Hukumu ya kucheza ngoma

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kucheza ngoma

Question

Ni nini hukumu ya kucheza ngoma?

Answer

Kucheza ngoma ni mkusanyiko wa miondoko ya mwili anayoifanya mtu kuelezea furaha, na hakuna andiko katika Sharia lililokuja kuharamisha jambo hilo; badala yake, imekuja katika Sunna kile kinachoashiria kuruhusiwa kwake. Kutoka kwa Mama wa Waumini Aisha (R.A.), amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alikuwa ameketi, tukasikia sauti za watu na sauti za watoto, Mtume S.A.W. akasimama, na mara akamuona mwanamke wa Kihabeshi anacheza ngoma na watoto wamemzunguka. Akasema: "Ewe Aisha, njoo utazame." Nikaja nikaweka kidevu changu juu ya bega la Mtume S.A.W, nikaanza kumtazama (yule mchezaji) kupitia nafasi iliyo kati ya bega na kichwa chake. Akaniambia: "Je, hujatosheka? Je, hujatosheka?" Nikawa nasema: "Bado," ili nione nafasi yangu (upendo wake) kwake”.

Ama mwanamke kucheza ngoma mbele ya wanaume (wasiokuwa maharimu wake), hilo ni jambo la Haramu kisharia. Lakini, ikiwa mwanamke anacheza ngoma mbele ya wanawake pekee, hilo ni jambo linalojuzu kwa sharti kwamba kusiwe na baadhi ya wanawake wasioaminika au watoto wenye utambuzi; kwa hofu kuwa wanaweza kuelezea sifa za mwili wa mwanamke huyo anayecheza ngoma kwa watu wengine.

Ama kuhusu mwanamke kuchezea ngoma mbele ya mume wake bila mtu mwingine yeyote kuwaona, hilo ni jambo linaloruhusiwa kisharia, na hata hupendekezwa ikiwa mke anafanya hivyo kwa ajili ya kumfurahisha / kumburudisha mume wake.

Maelezo

Kucheza (ngoma/kudensi/ kudengua) ni mkusanyiko wa miondoko ya mwili anayoifanya mtu katika minasaba mbalimbali kuelezea furaha na bashasha. Kucheza kuna aina nyingi, ikiwemo kucheza kwa panga, kwa kutumia farasi, na aina nyinginezo zinazorejea kwenye mila, desturi, na tamaduni mbalimbali.

Haikuja katika Sharia tukufu kile kinachoharamisha kucheza; badala yake, imekuja katika Hadithi ya Mtume kile kinachoashiria kuruhusiwa kwake (Muabaha). Kutoka kwa Anas bin Malik (R.A.) amesema: “Watu wa Habeshi walikuwa wakicheza (yazfinuna)[1] mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) na wanacheza huku wakisema: "Muhammad ni mja mwema." Mtume (S.A.W) akauliza: "Wanasema nini?" Wakasema: "Wanasema Muhammad ni mja mwema"”[2].

Na kutoka kwa Mama wa Waumini Aisha (R.A.) amesema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akisimama mlangoni mwa chumba changu, na watu wa Habeshi wakicheza kwa mikuki yao katika Msikiti wa Mtume( S.A.W.); ananisitiri kwa shuka yake ili niweze kutazama mchezo wao, kisha anabaki amesimama kwa ajili yangu mpaka mimi mwenyewe niondoke” [Imepokelewa na Muslim].

Na kutoka kwa Aisha (R.A.) amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alikuwa ameketi, tukasikia makelele na sauti za watoto. Mtume S.A.W. akasimama, na mara akamuona mwanamke wa Kihabeshi akicheza na watoto wamemzunguka. Akasema: "Ewe Aisha, njoo utazame." Nikaja nikaweka kidevu changu juu ya bega la Mtume (S.A.W), nikaanza kumtazama kupitia nafasi iliyo kati ya bega na kichwa chake. Akaniambia: "Je, hujatosheka? Je, hujatosheka?" Nikawa nasema: "Bado," ili nione nafasi yangu (upendo wake) kwake” [Imepokelewa na Al-Tirmidhi].

Hivyo basi, hadithi hizi kwa ujumla wake zinaonyesha kuruhusiwa kwa kucheza, sawa mchezaji awe mwanamume au mwanamke, na (kunaruhusiwa) kumtazama anayecheza maadamu jambo hilo halipelekei kutokea kwa fitna au mambo mengine ya haramu.

Ama mwanamke kucheza akiwa amevaa mavazi ya nusu uchi, kile kinachoitwa “Oriental Dance/Belly Dance”, hukumu yake ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Mwanamke kucheza ngoma mbele ya wanaume wasiokuwa maharimu kwa mavazi haya yanayodhihirisha mapambo yake na kuchora umbo la mwili wake ni jambo la Haramu kisheria na ni miongoni mwa madhambi makubwa; kwa sababu ndani yake kuna uenezaji wa machafu na uchochezi wa hisia na matamanio. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao. Hilo ni takaso zaidi kwao... Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika} [Al-Nur: 30-31].

Pili: Mwanamke kucheza ngoma mbele ya wanawake wenzake kwa mavazi haya ni jambo linalojuzu kisharia, lakini kwa masharti yafuatayo:

Mavazi hayo ya kuchezea yawe ni yenye kusitiri maeneo ya tupu nzito ya mwanamke.

Mwanamke asicheze mbele ya baadhi ya wanawake wasioaminika jambo ambalo linawanaweza kuzalisha wivu au husuda.

Mwanamke asicheze mbele ya watoto wenye utambuzi, kwa hofu kuwa wanaweza kuelezea sifa za mwili wa mwanamke huyo wakati akicheza.

Hairuhusiwi kupiga picha onyesho hili na kulisambaza, kwani jambo hilo ni haramu kisheria.

Tatu: Mwanamke kucheza ngoma mbele ya mume wake kwa mavazi haya ni jambo linaloruhusiwa (Mubaha), bali hupendekezwa (Mustahabb) ikiwa mke anafanya hivyo katika Faragha[3] na mume wake ili kumletea bashasha na furaha, ikiwa anajua kuwa mume wake anapenda na anafurahia jambo hilo.

Ama kuhusu kile kinachoitwa "Kucheza kwa Kizungu" “Western Dance”: Ambao sharti lake ni mwanamke kucheza ngoma pamoja na mwanamume kwa wakati mmoja, hukumu yake ni hivi:

Moja: Ikiwa uchezaji huu ni kati ya mwanamke na mwanamume asiye mumewe wala maharimu, ni jambo la Haramu kisheria.

Pili: Ikiwa uchezaji huu ni kati ya mwanamke na mume wake lakini mbele ya wanaume ajinabi, ni Haramu pia; bali hiyo ni miongoni mwa haramu mbaya zaidi zilizokatazwa na Uislamu. Kutoka kwa Abdullah bin Umar (R.A.), Mtume (S.A.W) amesema: “Watu watatu Mwenyezi Mungu amewaharamishia Pepo: Mlevi wa kudumu, Mwenye kuwatendea ubaya wake, na Mtu asie na wivu ambaye anaridhia machafu katika familia yake”.

Tatu: Ikiwa uchezaji huu ni kati ya mwanamke na mume wake ndani ya nyumba yao na hakuna anayewaona, basi ni jambo linalojuzu kisheria na halina kizuizi.

Tunapata faidia Kutokana na yaliyotangulia:

Halikuja katika Sharia katazo la jumla kuhusu kucheza; bali zimepokelewa baadhi ya hadithi za Mtume zinazoruhusu jambo hilo maadamu halipelekei katika kutumbukia kwenye fitna na mambo ya machafu.

Kile kinachoitwa “Belly Dance” na pia "Kucheza kwa Kizungu" “Western Dance”, haijuzu kufanywa mbele ya wanaume wasiokuwa maharimu na hata mbele ya ndugu, isipokuwa mbele ya mume pekee wakiwa faraghani.

Mwanamke kucheza ngoma mbele ya wanawake wenzake ni jambo linalojuzu kisheria, lakini kwa sharti kwamba kusiwe na baadhi ya wanawake wasioaminika au watoto wenye utambuzi; kwa hofu kuwa wanaweza kuelezea sifa za mwili wa mwanamke huyo anayecheza kwa watu wengine.

Kucheza kati ya mke na mume bila mtu mwingine yeyote kuwaona ni jambo linaloruhusiwa kisheria (Mubaha), bali hupendekezwa ikiwa mke anafanya hivyo kwa ajili ya kumfurahisha mume wake, na anapata thawabu kwa jambo hilo.

 

[1] «Yazfinuna»: Wanacheza na kudensi.

[2] Imepokelewa na Ahmad katika "Musnad" yake (20/17).

[3] «Faragha» (Al-Khalwa): Ni mwanamume na mwanamke kuwa sehemu moja ambayo hakuna anayewaona, kama chumba cha kulala na mfano wake.

Share this:

Related Fatwas