Hukumu ya biashara kwa Kulipa kidog...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya biashara kwa Kulipa kidogo kidogo)

Question

Ni nini hukumu ya Biashara kwa Kulipa kidogo kidogo)?

Answer

Biashara kwa malipo ya kidogo kidogo inajuzu kisharia, na hilo limethibitishwa na ujumla wa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara} [Al-Baqarah: 275], pia, imethibitishwa na kitendo cha Mtume (S.A.W.). Ongezeko la bei kama badala ya muda maalumu wa malipo linajuzu kisheria; kwani hilo ni miongoni mwa aina za biashara ya faida (Al-Murabaha). Biashara hii inashartiwa kubainishwa kwa bei na muda wa malipo wakati wa kufanya mkataba.

Maelezo

Mwenyezi Mungu Mtukufu Amehalalisha biashara na Akaharamisha riba; Yeye Amesema katika Qur’an: {Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na akaharamisha riba} [Al-Baqarah: 275]. Ujumla uliokuja katika Aya hii unaashiria kuruhusiwa kwa aina za biashara kwa ujumla wake, ikiwa zitafanyika kwa ridhaa ya pande mbili zinazofanya biashara.

Ni jambo lililothibiti kisharia kuwa biashara inasihi kwa malipo ya hapo kwa hapo (fedha taslimu)[1] na kwa malipo ya baadaye[2] hadi muda maalumu unaojulikana. Dalili ya hilo ni Hadithi ya Mama wa Waumini, Bibi Aisha (R.A.): “Kwamba Mtume (S.A.W.) alinunua chakula kutoka kwa Myahudi kwa malipo ya baadaye, na akaweka rehani ngao yake ya chuma”. Katika tamko lingine: “Alinunua chakula kwa mkopo (Nasi'ah)[3]” [Imepokelewa na Al-Bukhari].

Katika Hadithi hii kuna ushahidi wa kujuzu kwa kuuza kwa malipo ya baadaye, yaani: kucheleweshwa kwa malipo; kwani rehani inahitajika tu pale ambapo malipo yanakuwa ya baadaye, au pale ambapo malipo ya hapo hapo hayawezekani kwa kawaida, na hii ndio biashara kwa malipo ya kidogo kidogo.

Biashara hii -yaani kuuza kwa malipo kidogo kidogo -ina masharti mawili:

Kwanza: Kuweka wazi bei wakati wa kufanya mkataba; kama vile kusema: “Bidhaa hii kwa malipo ya sasa hivi ni pauni elfu moja, na kwa malipo ya kidogo kidogo  ni pauni elfu moja na mia mbili”

Pili: Kuweka wazi muda wa malipo wakati wa mkataba pia; kama vile kusema: “Ukimaliza kulipa ndani ya mwaka mmoja basi bidhaa ni pauni elfu moja na mia moja, na ukimaliza kulipa ndani ya miaka miwili basi ni pauni elfu moja na mia mbili” Ni juu ya mnunuzi kuchagua (aina moja ya malipo) wakati wa kununua. Ikiwa biashara itakamilika kwa makubaliano ya kuchelewesha malipo, basi huo unakuwa ni uuzaji wa Malipo kidogo kidogo (Bay'u Al-Nasi'ah), na juu ya hili kuna makubaliano (Ijmaa) kati ya Wanazuoni[4].

Na dalili ya hilo ni Hadithi ya Ibn Abbas (R.A.); amesema: “Mtume (S.A.W) alifika Madina na watu walikuwa wakifanya biashara ya malipo ya awali (As-Salam) katika tende kwa muda wa mwaka mmoja, miwili na mitatu. Akasema: "Mwenye kulipia mapema kitu (katika biashara), basi afanye hivyo kwa kipimo kinachojulikana na uzito unaojulikana hadi muda maalumu unaojulikana”[5].

Swali linalojitokeza hapa ni: Je, nini hukumu ya kuongeza bei kama badala ya kuchelewesha malipo (muda)?

Katika kujibu swali hilo tunasema: Hakika ongezeko la bei kama kwa sababu ya muda maalumu linajuzu kisheaia kulingana na msimamo wa Wanazuoni wengi (Al-Jumhur)[6]. Hii ni kwa sababu ongezeko hili ni miongoni mwa aina za Al-Murabaha[7] (biashara ya faida), nayo ni aina kati ya aina za biashara zinazojuzu kisharia ambazo inaruhusiwa ndani yake kuweka sharti la kuongeza bei kwa ajili ya muda; kwani muda, ingawa si mali halisi, lakini katika mlango wa (Murabaha) bei huongezwa kwa ajili yake.

Wala isisemwe kuwa jambo hilo ni miongoni mwa riba; kwa sababu hii ni biashara iliyofanyika kwa tamko la kuuza na kununua, na vimepatikana ndani yake thamani (bei) na bidhaa (Mubee’), na hizi ndizo nguzo za biashara. Kikubwa kilichopo hapa ni kucheleweshwa tu kwa malipo bidhaa hadi muda fulani au vipindi fulani, hivyo inaingia chini ya ujumla wa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara} [Al-Baqarah: 275]. Vilevile, imethibiti kifiqhi kuwa: “Bidhaa ikiwa ndiyo kiunganishi (kati ya muuzaji na mnunuzi), basi hakuna riba”.

Tunapata faidia kutokana na yaliyotangulia:

Hakika biashara kwa malipo kidogo kidogo inajuzu kisharia, na dalili ya jambo hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara}, na kadhalika imethibitishwa na kitendo cha Mtume (S.A.W.). Ongezeko la bei kama badala ya muda maalumu wa malipo linajuzu kisheria; kwani hilo ni miongoni mwa aina za biashara ya faida (Al-Murabaha). Biashara hii inashartiwa kubainishwa kwa bei na muda wa malipo wakati wa kufanya mkataba.

 

[1] «Bei ya hapo kwa hapo»: Kulipa thamani ya bidhaa kikamilifu wakati wa kuuza na kununua.

[2] «Bei ya baadaye»: Kuchelewesha ulipaji wa bei ya bidhaa au salio lake hadi muda mwingine maalumu baada ya wakati wa kuuza na kununua.

[3] «Al-Nasi'ah»: Kuchelewesha malipo ya bidhaa hadi muda unaojulikana.

[4] Fath al-Qadir cha Ibn al-Humam (14/205), na Rawdah al-Talibin cha Al-Nawawi (1/422), na Sharh Sahih al-Bukhari cha Ibn Battal (6/208).

[5] Imepokelewa na Al-Bukhari.

[6] Bada’i al-Sana’i cha Al-Kasani (5/ 224), Al-Sharh al-Kabir cha Sheikh Al-Dardir (3/ 58), Al-Muhadhhab cha Abu Ishaq al-Shirazi (1/ 289), na Al-Mubdi’ Sharh al-Muqni’ cha Ibn Muflih (4/ 310- 311).

[7] «Biashara ya Al-Murabaha»: Inamaanisha kuuza bidhaa kwa ongezeko juu ya thamani yake ya awali (gharama ya kununulia).

Share this:

Related Fatwas