Hukumu ya kuvaa tai iliyotengezwa kwa hariri
Question
Sisi ni wataalamu wa kushona na kutengeneza mavazi ya wanaume, na tunaingiza baadhi ya vitambaa kwa ajili ya kutengeneza tai. Baadhi ya vitambaa hivyo vinaweza kuwa vya hariri asilia, lakini ndani yake huwekwa ujazo wa sufu na bitana ya hariri ya viwandani. Tuna mtu anayehusika na utengenezaji wa tai hizi, lakini anakataa kufanya kazi kwa kutumia vitambaa vya hariri asilia, akidai kuwa ni haramu kwa wanaume.
Answer
Je, hukumu ya kazi hii ni ipi kwa mujibu wa sharia ya Kiislamu?
Jibu:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Imethibitika katika Sunna tukufu ya Mtume (S.A.W.) kwamba amekataza wanaume kuvaa hariri, kama alivyonukuliwa akisema (S.A.W.): "Msivae hariri wala dibaji, wala msinywe kwenye vyombo vya dhahabu na fedha, wala msile kwenye asahani zake; kwani hivyo ni kwao katika dunia, na ni vyenu katika Akhera." (Imepokelewa kwa makubaliano na Wanazuoni kutoka kwa Hudhayfah (R.A.). Na pia Mtume (S.A.W.) amesema: "Vazi la dhahabu na hariri limeharamishwa kwa wanaume wa umma wangu, na kuruhusiwa kwa wanawake wao." (Imepokelewa na Imamu Ahmad na At-Tirmidhiy na kuhesabiwa kuwa sahihi).
Lakini katazo hili linahusu hariri ya asili (hariri halisi) inayotolewa kutoka kwa bui bui wa hariri (mdudu wa hariri). Ama hariri ya viwandani, haijumuishwi katika katazo hilo, hata kama inakuwa laini kama ya asili. Na kwa kweli, mengi yanayodhaniwa kuwa hariri ya asili siku hizi si ya asili: mengine huchanganywa na nyuzi nyingine, na nyingine hufanana sana na ya asili ilhali yametengenezwa kwa nyuzi za kisasa za viwandani. Yote haya si haramu, hata yakipewa jina la “hariri”; kwa kuwa hukumu za kisharia huzingatia uhalisia wa kitu, si jina lake.
Pia, imepokelewa ruhusa kutoka kwa Mtume (S.A.W.) ya kutumia hariri ya asili ndani ya mavazi, kwa kiwango kisichozidi upana wa vidole vinne. Imepokelewa na Imamu Muslim katika Sahihi yake kutoka kwa Suwayd bin Ghafala, kwamba Umar bin Khattab (R.A.) alihutubu katika Jabiyah akasema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alikataza kuvaa hariri isipokuwa katika sehemu ya vidole viwili, au vitatu, au vinne"
Na imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.) Mwanachuoni mkuu wa Umma na mfasiri wa Qur’ani Tukufu, kwamba yeye alieleza kuwa katazo la Mtume linahusu mavazi yaliyotengenezwa kwa hariri safi tu. Naye Abu Dawud katika Sunan yake amepokea kutoka kwa Ibn Abbas akisema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alikataza vazi linalotengenezwa kwa hariri safi, lakini kuhusu sehemu ya hariri (alama au mapambo), au hariri iliyochanganywa kwenye nyuzi za vazi, hakuna ubaya."
Hukumu hii pia imetajwa na Al-Hakim kwa sanad sahihi, kama alivyosema Al-Hafidh Ibn Hajar katika Fathul-Bari, kwa maneno: "Alichokataza ni hariri safi." Na At-Tabarani katika njia nyingine ya riwaya: "Alikataza hariri safi, lakini ikiwa nyuzi zake zimetokana na pamba au kitani, basi hakuna ubaya." Na hii ina hukumu ya kuinuliwa (hadi kwa Mtume).
Na haya ndiyo yaliyoshikiliwa na Masahaba wengi (R.A.) hadi yameripotiwa kutoka kwa zaidi ya Maswahaba ishirini. Al-Hafidh Ibn Hajar Al-Asqalani alisema: "Imethibitika kuwa baadhi ya masahaba na wengine walivaa ‘khazz’ (aina ya nguo inayotengenezwa kwa kuchanganya hariri na nyuzi nyingine)." Abu Dawud alisema: "Watu ishirini miongoni mwa masahaba au zaidi walivaa khazz." Na Ibn Abi Shaybah amelipokea hili kutoka kwa kundi la Maswahaba na kutoka kwa baadhi ya wafuasi (tabi'in) kwa isnadi thabiti. Na riwaya mashuhuri zaidi ni ile iliyopokewa na Abu Dawud na An-Nasai kutoka kwa Abdullah bin Sa’d ad-Dashtaki kutoka kwa baba yake, aliyesema: "Nilimwona mtu juu ya Baghla (mnyama wa kupanda anayefanana na farasi na punda) akiwa amevaa kilemba cheusi cha khazz, akisema: Hiki nilivalishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.)"
Ibn Abi Shaybah amepokea kwa njia ya ‘Ammar bin Abi ‘Ammar, aliyesema: "Zilipelekwa kwa Marwan bin Al-Hakam nguo za aina ya khazz (nguo ya hariri iliyochanganywa na nyuzi nyingine), basi akawagawia Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.)"[1]
Imamu Ibn Qudamah Al-Hanbaliy alisema: "Hili lilienea, na hakuna kilichojitokeza kinyume chake, hivyo ikawa ni Ijmaa‘ (makubaliano ya pamoja)."[2]
Na hii ndiyo kauli ya Wanazuoni wengi wa Fiqhi, na ndio msimamo wa madhehebu manne yanayofuatwa – ijapokuwa kuna tofauti ndogo kati yao – ambapo walieleza kuwa Hadithi za katazo zinahusu hariri safi, na kama hariri imechanganywa na kitu kingine, basi hukumu inatolewa kwa kuangalia kile kilicho kingi kwa uzito au kinachoonekana zaidi.
Imamu Ibn Rushd Al-Malikiy alisema: "Kilichoharamishwa kwa mwanamume kukivaa ni nguo iliyotengenezwa kwa hariri safi tu, lakini nguo ya hariri iliyochanganywa na pamba, kitani au sufu siyo haramu."[3]
Imamu Abu Al-Fath Ibn Daqiq Al-‘Id alisema: "Hadithi inazungumzia hariri kwa ujumla, lakini kwa mujibu wa wanazuoni wengi, inahusu hariri safi kwa upande wa wanaume, na hili ni katazo la haramu. Ama hariri iliyochanganywa na vitu vingine, basi wanazuoni wametofautiana: baadhi yao wanaangalia uzito, na wengine wanaangalia kinachoonekana kwa macho."[4]
Al-Hafidh Ibn Hajar alisema: "Ibn Al-‘Arabi alitoa hoja ya uhalali kwa kusema: katazo linahusu hariri safi, na ruhusa kuhusu pamba na mfano wake ni wazi. Basi hariri ikichanganywa kiasi kwamba haijulikani tena kama hariri wala haijumuishwi na sababu ya uharamu, basi haiko tena katika yaliyokatazwa, hivyo inaruhusiwa."[5]
Wanazuoni wa Fiqhi wamesema wazi kuwa ikiwa nguo imefumwa au kutengenezwa kwa hariri na kitu kingine, basi haipaswi kuitwa nguo ya hariri.
Imamu Al-Rafi‘iy wa madhehebu ya Shafi alisema: "Ikiwa hariri (ibreesim) ndiyo yenye uzito zaidi, basi ni haramu. Na ikiwa zimechanganyika nusu kwa nusu – basi kuna maoni mawili: yenye nguvu zaidi ni kwamba si haramu, kwa kuwa haiitwi tena nguo ya hariri."[6]
Kutokana na hayo, miongoni mwa kanuni za kifiqhi zilizoainishwa na Wanazuoni ni kuwa uharamu wa hariri si kama ule wa dhahabu; kwa kuwa katazo la dhahabu linahusu kila sehemu yake, tofauti na hariri – kama tulivyoeleza. Kwa hivyo, kuna upana zaidi katika hukumu ya hariri kuliko ilivyo kwa dhahabu.
Imamu Al-Ghazali (R.A.) alisema: "Mambo yahusuyo hariri ni mepesi zaidi kuliko dhahabu; kwa kuwa hariri inayovaliwa bila dharura inaruhusiwa, lakini chombo kilichopambwa kwa dhahabu hakiruhusiwi."[7]
Imamu An-Nawawiy – Rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – alisema: "Katazo la hariri linahusu nguo zilizofumwa kwa hariri safi au yenye sehemu kubwa ya hariri. Sio linalokusudiwa kuwa kila sehemu ya hariri ni haramu, tofauti na pombe na dhahabu, ambapo kila sehemu yake ni haramu."[8]
Kufunga tai shingoni: ni kipande cha kitambaa kinachokatwa kwa vipimo maalumu na katika rangi mbalimbali, ili kiwekwe kwenye shingo ya shati — yaani kwenye kola — na kufungwa shingoni kama mkufu kwa njia mbalimbali za kufunga fundo. Kisha sehemu ya tai huteleza kutoka kwenye fundo, katika aina nyingi hufanana na mkia wa nywele na hufika kwenye kitovu au hata chini zaidi. Upana wake huongezeka kadri inavyoshuka hadi kufikia upana wa vidole vinne, na wakati mwingine hufikia vitano au sita.
Kwa sifa hizi, inaruhusiwa kutengeneza na kutumia tai hata kama imetengenezwa kwa hariri, kwa sababu zifuatazo:
Tai ya shingoni kimsingi ni kamba inayofungwa kwenye shati, na hii ndiyo maana ya neno libnat Al-jayb katika lugha ya Kiarabu, ambapo jayb ni sehemu ya mbele ya shati iliyo wazi kifuani, na libna ni ukingo unaozunguka shingo. Imethibitika katika hadithi ya Asmaa (R.A.) kwamba joho la Mtume (S.A.W.) libnat al-jayb yake ilikuwa ya dibaji (aina ya hariri safi), na hili linajumuisha iwe imeunganishwa moja kwa moja au imewekwa kwa juu. Basi hukumu ya ruhusa inajumlisha yote haya iwapo itachukuliwa kama sehemu ya "libnat al-jayb" kwa mujibu wa lugha, au kwa kipimo kwa hali iliyofanana kama ikizingatiwa kuwa "libna" ni ile tu iliyoshonwa pamoja na nguo.
Pia imepokelewa ruhusa ya kutumia mapambo ya hariri (alama au vipambo vilivyowekwa kwenye vazi), kama alivosema Ibn Abbas (R.A.): "Ama mapambo ya hariri na nyuzi zake katika nguo, basi hakuna ubaya." Na "alam" ya nguo ni kile kinachowekwa juu yake kwa kupamba, si sehemu ya nyuzi zake. Basi tai inahesabiwa kuwa ni alam ya shati kwa mazoea, hivyo inajumuishwa kwenye ruhusa.
Imamu Ibn Qudamah alisema: "Inaruhusiwa kuwa na mapambo ya hariri kwenye nguo mpaka vidole vinne au chini ya hapo, kwa mujibu wa riwaya ya Umar bin al-Khattab (R.A.) aliyesema: Mtume (S.A.W.) alikataza kuvaa hariri isipokuwa kwenye sehemu ya vidole viwili, vitatu au vinne." (Imepokewa na Abu Dawud na At-Tirmidhi, na akasema: Hadithi Hassan Sahih).
Na katika kitabu cha At-Tanbih: "Inaruhusiwa hata ikiwa imepambwa kwa dhahabu, na ndivyo ilivyo kwa viraka, libnat al-jayb, mapambo ya manyoya na mengineyo; kwa kuwa yote haya yanajumuishwa na Hadithi hiyo."[9].
Tai kwa kawaida haizidi upana wa vidole vinne, hivyo inabaki ndani ya kiwango cha ruhusa kilichoelezwa kisharia. Zaidi ya hayo, baadhi ya Wanazuoni waliona kwamba ruhusa ya mapambo ya hariri na mfano wake haikuzuiwa kwa kiwango fulani, bali walieleza kwamba kiasi kilichotajwa ni mfano, si kikomo.
Mwanachoni Shaykh Zadeh Al-Hanafiy alisema: "Katika Al-Siyar Al-Kabir’: Mapambo ya hariri yanaruhusiwa kabisa, iwe ni madogo au makubwa." Akaongeza: "Hili linatofautiana na yaliyotajwa katika vitabu vingine mashuhuri vinavyoweka mipaka ya vidole vitatu au vinne. Na hili lina ruhusa kubwa kwa wale waliokumbwa na jambo hilo, kama watu wa hadhi au wakubwa."[10]
Imamu Al-Baji Al-Malikiy alisema: "Ibn Habib alisema: Hakuna ubaya kwa mapambo ya hariri kwenye nguo, hata kama ni makubwa."[11]
Naye Al-Shawkani amesema: "Baadhi ya wanazuoni wa Malikiy wamesema jambo la ajabu, wakasema kuwa inajuzu kuwepo kwa mapambo ya hariri hata yakizidi upana wa vidole vinne."[12].
Kauli hii imekubaliwa pia na wanazuoni wa Madhehebu ya Imamu Shafi kuhusu nguo iliyopambwa kwa hariri pembezoni (mutarraf bil-harir) — yaani nguo ambayo sehemu za pembeni zimepambwa kwa vipande vya hariri. Hawakuweka mipaka ya idadi ya vidole vinne kwa hariri hiyo, bali waliangalia mazoea ya kawaida katika kila jamii. Hii ni tofauti na nguo iliyodairiziwa kwa hariri, ambapo waliweka mpaka wa vipande vya hariri visizidi vidole vinne.
Dalili ya kauli hii ni kauli ya Ibn ‘Abbas (R.A.) aliposema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alikataza nguo zilitengenezwa kwa hariri safi, lakini kuhusu mapambo ya hariri na nyuzi zake ndani ya nguo, hakuna ubaya wowote."
Dalili nyingine ni Hadithi ya Bi Asma’ bint Abi Bakr (R.A.) kuhusu maelezo ya joho la Mtume (S.A.W.) katika riwaya ya Imamu Ahmad katika Al-Musnad na Al-Bukhari katika Al-Adab Al-Mufrad, kwa lafudhi hii: "Lilikuwa na libna ya shibri (upana wa kiganja) ya dibaji (hariri safi), na sehemu za mbele zilipambwa kwa hariri hiyo."
Al-San‘ani alisema: "Inawezekana kupokelewa kuwa mapambo hayo yalikuwa ya vidole vinne au chini yake, au hata zaidi ikiwa si hariri safi ya moja kwa moja (musmat); ili kuzikutanisha dalili zote."[13]
Shawkani alitoa maelezo yake juu ya hayo aliyoyasema Al-San‘ani akisema: "Hadithi hiyo inaonyesha uhalali wa kuvaa mavazi yenye sehemu ya hariri ya kiasi hicho. Na baadhi wamesema kuwa inamaanisha hariri hiyo ilikuwa ndani ya kiwango cha vidole vinne au zaidi kidogo, kama haikuwa safi. Lakini maelezo ya hadithi: 'shibri ya dibaji' yanapingana na tafsiri hiyo, kwani inadhihirisha kuwa ilikuwa ya dibaji pekee, si mchanganyiko wake na kitu kingine – isipokuwa kwa kuichukulia kwa maana ya Istiara. Naam, inaweza kusemwa kuwa 'shibri' ilikusudiwa kuwa ni kipimo cha urefu wa mapambo hayo, si upana wake — jambo linaloondoa utata."[14] Lakini hili nalo linakosolewa kwa sababu maana ya wazi ya "shibri" hapa ni upana, si urefu.
Hivyo basi, kauli hii ni njia nzuri ya kufikia ruhusa kwa mtu kuvaa tai ya hariri hata kama upana wake unazidi vidole vinne, kwa kutegemea ruhusa zilizoelezwa katika dalili hizi.
Na urefu wa tai ukiwa zaidi ya vidole vinne hauiingizi nje ya mipaka ya ruhusa ya kisharia, kwani mipaka ya vidole vinne imewekwa tu kwa upana, na si kwa urefu — kama ilivyoelezwa na wanazuoni wa Madhehebu ya Hanafiyyah na Shafi‘iyyah.
Mwanachuoni Maarufu Ibn ‘Abidin Al-Hanafiy alisema katika Hashiyah yake: "Je, kinachokusudiwa ni kwamba mapambo yasizidi vidole vinne kwa upana na urefu, au ni upana tu – hata kama urefu ukizidi? Maana inayoeleweka haraka katika kauli zao ni ya pili, na pia maelezo ya sharh kutoka kwa Al-Hawi Al-Zahidi yanayokuja yanaunga mkono hilo."[15]
Na Mwanachuoni Maarufu Sulayman Al-Jamal Al-Shafi‘iy alisema katika Hashiyah yake: "Kilichopatikana kutokana na kauli zao ni kwamba ni haramu kuzidisha upana wa vidole vinne vilivyokunjwa pamoja, lakini hakuna kikomo kwa upande wa urefu."[16]
Tai ya shingoni huvaliwa kama sehemu ya vazi jingine, si kama vazi lenyewe, kwani haiwekwi peke yake bali huambatana na shati na kuwa mfuatano wake, si kitu huru kinachojitegemea. Na katika kanuni za kifiqhi, Yanajuzu katika kitu kikuu yasiojuzu katika kidogo chake, Hili ndilo walilolieleza Wanazuoni kwa kauli zao “Husamehewa katika vitu vidogo visivyosamehewa katika vnginevyo,” au “Husamehewa katika jumla ya kitu yasiyosamehewa katika kitu chenyewe,” au “ Husamehewa katika vitu vya pili visivyosamehewa katika vipaumbele.”
Hii ndiyo maana ya kuruhusiwa kwa mapambo ya hariri katika nguo, na kwa sababu hii, wanazuoni walikubaliana juu ya uhalali wa kutumia vitu vidogo vinavyohusiana na mavazi kuwa vya hariri safi, kama vile: Kamba ya kofia ya tarabushi (iwe kikubwa au kidogo), kamba za mapambo (qayṭān) za joho au suti, mapambo ya kilemba, kamba za kufungia nguo, mashimo ya vitufe vya shati, vifungo vyenyewe, na vinginevyo.
Sheikh Burhānuddīn Māzah Al-Najārī Al-Hanafiy alisema: "Imepokewa kutoka kwa Hishām kutoka kwa Abū Ḥanīfa (R.A.) kuwa hakuona ubaya kuwa na mapambo ya hariri katika nguo kiasi cha vidole vinne; akasema: kwa sababu mapambo ni mfuatano wa nguo, si sehemu ya nguo kwa maana halisi. Katika ‘Nawādir Ibn Samā‘ah’ kutoka kwa Muḥammad: Ikiwa mtu ataweka hariri kwenye shati lake, au mashimo ya vitufe, au vitufe vyenyewe – sioni ubaya wowote, kwani vinafuata nguo na si sehemu ya msingi; lakini akitumia peke yake, haifai. Pia alisema: nachukia kamba ya hariri kwa sababu huvaliwa peke yake. Hii ni kwa sababu ikiwa kitu hicho kinapatikana pamoja na nguo nyingine, basi hakihesabiki kama kilichovaliwa kwa uhakika; bali kinakuwa kimefuatana nayo tu. Na kilichoharamishwa ni kuvaa hariri kwa uhakika. Katika ‘Sharḥ Al-Jāmi‘ Al-Ṣaghīr’ baadhi ya masheikh walisema: Hakuna ubaya kwa mwanamume kutumia kamba ya hariri kwa mujibu wa Abū Ḥanīfa (R.A.)"[17]
Mwanachuoni Sīdī Abū Al-Barakāt Al-Dardīr Al-Mālikiy alisema katika Al-Sharḥ Al-Kabīr’: "Mifano ya yanayoruhusiwa kufanywa kwa hariri ni mistari ya mapambo na kushonea kwa hariri, na pia kamba za mapambo za joho (qayṭān al-jūkh)... Na kuhusu mapambo yaliyo makubwa, itatazamwa; lakini ikiwa ni kama vidole vinne, basi kauli yenye nguvu ni kwamba inajuzu."[18]
Mwanachuoni Maarufu Ibn Ḥajar Al-Haytamī Al-Shāfi‘iy alisema: "Inajuzu pia vifungo vya shati... na mifuko midogo ya kuhifadhia sarafu hata kama unaitumia, na pia mfuniko wa kilemba."[19]
Mwanachuoni Maarufu Al-Sharwānī alisema: "Baadhi ya wanazuoni walisema kuwa kamba ya tarbaushi ni halali, na baadhi waliiharamisha. Lakini kwa kuwa matumizi yake yameenea sana katika zama hizi, basi inafaa kufuata kauli ya uhalali ili kuepuka dhambi."[20]
Mtaalamu Maarufu Sulaymān Al-Jamal Al-Shāfi‘iy alisema katika ḥāshiyah yake: "Baadhi ya masheikh walikubaliana kuwa kamba ya tarbaushi ni halali, kiwe kikubwa au kidogo; kwani haina tofauti na vipande vya hariri vinavyowekwa juu ya nguo (ṭirāz), navyo pia ni halali. Lengo la yote hayo ni mapambo."[21]
Kile kilichokatazwa kisharia ni kuvaa hariri halisi, kama ilivyo katika Hadithi ya Sahih Bukhari na Muslim: “Msivae hariri wala dibaji.” Asili ya neno "kuvaa" katika lugha ya Kiarabu inamaanisha mchanganyiko wa moja kwa moja au kufunika mwili kwa nguo, kama walivyosema Ibn Fāris[22] na Al-Ṣāḥib Ibn ‘Abbād[23]. Na kuvalia nguo ni kujifunika nayo mwilini, kama ilivyoelezwa katika Al-Mu‘jam Al-Wasīṭ. Hii yote inaonyesha kwamba kigezo cha uharamu ni kuvaa nguo za hariri zinazomfunika mtu, lakini tai ya shingoni haihesabiwi kuwa nguo wala si vazi linalofunika mwili kama mashati, suruali au joho, hivyo haijumuishwi moja kwa moja katika uharamu. Na kama ikiitwa “vazi” basi hiyo ni kwa njia ya majazi tu (istiara), kwa sababu imefungwa kwa nguo ya yenyewe, na si kama vazi linalojitegemea. Na kilichokatazwa ni uvaaji wa hariri halisi, si ule wa majazi au wa kimila, kwa kuwa asili ya hukumu za kisharia ni kuzingatia maana halisi.
Wanazuoni pia wametaja wazi kidhibiti hiki – kwamba uharamu unatokana na kuvaa: Basi kilicho haramu kwa hariri ni kile kinachojulikana wazi kuwa vazi la kuvaa. Kisichokuwa vazi, si haramu,. Katika kitabu cha Al-Muḥīṭ, mwandishi amesema: "Hii ni kwa sababu ikiwa kitu hicho kipo pamoja na nguo nyingine, basi si vazi kwa maana ya moja kwa moja, bali ni kimeambatanishwa na vazi, na kilichokatazwa ni kuvaa hariri yenyewe."[24].
Kwa sababu hiyo, Wanazuoni waliruhusu kutumiwa kwa vitu vingi vilivyotengenezwa kwa hariri ambavyo havihesabiki kuwa ni “mavazi” kwa maana halisi, bali kwa njia ya tamko la kifasihi au kwa kuwa ni vitu vinavyofuatana na mavazi—kama ilivyoelezwa katika kipengele cha nne hapo kabla—au ambavyo havihesabiwi kuwa mavazi hata kidogo, kama vile: neti ya kuzuia mbu, vijipambo vya tasbihi, kamba ya funguo au ya mizani, mfuko wa sarafu, kamba za mizigo, kitambaa cha kufutia kalamu (wino), kifuniko cha kikombe au jagi, kamba ya kushikilia msahafu, kamba ya kushikilia kisu au upanga, na vinginevyo kama hivyo.
Imenukuliwa katika "Al-Fatāwā Al-Hindiyyah" kwa mujibu wa Madhehebu ya Hanafi: "Kutumia blanketi la hariri (ibrisim) si halali, kwa kuwa ni aina ya mavazi. Lakini hakuna ubaya kuweka shuka ya hariri juu katika kitanda cha mtoto mchanga, kwa kuwa hiyo si vazi. Vivyo hivyo, kutumia chandarua ya hariri kwa wanaume siyo haramu, kwani ni kama nyumba." Pia imesemwa katika kitabu cha Al-Tamartāshī: "Hakuna ubaya kufanya kitambaa cha kufunika kuwa cha hariri."[25]
Mwanachuoni Maarufu Sīdī Al-Dardīr alisema: "Kama vile kuutundika kama pazia bila kutegemea, vivyo hivyo chandarua... na tasbihi; pia inaruhusiwa bendera ya vita."[26]
Mwanachuoni Maarufu Ibn Ḥajar Al-Haytamī Al-Shāfi‘iy alisema: "Inaruhusiwa kutumia kitambaa cha kufutia wino... na imeelezwa katika 'al-Majmū‘' kuwa inaruhusiwa kamba ya tasbihi ya hariri."[27].
Al-Sharwānī amesema: "Sheikh Sam amrsema katika Al-Minhāj’: Imamu Al-Ramlī alikubali uhalali wa kamba ya tasbihi kuwa ya hariri, na vivyo hivyo vipambo vyake kwa kuwa vinafuata kamba hiyo. Amesema: Inafaa pia kutumia kamba ya hariri kwa ajili ya funguo, iwapo kuna haja."[28].
Zaidi ya hayo, baadhi ya Wanazuoni wa Hanafi walinukuu kutoka kwa Imamu Abū Ḥanīfah (R.A.) kuwa ana kauli inayoruhusu kuvaa hariri iwapo haitagusa ngozi ya mwili, na hii imetajwa na Al-Ḥalwānī kutoka kwa Ibn ‘Abbās (R.A.). Inaelekea kuwa msingi wa hoja hii ni kwamba neno "kuvaa" (libās) kwa asili linamaanisha kuingiliana au kugusana moja kwa moja, hivyo walichukua hilo kama sharti la kuwepo kwa uvaaji wa kweli.
Mwanachuoni Shaykh Zāda alisema: "Katika Al-Qunyah’, ikinukuliwa kutoka kwa Burhān mwandishi wa Al-Muḥīṭ’: Kwa mujibu wa Imamu, haichukizwi kuvaa hariri ikiwa haitagusana moja kwa moja na ngozi, hata mtu akiivaa juu ya shati la pamba au mfano wake, siyo karaha kwake. Itakuwaje ikiwa ameivaa juu ya koti au kitu kingine kilichojazwa (kisicho cha hariri), na koti hilo ikiwa la hariri lakini foronya yake si hariri, au akaiweka juu ya shati la pamba? Akasema: Hii ni ruhusa kubwa katika jambo ambalo watu wengi wamekumbwa nalo. Lakini nilipotafuta kauli hii ya Imamu katika vitabu vingi sikuipata isipokuwa hapa." Kisha akasema kwa kunukuu kutoka kwa Al-Ḥalwānī: "Watu wengine wanasema kuwa uvaaji wa hariri unachukiza ikiwa tu itagusa ngozi, kama sivyo siyo haramu. Na kutoka kwa Ibn ‘Abbās (R.A.) ilisemwa kwamba alikuwa amevaa koti la hariri, akaambiwa kuhusu hilo, akajibu: ‘Huoni kuwa hakuna inachogusa mwili?’ Na chini yake kulikuwa na vazi la pamba." Kisha akasema: "Lakini kauli sahihi zaidi ni ile tuliyoitaja hapo juu: kwamba yote ni haramu."[30]
Kwa msingi huo, na kwa mujibu wa swali lililoulizwa: Inaruhusiwa kutengeneza na kutumia tai (kitambaa cha shingoni) cha hariri kwa wanaume, kwa mujibu wa kauli ya Wanazuoni wengi wa Kiislamu kuwa makatazo ya kutumia hariri yanahusu mavazi ya hariri ya asili au yale ambayo sehemu kubwa ni hariri. Ama pale ambapo hariri hutumiwa kama pambo au kwa haja ya mapambo, basi hiyo haimo katika makatazo, kwa kuwa haitachukuliwa kuwa ni “kuvaa” hariri, bali ni kutumia hariri kama pambo—na hili linajuzu. Hali hii inahusiana moja kwa moja na tai za hariri, kwa kuwa hazihesabiki kuwa ni mavazi au nguo, bali ni mapambo yanayowekwa juu ya mavazi kwa madhumuni ya uzuri. Kwa hivyo, zinakuwa kama pambo la hariri lililoruhusiwa, na hazivaliwi kama vazi huru, bali huvaliwa kama kiambatisho cha nguo nyingine, hivyo basi zinachukuliwa kuwa ni kiambatisho siyo vazi kamili. Kwa mantiki hii, zinahusiana na yale yaliyopokelewa kama ruhusa ya kisharia kwa wanaume kutumia hariri katika hali kama hizo.
Ama ikiwa upana wa tai unazidi vidole vinne, basi katika hilo kuna mitazamo miwili ya Wanazuoni: Wengi wao wamekataza, lakini Wanazuoni wa Madhehebu ya Hanafi na Maliki wameruhusu, na hakuna kizuizi cha kuchukua rai ya ruhusa, kama ilivyotangulia kuelezwa.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi
[1] Fathul-Bary, 10/259, toleo la Darul-Maarifa.
[2] Al-Mughny, 1/663, toleo la Darul-Fikr.
[3] Al-Bayan wa Al-Tahseel, 1/267, toleo la Darul-Gharb Al-Islamy
[4] Ihkam Al-Ahkam, 1/485, toleo la Shirika la Al-Risala.
[5] Fathul-Bary, 10/295.
[6] Fathul-Aziz kwa Sharhul-Wageez kinachoitwa Al-Sharh Al-Kabiir, 5/29, toleo la Darul-Fikr.
[7] Al-Waseet, 2/321, toleo la Darul-Salaam.
[8] Sharh Sahih Muslim, 14/44, toleo la Dar Ihyaa Al-Turath Al-Araby.
[9] Al-Mughny, 1/660.
[10] Majma’a Al-Anhar kwa Sharh Multaqa Al-Abhar, 4/193, toleo la Dar Al-Kutub Al-Ilmiyya.
[11] Al-Muntaqa, Sharhul-Muwataa, 7/222, toleo la nyumba ya uchapisho ya Al-Sa’ada.
[12] Naylu-Awtar, 2/79, idara ya machapisho ya Al-Muniriya.
[13] Subul As-Salaam, 2/88, toleo la Mustafa Al-Halaby.
[14] Naylu-Awtar, 2/79- 80.
[15] Radul-Mukhtar Ala Al-Durr Al-Mukhtar, 6/351, toleo la Darul-Fikr.
[16] Futuhat al-Wahhab bi-Tawdih Sharh Minhaj al-Tullab ya Shaykh al-Islam Zakariyya al-Ansari, 3/472, chapa ya Darul-Fikr.
[17] Al-Muheet Al-Burhany, 5/190, chapa ya Ihyaa Al-Turath Al-Araby.
[18] Al-Sharh Al-Kabiir, 1/220, chapa ya Ihyaa Al-kutub Al-Arabiyyah.
[19] Tuhfat Al-Muhtaj bi Sharh Al-Minhaj, 3/28, chapa ya Al-Maktaba Al-Tujariyyah.
[20] Hashiyat Al-Sharawany ala Al-Tuhfa cha Ibn Hajar, 3/29.
[21] Futuhat al-Wahhab bi-Tawdih Sharh Minhaj al-Tullab, 3/471-472.
[22] Kamusi la Maqayiis Allugha, 5/230, chapa ya Darul-Fikr.
[23] Al-Muheet fi Allugha, 8/329, chapa ya Alam Al-Kutub.
[24] Al-Muheet Al-Burhany, 5/190.
[25] Al-Fatawa Al-Hindiyyah, 1/73, chapa ya Darul-Fikr.
[26] Al-Sharh Al-Kabiir, 1/220.
[27] Tuhfat Al-Muhtaj, 3/28.
[28] Hasiyat Al-Sharawany ala Al-Tuhfa cha Ibn Hajar, 3/29.
[29] Al-Fatawa Al-Hindiyyah, 1/73.
[30] Mujamaa Al-Anhar, 4/193.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
