Kumtazama mwanamke wa kando (asiye...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kumtazama mwanamke wa kando (asiye maharimu)

Question

Ni ipi hukumu ya kumtazama mwanamke wa kando?

Answer

Hijabu ni faradhi kwa mwanamke Muislamu anapofikia umri wa kuwajibika kisharia; hivyo hairuhusiwi kuonekana kwake isipokuwa uso na viganja vya mikono.

Namwanaume kumtazama mwanamke wa kando (asiye mahramu) kwa matamanio ni jambo lililoharamishwa kisharia na linakwenda kinyume na amri ya Sheria ya kuinamisha macho. Ama ikiwa ni bila ya matamanio kwa ajili ya miamala katika nyanja mbalimbali za maisha kama kuuza na kununua, elimu na mengineyo, basi hilo linajuzu kisharia wala halina ubaya.

Ama kumtazama sehemu za siri za mwanamke wa kando, hilo halijuzu kisharia isipokuwa kwa dharura au haja ya kitabibu na mfano wa hayo.

Maelezo

Katika mambo yaliyothibiti kisharia kwa makubaliano ya Wanazuoni wa Kiislamu kwamba hijabu[1] ya mwanamke Muislamu ni faradhi kwa kila anayefikia umri wa kuwajibikiwa, nao ni umri ambao mwanamke huanza kuona damu ya hedhi. Wakati huo anawajibika kuusitiri mwili wake isipokuwa uso na viganja vya mikono. Mwenyezi Mungu anasema: “… wala wasionyeshe mapambo yao isipokuwa yaliyo wazi; na wajisitiri vifua vyao kwa shungi zao …” [An-Nur: 31]. Aya hii imewakataza waumini wanawake kuonyesha mapambo yao, isipokuwa mapambo yaliyo wazi ambayo inajuzu kwa mwanamke kuyaonyesha, nayo ni uso na viganja vya mikono; na hii ndiyo kauli ya wanazuoni wengi[2].

Imepokewa kutoka kwa Aisha R.A kwamba: “Asma bint Abi Bakr R.A  aliingia kwa Mtume (S.A.W)  akiwa amevaa nguo nyepesi; Mtume akamgeukia pembeni na akasema: ‘Ewe Asma, mwanamke anapofikia hedhi hafai kuonekana kwake isipokuwa hiki na hiki,’ akaashiria uso wake na viganja vyake.”[3].

Na Wanazuoni wengi wanaona kwamba niqabu[4] ambayo mwanamke hufunika uso wake si wajibu. Ama hadithi ya Aisha R.A aliyosema: “Wapandafarasi walikuwa wakitupita sisi hali ya kuwa tuko pamoja na Mtume (S.A.W) tukiwa katika ihramu; walipokuwa wakitukaribia, mmoja wetu alishusha jilbabu yake kutoka kichwani hadi usoni; na walipopita tuliifunua.”[5] Usahihi ni kuwa hakuna dalili ndani yake inayothibitisha wajibu wa kufunika uso wa mwanamke kwa sababu zifuatazo:

Kwanza: Imefahamika kwamba kitendo cha Maswahaba peke yake hakioneshi ulazima wa jambo walilolifanya; huenda kikawa ni kwa njia ya kupendekezwa tu.

Pili: Inawezekana hukumu hiyo ilikuwa ni ya kipekee (mahsusi) kwa Mama wa Waumini, kama walivyohusishwa na uharamu wa kuolewa baada ya Mtume (S.A.W) .

Tatu: Imepokewa kutoka kwa Ibn Umar R.A kwamba Mtume (S.A.W) amesema: “… wala mwanamke aliye katika ihramu asivae niqabu wala soksi za mikono (glavu.)” Hii inaonesha kwamba uso na viganja vya mwanamke si sehemu za uchi, kwani Sheria hairuhusu kufunua uchi katika swala wala katika ihramu.

Ama kuhusu mwanaume kumtazama mwanamke wa kando, hukumu yake ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Iwapo mwanaume atamtazama mwanamke wa kando kwa matamanio, basi hilo ni jambo lililoharamishwa kisharia; kwa kuwa humuingiza katika fitna, na ni kinyume na alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu kuinamisha macho. Mwenyezi Mungu anasema: “Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao; hayo ni usafi zaidi kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyafanya.” [An-Nur: 30].

Pili: Ikiwa kumtazama ni bila matamanio na hapatatokezea fitna, basi huko kunajuzu kisharia wala hakuna ubaya; kwani mwanaume humtazama mwanamke wakati wa kuuza na kununua, katika vikao vya elimu na katika nyanja mbalimbali za maisha.

Tatu: Ikiwa mwanaume atatazama sehemu za siri za mwanamke wa kando, basi jambo hilo halifai kisharia isipokuwa kwa dharura au haja ya kitabibu inayolazimisha hivyo.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Hijabu ni faradhi kwa mwanamke mwislamu anapofikia umri wa kuwajibika kisharia; hairuhusiwi kuonekana kwake isipokuwa uso na viganja vya mikono.

Mwanamme kumtazama mwanamke wa kando kwa matamanio ni jambo lililoharamishwa kisharia na ni kinyume na amri ya kuinamisha macho.

Mwanamme kumtazama mwanamke wa kando bila matamanio ni jambo linalojuzu kisharia wala halina ubaya.

Mwnamme kutazama sehemu za siri  za mwanamke wa kando jambo hili halifai  kisharia isipokuwa kwa dharura au haja ya kitabibu na mfano wa hayo.

 

[1] Ni vazi linalofunika mwili wa mwanamke isipokuwa uso wake na viganja vyake viwili.

[2] “Al-Hidayah ila Bulugh an-Nihayah” la Al-Qurtubi (8/5071).

[3] Abu daudi

[4] Niqab: kifuniko cha uso kwa mwanamke kinachoonyesha macho yake pekee.

[5] Ahmed katika Sunnan.

Share this:

Related Fatwas