Kuamua Jinsia ya Kijusi
Question
Nini hukumu ya kuamua jinsia ya kijusi, na je, hilo linahesabika kuwa ni kupingana na utashi wa kimungu?
Answer
Imekuwa inawezekana kuingilia kati ili kuamua jinsia ya kijusi kabla ya ujauzito au katika hatua zake za kwanza; hiyo ni kulingana na matakwa ya wazazi au kwa sababu za kimatibabu, kutokana na maendeleo makubwa katika teknolojia ya kisasa ya matibabu. Njia hizi, ziwe za kiasili au za kimatibabu, hazina kizuizi kisharia, na ni katika mlango wa kuchukua sababu ambao haupingani na matakwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kuzingatia vigezo vya kisharia vya kutomdhuru mtoto atakayezaliwa, na kwamba jambo hilo lifanyike chini ya usimamizi wa Wataalamu wa tiba wenye ujuzi, na liwe katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na si katika ngazi ya umma; kwa sababu wakati huo litasababisha kuvurugika kwa usawa wa kiasili aliouweka Mwenyezi Mungu.
Maelezo
Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu katika umbo lenye usawa, akamfanya kuwa jozi mbili, mwanamume na mwanamke, na aina hii ya uumbaji na usawa katika asili ndivyo ilivyohitaji hekima ya Mwenyezi Mungu Mjuzi wa kila kitu. Amesema : {Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume. Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza} [Ash-Shura: 49-50].
Na kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia ya kisasa ya matibabu, imewezekana kuingilia kati ili kuamua jinsia ya kijusi kabla ya ujauzito au katika hatua zake za kwanza; hiyo ni kulingana na matakwa ya wazazi au kwa sababu za kimatibabu.
Na kuamua jinsia ya kijusi kulikuwa kukifanyika kwa njia za kiasili — zisizo za kimatibabu — ambazo inaaminika kuwa zinaathiri jinsia ya kijusi kama vile kufuata mfumo fulani wa chakula, au kupanga muda wa kujamiiana kwa kutafuta wakati wa kutoa yai.
Na kwa uvumbuzi wa kisasa wa matibabu, madaktari wameweza kuamua jinsia ya kijusi kimatibabu kwa kutenganisha mbegu ya kiume inayohusika na uume au uuke, na kisha yai kurutubishwa kwayo mahali pake ndani ya mwili, au mbegu ya mume na yai la mke huwekwa nje ya mji wa mimba katika maabara, kisha baada ya muingiliano na urutubishaji wao katika mrija nje ya mji wa mimba wa mke, yai lililorutubishwa hurejeshwa katika mji wa mimba wa mke huyo huyo bila kubadilishwa au kuchanganywa na mbegu za mtu mwingine.
Njia hizi, ziwe za kiasili au za kimatibabu, hazina kizuizi kisharia; kutokana na kile kilichothibiti kuwa: «Asili ya vitu ni uhalali mpaka itokee dalili ya uharamu».
Kama ambavyo kuamua jinsia ya kijusi ni katika mlango wa kuchukua sababu, na Sharia tukufu imeruhusu kuchukua sababu, maadamu hazigongani na malengo ya Sharia na misingi yake inayozingatiwa, kama vile "Al-Azl" (kutoa mbegu nje) ambacho kilikuwa kikifanyika na kuruhusiwa katika zama za Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), ambapo Maswahaba walikuwa wakikitumia kama sababu ya kuzuia ujauzito na kupanga upatikanaji wake.
Imepokelewa kutoka kwa Jabir bin Abdillah (R.A): «Tulikuwa tukifanya Al-Azl katika zama za Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), na jambo hilo likamfikia Nabii wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), na wala hakutukataza» (Imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslim).
Inafaa kuashiria hapa kuwa kuamua jinsia ya kijusi katika baadhi ya hali inaweza kuwa ndiyo suluhisho bora la kuepuka baadhi ya magonjwa yanayoweza kupata jinsia moja, kama kuwepo kwa magonjwa ya kurithi yanayowapata wanawake pekee na si wanaume au kinyume chake, ambapo lengo huwa ni kuepuka kuhamisha magonjwa haya kwa watoto; hiyo ni kwa kuegemea kile kilichothibitishwa na Sharia tukufu kuhusu wajibu wa kuondoa madhara. Kutoka kwa Ubadah bin Al-Samit (R.A): «Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alihukumu kuwa kusiwe na kudhuru wala kulipiza dhara»[1].
Uingiliaji wa kimatibabu ili kuamua jinsia ya kijusi haupingani na kuridhika na kadari, na wala ndani yake hamna kupingana na utashi wa kimungu; kwa sababu si zaidi ya kuwa ni sababu miongoni mwa sababu halali anazochukua mtu ili kufikia kile anachokitaka au kuepuka kinachomdhuru, maadamu hilo halitoki nje ya mipaka ya Sharia na vigezo vyake.
Inajulikana kuwa kuchukua sababu hakupingani na utashi wa Mwenyezi Mungu wa kuwa Yeye: {anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume} [Ash-Shura: 49]; kwa sababu sababu ambazo Mwenyezi Mungu alihukumu ziwe sababu za matokeo yake hazitoki nje ya mpango Wake na utashi Wake, bali ni miongoni mwa jumla ya uumbaji Wake na matakwa Yake, kama ambavyo zenyewe hazijitegemei katika kuleta athari, bali zinahitajika kwa amri ya Mwenyezi Mungu , kwani amesema: {Wala hamwezi kutaka ila atakapo Mwenyezi Mungu} [Al-Insaan: 30], na akasema : {Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya!} [As-Saffat: 96], na akasema : {Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu} [Az-Zumar: 62].
Mtume (S.A.W) aliruhusu Al-Azl, imepokelewa kutoka kwa Jabir Ibn Abdillah (R.A) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alisema: «Fanya Al-Azl naye ukitaka, kwani hakika kitamfikia kile alichokadiria (Mungu)» (Imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslim). Ikiwa Mtume (S.A.W) ameruhusu Al-Azl, na akabainisha kuwa hakupingani na uwezo wa Mwenyezi Mungu na matakwa Yake, pamoja na kuwa ndani yake kuna kuzuia uume na uuke kwa pamoja, basi kuruhusiwa kile chenye mmoja wao kunaruhusiwa zaidi (awla).
Pamoja na kusema kuwa inajuzu kutumia teknolojia hizi, lakini inashurutishwa kuzingatia vigezo vya kisharia vifuatavyo:
Kwanza: Kusiwe na madhara kwa mtoto katika siku zake zijazo na mustakabali wake kutokana na kuamua jinsia kwa moja ya njia hizi, na jambo hili linarejeshwa kwa wamu, kwani haikubaliki mwanadamu kuwa sehemu ya majaribio na uchezaji.
Pili: Jambo hilo lifanyike chini ya usimamizi wa Wataalamu wa tiba wenye ujuzi.
Tatu: Jambo hilo liwe katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na si katika ngazi ya umma; kwa sababu wakati huo litapelekea kuvurugika kwa usawa wa kiasili aliouweka Mwenyezi Mungu , na kuvurugika kwa usawa wa idadi kati ya wanaume na wanawake jambo ambalo litaathiri kuendelea kwa uzazi wa mwanadamu.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Kwamba uingiliaji wa kimatibabu ili kuamua jinsia ya kijusi hauna kizuizi kisharia ikiwa kuna haja inayopelekea hilo: kama kuepuka baadhi ya magonjwa ya kurithi kwa wanaume au wanawake, au watoto wengi wa mtu wanakuwa wa aina moja, akapenda kuwa na mtoto wa aina nyingine, kwa sharti jambo hilo lifanyike kwa sura ya mtu mmoja mmoja na si wito wa jumla, na lifanyike chini ya usimamizi wa wamu, bila kutokea madhara kwa mtoto katika siku zake zijazo na mustakabali wake, na wala ndani yake hamna kupingana na matakwa ya Mwenyezi Mungu na utashi Wake; kwani ni sababu miongoni mwa sababu ambazo ni sehemu ya uumbaji Wake na matakwa Yake, kama ambavyo zenyewe hazijitegemei katika kuleta athari, bali zinahitajika kwa amri ya Mwenyezi Mungu .
[1] Imepokelewa kutoka kwa Ibn Majah katika «Sunan» yake.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
