Umma wake kuwa bora kwa Ibada za Jamaa
Question
Neema zimekuwa nyingi katika umma huu wa Muhammad; na huu ni ukarimu wa Mwenyezi Mungu kwa Umma huu na kutukuza utu wa Mtume wake S.A.W.,
Answer
Neema zimekuwa nyingi katika umma huu wa Muhammad; na huu ni ukarimu wa Mwenyezi Mungu kwa Umma huu na kutukuza utu wa Mtume wake S.A.W., Mwenyezi Mungu Akauneemesha umma huu kwa ibada za jamaa kwa masilahi yake hapa duniani na Akhera, miongoni mwa ibada hizo ni ibada ya Saumu ambayo ni faradhi katika faradhi za Uislamu, na ibada inayojirudia kila mwaka; na kujirudia athari yake na fadhila zake kubwa, na kuleta matunda yake kila mwaka kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Ikiwa Saumu kama Alivyosema Mwenyezi Mungu ni Ibada katika umma zilizotangulia, basi katika Uislamu ni Ibada na zaidi ya Ibada; kwani pamoja na kuwa faradhi lakini pia katika Uislamu ni kafara ya Madhambi, na inamuweka mja karibu na Mola wake katika Funga za Sunna na Faradhi na nadhiri na kafara, pamoja na kuwa kizuwizi kati ya mja na Aliyoharamisha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu Anasema: (Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu) [Al-Baqarah:185], Mwenyezi Mungu Anasema katika kafara ya dhihar: (Na wale wanao jitenga na wake zao, kisha wakarudia katika yale waliyo yasema, basi wamkomboe mtumwa kabla hawajagusana. Mnapewa maonyo kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu Anayajua yote mnayo yatenda. Na asiye pata mtumwa kumkomboa, basi na afunge miezi miwili mfululizo kabla hawajagusana. Na asiye weza hayo basi awalishe masikini sitini. Hayo ni hivyo ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na kwa makafiri iko adhabu chungu.)[Mujadila:3-4], na Mtume S.A.W. anasema: “Saumu ni Kinga”([1]), na katika Hadithi nyingine: “Enyi Kundi la vijana, mwenye kuwa na uwezo miongoni mwenu basi na aoe, na asie na uwezo basi afunge, kwani Funga inamzuia na machafu”([2]), na akasema Mtume S.A.W.: “Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na mategemeo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia”([3]).
Yote haya yanaelezea Saumu kama ibada inayokusanya kheri na kuzuia shari, na inatosha dalili ya hilo, kwamba kufungua kwa makusudi siku moja pasi na udhuru wa hilo, kwamba mwenye kufanya hivyo basi ametenda dhambi kubwa, na imepokewa katika athari: “Mwenye kufungua siku moja katika Ramadhani pasi na ruhusa, hailipi kwa kufunga milele”([4]).
Mwenyezi Mungu Amefaradhisha Funga katika mwezi huu kwa umma huu; ili kuutukuza na kumtukuza Mtume wake S.A.W., na amefaradhisha kwa mapenzi yake kwa umma huu, hili linathibitishwa na hitimisho la Aya ya Saumu ambayo Mwenyezi Mungu Anasema: (Mwenyezi Mungu Anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.) [Baqarah:185], na maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu hakufaradhisha Saumu ili kuua mili na kuwanyima alivyowahalalishia miongoni mwa chakula, vinywaji na yote yaliyohalali, bali lengo kuu katika kufaradhisha Saumu na lengo la msingi la wajibu wake ni afya ya mwili, usalama wake na usafi wa moyo na usafi wa nia na mawazo mazuri, yote haya yanafikisha katika tabia njema na kufikisha katika kilele cha furaha na ukamilifu mzuri, na kwanini isiwe hivyo?! Na Mwenyezi Mungu Ameupa mwezi huu umaalumu ambao hakuupa mwenzi mwingine katika aina za Ibada na utiifu, “huu ni mwezi wa ukombozi...katika mwezi huu wadudu hubadili ngozi zao zilizochakaa, na kobe huondoa gamba lake gumu, na ngamia hupunguza uzito wa nundu lake kudhihirisha kufunga kwake, na mwanadamu huachana na matatizo yake na makosa yake... ama kasuku wakifungiwa katika matundu yao huacha kutaga; ili wasiwarithishe watoto wao utumwa, na Mwenyezi Mungu Amesema kweli Aliposema: (na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao) [Al-Aaraf:157].
Uhuru wa mtu mmoja mmoja, na uhuru wa makundi, na uhuru wa raia, hautufanyi kuacha kufunga katika mwezi wa Saumu kwa ugumu wake, na kusimama katika mwezi wa kisimamo kwa kutekeleza wajibu wake”([5]).
Na si haya tu bali Saumu “Inasafisha nafsi, na mazoezi ya mwili, na inalingania wema, Saumu ni kinga kwa binadamu, na inalinda umoja, katika kuuweka mwili na njaa kunasafisha moyo, na kuchoma mabaya, na kuwa na maono; kwa sabau shibe huleta uzembe, na hupofua nyoyo, na hukithirisha ukavu kichwani ubongo huwa unaganda, na mtoto akila sana basi hifadhi yake huondoka, na ubongo wake huaribika, zifanyeni nyoyo zenu kuwa hai kwa kucheka kidogo na kutoshiba sana, na zisafisheni kwa njaa zitakuwa safi na zitalainika”([6]).
Haya yote yanabainisha ukubwa wa fadhila za Funga na athari zake kubwa, na jambo hili linaongezeka uwazi kwa kuangalia hekima yake katika wajibu na Funga.
Na kabla ya kuchambua faida za ibada hii tukufu, kunatakikana tukubali kwamba Mwenyezi Mungu hakutulazimisha kitu chochote katika ibada, au utiifu au kujikurubisha, isipokuwa kuna manufaa kwa waliolazimishwa, hata kama watahisi uzito katika ibada hiyo, na mbali na hatua za kukalifishwa, na mpangilio wa hukumu; hakika Mwenyezi Mungu Ameweka amri zake hekima ambazo baadhi anaweza kutudhihirishia na kuzificha nyingine nyingi, na sisi hatufanyi ibada kwa ajili ya hikima, bali tunamuabudu Mwenyezi Mungu kwa amri zake na makatazo wake hata kama hekima hazijatudhihirikia, na hii ndiyo adabu inayopasa kwa mja, na hili ndilo aliloelezea Mwenyezi Mungu katika kauli yake: (Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufanikiwa) [An-Nour:51].
Wanazuoni wa Kiislamu wamejaribu kutafuta sababu na hekima zilizo nyuma ya amri na makatazo haya, na wameziandika katika vitabu vyao, wapo walioziandika kwa ufupi na kwa urefu, ili kuonesha utukufu wa Dini, na hekima ya kukalifishwa, na uzuri wa amri, na kujilinda na makatazo, miongoni mwa hayo ni yale yaliyo katika ibada ya Saumu miongozi mwa hekima tukufu.
Miongoni mwa hekima za Saumu ambazo zinabainika kwa wanaozingatia: Kufikia uchamungu, na hili limetajwa katika Aya za Saumu katika Surat Al-Baqara, na kufikia usalama wa mwili, na kuiongezea roho mahitaji yake ya virutubisho, na kupunguza njia za Shetani katika mishipa ya damu ya mwanadamu, na kuizuia nafsi na shari na yanayopelekea shari, katika yafuatayo tunaelezea baadhi ya faida tukufu za Ibada ya Saumu:
Kwanza- Kufikia Uchamungu:
Inawezekana wasomi wengi wanaona kwamba uchamungu ni ndoto iliyombali sana kuifikia, na wanaposikiliza simulizi za wachamungu wanajenga taswira kwamba zama zao zimeshapita na haziwezi kurudi, lakini mwenye kuzingatia ibada ya Saumu anakuta kwamba lengo lake limetangazwa wazi mwisho mwa Aya ya kufaradhisha Saumu, nayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu: (Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu) [Al-Baqarah:185].
Miongoni mwa malengo makubwa ya Saumu na hekima zake na siri zake na faida zake ni kufikia uchamungu katika nafsi ya mfungaji. Na kufikia uchamungu kunakokusudiwa hapa kunadhibitika katika jumla ya anayoyafanya mwanadamu katika Saumu yake; anaacha vinavyopendwa na nafasi yake na matamanio yake: Kula na kunywa, akitafuta radhi za Mwenyezi Mungu pekee, pasi na kuangalia wanadamu wanaomuangalia au kumchunga, wala thawabu zake au adhabu yake.
Tukiongezea upande huu wa kiimani ambao mja anachunga uwepo wa Mola wake, na kuchunga kwake, Saumu inakuwa nyepesi kwa mja kwanza, na juu ya hilo hungezeka anachokiweza katika njia ya kuheshimu ibada, basi huzuia viungo vyake kufanya maasi, na kuvilinda na kufanya makosa, na kuvifanya vinafunga kwa funga yake, na kujizuia kwa kujizuia kwake, vikifanya ibada kwa ibada yake.
Al-Mawirdy anasema: “Hakika katika Saumu kuna sababu inayompelekea mtu wake katika kumcha Mwenyezi Mungu; Kwa yaliyomo ndani ya Saumu katika kuitenza nguvu nafsi, na kukata matamanio, na kuondosha kibri”([7]), Abu Abdullah Al-Halimy anasema katika kufafanua maneno yake: “Mwenyezi Mungu Amebainisha kwamba Saumu ni katika sababu za uchamungu, na uchamungu wa kweli ni kufanya yaliyoamrishwa, na yanayopendeza, na kujiepusha na yaliyokatazwa, na yanayochukiza, na yanayoepukwa; kwa sababu kinachokusudiwa katika ucha Mungu ni mja kuikinga nafsi yake na moto, nako hakika hakuna vingine ni kuikinga nafsi yake kwa kilichotajwa”([8]).
Na uchamungu ni matunda ya kumchunga Mwenyezi Mungu na kufanya ibada kwa ajili yake, na kuacha maovu kwa ajili yake, na mja anapomchunga Mola wake basi hukaribia kumchunga Mwenyezi Mungu katika kila jambo lake, hivyo anakuwa katika watu wa Mwenyezi Mungu ambao anafanya lengo lao ni Mwenyezi Mungu, na ambao Mwenyezi Mungu Ameelezea hali zao katika kauli yake: (Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu.), [Al-Anaam:162-163].
Pili: Kuisafisha nafsi na kuitwaharisha na uchafu:
Safari ya kujisafisha ameitangaza Mwenyezi Mungu katika Qur’ani Tukufu katika mtindo wa kusisitiza, na hakuelezea bila ya kuisisitiza, bali Mwenyezi Mungu Amesema: (Hakika amefanikiwa aliye itakasa) akasisitiza kufanikiwa kwa mwenye kuitakasa nafsi yake kwa neno {Hakika} na kwa viapo kumi na moja kabla ya Aya hii kuanzia kauli yake Mwenyezi Mungu: (Naapa kwa jua na mwangaza wake).
Inakuja ibada ya Saumu ili kufikia kutakasa nafsi ambayo ni katika hukumu za Saumu na makusudio yake na siri zake, na Saumu imekuwa kitakaso cha nafsi kwa sababu inamuweka mbali na uchafu wa maasi na maovu, na inazima mianya ya matamanio na inazuia sababu za makosa.
Na inawezekana maana inayopasa kuifahamu katika Hadithi ya Mtume S.A.W.: “Mwenye kufunga Ramadhani, kwa imani na mategemeo atasemehewa dhambi zake zilizotangulia”([9]), kunapasa kuelewa katika maana hii, hivyo Saumu si imani ya kusadikisha ahadi ya Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu Ameweka faradhi na imetosha, lakini imani hii huwa na matawi ya kukalifishwa kiimani ambayo inafikia kwayo imani ya mja, na mja anatoa kwa saumu matunda ya imani yake kwenda kwa mwingine katika viumbe vya Mwenyezi Mungu.
Ibanu Hamam anaeleza kwamba miongoni mwa faida za Saumu ni kwamba Mwenyezi Mungu, “Ameifaradhisha kwa faida zake ambazo kubwa yake ni kuituliza nafsi inayoamrisha mabaya, na kukata utawala wake katika kuingia katika mambo yanayohusiana na viungo vyote, kama jicho, ulimi, sikio na tupu, kwani kwa hiyo Saumu harakati za hisia za viungo vyake zinadhooofika, hivyo kukasemwa, nafsi ikishikwa na njaa viungo vyote vikashiba, na ikishiba viungo vyote vinakuwa na njaa, pia ndani yake kuna kusafisha moyo na uchafu, kwani kinachosababisha uchafu wake ni ulimi na jicho na vinginevyo, na kwa kusafika kwake hupatikana masilahi na daraja”([10]).
Na ikiwa watu wengi wanaijua Hadithi ya Mtume S.A.W.: “Funga ni kinga”([11]); basi kunatakikana kuelewa kwamba Saumu ni kinga na ulinzi na sitara ya madhambi na maasi na makosa ya duniani, na kinga ya moto na adhabu ya moto wa Jahiim huko Akhera, na katika mzunguuko wa maana hii, kunatakikana waliofunga kupita humu ili kufikia kinga hii na ulinzi ili wafaulu kupata dunia na Akhera.
Na miongoni yanayounga mkono njia hii iliyowajibu kwa waliofunga ni Hadithi Mtume S.A.W. isemayo: “Mwenye kufunga siku moja tu katika njia ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu Atamuweka mbali na Moto kwa mwendo wa miaka sabini”([12]), je, Mwenyezi Mungu Atamuweka mbali na moto aliyefunga kwa kuacha tu kula na kunywa, je, watakuwa sawa kati ya yule aneacha kula na kunywa tu na yule aliyejizuia kula na kunywa na maasi mengine ya viungo?!
Tatu: Kudhoofisha visababisha shari na vishawishi katika nafasi ya aliyefunga:
Miongoni mwa hekima za Saumu ambayo inafungamana na kuisafisha nafsi na kuitaharisha na uchafu, ni kudhoofisha vishawishi vya shari na vichochezi vyake, kwa kile ambacho Saumu inakiacha katika nafsi za waliofunga, miongoni mwa unyeyekefu na utulivu, kwa kutanguliza matakwa ya Mwenyezi Mungu kabla ya matakwa ya nafsi, na kutanguliza mahitaji ya Mwenyezi Mungu kabla ya mahitaji ya mwili, na Mtume S.A.W. amesema: “Hakika Shetani anapita mapito ya damu kwa mwanadamu” ([13]), je, Saumu kwa hili haiwi kubana njia za shetani, na kumzuia katika harakati na kupita katika damu zetu.
Miongoni mwa mambo yanayounga mkono maana hii, ni Hadithi ya Mtume S.A.W. ambayo anawanasihi vijana akiwaambia: “Enyi Kundi la vijana, mwenye kuwa na uwezo miongoni mwenu basi na aoe, kwani ndoa inasitiri macho na inalinda tupu, na asie na uwezo basi afunge, kwani Funga inazumzuia na machafu”([14]).
Na tukiongeza katika amri hizi za wazi zilizoelekezwa kwa wafungaji, kuwa wazuie ndimi zao na shari, na kusema mabaya, na kutamka maovu; miongoni mwazo: kauli ya Mtume S.A.W.: “Siku mmoja wenu akifunga, basi asifanye uovu wala asitukane, akitukanwa na yeyote, au akampiga, basi aseme hakika mimi nimefunga”([15]); na Mtume S.A.W. amefanya kuajitaharisha huku na uchafu wa tabia kuwa lengo katika malengo ya Saumu; akasema: “Ambaye hakuacha maneno ya uzushi na kuyafanyia kazi, basi Mwenyezi Mungu hana haja na Saumu yake kwa kuacha kula na kunywa” ([16]).
Na imekuja katika fathul bary: “Ibn Al-Araby amesema: Muktadha wa Hadithi hii ni kwamba, mwenye kufanya yaliyotajwa, basi halipwi thawabu za Saumu yake, na maana yake: kwamba thawabu za Saumu hazisimami katika mzani kwa madhambi ya uzushi na yaliyotajwa pamoja nao.
Al-Baydhawy amasema: Kufaradhishwa Saumu hakukusudiwi kukaa na njaa na kiu,bali yale anayoyafauata miongoni mwa kukata matamanio, kuilazimisha nafsi inayoamrisha maovu ili kuwa nasfi iliyotulia, likipatikana hilo, Mwenyezi Mungu hamuangalii kwa jicho la kukubaliwa”([17]).
Nne: kutakasika kwa hisia na tabia, na kushirikiana na wanaohangaika katika mateso yao:
Na miongoni mwa malengo ya Saumu, hekima na siri zake kuwa huikumbusha nafsi na kuitanabahisha hali anayoishi wasio weza na masikini kwa uchungu wa njaa na mateso ya kutoweza kujimudu kwa mahitaji ya maisha, na maumivu ya kukosa, na majuto na huzuni ya wanaojutia waliyoyakosa, basi nafsi ya Muislamu humsukuma awafanyie wema na hisani na awape pole na msaada.
Imesimuliwa kuwa Yusufu (A.S.) hakuwa akishiba ndani ya miaka ya njaa iliyotokea nchini Misri, akaambiwa: Mbona unabaki na njaa ilhali unadhibiti mifuko ya fedha na chakula cha nchi nzima? Akasema: naogopa nikishiba nitasahau taifa la nchi walio na njaa, akaamuru wapishi wa Mfalme wacheleweshe chakula cha mchana cha Mfalme mpaka katikati ya usiku, akataka Mfalme ahisi njaa kama wanavyohisi raia wake, hivyo asisahau wenye njaa, na kuwafanyia masikini hisani.[18]
Na Ibn Al-Hammam alieleza, akionesha baadhi ya hekima zilizomo katika kufunga, akasema:
“Kuwa kwake (yaani Swaumu) ni sababu ya kuleta huruma na kuwahurumia masikini; kwani mtu anapopata ladha ya maumivu ya njaa kwa nyakati fulani, anakumbuka wale ambao hali hiyo kwao ni ya daima. Hivyo, moyo wake hujaa huruma kwao, na huruma kwa hakika yake kwa mwanadamu ni aina ya maumivu ya ndani yanayomsukuma kuchukua hatua ya kuwasaidia kwa kuwafanyia ihsani. Kwa kufanya hivyo hupata malipo bora yaliyo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.” Na miongoni mwa hekima hizo pia ni: Kuwa sawa na masikini kwa kubeba baadhi ya yale wanayobeba mara kwa mara, na kwa kufanya hivyo hadhi yake huinuliwa mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kama alivyopokea Bishr Al-Hāfī kuwa mtu mmoja alimuendea wakati wa baridi kali, akamkuta ameketi akitetemeka, na nguo yake ilikuwa imening'inizwa kwenye ndoano. Huyo mtu akamuuliza: “Wakati kama huu wa baridi, unavua nguo?” Yaani, maana yake ni kwa nini huvai ili ujihifadhi. Akamjibu: “Ewe ndugu yangu, masikini ni wengi, nami sina uwezo wa kuwasaidia wote kwa kuwapatia nguo, basi ninawasaidia kupatwa na baridi kama wanavyopatwa wao.”[19]
Haifichiki hekima kubwa ya kijamii iliyomo katika kufunga, hasa katika nyakati hizi ngumu zinazowakumba watu, ambazo zinawalazimu matajiri kuwasaidia waliodhulumiwa kwa sehemu ya neema za Mwenyezi Mungu walizonazo.
Na huenda ibada ya Swaumu ikawa ndiyo ibada iliyo karibu zaidi na huruma hii ya kijamii na usaidianaji mpana wa kijamii, hasa ikizingatiwa kuwa Hadithi nyingi za Mtume (S.A.W.) zinaashiria hilo. Miongoni mwa Hadithi hizo ni ile inayohamasisha na kuhimiza kufuturisha watu wanaofunga na kuahidi thawabu kubwa kwa hilo. Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: “Yeyote atakayemfuturisha aliyefunga, atapata thawabu kama zake (za aliyefunga), bila kupunguza chochote katika thawabu za aliyefunga”[20]
Tano: Afya ya Miili na Usalama wake:
Imepokelewa katika Hadithi: “Kwa hakika mwanaadamu hajawahi kujaza chombo kibaya zaidi kuliko tumbo lake. Inamtosha mwanadamu matonge machache ya chakula kuuweka uti wake wa mgongo imara. Na ikiwa hana budi, basi theluthi moja iwe kwa chakula chake, theluthi kwa kinywaji chake, na theluthi kwa pumzi yake."[21] Kwa sababu hii, watu wema walijitahidi kulitekeleza hili na wakahimizana juu yake. Imepokelewa kutoka kwa Dhun-Nun – Mwenyezi Mungu amrehemu – kwamba alisema: "Ewe Mwana wa Adamu! Funga wakati wa mchana, na usimame usiku wa manane kwa ibada – utaona maajabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Muweza wa yote."[22] Pia imepokelewa kutoka kwa Luqman Al-Hakim katika nyasia zake kwa mwanawe, kwamba alimwambia: "Ewe mwanangu, tumbo likijaa, fikra hulala, hekima hunyamaza, na viungo huacha ibada."[23]
Na kutokana na hekima na faida hizi, inaonekana wazi kwamba ibada hii ya kina inathibitisha wema wa umma huu, kwa yale inayoyaacha katika nafsi za wanaofunga – yaani, umoja juu ya maadili mema, kukutana kwa ajili ya mema, na kuelekea kwenye mambo ya heshima na ukarimu.
Mwenyezi Mungu Akubali funga yetu na yenu, na atukutanishe na Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) mahali pa kweli mbele ya Mfalme Mwenye uweza.
([1]) Sahih Muslim, Mlango wa Saumu. 2/806.
([2]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, 3/7.
([3]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, 1/16.
([4]) Musnad Ahmad.
([5]) Al-Siyaam Junna, Abullatuf Mash’hary uk 46.
([6]) Ihyaa Uluum Ad-Din, Imamu Al-Ghazaly, 3/84.
([7]) An-Nukt wa Al-Uyoun, Al-Mawirdy.
([8]) Shuab Al-Iman
([9]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, Sahih Al-Bukhar, Mlango wa Imani 1/16.
([10]) Fat’hul Qadar, Ibn Hamam, 2/300-301.
([11]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, Sahih Al-Bukhari, Mlango wa Saumu, 3/24
([12]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, Sahih Al-Bukhari, Mlango wa Saumu 2/808.
([13]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, Sahih Al-Bukhari, Mlango wa Itikafu 3/50 .
([14]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, 3/7.
([15]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, Sahih Al-Bukhari, mlango wa Funga, 3/26.
([16]) Hadithi hii imepokelewa na Shaykhan, Sahih Al-Bukhari, 3/26.
([17]) Fat’hhul Bary, Ibn Hajar. 4/11.
[18] Al-Kashf wa Al-Bayan juu ya Tafsiri ya Qurani, Imamu Tha’alaby, uhakiki: Imamu Abu Mohammed bin A’ashur (5/234), Dar Ihyaa Al-Turath Al-Araby, Beirut, Toleo 1, 1442 H.J. – 2002 B.K.
[19] Fathul-Qadiir, Ibn Al-Hammam (2/301)
[20] Sunan Al-Tirmidhiy, Sura ya: Swaumu, mada ya Fadhila ya anayemfuturisha mfunga swaumu, (3/162), Na. (807).
[21] Sunan Al-Tirmidhiy, Sura ya: Kuitakasa nafsi, mada ya: Kuchukia kula kwa wingi, (4/590), Na. (2380).
[22] Bustana Al-Waidhiin wa Riyadh Al-Samiin, Ibn Al-Jawzy, uhakiki wa Ayman Al-Beheiry, (1/234), Taasisi ya Al-Kutub Al-Thakafiya, Beirut, toleo la 2, 1419 H.J. – 1998 B.K.
[23] Ihyaa Ulum Al-Diin, Imamu Abu Hamed Al-Ghazaly, 3/82.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
