Hali ya Usimamizi wa Mwenyezi Mung...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hali ya Usimamizi wa Mwenyezi Mungu na Wingi wa baraka za Mola katika kuzaliwa kwake (S.A.W.)

Question

Kuzaliwa kwa Mtume (S.A.W.) kulijawa na bishara njema, iliyojaa aina za Utukufu na hali ya heshima, na kumezungukwa na mazingira ya matukio na mazingira ambayo huwaongoza wale wanaoyatafakari au kuyaangalia kuelekea kwenye mabadiliko yanayotarajiwa. Ilikuwa ni kana kwamba maisha yote, pamoja na wote waliokuwemo, walikuwa wakijiandaa kupokea jambo muhimu, tukio muhimu sana, tukio la kipekee, na msafara mkubwa, yaani, mapokezi ya kuzaliwa kwa Mtume na Nabii

Answer

Kuzaliwa kwa Mtume (S.A.W.) kulijawa na bishara njema, iliyojaa aina za Utukufu na hali ya heshima, na kumezungukwa na mazingira ya matukio na mazingira ambayo huwaongoza wale wanaoyatafakari au kuyaangalia kuelekea kwenye mabadiliko yanayotarajiwa. Ilikuwa ni kana kwamba maisha yote, pamoja na wote waliokuwemo, walikuwa wakijiandaa kupokea jambo muhimu, tukio muhimu sana, tukio la kipekee, na msafara mkubwa, yaani, mapokezi ya kuzaliwa kwa Mtume na Nabii wa Mwisho (S.A.W) kana kwamba ulimwengu unajiandaa kumkaribisha kwa furaha na shangwe, heshima na sifa. Na kwa nini isiwe hivyo? Na amekuja mbora wa wale walioikanyaga ardhi, mtukufu zaidi ya wale walioikaa, mkubwa zaidi ya wale waliopita katika wito wake, na msafi zaidi ya wale walioipanda katika safari ya maisha yake kufikia nyumba ya milele ambapo yuko rafiki wa juu zaidi na uwepo wa Mwenyezi Mungu. Ni kuzaliwa kwa mwanadamu mtukufu kuliko wote, na kuheshimiwa kuliko wote wanaojulikana. Na kwanini isiewe hivyo? Alipanga maisha ya mwanadamu kwa njia bora zaidi: kwa haki, ujuzi, hekima, ukarimu, na ukamilifu. Hilo lilitukia katika wakati ambapo ujinga ulikuwa umeenea, upotofu ulikuwa umeenea, na desturi chafu, sheria zisizo za haki, na hukumu zisizo za haki zilikuwa zimeenea. Kuzaliwa kwake (S.A.W), kulikuwa ni kuzaliwa kwa mwongozo na nuru. Kuzaliwa kunakochukuliwa kuwa ni nafasi ya muujiza, chemchemi ya heshima, mahali pa heshima, mahali pa kuthaminiwa, uwanja wa heshima, na chanzo cha viashiria kwamba kuna mabadiliko yanakuja katika ulimwengu, na kuupeleka kwenye usalama, huuweka huru kutokana na uchafu wa uovu, giza la kiburi, na pingu za giza hadi kwenye utukufu wa nuru na imani. Pia huuweka huru kutokana na athari za ushabiki wa chuki na mila na desturi potofu kwa jamii ya upendo na mazingira ya wema.

Mtume (S.A.W.) amezaliwa katika familia safi, na inayojulikana sana ya nasaba tukufu, iliyotofautishwa na sifa zao njema na fadhila kubwa. Familia yake Mtume (S.A.W) iliunganisha asili ya wema wa Waarabu, ikakumbatia sifa zao za kipekee, na ikajiepusha na kitu chochote ambacho kingeweza kuwa cha aibu au dharau katika tabia. Haya ndiyo aliyoyaeleza Mtume (S.A.W) katika kauli yake: “Mwenyezi Mungu alimteuwa Kinana katika kizazi cha Ismaili, akawateuwa Maquraishi kutoka kwa Kinana, akachagua Banu Hashim kutoka kwa Maquraishi, na akanichagua mimi kutoka kwa Banu Hashim. ([1]).

 Ibn Ishaq anatueleza kuhusu kuzaliwa kwake Mtume (S.A.W), akisema: “Mtume (S.A.W) alizaliwa katika Mwaka wa Tembo. Alikabidhiwa kwa mama yake, na wakatafutiwa mama wanyonyeshaji. Halimah binti wa Abu Dhu’ayb alikuwa ndiye aliyemnyonyesha. ([2]).

Imamu Al-Suhayliy alisema kwamba “Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alizaliwa Jumatatu, usiku wa tarehe kumi na mbili wa Mwezi wa Rabi' Al-Awwal, (Mfungo sita) Mwaka wa Tembo.” ([3]) Ibn Hisham akafuata rai hiyo([4]).

Imamu Al-Suheili anatusimulia sehemu ya kisa cha kuzaliwa kwa Mtume (S.A.W) akisema: “Hakika Amina binti Wahb, mama yake Mtume wa Mwenyezi Mungu, (S.A.W), alikuwa akisimulia kwamba alijiwa alipobeba mimba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, (S.A.W), na akaambiwa: 'Wewe umebeba mimba ya bwana wa umma huu. Atakapotua ardhini, sema: 'Namuombea hifadhi kwa Aliye Mmoja kutokana na shari ya kila mwenye husuda,' kisha mpe jina Muhammad.' Na aliona alipobeba mimba yake kuwa nuru ilitoka kwake, nuru ambayo aliona kwayo majumba ya Basra, katika ardhini ya Sham.” ([5])

Bishara na ishara zilizotangulia kuzaliwa kwake Mtume (S.A.W) zilikuwa nyingi na za aina mbalimbali. Hili linaonesha jinsi Mwenyezi Mungu alivyomtaka na alivyomjaalia kuwa na hadhi ya juu, na jinsi alivyomkirimu na kumpa utukufu. Miongoni mwa bishara hizo ni maneno ya Sayyidna Hassan bin Thabit, ambaye alisema: “Wallahi nilikuwa mvulana mdogo, mwenye umri wa miaka saba au minane, na nilielewa kila nilichosikia nilipomsikia Myahudi akipiga kelele kwa sauti ya juu kutoka juu ya paa la nyumba ya Yathrib: ‘Enyi kundi la Mayahudi!’ Mpaka walipomkusanyikia, wakamwambia: “Ole wako, una nini?” Akajibu: “Usiku wa leo imewaka nyota ya Ahmad, ambaye amezaliwa nayo.” ([6])

Miongoni mwa bishara na ishara zilizoandamana na kuzaliwa kwake Mtume (S.A.W), ni yale yaliyompata Abrahah na jeshi lake, na yale yaliyowakuta. Hili ni tukio kubwa, tukio la ajabu, na jambo la pekee na lisilo na kifani ambalo akili haiwezi kulichukua, ingawa ni ukweli ulio thabiti. Nalo ni kuangamia jeshi la Abrahah kwa mawe madogo yaliyowaangukia vichwani, yakiwafanya wawe kama majani yaliyotafunwa. Ndio, akili haiwezi kuelewa kwamba mawe madogo yana uwezo wa kiakili unaowezesha kupenya kichwa na kuua, baada ya kila jiwe kuelekea kwa yule linayemtaka kumuua, bila kukosea hata kidogo! Je, jiwe dogo linaweza kupanga, kuua, na kufanya yote haya? Hakika hili ni tukio lililo juu ya kiwango cha akili. Lakini lilitokea, kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:{Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo watenda wale wenye tembo? Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika?  Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi, Wakiwatupia mawe ya udongo wa Motoni Akawafanya kama majani yaliyo liwa} [Surat Al-Fil: 1-5]. ([7])

Bishara na ishara hizi hazikuishia hapo. Baadhi ya watu wanasema kuwa ishara zingine zilitokea wakati wa kuzaliwa kwake, zikiwemo kutikisika kwa jumba la mfalme wa Uajemi, Kisra, kuanguka kwa sehemu 14 za juu za jumba hilo, na kuzimika kwa moto wa Wamajusi waliokuwa wakiuabudu. Imamu At-Tabari na wengine wamesema: "Hakika, usiku ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alizaliwa, jumba la Kisra lilitikisika, na sehemu zake 14 za juu zilianguka. Moto wa Uajemi ulizimika, na haukuwahi kuzimika kabla ya hapo kwa miaka elfu moja. Ziwa la Sawah lilipungua maji, na Mubadhani ([8]) (kiongozi wa kidini wa Wamajusi) aliona ndoto ya ngamia wakiongoza farasi wazuri, wakivuka mto wa Digla na kuenea katika nchi yao.

Asubuhi ilipofika, Kisra alishtushwa na kile alichokiona. Akajipa moyo, kisha akaamua kutowaficha mawaziri wake na watawala wa majimbo. Akavaa taji lake, akaketi kwenye kiti chake cha enzi, na akawakusanya. Walipokusanyika, aliwafahamisha kwa nini amewaita. Wakati wakiwa katika hali hiyo, barua ilimfikia ikimjulisha kuzimika kwa moto, na hivyo huzuni yake iliongezeka. Kisha akawaeleza alichokiona na kilichomshitua.

Mubadhani akasema: 'Na mimi pia -Mola aufanye ufalme huu kuwa bora- nimeona ndoto ile ile usiku huu.' Kisha akasimulia ndoto ya wale ngamia. Kisra akamuuliza: 'Hili lina maana gani, ewe Mubadhani?' - Na alijua zaidi ya wote waliohudhuria. Mubadhani akajibu: 'Hili ni tukio litakalotoka kwa Waarabu.' Baada ya kutafsiri ndoto hiyo, ilisemwa: “Ikiwa usomaji utaongezeka, na akapewa utume mbeba fimbo (Mtume S.A.W), na bonde la Samawa likafurika maji, na ziwa la Sawah likapungua maji, na moto wa Uajemi ukazimika, basi Sham haitakuwa Sham tena kwa Satih, na watatawala Wafalme na Malkia, kulingana na idadi ya sehemu za majumba. Na hakika kila jambo linalokuja litakuja.” ([9])

Imamu Al-Busiri alieleza matukio hayo katika mashairi yake maarufu, akisema:

"Kuzaliwa kwake kulionesha utakatifu wa asili yake. Ewe utukufu wa mwanzo na mwisho wake.

Ni siku ambayo Waajemi waliona dalili kuwa Wanaonywa juu ya kufika kwa maangamizi na mateso.

Na ikawa jumba la mfalme Kisra limebomoka, Kama vile kundi la wafuasi wa Kisra lisivyokusanyika tena.

Na moto wa Uajemi ulikuwa umezimika kwa majonzi, Na mto ulikuwa ukitazama kwa huzuni.

Na lilimhuzunisha Sawah kuwa ziwa lake lilipungua maji, Na aliyekuja kutafuta maji alirudishwa akiwa na hasira alipokuwa na kiu." ([10])

Miongoni mwa ishara za kuzaliwa kwake Mtume (S.A.W) ni kuzuiliwa kwa mashetani kusikiliza siri za mbinguni. Hili lililodokezwa na Ibn Hisham, aliposema: "Mashetani walipigwa kwa vimondo kama ishara ya kufika kwa Mtume (S.A.W). Ilipokaribia wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ulipofika wakati wa kutumwa kwake, mashetani walizuiwa kusikiliza siri za mbinguni. Walizuiliwa kufika kwenye viti walivyokuwa wakikalia kwa ajili ya kusikiliza, na ndio maana walipigwa kwa nyota (vimondo). Hapo ndipo majini walipotambua kuwa hili limetokea kwa sababu ya jambo kubwa ambalo Mwenyezi Mungu ameamuru kwa waja." ([11]).

Miongoni mwa ishara hizo, kama ilivyosimuliwa na mwanazuoni Ibn Kathir, "Kutoka kwa Usamah bin Zaid, alisema: 'Zaid bin Amr bin Nufail aliniambia kuwa mwanazuoni wa Kiyahudi kutoka Sham aliniambia: 'Kuna nabii aliyetokea katika nchi yako, au atatokea. Nyota yake tayari imetokea. Rudi nyumbani, muamini, na umfuate.' Bibi Amina alisema: 'Nilipomzaa, nuru ilitoka kwangu iliangaza majumba ya Sham.'"([12]).

Yeyote anayesoma kisa cha Halima As-Saadiya na hali yake kabla na baada ya kumchukua (Mtume S.A.W), atatambua kiasi cha Usimamzi ulezi wa Mwenyezi Mungu. Yeye alikuja Makkah na wanawake wengine kutoka kabila la Banu Saad bin Bakr, wakitafuta watoto wa kunyonesha. Alikuja kwa punda wake dhaifu, na mara tu alipomchukua (Mtume S. A.W) na kaanza safari yake ya kurudi, dalili za heri zilianza kuonekana na baraka ziliongezeka. Riziki zake ziliongezeka, na wema wake ulienea hadi alipoambiwa: "Wallahi, umechukua kiumbe kilichobarikiwa."

Yeyote anayefuatilia kisa cha Bibi Halima na kukiangalia kwa makini, lazima atastaajabu na kushangazwa na wingi wa mafunzo na mifano. Hili ni tukio ambalo linaonesha kuwa mtoto huyu alitayarishiwa mazingira mazuri, alizungukwa na Usimamizi kamili wa Mwenyezi Mungu, na uangalifu wa juu kabisa wa Kimwenyezi Mungu. Kuzaliwa kwake kulifanya mambo makubwa na matatizo yaliyokuwa magumu kuwa na wepesi. Sababu zikawa nyepesi, na viumbe vyote vilimnyenyekea, kana kwamba viliamriwa kumpokea kwa uzuri, vikatoa vilivyo bora zaidi, na vya thamani zaidi. Hili linaonesha hadhi yake kubwa na cheo chake cha juu, kana kwamba yeye ni chemchemi inayotoa baraka, inayomwaga nuru ya wema, na inayomwathiri kila mtu anayekuwa naye, viumbe vyote, na kila mahali alipopita, yeye na wale wote wanaotekeleza amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kumuhudumia (Mtume S.A.W).

Imamu Al-Suheili ameeleza kwamba "Ibilisi (laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake) alipiga kelele mara nne: alipolaaniwa, aliposhushwa (duniani), alipozaliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), na ilipoteremshwa Sura ya Al-Fatiha. Kupiga Kelele na na mikoromo ni katika vitendo vya shetani."

Imepokelewa kutoka kwa Uthman Ibn Abi Al-Aas, kutoka kwa mamake, Ummu Uthman Ath-Thaqafiyyah, ambaye jina lake halisi ni Fatmah binti Abdullah, alisema: "Nilihudhuria kuzaliwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), na niliona nyumba nzima ilijaa nuru, na niliona nyota zikikaribia mpaka nikadhani zitaniangukia." - At-Tabari ameitaja hadithi hii. ([13])

Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alizaliwa akiwa tayari ametairiwa na kitovu chake kimekatwa. Mama yake alikuwa akisimulia kwamba alipokuwa mjamzito, hakuwahi kuhisi uchungu, wala hamu ya kula, wala maumivu kama wanawake wengine wajawazito. ([14]).

Yeyote anayetafakari matukio haya yaliyotangulia atatambua kwa yakini kwamba Mtume (S.A.W) alipewa sifa za kipekee zinazoonesha kuwa alikuwa tofauti na watoto wengine. Alikuwa amebarikiwa kila alipokuwa, hata akiwa tumboni mwa mama yake, kwani mama yake hakupata maumivu au maradhi yanayowapata wanawake, maumivu ambayo Mwenyezi Mungu ameyaeleza katika Qur'ani tukufu:

"Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio." (Luqman: 14)

Baraka ziliendelea kumshika, na hazikumuachana kamwe, tangu kuumbwa kwake tumboni mwa mama yake, wakati wa kuzaliwa, na hata baada ya hapo, hadi alipofikiwa na mauti, huku akiwa mwenye furaha kwa kumpendeza Mola wake.

Pia, maandiko yanaonyesha kuwa Mtume (S.A.W) alizunguukwa na uangalifu wa Mwenyezi Mungu, na msaada za Rehema ya Mwenyezi Mungu zilimfikia. Kuzaliwa kwake kulikuja na ishara za kimwili zinazoonesha hilo kikamilifu, haswa kuzaliwa kwake akiwa tayari amehitaniwa. Pia, kuzaliwa kwake kulizungukwa na bishara za kiroho zinazoelezea utukufu wa nafasi yake.

Miongoni mwa mambo mazuri ni kwamba Abdul-Muttalib alifunguliwa kumpa jina la Muhammad. Hili lilikuwa jina alilosaidiwa kulichagua na malaika mtukufu. Waarabu hawakuizoea majina haya, ndiyo maana walimwuliza: "Mbona umeliacha jina la baba zake?" Naye akajibu: "Nilitaka Mwenyezi Mungu amsifu mbinguni, na viumbe wamsifu duniani." Kwa hivyo, hamu hii ilikuwa kama utabiri wa mambo yajayo, kwani hakuna kiumbe miongoni mwa viumbe wa Mwenyezi Mungu anayestahili shukrani na sifa kwa matendo yake, kama Nabii wa Kiarabu, Muhammad (S.A.W). ([15]).

Siri ya kuitwa kwake Muhammad (S.A.W) ni kwamba jina hilo linafunua sifa zake, linaelezea tabia zake, na linafichua uzuri wake. Hili linaeleza kwa usahihi wa hali ya juu maana yake, kwani neno (H-M-D) linazunguka katika mzunguko wa maana zinazohusiana na: wingi wa sifa, matendo mema, kuridhika, na sifa zingine za juu na tabia nzuri.

Hizi ndizo sifa zilizomuandaa Mtume (S.A.W) kuwasiliana na ufalme wa juu wa Mwenyezi Mungu, kwani sifa hizo husababisha kuchaguliwa, kuteiliwa, na kutumwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ujumbe Wake.

Kwa sababu hiyo, mwanachuoni Abul-Su'ud alisema: "Msingi wa kuchaguliwa kwa utume ni kuwa na sifa na tabia nzuri, na kuwa wa kwanza katika kupata fadhila na heshima, kwa asili na kwa juhudi. Na hakuna shaka yoyote kwamba Mtume (S.A.W) alikuwa katika daraja la juu kabisa na mwisho wa kila daraja katika madaraja ya juu." ([16])

Al-Khalil alisema: "Neno Hamd (sifa) ni kinyume cha kulaumiwa. Ikiwa utasema balawtu faahmadtu (nilimjaribu na nikampata), maana yake ni: nilimpata mwenye sifa nzuri, mwenye matendo yanayosifiwa. Na ninasema hamidtu (ninasifu) kwa sababu hiyo. Na kutoka hapo linatoka neno Mahmada (uzuri). Na Humadaka (sifa yako) ni kwamba utafanya hivi, maana yake: sifa yako ni hii. Na Tahmid (kumshukuru Mwenyezi Mungu) ni kumshukuru Mwenyezi Mungu sana kwa sifa nzuri. Na Ahmad arrajul, maana yake: alifanya kitendo kinachosifiwa. Hamd ni sifa. Na kauli yao: ahmadu ilayka Allah (ninamshukuru Mwenyezi Mungu pamoja nawe), maana yake: ninamshukuru Mwenyezi Mungu pamoja nawe. Na inasemekana kuwa ni sawa na kusema: nakulalamikia. Na kauli yake: inni ahmad ilaykum, maana yake: ninaridhika nanyi." ([17])

Ibn Faris alisema: "Neno (H-M-D) ni neno moja lenye asili moja, linalomaanisha kinyume cha kulaumiwa. Utasema: hamidtu fulanan ahmaduhu (nilimsifu fulani). Na mtu anaitwa Mahmud au Muhammad ikiwa sifa zake nzuri ni nyingi na hajalaumiwa. Na kwa sababu hii, Mtume wetu (S.A.W) alipewa jina la Muhammad. Waarabu wanasema: humadaka an taf'al kadha, maana yake: lengo lako ni kufanya hili, na kitendo chako kinasifiwa na hakilaumiwi. Na unasema ahmadtu fulanan, ikiwa umempata mwenye kusifiwa." ([18]).

Hivyo, Mtume (S.A.W) alijulikana kwa tabia njema, asili ya ukarimu, na sifa nzuri. Kwa ruhusa ya Mola wake, alijumuisha sifa zote njema, na ndiyo maana watu wa mbinguni na duniani walimsifu. Hili linathibitishwa na kauli ya mama wa Waumini, Aisha, aliposema: "Tabia yake ilikuwa Qur'ani." ([19]) Hii inatupeleka kwenye uelewa mpana na wa jumla kwamba kila tabia njema iliyotajwa katika Qur'ani, Mtume (S.A.W) aliitumia. Yeye alikuwa tafsiri hai na mfano mzuri wa utekelezaji wake.

Alikuwa kama Qur'ani inayotembea ardhini, akiwakilisha Qur'ani kwa kauli na vitendo, kwa wito na tabia, kwa amri na makatazo, kwa uthubutu na kujizuia, kwa kukubali na kukataa.

Miongoni mwa matokeo mazuri ya jina hili, ni kwamba lilitumika kama kinga kwa Mtume (S.A.W), silaha ya kujibu maadui zake, na dawa ya faraja. Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alisema: "Je, hamstaajabishwi jinsi Mwenyezi Mungu anavyozizuia matusi na laana za Maquraishi kwangu? Wanamtusi Mudhmmam (mwenye kulaumiwa) na kumlaani Mudhmmam, lakini mimi ni Muhammad (mwenye kusifiwa)." ([20])

Kuzungumzia kuzaliwa kwake (S.A.W), kwa kweli kunaelezea ishara za uangalizi wa Mwenyezi Mungu na baraka za Mola ambazo zilihusisha tukio hili la kipekee ambalo lilibadilisha ramani ya dunia. Lilileta utaratibu mpya unaoelezea hadhi yake na umuhimu wake. Pia, lilionesha matokeo ya kuzaliwa kwake, ambayo yaliwakilishwa katika wito ulioleta wema wote na kuondosha shari ya aina zote. Kwa sababu hii, kuzaliwa kwake kulikuwa ni tangazo la mwisho wa dhulma, kutoweka kwa zama zake, na tiba ya athari zake.

Kuzaliwa kwake (S.A.W) kulikuwa ushahidi wenye kung'aa wa utunzaji wa Mwenyezi Mungu. Labda matukio na ishara zilizofuatana na kuzaliwa kwake zinathibitisha kwamba kuzaliwa kwake kulikuwa ni kuzaliwa kwa wema, ulioirudisha ubinadamu kwenye njia sahihi. Uliikomboa dunia kutokana na uchafu wa ulimwengu na giza la ujinga, na dalili za mwisho wa dhulma zilianza kuonekana. Matukio yaliyoambatna na kuzaliwa kwake yalionesha upekee na utofauti wake. Ubinadamu haujawahi kuona mfano wake, na hakuna mfano wake. Sifa zote nzuri zilikusanyika kwake, na tabia zote zilikamilika kwake. Alikuwa kama alivyosema Mola wake: " Na hakika wewe una tabia tukufu." (Al-Qalam: 4)

Na alikuwa kama alivyoelezea mwenyewe (S.A.W); imesimuliwa: "Baadhi ya masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) walimwambia: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tuambie kuhusu nafsi yako.' Akasema: 'Ndiyo. Mimi ni maombi ya baba yangu Ibrahim, na bishara ya ndugu yangu Isa. Mama yangu aliona wakati wa mimba yangu kuwa nuru ilitoka kwake na ikawaangazia majumba ya Sham, na nilinyonyeshwa maziwa na kabila la Banu Saad bin Bakr. Nilipokuwa na ndugu yangu nyuma ya nyumba zetu, tukichunga mbuzi wetu, walinijia wanaume wawili waliovaa nguo nyeupe, wakiwa na beseni la dhahabu iliyojaa theluji. Kisha walinishika, wakapasua tumbo langu, na wakautoa moyo wangu. Wakaupasua, na wakatoa kipande cheusi cha damu, wakakitupa. Kisha wakasafisha moyo wangu na tumbo langu kwa theluji hiyo mpaka vikang'aa. Kisha mmoja wao akamwambia mwenzake: 'Mpime sawa na watu kumi katika umma wake.' Wakanipima na nikafikia uzani wao, na mimi nikawa mzito kuliko wao. Kisha akasema: 'Mpime sawa sawa na watu mia moja katika umma wake.' Wakanipima na nikafikia uzani wao, na mimi nikawa mzito kuliko wao. Kisha akasema: 'Mpime sawa na watu elfu katika umma wake.' Wakanipima na nikafikia uzani wao, na mimi nikawa mzito kuliko wao. Kisha akasema: 'Mwache! Wallahi, ukimpima na umma wake wote, atakuwa mzito kuliko wao.'"([21])

Imamu Ahmad alisimulia kutoka kwa Irbadh Ibn Sariya, alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alisema: "Mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, hitimisho la Manabii, na Adam alikuwa bado amelala katika udongo wake. Na nitawafahamisha mwanzo wa hilo: ni maombi ya baba yangu Ibrahim, bishara ya Isa juu yangu, na ndoto ya mama yangu aliyoyaona." ([22]).

 

 

 

 


([1])  Sahih Muslim, Kitabu: Wema, Sura: Fadhila za ukoo wa Mtume, (S.A.W), na salamu ya jiwe juu yake Mtume (S.A.W), kabla ya utume, (4/1782), No.: (2276).

([2])   Wasifu wa Ibn Ishaq, umehaririwa na: Suhail Zakar, uk. 48, Dar Al-Fikr - Beirut, chapa ya 1, 1398 AH - 1978 AD.

([3]) Al-Rawd Al-Anf katika Kuelezea Wasifu wa Mtume cha Ibn Hisham, cha Abu Al-Qasim Abd Al-Rahman bin Abdullah bin Ahmed Al-Suhayli (aliyefariki 581 AH), kilichohaririwa na: Omar Abd Al-Salam Al-Salami, (2/93), Dar Ihya Aluttion, Al-Turath Al-Turath, 1421 AH - 2000 AD.

([4]) Sira ya Mtume ya Ibn Hisham, kilichohaririwa na: Mustafa Al-Saqa, Ibrahim Al-Ibyari, na Abdul Hafeez Shalabi, (1/158), Kampuni ya Maktaba na Uchapishaji wa Mustafa Al-Babi Al-Halabi na wanawe katika Misri, chapa ya 2, 1375 AH - 1955 AD.

([5])   Al-Rawd Al-Anf (2/92).

([6]) Sira ya Mtume wa Ibn Hisham, (1/159).

([7])  Sira ya Mtume na Wito katika Enzi ya Makka, Ahmad Ahmad Ghuloush, uk. 166, Taasisi ya Al-Risala, toleo la 1, 1424 AH - 2003 AD.

([8])  Mawbadan ni kwa Majusi jinsi Jaji Mkuu alivyo kwa Waislamu. Mwandishi wa kamusi alisema: Mawbadan ni faqihi wa Kiajemi na mtawala wa Majusi (1/339).

([9])   Historia ya Al-Tabari, 2/166, Dar Al-Turath - Beirut, chapa ya 2, 1387 AH.

([10])   Burdah ya Al-Madih, Al-Busayri, uk. 12, Dar Al-Turath Al-Budaylmi.

([11])  Sira ya Mtume ya Ibn Hisham, (1/204) yenye marekebisho kidogo.

([12]) Tazama: Al-Bidayah wa al-Nihayah, Ibn Kathir, kilichohaririwa na: Abdullah bin Abdul Mohsen Al-Turki, (3/394), Dar Hijr kwa Uchapishaji, Uchapishaji, Usambazaji na Utangazaji, toleo la 1., 1418 AH - 1424 3 3 AH = 19 BK = 20 Sira ya Mtume. Zama za Meccan, uk. 154.

([13])   Historia ya Al-Tabari, (2/157).

([14])  Al-Rawd Al-Anf, (2/93 na zifuatazo), na baadhi ya marekebisho.

([15])  Fiqh Al-Seerah, Muhammad Al-Ghazali, uk. 62, Dar al-Qalam - Damascus, toleo la 1, 1427 AH.

([16])  Tafsiri ya Abu al-Su`ud, 4/117, Dar Ihya’ al-Turath al-`Arabi – Beirut.

([17])  Al-Ain, Al-Khalil bin Ahmed Al-Farahidi (aliyefariki mwaka 170 AH), kilichohaririwa na: Dk. Mahdi Al-Makhzoumi, Dk. Ibrahim Al-Samarra’i, 3/188-189, Dar na Maktaba ya Al-Hilal - imetoholewa. Kifungu: (H M D).

([18])  Viwango vya Lugha, Ibn Faris, (aliyefariki 395 AH), kilichohaririwa na: Abdul Salam Muhammad Harun, 2/100 Dar Al Fikr 1399 AH - 1979 AD – ilichukuliwa.

([19])  Musnad Ahmad, 42/183, No. (25302).

([20])   Sahih Al-Bukhari: Kitabu: Wema, Sura: Yaliyotajwa kuhusu majina ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, (S.A.W), (4/185), No.: (3533).

([21])   Sira ya Mtume na Ibn Hisham, (1/166-167), imebadilishwa kidogo. Historia ya Al-Tabari: 2/165, imerekebishwa kidogo. Al-Rawdh Al-Anf, (2/108 na ifuatayo), iliyorekebishwa kidogo.

([22])   Musnad Ahmad, (28/379), Na.: (17150).

Share this:

Related Fatwas