Hukumu ya Mmoja wa mwanandoa kuchunguza simu ya mwenzake
Question
Ni nini hukumu ya kisharia kuhusu Mmoja wa mwanandoa kuchunguza [1]simu ya mwenzake?
[1] «Ujasusi»; ni kutafuta na kupekua mambo yaliyofichikana na hali za siri (za watu).
Answer
Sharia tukufu (Uislamu) imekataza ujasusi na kuchunguza siri za watu, na anaefanya jambo hilo adhabu huko Akhera.
Mwanandoa mmoja kumfanyia ujasusi mwenzake kwa kusikiliza mazungumzo yake ya simu, au kupekua barua zake, mazungumzo yake ya kielektroniki (chats), na vifaa vyake vya mawasiliano ni jambo ambalo sharia tukufu inalikataa; kwani jambo hilo linakwenda kinyume na maadili pamoja na tabia njema ambazo Uislamu umezihimiza katika kuishi kati ya wanandoa kwa wema.
Kitendo hiki kinachukuliwa kuwa ni miongoni mwa njia za Shetani za kumtumbukiza mchunguzaji katika mambo ambayo anaweza kuyaelewa na kuyatafsiri vibaya, jambo ambalo mwisho wake hupelekea kubomoa familia na kuleta utengano kati ya wanandoa.
Maelezo
Miongoni mwa makusudio makuu ya ndoa katika sharia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyotakasika ni kuenea kwa mapenzi na huruma kati ya wanandoa; Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na katika ishara Zake ni kuwa amekuumbieni wake kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao, na amejalia kati yenu mapenzi na huruma. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaofikiri} [Ar-Rum: 21]. Aya hii tukufu inaonesha kuwa ni wajibu kwa maisha ya ndoa kujengeka juu ya mapenzi, huruma, kuaminiana, na kudhaniana kheri kati ya mume na mke.
Sharia tukufu imekataza ujasusi, kufuatilia siri (mambo ya ndani ya mtu), na kudhaniana vibaya[1]; Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi mliomwamini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msifanyiane ujasusi, wala msisengenyane ninyi kwa ninyi. Je, mmoja wenu anapenda kula nyama ya ndugu yake aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu} [Al-Hujurat: 12].
Na Mtume (S.A.W.) amesema: “Jiepusheni na dhana, kwani hakika dhana ni mazungumzo ya uongo kuliko yote. Wala msipeleleze, wala msifanyiane ujasusi, wala msiuziane kwa hadaa (kuzidiashiana bei), wala msihusudiane, wala msichukiane, wala msipeane migongo; na kuweni waja wa Mwenyezi Mungu ndugu” [Imepokelewa na Al-Bukhari].
Vilevile, Mtume (S.A.W.) amekataza mtu anayetoka safarini kumvizia mke wake kwa kuingia nyumbani ghafla anaporudi bila kumpa taarifa mapema; kutoka kwa Jabir (R.A.) amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amekataza mtu kuwafanyia "turuq" (kuwaingilia ghafla) watu wa nyumbani kwake usiku akitafuta khiana yao au akifuatilia makosa yao”[2]. Na "Al-Turuq", kama wanavyosema Wanazuoni ni: Kurudi usiku kutoka safarini au kwingineko kwa ghafla bila kutarajiwa.
Na maana ya neno: “akitafuta khiana yao”, ni: Kudhania khiana yao na kuchunguza siri zao ili kuona kama wamefanya khiana au la. Wanazuoni wamehusisha katazo la kuingia nyumbani usiku kwa kushtukiza na katazo la upekuzi na dhana mbaya; kwa kuzingatia kuwa kukusudia kushtukiza katika hali hii kunaashiria kuwepo kwa dhana mbaya.
Kwa hiyo, matini hizi zinaonesha uharamu wa ujasusi kwa ujumla, na uharamu huo unasisitizwa zaidi ikiwa tabia hiyo itatoka kwa mmoja wa wanandoa kwa sababu zifuatazo:
Kwa sababu inakinzana na maadili ya kijamii ambayo sharia tukufu imekusudia kuzitumia katika kusimamisha maisha ya ndoa; Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na ishi nao kwa wema} [An-Nisa: 19], na si katika wema kufanya ujasusi kwenye simu ya mwenzako, au kupekua barua zake, mazungumzo yake ya kielektroniki, na vifaa vyake vya mawasiliano.
Ndani yake kuna ukiukaji wa katazo la kisharia kuhusu kuwafanyia ujasusi Waislamu kwa ujumla, kufuatilia siri zao, na kuwadhania vibaya. Bali sharia imeharamisha hata kuangalia maandishi au barua ya Muislamu bila idhini yake; Mtume (S.A.W.) amesema: “Mwenye kuangalia katika barua/kitabu cha ndugu yake bila idhini yake, basi hakika anaangalia motoni”[3].
Tabia hii mbaya inaweza kusababisha kuvurugika kwa maisha kati ya wanandoa, na pengine ikawa ni njia ya Shetani ya kuwatenganisha na kubomoa familia. Na wala mapenzi ya mwanamke kwa mumewe au wivu wake kwake si kisingizio cha kumfanya apekue mambo yake binafsi (privacy).
Tunapata faidia kutokana na yaliyotangulia:
Sharia tukufu (Uislamu) imekataza ujasusi na kuchunguza siri za watu, na imeweka adhabu huko Akhera kwa mtendaji wa jambo hilo.
Mwanandoa mmoja kumchunguza mwenzake kwa kusikiliza mazungumzo yake ya simu, au kupekua barua zake, mazungumzo yake ya kielektroniki, na vifaa vyake vya mawasiliano ni jambo ambalo sharia tukufu inalikataa; kwani jambo hilo linakwenda kinyume na maadili pamoja na tabia njema ambazo Uislamu umezihimiza katika kuishi kati ya wanandoa kwa wema.
Kitendo cha mwanandoa mmoja kuchunguza simu ya mwenzake kinaweza kuwa ni miongoni mwa njia za Shetani za kumtumbukiza anaechunguza katika mambo ambayo anaweza kuyaelewa na kuyatafsiri vibaya, jambo ambalo mwisho wake hupelekea kubomoa familia na kuleta utengano kati ya wanandoa.
[1] «Dhana mbaya»: Maana yake ni tuhuma na kumfanyia mtu khiana (kutokuwa na imani naye).
[2] Imepokelewa na Muslim.
[3] Imepokelewa na Abu Dawud.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
