Ni yale alivyohusishwa navyo –upeke...

Egypt's Dar Al-Ifta

Ni yale alivyohusishwa navyo –upekee- (S.A.W) miongoni mwa miujiza

Question

Vipengele vya ukuu katika haiba ya Mtume (S.A.W) ni vingi na vya aina mbalimbali; na miongoni mwake ni yale alivyohusishwa navyo vya miujiza na alivyoboreshwa kupitia Aya. Kwani miujiza yake imekuwa mingi zaidi ya kuhesabiwa kwa maneno, na tukufu zaidi ya kuelezwa na kauli, na kukusanywa na vitabu, au kuzingirwa na matukio.

Answer

Vipengele vya ukuu katika haiba ya Mtume (S.A.W) ni vingi na vya aina mbalimbali; na miongoni mwake ni yale alivyohusishwa navyo vya miujiza na alivyoboreshwa kupitia Aya. Kwani miujiza yake imekuwa mingi zaidi ya kuhesabiwa kwa maneno, na tukufu zaidi ya kuelezwa na kauli, na kukusanywa na vitabu, au kuzingirwa na matukio.

Na hizi hapa baadhi ya athari ndogo mno miongoni mwake — zinazoonyesha wingi wake, na kuonesha tofauti na aina zake, na kuvutia macho kuelekea upana wa aina yake. Na miongoni mwa miujiza yake ya kwanza ni Qur’ani Tukufu — muujiza wa kudumu — iliyokuja kutokana na aina ya yale ambayo watu wake walibobea, lakini ikaja kwa mtindo wa pekee, mpangilio wa ajabu, na uwiano wa kupendeza. Walipoisikia, walishindwa kuifananisha. Washirikina wakadai kuwa Muhammad (S.A.W) ndiye mwenye kuiandika, basi Mweenyezi Mungu aliyetukuka akateremsha kauli Yake: “Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini! Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli.” [Aṭ-Ṭūr: 33–34]

Kisha akawapinga waje na sura kumi, wakashindwa. Na Mwenyezi Mungu akasimulia hilo akisema: “Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni Sura kumi zilizo zuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.  Na wasipo kuitikieni, basi jueni ya kwamba (hii Qur'ani) imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana mungu ila Yeye. Basi je! Nyinyi ni Waislamu?” [Hūd: 13–14]

Kisha akawapinga waje na sura moja tu, wakashindwa. Na Qur’ani ikalitaja hilo katika sehemu tofauti; Mwenyezi Mungu akasema: “Na ikiwa mko katika shaka juu ya yale tuliyoteremsha kwa mja wetu, basi leteni sura moja mfano wake. Na waiteni mashahidi wenu badala ya Allah ikiwa nyinyi ni wakweli. Lakini msipofanya — na kamwe hamtaweza kufanya — basi jihadharini na moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa kwa ajili ya makafiri.” [Al-Baqarah: 23–24] Na akasema: “Au wanasema ameizua? Sema: ‘Basi leteni sura moja mfano wake na waiteni muwezavyo badala ya Allah ikiwa nyinyi ni wakweli.’” [Yūnus: 38]

Hakika changamoto hii aliyoisimulia Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwetu, ni kwa ajili ya kufichua udhaifu wa wazi wa kuweza kuifananisha au kuja na kitu mfano wake. Na hili ndilo linalothibitishwa na maandiko ya kidini; Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Sema: Lau wanadamu na majini wakikusanyika ili walete mfano wa Qur’ani hii, hawataleta mfano wake hata wakisaidiana wao kwa wao.” [Al-Isra: 88]

Na katika hadithi kutoka kwa Abū Hurayrah (RA) kutoka kwa Mtume (S.A.W) amesema: “Hakuna nabii yeyote miongoni mwa manabii isipokuwa alipewa ishara ambazo watu waliziamini kwa sababu yake. Na hakika nilichopewa mimi ni Wahyi aliyonifunulia Mwenyezi Mungu, na ninatarajia kuwa mimi ndiye nitakayekuwa na wafuasi wengi zaidi Siku ya Kiyama.”

Hakika tupo mbele ya maandiko haya, inadhihirika kwetu ukuu wa haiba hii na upekee wake — kutokana na yale aliyopewa ya miujiza, hata kama walishirikiana na manabii wengine katika sifa hii. Lakini miujiza yake na aina zake mbali mbali zinaonesha ukuu wake, na zinaweka wazi nafasi yake, na zinaashiria upekee wake, na zinathibitisha daraja yake Na miujiza hiyo ilikuja kwa aina mbili: ya kiroho (ya kiakili) na ya kihisia.[1]

Ama ya kiroho (ya kiakili) basi ni ya kiakili na ni ya kudumu, na sifa hii inafaa kwa asili ya risala aliyoileta Mtume (S.A.W)    kwani ilikuwa ndiyo risala ya mwisho na kwa watu wote hadi Siku ya Kiyama. Na kwa sababu hiyo, Imamu As-Suyuti (RA) akasema:

 “Kwa sababu sheria hii ilipokuwa ya kudumu katika kurasa za zama hadi Siku ya Kiyama, ikahusishwa kwa muujiza wa kiakili wa kudumu; ili watu wa wenye kuona kwa basira waione.” Na kama alivyosema (S.A.W): ‘Hakuna Nabii yeyote miongoni mwa Manabii isipokuwa alipewa miongoni mwa ishara ambazo watu waliziamini kwa sababu yake. Na hakika nilichopewa mimi ni Wahyi aliyonifunulia Mwenyezi Mungu, na ninatarajia kuwa mimi ndiye nitakayekuwa na wafuasi wengi zaidi Siku ya Kiyama.[2]

Imesemwa kwamba maana yake ni kwamba miujiza ya Manabii wengine ilitoweka kwa kutoweka kwa zama zao; basi hakuihushuhudia isipokuwa yule aliyekuwepo. Na muujiza wa Qur’ani ni wa kudumu hadi Siku ya Kiyama na unazivunja ada kwa mtindo wake na ufasaha wake na habari zake za mambo yasiyoonekana, na hakuna zama zinazopita isipokuwa hufichuka ndani yake baadhi ya yale aliyotangaza kuwa yatakuwa — yanayoashiria usahihi wa dai lake.

Na imesemwa: maana yake ni kwamba miujiza ya wazi ya kale ilikuwa ya kihisia inayoonekana kwa macho — kama ngamia wa Swaleh na fimbo ya Musa — na muujiza wa Qur’ani unaonekana kwa wazi; basi yule anayefuata kwa ajili yake ni wengi zaidi. Kwa sababu yule anayeshuhudia kwa macho ya kichwani hupotea kwa kupotea kwa waliokuwa pamoja naye, na yule anayeshuhudia kwa macho ya akili hubakia na hushuhudiwa na kila anayekuja baada ya wa mwanzo kwa mwendelezo.”[3]

Na alichokitaja Imamu As-Suyuti, kilithibitishwa na Al-‘Allama Ibn Khaldun kwa kauli yake: “Tambua kwamba muujiza mkubwa zaidi, mtukufu zaidi, na wa wazi zaidi kwa dalili ni Qur’ani Tukufu iliyoteremshwa kwa Nabii wetu Muhammad (S.A.W) Kwani kwa kawaida miujiza hutokea kuwa tofauti na Wahyi anaopokea Nabii na huja muujiza kama ushahidi wa ukweli wake. Na Qur’ani yenyewe ndiyo Wahyi anaodai, nayo ndiyo muujiza wa kuvunja ada. Basi ushahidi wake umo ndani yake yenyewe na haihitaji dalili nyingine tofauti nayo kama zilivyo miujiza mingine pamoja na Wahyi. Basi ni dalili iliyo wazi zaidi kwa sababu dalili na kinachodhihirishwa zimeungana ndani yake. Na hii ndio maana wa kauli yake (S.A.W): ‘Hakuna nabii yeyote miongoni mwa manabii isipokuwa alipewa miongoni mwa ishara ambazo watu waliziamini kwa sababu yake. Na hakika nilichopewa mimi ni Wahyi aliyonifunulia Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ninatarajia kuwa mimi ndiye nitakayekuwa na wafuasi wengi zaidi Siku ya Kiyama.’”[4]

Anaashiria kwamba muujiza unapokuwa katika daraja hii ya uwazi na nguvu ya dalili na kuwa ndiyo Wahyi wenyewe — basi kuamini kwake huwa kwa wingi zaidi kwa uwazi wake, hivyo wakaongezeka wenye kusadiki na kuamini, ambao ndiyo wafuasi na umma.”[5]

Top of Form

Bottom of Form

Na kwa msingi huu, Qur'ani Tukufu ni mojawapo ya miujiza ya Mtume (S.A.W)  na ndiyo yenye athari kubwa zaidi na manufaa makubwa zaidi, nayo inaonesha dalili za ukubwa katika utu wake (S.A.W)  kwa mambo kadhaa; miongoni mwa hayo ni:

Kwanza: Kwamba Qur'ani Tukufu ni muujiza, na kwa kuwa ni muujiza ni lazima ibaki katika maandiko haya haya, la sivyo ingepotea sifa ya kuwa muujiza.[6] Na kwa ajili hiyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu amechukua dhamana ya kuihifadhi; Amesema: "Hakika Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho (Qur'ani), na hakika Sisi ni Wenye kuihifadhi." [Al-Hijr: 9]

Na hili halikupatikana kwa vitabu vingine vilivyoteremshwa, na ndiyo inayodhihirisha juu ya utukufu wa daraja yake na cheo chake (Rehma na amani zimshukie), jambo linalothibitisha ukubwa wake.

Pili: Kwamba dalili ya Qur'ani Tukufu juu ya Utume wa Muhammad (S.A.W) si kama dalili ya miujiza mingine; kwa sababu mingine — hata ikiwa ni matendo yasiyoonekana isipokuwa kwa mikono ya Manabii — imekatika uhusiano na kazi ya utume, malengo ya wahyi, na maana ya sharia. Ama Qur'ani Tukufu, dalili yake juu ya ukweli wa utume na hakika ya dini ni kama dalili ya kuponya kwa tabibu, na Qur'ani Tukufu inaubeba muujiza wake ndani yake yenyewe; ili ibaki kuwa shahidi na ushahidi juu ya ukweli wa madai na ujumbe kwa pamoja.

Na kwa hiyo, Qur’ani Tukufu ni kuendelea kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa watu, na ni ushahidi kwa kila mtu aliyefikiwa na Aya za Qur’ani hii na kuelewa yale yaliyo ndani yake ya wito kwa Mwenyezi Mungu; ndiye mtume kwa watu mpaka Mwenyezi Mungu atakaporejesha ardhi na walio juu yake; Mwenyezi Mungu amesema: “Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami ni mbali na mnao washirikisha." [Al-An‘am: 19]

Tatu: Qur’ani Tukufu imejumuisha yote yaliyokuja kwa mitume na vitabu vyao katika yanayohusu imani, sheria, amri, na maadili, huku ikiongoza kwa ustawi.

Nne: Ukweli wa Qur’ani haupingani na akili yenye afya wala sayansi thabiti yenye uhakika; kwa sababu ni kweli ambayo uongo hauwezi kuja kwake, na kwa sababu ni uteremsho kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye hekma na Mwenye kusifiwa; Mwenyezi Mungu amesema: "Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa." [Fussilat: 42]. Kwa hiyo, ni lazima iongoze juu ya mengine, pamoja na sifa nyingine nyingi zinazohitaji muda mrefu kuzitaja.

Qur’ani Tukufu ni kitabu cha juu zaidi miongoni mwa vitabu vilivyoteremshwa, cha maneno ya kweli zaidi, cha sifa kamili zaidi, cha hadhi ya juu zaidi, cha athari kubwa zaidi, na cha ufafanuzi mkali zaidi. Zaidi ya hayo ni kitabu chenye lugha nzuri na kumbukumbu yenye hekima, kinajumuisha:

Kuonyesha ukweli wa yaliyopita kwa usahihi na kuunga mkono kwa ushahidi kutoka vitabu vya watu wa Kitabu, pamoja na kwamba kimeteremshwa kwa mtu ambaye hakujua kusoma na kuandika, na hakuwahi kupata elimu za zamani wala habari za waliotangulia;

Wala habari za waliotangulia, watu hawakupata kushangaa isipokuwa kwa wahyi wake kuhusu yaliyokuwa ya habari zenye manufaa, ambazo yafaa kutajwa kwa mazingatio kwayo, za habari za mataifa pamoja na manabii, na yaliyokuwa kutoka kwao katika mambo yao pamoja nao, na jinsi Mwenyezi Mungu alivyowaokoa waumini na kuwaangamiza makafiri, kwa maneno ambayo hapana mwanadamu awezaye kuja na mfano wake milele, na zama zote;  mahali pengine kisa huelezwa kwa muhtasari kwa ukamilifu wa bayana na ufasaha, na wakati mwingine hurefushwa, basi hapana utamu zaidi, wala dhahiri zaidi, wala bora zaidi kuliko muktadha huo, hata kwamba msomaji au msikilizaji huwa kama anashuhudia yaliyokuwa yupo hapo, anaona habari hiyo mwenyewe.[7]

Basi tukiendelea kwenye aina ya pili ya mwujiza wake (S.A.W)   ambayo ni mwujiza wa hisia ambao unatofautiana na aina ya kwanza kwa kuisha kwa matendo yake na kubaki kwa athari, mafundisho na siri zake, tunagundua kuwa aina hii ni nyingi mno kuzihesabu na kubwa mno kuhesabika, jambo ambalo linathibitishwa na kutokea kwake katika vitu visivyo hai, mimea, wanyama, na uponyaji wa wagonjwa.

Ipo mingi na inayotafautiana, lakini mimi nitaweka mkazo kwenye moja tu ya mwujiza hizi, ambayo ni mwujiza wa l-Isra na Miraji[8] Mwujizahuu umetajwa katika Qur’ani Tukufu sehemu mbili:

Mahali pa kwanza: Inazungumzia kuhusu Israa kwa ufupi katika Aya yake Mwenyezi Mungu anasema: SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.}[Al-Isra’: 1]

Aya hii ni wazi na imethibitisha tukio la Israa, na wafasiri wote wanataja maana yake kwa tukio la Israa; Qur’ani Tukufu inatuambia kuhusu usafiri wake (S.A.W) usiku kutoka Msikiti Mtukufu (Haram) na kwenda Msikiti wa Aqsa, ambalo uko Baytul-Muqaddas.

Mahali pa pili: Inazungumzia kuhusu safari ya Miraji kwa ufupi katika aya za Qur’ani zifuatazo:

{1-Naapa kwa nyota inapo tua, 2. Mwenzenu huyu hakupotea, wala hakukosea. 3. Wala hatamki kwa matamanio.4. Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa; 5. Amemfundisha aliye mwingi wa nguvu, 6. Mwenye kutua, akatulia,7. Naye yuko juu kabisa upeo wa macho. 8. Kisha akakaribia na akateremka.  9. Akawa ni kama baina ya mipinde miwili, au karibu zaidi. 10. Akamfunulia mja wake (Mwenyezi Mungu) alicho mfunulia. 11. Moyo haukusema uwongo uliyo yaona.12. Je! Mnabishana naye kwa aliyo yaona? 13. Na akamwona mara nyingine, 14. Penye Mkunazi wa mwisho. 15. Karibu yake ndiyo ipo Bustani inayo kaliwa. 16. Kilipo ufunika huo Mkunazi hicho kilicho ufunuika. 17. Jicho halikuhangaika wala halikuruka mpaka.18. Kwa yakini aliona katika Ishara kubwa kabisa za Mola wake Mlezi.} [An-Najm: 1-18]

Hii ni moja ya miujiza iliyochaguliwa kwa sababu ya malengo na siri zake, na pia kwa vile inakumbusha kuhusu haki na wajibu na miongoni mwa mambo mengine ambayo ni:

Kwanza - Heshima kwa Nabii (S.A.W) na Kuinuliwa kwa cheo chake:

Miongoni mwa malengo ya muujiza huu ni kwamba Mwenyezi Mungu  alitaka kumuonyesha Mtume wake (S.A.W) dalili zake kuu na ushahidi wake mkubwa katika uumbaji wa mbingu na ardhi, kumuonyesha malaika wake wa juu, na kukutana na ndugu zake miongoni mwa Manabii na Mitume, kisha kumwinua kupitia mbingu kuanzia ya kwanza hadi ya saba, halafu hadi Sidratul Muntaha, mahali ambapo anaweza kusikia sauti za kalamu na mazungumzo ya Malaika; yote hayo ni kwa ajili ya kumheshimu, kuonyesha nafasi yake, na kumfahamisha kuhusu hadhi na daraja lake, ambayo ilifafanuliwa katika mwanzo wa sura ya Al-Isra’ kwa kusema: (ili tuonyeshe baadhi ya dalili zetu). Aya hiyo inaonyesha kwamba Mwenyezi Mungu alitaka kufunua uwezo wake na kumuonyesha Mtume nafasi yake.[9]

Hasa kwa kuwa safari hii yenye baraka – kwa maoni yanayokubalika zaidi – ilitokea katika mwaka wa huzuni; kwa hiyo lengo kuu lilikuwa kumfariji na kumtuliza Mtume Muhammad (S.A.W) baada ya majonzi na majaribu mengi yaliyomkumba (S.A.W)  katika maisha yake; kuanzia kifo cha mke wake mama wa Waumini Sayyida Khadija bint Khuwaylid  aliyempa msaada wa kifedha na kiroho, kisha kifo cha mjomba wake Abu Talib aliyejitahidi kwa dhati kumsaidia na kumlinda, na pia baada ya ukatili wa watu wa Ta’if na jinsi alivyodhihakiwa na vijana na wasiofahamu, pamoja na kuingia kwake kwa hifadhi kwenye ulinzi wa  Almutem bin ‘Adi.

Pili - Kuhamisha Mtume (S.A.W) kutoka maarifa ya yakini hadi kuona kwa macho ya yakini:

Miongoni mwa malengo ya safari hii yenye baraka ni kutimiza lengo hili la juu, na kumfanya (S.A.W) atoke kwenye kuamini kwa kusikia hadi kuona kwa macho; ili aone kwa macho yake mbingu za juu, yaliyomo ndani yake na yale yaliyomo juu yake; ili kile kilichokuwa ni cha kusikika kinakuwa kinachoonekana kwa macho. Ibnu Kathir alisema: «Na kwa kuwa usiku wa Isra’ alipelekwa kutoka mbingu moja hadi nyingine mpaka akamsalimia  Idris, ambaye alikuwa katika mbingu ya nne, kisha akapita kwenye ya tano, halafu kwenye ya sita, akamsalimia Musa hapo, kisha akapita kwenye ya saba, akamsalimia Ibrahim Al-Khalil karibu na Bayt Al-Ma’mur, kisha akapita zaidi ya hapo, akapandishwa hadi mahali ambapo anasikia sauti za kalamu, akafika Sadrat al-Muntaha, akaona Peponi na Moto wa Jahannam na dalili nyingine kuu, akaongoza swala pamoja na manabii, akafuatwa na wakaribishwa kutoka kila mbingu, na radhi ya Mungu ikamsalimia mlinzi wa Peponi na mlinzi wa Moto wa Jahannam. Hii ndiyo heshima, hii ndiyo hadhi, hii ndiyo utukufu, tangazo, kuwa mbele, juu na ukubwa, sala na amani za Mungu ziwe juu yake na manabii wote wa Mwenyezi Mungu.”[10]Top of Form

Bottom of Form

Tatu - Kukata uhusiano wa moyo kwa sababu:

Hili ni moja ya malengo makuu ya safari hii; kwani Mwenyezi Mungu – Mtukufu – aliumba ulimwengu na kuweka kanuni za muunganisho kati ya vipengele vyake au kati ya sababu na matokeo; lakini mara nyingine sababu na matokeo yanaweza kusimamishwa bila kufanya kazi pale ambapo Mwenyezi Mungu anataka hivyo; Mwenyezi Mungu alisema:{Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani zipitazo mito kati yake. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda atakayo.} [Al-Hajj: 14] Mwenyezi Mungu – Mtukufu – ingawa huunganisha matokeo na sababu, ndiye Muumba wa vyote viwili; tukitazama vitu vinavyosababisha athari na kufikiria kwa kina, tunagundua kuwa si lazima akili iangalie vitu hivyo kama visababisha moja kwa moja athari hizo; mfano joto hulainisha barafu na baridi hupeleka maji kuwa ya mgando; lakini kwa uhalisia wa vitu hivyo akili haoni sababu ya moja kwa moja inayolazimisha athari ya matokeo hayo.[11]

Kwa hivyo, kuendelea kwa matukio katika muktadha wa kawaida tunayoiona si lazima; bali ni matokeo ya tabia ya kawaida, na uhusiano kati ya sababu na matokeo si lazima kila wakati; hili linaonekana wazi katika safari hii yenye baraka; kwa wakati ambapo kawaida kuchukua miezi miwili au zaidi kuvuka umbali kati ya msikiti wa Haram na Msikiti wa Aqsa, Mtume Muhammad (S.A.W) alivuka umbali huo ndani ya saa chache tu, jambo ambalo lisilowezekana kwa hali halisi.

Hivyo, amri ya Mwenyezi Mungu inathibitisha tukio hili, na Mtume (S.A.W) anawaambia watu wake kuhusu kilichotokea kwake akiwa na ufahamu wa majibu yao, mwenendo wao mbaya, na jitihada za kuwahamasisha wasiotia shaka waliokuwa tayari kuamini ujumbe wake; lakini hakujali chochote kuhusu haya yote, kwani alivua uhusiano wa moyo na sababu, na aliungana moja kwa moja na Mhusika mkuu, ambaye ni Mwenyezi Mungu.

Nne - Pia moja ya malengo ya safari hii ni kuwakumbusha umuhimu wa kuwa na imani kamili katika uwezo wa Mwenyezi Mungu na ukomo wa uwezo wa binadamu pamoja na maarifa yake:

Kwani safari hii ilionyesha kuwa binadamu kwa akili na maarifa yake, pamoja na msaada wa wanadamu wengine na kile alichokifikia kwa ugunduzi na uvumbuzi, ana uwezo mdogo na maarifa hafifu, hivo hawezi kufikia isipokuwa ndani ya mipaka maalumu na wala hafikii mbinguni; kwa maana hili ni suala la akili ya binadamu, lakini katika safari hii yenye baraka jambo hilo ni la Mwenyezi Mungu peke yake ambaye hakuna kitu kinamshinda.

Uwezo wa Mungu ulionekana wazi katika tukio hili ambalo lilizidi vipimo vya muda, na hakuna cha kushangaza kuhusu hilo; maana akili ni dhaifu, taswira ni dhaifu, vifaa ni duni, na yote yanategemea imani sahihi kwa Mwenyezi Mungu — kiini chake, sifa zake, uwezo wake, uumbaji wake na uundaji wa ulimwengu na kila kilicho ndani yake.

 

 

Tano - Kusisitiza uhusiano wa kiroho kati ya Waislamu:

Safari hii ilikuja kama mfano wa muunganiko wa kiroho kati ya Waislamu walioko katika mataifa mbalimbali, tamaduni tofauti, lugha tofauti, na rangi mbalimbali, na kwa wakati huo huo kama ishara ya kuleta umoja wa Sharia za mbinguni na umoja wa ujumbe wa mbinguni katika lengo na mwongozo wake. Hili linaonekana katika kuunganika kwa Msikiti Haram na Msikiti Al-Aqsa; Na Masjid Al-Aqsa, ambao ni kibla ya kwanza kati ya qibla mbili na msikiti wa tatu mtukufu.  na Msikiti Haram ni mahali pa kupokea wahyi uliopokelewa na Khalilur Rahman Ibrahim na mwanawe Ismail (RA), na baadaye Mtume wetu Muhammad (S.A.W) Nyumba ya Haram ni nyumba ya kwanza iliyowekwa kwa ajili ya watu; Mwenyezi Mungu amesema: "Hakika nyumba ya kwanza iliyowekwa kwa ajili ya watu ni ile iliyo Makka, iliyo barikiwa na kuwa ni mwongozo kwa walimwengu wote." [Āl ‘Imrān: 96].

Na muujiza katika tukio hilo ni mkubwa na wenye matawi mengi, nami nitakidhi kwa mtazamo huu mfupi unaothibitisha kwamba ni safari yenye baraka iliyobeba malengo mengi, siri nyingi, na hadhi za juu, zilizomfikia Mtume (Rehma na amani zimshukie) bila mtu mwingine. Na thibitisho la upande wa muujiza ni kauli yake (S.A.W) "Kisha nikapandishwa"[12];  maana ya kupanda ni ishara ya muujiza, na uelewa wa unabii, na uthibitisho wa risala, kwa sababu ni kuthibitisha ukweli, na ingawa haikuwepo wazi wakati Qur’an ilipoteremshwa, ni miongoni mwa mambo yaliyothibitishwa katika enzi ya maendeleo ya kisayansi na ugunduzi wa kisasa; ambapo imejulikana kuwa njia ya kupanda juu ni kwa njia za mizunguko, maana ulimwengu wote ni mduara, na hakuna njia ya moja kwa moja.

 

 

 


[1] -  Moqademat Ibn Khalduon, Tahqiq Khalil Shahadah Uk. 119, Ch. Dar El Fikt, Bairut, Chapa ya pili, 1408 Hijra, 1988.

[2] Maelezo yake yametangulia.

[3] Kitabu: Al-Itqān fī ‘Ulūm al-Qur’ān, cha Imamu as-Suyūṭī, tahkiki: Muhammad Abu al-Faḍl Ibrahim, (juzuu ya 4, ukurasa 3-4), Mamlaka ya Vitabu ya Serikali ya Misri, 1394 Hijria — 1974 Miladia.

[4] Maelezo yake yametangulia.

[5] Muqaddimah Ibn Khaldūn, tahkiki: Khalīl Shahāda, ukurasa wa 119, Dar al-Fikr, Beirut, toleo la 2, 1408 Hijria — 1988 Miladia.

[6] Tazama: Muujiza wa Qur'ani, Sheikh Muhammad Mitwallī Ash-Sha‘rāwī, ukurasa wa 10, Al-Mukhtār Al-Islāmī ya Uchapishaji, Usambazaji na Uenezi — Cairo, toleo la 1, 1398 Hijria — 1978 Miladia.

[7] Miujiza ya Mtume (Rehma na amani zimshukie) (kutoka katika kitabu Al-Bidāyah wa an-Nihāyah cha Ibn Kathīr), tahkiki na maelezo: Sayyid Ibrāhīm Amīn Muhammad, ukurasa wa 11 na kuendelea, Maktaba ya At-Tawfīqiyyah.

[8] Hakika safari hii kwa malengo yake inafichua hadhi ya Msikiti wa Al-Aqswa na nafasi yake ya kipekee katika risala za mbinguni, na hili linavunja madai haya ya uongo ambayo Wayahudi wa Kizayuni wanajaribu kuyafuta na kuyapotosha, kupitia madai yanayohusiana na hekalu linalodaiwa, ambalo Wayahudi wanadai kuwa Msikiti wa Al-Aqswa umejengwa juu ya magofu yake. Kisha uhusiano huu kutoka upande mwingine unafichua hadhi ya manabii na kiwango cha uhusiano wao wao kwa wao; kutokana na umoja wa dini, na bila shaka hili linafichua uongo wa kauli zao kuhusu Mitume wa Mwenyezi Mungu wote, hasa bwana wetu Daudi ambaye walimnasibishia kumuua Uria Mhiti, na bwana wetu Suleiman ambaye walimnasibishia kuingiza masanamu mwishoni mwa maisha yake kwa ajili ya kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu. Na kutokana na hayo, ikaja uongozi wa Mtume (rehma na amani zimshukie) kwa ndugu zake Manabii katika safari hii; kama kukanusha uwongo huu na kuthibitisha uhusiano huu wa kiroho na kidini. (Tazama: Ulinzi wa Mtume Suleiman bin Daudi (amani iwe juu yake) kutokana na yale waliyomnasibishia Wayahudi katika Agano la Kale na riwaya za Kiebrania — uchambuzi wa kina wa kiukosoaji, Dkt. Fathi Muhammad Az-Zughbi, uk. 97 na kuendelea, Dar Al-Bashā’ir Al-Islāmiyyah, toleo la 1, 1432H–2011M, na Kubatilisha madai ya Kizayuni kuhusu Hekalu la Suleiman, Saleh Hussein Ar-Ruqayb, Chuo Kikuu cha Kiislamu Gaza–Kitivo cha Asili ya Dini, na Ukweli wa Hekalu linalodaiwa la Suleiman katika vitabu vya mbinguni na Sayansi ya Mambo ya Kale, Umuhimu wa Al-Quds na Hekalu katika fikra ya harakati ya Kizayuni, Mustafa Anshasi, Kituo cha Yemeni cha Tafiti za Kistratejia, 2004, 2005M, na Muhtasari wa Historia ya Al-Quds, Arif Al-Arif — na ameeleza simulizi kamili katika kitabu chake kilichochapishwa pamoja na jarida la Al-Azhar, toleo la Jumada Al-Akhirah 1445H, kama ilivyopokelewa katika Taurati na kusimuliwa kama ilivyoandikwa katika kitabu chao).

 

[9] Tazama: Al-Isra na Al-Mi’raj – Malengo na Siri Zake, Dkt. Khalid Ahmad Al-Bashir, ukurasa wa 14, Jarida la Al-Qazam la Kielimu kwa Masomo ya Kiislamu, toleo la kumi, Ramadhani 1444H – Machi 2023M.

[10] Albidaya wannihayah, Ibn Kathir, (9/373).

[11] Kisa cha Imani kati ya Falsafa, Sayansi na Qur'ani, Sheikh: Nadim Al-Jisr, ukurasa wa 218-219, Maktaba ya Kiislamu, Toleo la 3, 1389 Hijria - 1969 Miladia

[12] Imepokewa na Sheikhan: Sahihi ya Al-Bukhari, Kitabu cha: Swala, Mlango wa: Vipi swala ilifaradhishwa katika Israa? (1/78), Na. (349); na Sahihi ya Muslim, Kitabu cha: Imani, Mlango wa: Safari ya Israa ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ kwenda mbinguni na faradhi ya swala, (1/145), Na. (162).

Share this:

Related Fatwas