Hukumu ya kusambaza video zisizo na maadili
Question
Hivi karibuni wapo baadhi ya watu wanaojiita "bloggers", ambao huchapisha video kwenye mitandao ya kijamii zenye maneno na ishara zinazokiuka haya ya heshima, kwa lengo la kuongeza idadi ya watazamaji na kupata faida ya kifedha. Naomba kufafanuliwa nafasi ya Sharia Tukufu ya Kiislamu kuhusu vitendo hivi wanavyofanya.
Answer
Muhtasari wa jibu
Kitendo cha waundaji wa maudhui wanaojulikana kwa “bloggers” cha kusambaza video zisizo na maadili kwenye majukwaa ya vyombo vya habari vya kidijitali ili kuongeza mwingiliano kwa njia ya maoni, kushiriki, au kupenda, ni kitendo kilichoharamishwa kisharia, na ni kinyume na kanuni. Kwani kuna kueneza maovu katika jamii, na pia kusambaza aibu na video zisizo na maadili kupitia wengine kunahesabiwa kama kusengenya kuliko haramishwa; kwa kuwa kunahusisha kumtaja mtu kwa jambo analolichukia kutajwa, iwe ni kwa mwili wake, dini yake, mali yake, au nafsi yake.
Maelezo
Maendeleo makubwa ya kiteknolojia yanatupa fursa ya kutumia zana zake kufanikisha maendeleo na manufaa, jambo ambalo Uislamu unalihimiza, mradi tu manufaa haya yatimizwe kwa kufuata maadili ya Sharia ya Kiislamu ambayo yanaweka mipaka wazi ya kulinda heshima ya binadamu na faragha yake.
Hivyo, kutumia teknolojia kwa ajili ya kupeleleza, kufuatilia watu, au kutishia uthabiti wa jamii na maadili yake ya malezi, ni kutoelekea njia sahihi na kubadilisha zana yenye manufaa kuwa chombo cha uharibifu.
“Vyombo vya habari vya kidijitali,” kwa kuenea kwake na kasi ya athari zake, vinaweza kuonesha mifano inayokiuka maadili na heshima, ikiwemo baadhi ya kundi la “bloggers” — neno la kigeni asili yake ni “Blogger,” linalotumika kwa waandaaji wa maudhui ya kuona kwenye majukwaa — kwani baadhi ya maudhui yao husambaza aibu na mambo yasiyo na maadili ili kuongeza mwingiliano kwa njia ya maoni, kushiriki au kupenda.
Na hata video nyingi fupi zinazotoa ushauri au hadithi kutoka kwa waandaaji hawa wa maudhui, kwa asili yake hazitofautiani na kile ambacho wauzaji wa dawa za kulevya hutoa; zote ni uraibu, uharibifu na usambazaji, na utajiri wake wa haraka. Kuchapisha video hizi zisizo na maadili kunasambaza aibu katika jamii, jambo ambalo ni dhambi aliyoionya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama alivyosema: {Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. } [An-Nur: 19].
Aya ni kwa ujumla kwa wale ambao wanatafuta au kufichua mapengo ya aibu ya wengine, wanavunja heshima na faragha, na kusambaza maovu.
Hivyo Aya hii, ingawa ilishushwa kuhusiana na kashfa dhidi ya Aisha (R.A) lakini somo kuu ni kwa ujumla wa maneno na siyo kwa sababu maalumu; kwa hivyo ni lazima itekelezwe kwa maana yake ya jumla. Kile kinachoonesha kuwa haiwezi kuhusishwa tu na kashfa ya Aisha (R.A) ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {wale walio amini}, kwani ni kwa tamko la jumla; kama angekusudiwa Aisha (R.A) peke yake, basi isingelipaswa isomeke hivyo.
Na kwa hakika Uislamu umejaalia kwamba kusambaza movu au kuyafanya ni dhambi sawa, kutokana na madhara makubwa yanayotokana katika hali zote mbili. Imamu Bukhari amepoke kutoka kwa Ali bin Abi Talib (R.A) akisema: “Yule anayesema jambo la uovu na yule anayelieneza ni sawa katika dhambi[1],” na Atwa alisema: “Yeye anayesambaza aibu lazima aadhibiwe, hata kama alisema kweli[2].”
Pia, Mtume (S.A.W) amefanya kuwa adhabu kubwa kwa dhambi ya kusambaza aibu; akasema (S.A.W) “Mtu yeyote anayesambaza juu ya mtu mwingine Muislamu neno ambalo ametakasika nalo, na kumdhuru katika dunia hii, ni haki kwa Mwenyezi Mungu kumyayusha katika Moto Siku ya Kiyama hadi athibitishe kile alichosema.” Amepokea Imamu At-Tabarani.
Mtume Muhammad (S.A.W) ameweka wazi ubaya wa matokeo kwa wale wanaowazushia wenzao na kueneza mapungufu yao; amesema katika Hadithi iliyopokelewa na Bukhari na Muslim: “Yeyote anayetaka kusikilizwa basi Mwenyezi Mungu atamsikilizisha; na yeyote anayetaka kuonekana, basi Mwenyezi Mungu atamuonesha.”
Na kutoka kwa Thawbaan (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) alisema: “Msiwakere waja wa Mwenyezi Mungu, wala msiwaaibishe, na msitafute makosa yao, kwani yeyote anayetafuta makosa ya ndugu yake Muislamu, Mungu atatafuta makosa yake hadi atakapomfedhehesha nyumbani kwake..” (Imetolewa na Imamu Ahmad)
Hivyo basi, kila aliyeeneza mapungufu ya watu na kuyaweka wazi, naye Mwenyezi Mungu ataziweka wazi aibu zake na atawasikilizisha watu aibu zake anazochukia kujulikana.
Kama ambavyo kusambaza mfano wa aibu kama hizi za watu kwa njia ya “blogger” huwa ni kinyume kabisa na mahimizo kwa mujibu wa Sharia ya juu ya kusitiriana na kufichiana; kwani mambo ya watu binafsi ni ya sitara. Haipasi kufichua sitara ya Mwenyezi Mungu juu yake au kwa mwingine. Mtume (S.A.W) amesema kama ilivyopokea Abu Huraira (R.A) “Mwenye kumsitiri Muislamu, Mwenyezi Mungu atamsitiri duniani na Akhera”. Imepokelewa na Imamu Muslim)
Na katika mapokezi ya Ibn Majah: “Yeye aliyesitiri mapungufu ya ndugu yake Muislamu, Mwenyezi Mungu atasitiri mapungufu yake siku ya Kiyama; na yeyote mwenye kufichua mapungufu ya ndugu yake, Mwenyezi Mungu naye atafichua mapungufu yake hadi amfedheheshe nyumbani kwake.” Hivyo basi, kusitiriana ni wajibu kwa Muislamu katika nafsi yake iwapo amefanya dhambi, na pia ni wajibu kwake kwa wengine.
Sharia pia inatufundisha kwamba mtu aliyekumbwa na dhambi asiitangaze, bali afiche, na amuombe msamaha Mwenyezi Mungu Mtukufu na atubu; kama alivyosema Mtume (S.A.W): “Yeyote anayefanya mojawapo ya matendo haya ya aibu ajifiche kwa sitara ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwani yeyote anayefunua kwetu kurasa zake, tutatumia kitabu cha Mwenyezi Mungu kwake[3].”
Kulingana na hili, Wanazuoni wamesema kwamba inapendeza kwa mtu aliyetenda dhambi kuificha kwake mwenyewe na kwa wengine. Kwani kuficha ni wajibu na kueneza ni haramu., kulingana na Hadithi: " Yeyote anayefanya mojawapo ya matendo haya ya aibu ajifiche kwa sitara ya Mwenyezi Mungu,."
Iwapo ikitokezea mtu ametenda dhambi kisha akamwelezea mtu mwingine, hairuhusiwi kwa mtu huyo mwingine kufichua siri yake ili kujipatia umaarufu, kama vile hairuhusiwi kwa mtu aliyepewa dhamana ya kitu kumweleza mwingine. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na timizeni ahadi. Hakika, ahadi hiyo itaulizwa.} [Al-Isra: 34] Na imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah, (R.A), kutoka kwa Mtume (S.A.W), alisema: "Alama za mnafiki ni tatu: anaposema, husema uongo; anapotoa ahadi, huivunja; na anapoaminiwa, hufanya khiana." Bukhari na Muslim.
Na kutoka kwa Abu Sa’id al-Khudri (R.A), Mtume (S.A.W) alisema: “Hakika miongoni mwa watu wabaya Zaidi mbele y Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama ni yule mwanaume anayemfichulia siri yake mkewe, naye akamfichulia yeye, kisha akaeneza siri yake.[4]”
Uislamu umeagiza wafuasi wake kuwa na tabia ya kuficha mapungufu ya wengine, kupuuzia makosa yao na kutochunguza mapungufu yao; ili kuwasaidia kutubu na kuboresha nafsi. Mtume (S.A.W) amesema: “Yeye aliyemsitiri Muislamu, Mwenyezi Mungu atamsitiri duniani na Akhera, na Mwenyezi Mungu yupo kumsaidia mja, ilivyokuwa mja humsaidia ndugu yake[5].”
Zaidi ya hayo, kusambaza aibu kama hizi na video zisizo za maadili kupitia wengine kunachukuliwa kuwa ni usengenyanji ulioharamishwa; kwa sababu kunahusisha kumtaja mtu kwa jambo analolichukia kutajwa, iwe ni mwili wake au dini yake au maisha yake ya dunia au nafsi yake au maumbile yake ya nje au tabia yake au mali yake au watoto wake au wazazi wake au mke wake au mtumishi wake, au anayemmiliki au nguo yake au namna ya kutembea na harakati zake au uso wake na sura yake ya wazi au kukasirisha, au mambo mengine yote yanayomhusu; iwe umevitaja kwa maneno yako, kitabu chako, ishara, au alama, kwa macho yako, mkono wako, kichwa chako, au kwa namna nyingine yeyote.
Pamoja na yote, nchi ya Misri imepiga marufuku kwa msambazaji wa habari kusambaza taarifa zisizo sahihi na zilizopotoshwa, kwa hivyo ikaidhinisha Sheria nambari (175) ya mwaka 2018 kuhusu Kupambana na Uhalifu wa Teknolojia ya Habari, na kuingiza katika sheria hiyo masharti yanayohusiana na upande wa jinai wa maudhui ya habari yasiyo halali. Kifungu cha 25 cha sheria hiyo kinasema:
“Yeyote anayekiuka maadili yeyote au thamani za kifamilia katika jamii ya Misri, au kuvunja uhuru wa maisha binafsi, au kutuma kwa wingi barua pepe kwa mtu fulani bila idhini yake, au kutoa data binafsi kwa mfumo au tovuti ili kutangaza bidhaa au huduma bila idhini yake, au kusambaza kupitia mtandao wa habari au kwa njia yeyote ya teknolojia ya habari taarifa, habari, picha au vitu vinavyohusiana navyo vinavyokiuka faragha ya mtu bila ridhaa yake, iwe taarifa zilizotolewa ni sahihi au si sahihi, atahukumiwa kwa kifungo kisichopungua miezi sita na faini isiyopungua pauni 50,000 hadi 100,000, au moja ya adhabu hizi mbili.”
Yeyote anayekiuka kanuni au maadili ya kifamilia katika jamii ya Misri, au kuvunja uhuru wa maisha binafsi, au kutuma kwa wingi barua pepe kwa mtu fulani bila idhini yake, au kutoa taarifa binafsi kwa mfumo au tovuti ili kutangaza bidhaa au huduma bila idhini yake, au kusambaza kupitia mtandao wa habari au kwa njia yoyote ya teknolojia ya habari taarifa, habari, picha, au vitu vinavyofanana navyo vinavyokiuka faragha ya mtu bila ridhaa yake, iwe taarifa zilizochapishwa ni sahihi au si sahihi.
Kifungu cha 26 kinasema pia: “Ataadhibiwa kwa kifungo kisichopungua miaka 2 na kisichozidi miaka 5, na faini isiyopungua pauni 100,000 na isiyozidi pauni 300,000, au kwa mojawapo ya adhabu hizi mbili: yeyote aliyekusudia kutumia programu ya kompyuta au teknolojia ya habari kuchakata taarifa binafsi za wengine ili kuziunganisha na maudhui yanayokinzana na maadili ya umma, au kuonesha taarifa hizo kwa njia inayoweza kuharibu heshima yake au heshima ya jina lake.”
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Wanayoyafanya watengeneza maudhui wanaojulikana kama “blogger” ya kusambaza video zisizo za maadili kwenye majukwaa ya vyombo vya habari vya kidijitali ili kuongeza ushawishi ni kitendo kilichoharamishwa kisharia na humtia mtu makosani. Kwani kinahusisha kusambaza maovu katika jamii, ambayo ni kosa lenye adhabu kubwa iliyowekwa na Sharia ya Mwenyezi Mungu, pamoja na ukweli kwamba uenezi wa maudhui haya kinyume kabisa na kuhimiza kuficha na kufichiana kama kulivyoagizwa na Sharia.
Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri inasisitiza wazazi kuwa na jukumu la kuwalinda watoto wao wasiendelee kuendeleza maudhui hizi za kipuuzi zinayowasilishwa kwa jina la burudani, pamoja na kuwaeleza umuhimu kwenye burudani mbadala zenye faida na zinazofaa.
[1] Imetolewa na al-Bukhari katika kitabu chake ‘Al-Adab Al-Mufrad’.
[2] Imetolewa na Ibn Abi Hatim katika kitabu chake cha tafsiri (tafsiri yake).”
[3] Imetolewa na Imam Malik katika “Al-Muwatta.”
[4] Ameitoa Imam Muslim.
[5] Imeitoa Imam Muslim.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
