Kuua wanyama kwa rehema (Euthanasia...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuua wanyama kwa rehema (Euthanasia)

Question

Je, inajuzu Kuua wanyama kwa rehema (Euthanasia) kwa paka na mbwa wanapoumwa na hakuna tiba ya ugonjwa wao?

Answer

Kuua wanyama kwa rehema (Euthanasia) ni jambo linalofaa kisharia ikiwa kunasababisha kumwondoshea  mnyama maumivu makali yaliyodumu kwa muda mrefu. Hakuna mateso katika kumuua mnyama mgonjwa ambaye hatarajiwi kupona. Lakini huwa ni adhabu kumwacha aendelee kuumia kwa ugonjwa wake usiotarajiwa kupona. Wala jambo hilo halihesabiwi kuwa ni uharibifu wa mali; isipokuwa  kumwacha hai katika hali hiyo ndiyo hasara yenyewe ya mali, kwa kuwa mmiliki wake atalazimika kumhudumia bila faida, na kwa kuwa haifai kumwacha mpaka afe bila chakula au kinywaji.

Isipokuwa kuna sharti muhimu, nalo ni kwamba mauaji yafanywe kwa njia inayofaa isiyo na madhara wala mateso kwa mnyama; kwa mujibu wa hadithi ya Mtume (S.A.W) «Hakika Mwenyezi Mungu ameandika wema juu ya kila kitu; basi mnapoua, ueni kwa wema; na mnapochinja, chinjeni kwa wema. Na mmoja wenu akinoe kisu chake na ampumzishe mnyama wake.»

Maelezo

Uislamu ni dini ya huruma, na huruma hii inajumuisha kila alichokiumba Mwenyezi Mungu Mtukufu, iwe ni Muislamu au asiye Muislamu, na pia inajumuisha ndege na wanyama kama paka, mbwa na wengineo. Mwenye kumiliki mnyama, awe paka au mbwa, ni lazima awe na huruma naye; kama vile kumletea chakula kinachomfaa, kumpa maji, kumtibu anapougua, na asimpige wala kumdhuru kwa aina yoyote ile.

Huruma kwa mnyama na kuwafanyia upole ni mlango wa kuingia Peponi, na ukatili na kuwatesa kwa namna yoyote ni mlango wa kuingia Motoni. Imepokewa katika hadithi kutoka kwa Abu Huraira R.A kwamba Mtume (S.A.W) amesema: «Alisamehewa mwanamke kahaba aliyemkuta mbwa aliyekuwa juu ya kisima akihema; akasema: karibu kiu imuue. Basi akavua kiatu chake, akakifunga kwa mtandio wake, akamchotea maji, na kwa sababu hiyo akasamehewa[1].»

Na kutoka kwa Abdullah bin Umar R.A kwamba Mtume (S.A.W) amesema: «Mwanamke aliadhibiwa kwa sababu ya paka aliyemfunga mpaka akafa; akaingia Motoni kwa sababu yake. Hakuwa akimlisha wala akimnywesha alipomfunga, wala hakumuacha ale katika wadudu wa ardhini[2].»

Iwapo mtu akiwa anamiliki mnyama analazimika kumwonea huruma na kumfanyia wema kwa kumlisha, kumnywesha na kumtibu. Na ikiwa mnyama huyu ataugua ugonjwa ambao mmiliki wake amekata tamaa ya kupona kwake, au ugonjwa unaomsababishia maumivu makali na hatarajiwi kupona, na hakuna njia ya kumfariji na kumwondolea madhara na maumivu hayo isipokuwa kwa kumuua; wanazuoni wamekhitilafiana kuhusu kumuua kwa nia ya huruma kwa kauli mbili:

Kauli ya kwanza: Haijuzu kumuua kwa rehema (Euthanasia) kwa sababu ya ugonjwa wake hata kama ni kwa nia ya huruma; kwa kuwa kumuua ni kumtesa, na kwa kuwa mnyama ni mali na kumuua ni kuharibu mali hiyo.

Kauli ya pili: Inajuzu, bali inapendekezwa, kumuua mnyama kwa rehema (Euthanasia) anapougua na hatarajiwi kupona, na anapata maumivu makali kutokana na ugonjwa wake kwa kumwonea huruma.

Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri (Dar al-Iftaa Al Misry) imechagua kauli ya pili ya kujuzu kumuua mnyama  kwa rehema (Euthanasia) ili kuondoa maumivu yao yanayoendelea; kwa sababu kadhaa:

Hakuna adhabu katika kumuua mnyama mgonjwa kwa rehema (Euthanasia) ambaye hatarajiwi kupona; bali mateso ni kumwacha aendelee kuumia kwa ugonjwa wake usiotarajiwa kupona.

Kuua mnyama katika ugonjwa usiotarajiwa kupona hakuhesabiwi kuwa ni kuharibu mali; bali kumwacha hai katika hali hiyo ndiyo hasara yenyewe ya mali, kwa kuwa mmiliki atalazimika kumhudumia bila faida, na haijuzu kumwacha mpaka afe bila chakula au kinywaji.

Lakini pia kuna sharti muhimu la kutekeleza kauli hii ya pili, nalo ni kwamba mauaji yafanywe kwa njia inayofaa isiyo na madhara wala mateso kwa mnyama; kwa mujibu wa hadithi ya Mtume (S.A.W ): «Hakika Mwenyezi Mungu ameandika wema juu ya kila kitu; basi mnapoua, ueni vizuri; na mnapochinja, chinjeni vizuri. Na mmoja wenu akinoe kisu chake na ampumzishe mnyama wake[3].»

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

 Ni kuwa inafaa kuua kwa rehema (Euthanasia) mnyama anapougua ugonjwa unaomsababishia maumivu makali na hakuna matumaini ya kupona, wala hakuna njia nyingine ya kumfariji na kumwondolea maumivu hayo kwa kumuonea huruma; lakini kwa sharti kwamba jambo hilo lifanywe kwa njia inayofaa isiyo na madhara wala mateso kwake.

 

[1] Amepoke Imam Bukhari.

[2] Bukharin a Muslim.

[3] Amepokea Imam Muslim.

Share this:

Related Fatwas