Hukumu ya kucheza na kuisikiliza mu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kucheza na kuisikiliza muziki

Question

Ni ipi hukumu ya kucheza na kuisikiliza muziki?

Answer

Hakuna andiko la kisharia linaloharamisha utumiaji wa ala za muziki, au linaloharamisha kusikiliza muziki. Aidha, imekuja katika Sunna ya Mtume (S.A.W.) yale yanayoonesha kujuzu kwa utumiaji wa ala za muziki kama vile kupiga dufu na mfano wake. Imesimuliwa kutoka kwa Rubayyi’ bint Mu’awwidh bin Afraa amesema: “Mtume (S.A.W.) aliingia kwangu siku ya harusi yangu, akaketi mahali pa kitanda changu hiki, na kando yangu walikuwepo wasichana wawili wakipiga dufu na kuwataja kwa sifa (kuwaomboleza) baba zangu waliouawa siku ya Badr. Wakasema katika yale waliyokuwa wakiyasema: "Na miongoni mwetu yumo Mtume anayejua yatakayokuwa leo na kesho". Mtume (S.A.W.) akasema: Ama hili, msiuseme”.

Hadithi hii inaonesha kukataza kwa Mtume (S.A.W.) kuhusu kauli ya wasichana hao kwamba Mtume (S.A.W.) anajua yaliyomo kesho, na haya ni katika mambo ya ghaibu asiyoyajua yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu; lakini hakuwakataza kupiga dufu, nalo ni aina miongoni mwa aina za muziki.

Na Mtume (S.A.W.) amesema: “Kipambanuzi kati ya halali na haramu, ni (kupiga) dufu na sauti (ya nyimbo) katika ndoa”.

Hivyo basi, hukumu yenye nguvu inayokubaliwa zaidi kwa wanazuoni ni kwamba kusikiliza muziki ni jambo linalojuzu kisharia, maadamu haliambatani na yale yanayolingania katika kutenda machafu au kuchochea matamanio.

Maelezo

Imeamuliwa miongoni mwa Wanazuoni kwamba hakuna andiko la kisharia lililokuja kuharamisha upigaji wa muziki na kuusikiliza; bali zimekuja katika Sunna ya Mtume baadhi ya hadithi zinazoonyesha uhalali wa jambo hilo.

Imesimuliwa kutoka kwa Rubayyi’ bint Mu’awwidh bin Afraa amesema: “Mtume (S.A.W.) aliingia kwangu siku ya harusi yangu[1], akaketi[2] mahali pa kitanda changu hiki, na kando yangu walikuwepo wasichana wawili wakipiga dufu na kuwataja kwa sifa (kuwaomboleza)[3] baba zangu waliouawa siku ya Badr. Wakasema katika yale waliyokuwa wakiyasema: "Na miongoni mwetu yumo Mtume anayejua yatakayokuwa leo na kesho". Mtume (S.A.W.) akasema: Ama hili, msiuseme”[4].

Hadithi hii inaonyesha kukataza kwa Mtume (S.A.W.) kuhusu kauli ya wasichana hao kwamba Mtume (S.A.W.) anajua yaliyomo kesho, na haya ni katika mambo ya ghaibu asiyoyajua yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu; lakini hakuwakataza kupiga dufu, nalo ni aina miongoni mwa aina za muziki.

Pia imepokelewa kutoka kwa Muhammad bin Hatib (R.A.) amesema: Mtume (S.A.W.) amesema: “Kipambanuzi kati ya halali na haramu, ni (kupiga) dufu na sauti (ya nyimbo) katika ndoa” [Imepokelewa na Ibn Majah].

Na makusudio ya hadithi hii ni kwamba Mtume (S.A.W.) aliwaamuru Maswahaba (R.A.) watangaze ndoa kwa kupiga dufu.

Lakini kuna baadhi ya wanazuoni walioharamisha kusikiliza muziki, na wakatoa ushahidi kwa kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Na wanapoona biashara au pumbao (lao), hutawanyika kwenda huko na kukuacha umesimama; sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko pumbao na kuliko biashara; na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanaoruzuku} [Al-Jumu'ah: 11].

Wakasema: Hakika muziki ni aina miongoni mwa aina za pumbao (lahw) lililoharamishwa, na Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta'ala anawasifu waumini kwa kusema: {Na wale ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi (laghw)} [Al-Mu'minun: 3]. Pia wakatoa ushahidi kwa kauli ya Mtume (S.A.W.): “Watakuwepo katika umma wangu watu watakaohalalisha zinaa, hariri (kwa wanaume), pombe, na ala za muziki (ma'azif)...»[5].

Wakasema: Hakika muziki ni aina miongoni mwa aina za ma'azif ambazo Mtume (S.A.W.) amezikataza.

Majibu dhidi ya msimamo huu ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Makusudio ya aya tukufu waliyoitolea ushahidi ni kukataza kushughulika na mambo mengine ukaacha ibada kama sala ya Ijumaa na mfano wake kwa aina yoyote ya pumbao, na makusudio si kuharamisha kusikiliza muziki katika wakati usio wa ibada.

Pili: Makusudio ya "laghw" (upuuzi) ambao Muislamu anajiepusha nao, ni ule unaolingania katika machafu au kuchochea matamanio kuelekea kwenye shahawa.

Tatu: Kuharamisha kwa Mtume (S.A.W.) kuhusu ma'azif, makusudio yake ni zile (ala) zinazoambatana na unywaji wa pombe, utendaji wa mambo yaliyoharamishwa na mengineyo ambayo Sharia tukufu imeyakataza.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

1- Hakuna matini yoyote katika Sharia inayoharamisha utumiaji wa ala za muziki, au inayoharamisha kusikiliza muziki.

2- Imekuja katika Sunna ya Mtume (S.A.W.) yale yanayoonyesha kujuzu kwa utumiaji wa ala za muziki kama vile kupiga dufu na mfano wake.

3- Msimamo wenye nguvu unaokubaliwa zaidi kwa wanazuoni ni kwamba kusikiliza muziki ni jambo linalojuzu kisharia, maadamu haliambatani na yale yanayolingania katika kutenda machafu au kuchochea matamanio.

 

[1] «Siku ya harusi yangu»: Siku ya zafa langu.

[2] «Akaketi»: Alikaa.

[3] «Wakiwataja kwa sifa njema»: Maana yake ni kuwataja waliokufa kwa sifa zao bora, jambo ambalo huamsha shauku kwao na kilio.

[4] Imepokelewa na Ahmad katika «Musnad» yake (44/ 570).

[5] Imepokelewa na Al-Bukhari.

Share this:

Related Fatwas