mgongano katika kuruhusiwa safari yake bila ya mahrimu katika aina zote za safari, za lazima, zinazopendekezwa, na zinazoruhusiwa, kulingana na kauli ya Malik na wengine; kwani hakuna tofauti kati ya yale yaliyotajwa hapo juu na mji." Hivyo alivyosema Al-Qabasi[3].

Kutokana na hayo, inaruhusiwa kwa wasichana kusafiri kwenda kushiriki katika kambi za mafunzo kwa ajili ya kufanya kazi za kijamii, mradi tu sehemu watakayokwenda iko salama, hakuna hatari yoyote kwao, na hakuna kizuizi chochote cha kisheria kwao wala kwa walezi wao. Na Mwennyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

[1] Sharhi sahihi Bukhary, 4/532,  chapa Maktabat Rushdy.

[2] Al muntaqy sherh Almuwatwa, 3/95.

[3] Mawaheb Al Jaliyl Sherh Khalil, 2/523, chapa Dar Fikr.

Share this:

Related Fatwas