Kuondosha wasiwasi

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuondosha wasiwasi

Question

Ni ipi namna ya Kuondosha wasiwasi (fikra zinazomsumbua mtu)?

Answer

Miongoni mwa rehema za Mwenyezi Mungu kwa waja Wake kwamba hawahesabii dhambi kwa wasiwasi unaoweza kupita vifuani mwao, na huu ni katika upana wa wepesi wa Uislamu. Matibabu ya wasiwasi ni kwa kujikinga kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya Shetani aliyelaaniwa (Audhubillahi mina shaytani rajim), na kujilinda kwa kusoma Qurani Tukufu, hasa Suratun-Nas, na kukithiri kumdhukuru Mwenyezi Mungu, kuomba dua, na kumsalia Mtume (S.A.W.)

Ama mtu anayepatwa na wasiwasi wakati akitekeleza baadhi ya ibada, ni lazima akamilishe ibada yake na asishughulishwe na wasiwasi huo.

Maelezo

Miongoni mwa rehma za Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni kwamba hawahesabii waja Wake kwa yale yanayozunguka vifuani mwao, hata kama fikra hizo ni katika mambo ambayo hayajuzu kisharia, kwa sharti ya  kutoyafanya mambo hayo, Mwenyezi Mungu Anasema: {Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyho. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo yachuma ni juu yake pia. (Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya makafiri}. [Al Baqara 286].

Kutoka kwa Abou Hurayrah (R.A.) kutoka kwa Mtume (S.A.W.) amesema: (Hakika Mwenyezi Mungu ameusamehe umma wangu kwa yale yanayopita katika nafsi zao, ilimradi hawajayafanyia kazi au kuyazungumza) Imepokelewa na Bukhari.

Hadithi hii tukufu ni ushahidi kwamba mwanadamu, kwa maumbile aliyoumbiwa na Mwenyezi Mungu, anaweza kupata mawazo na mambo mbalimbali akilini mwake ambayo hayaruhusiwi kisharia. Hata hivyo, hawezi kuyazuia au kuyaweka mbali na fikra zake, jambo ambalo humfanya apate maumivu na kuhisi hatia na dhambi kila wakati. Wakati mwingine, hali hii inaweza kufikia hatua ya hofu kubwa kutokana na mawazo hayo, mpaka inakuwa kile ambacho baadhi ya watu hukiita "Wasiwasi wa Kutenzwa nguvu"

Aina za wasiwasi wa kutenzwa nguvu na namna ya kukabiliana nazo:

Wasiwasi wakati wa kukoga au udhu: Mtu hutilia shaka usahihi wa udhu wake na kurudia kuosha viungo mara kwa mara.

Tiba yake: Inatosha kwa mtu kutia udhu mara moja tu na kuamini kuwa ni sahihi, bila kugeukia wasiwasi huo tena, kwani sharia imetupunguzia uzito katika makosa na kusahau. Kutoka kwa Abu Dharr Al-Ghifari (R.A), amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W). Amesema: "Hakika Mwenyezi Mungu ameusamehe umma wangu makosa (yaliyofanywa bila kukusudia), kusahau, na kile walicholazimishwa (kwa nguvu)." Imepokelewa na Ibn Majah

Wasiwasi wakati wa Swala: Humfanya mtu anaeswali akose unyenyekevu au asahau idadi ya rakaa alizoswali.

Tiba yake: kujikinga kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya Shetani aliyelaaniwa (Audhubillahi mina shaytani rajim. Ikiwa amesahau idadi ya rakaa, ajengee juu ya idadi ndogo ya rakaa anazozikumbuka na asujudu sijdatus-sahwi mwishoni mwa Swala;

Imepokewa Kutoka kwa Abu Hurayrah (R.A). amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: "Adhana ya Swala inapotolewa, Shetani hukimbia huku akitoa ushuzi ili asiisikie ile adhana. Adhana inapomalizika, hurejea. Iqama inapotolewa, hukimbia tena, na inapomalizika, hurejea mpaka anaingia kati ya mtu na nafsi yake, akimwambia: 'Kumbuka hili na lile,' mambo ambayo hakuwa akiyakumbuka, mpaka mtu anabaki hajui ameswali rakaa ngapi. Basi mmoja wenu asipojua kama ameswali rakaa tatu au nne, na asujudu sijda mbili akiwa akiwa amekaa." Imepokelewa na Al-Bukhari.

Kutoka kwa Uthman bin Abi Al-Aas (R.A). amesema: "Alimwendea Mtume (S.A.W). na kumwambia: 'Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika Shetani ameingia kati yangu na Swala yangu pamoja na usomaji wangu, akinitia shaka na kunivurugia.' Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) akasema: 'Huyo ni shetani anayeitwa Khanzab. Ukimhisi, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu kutokana naye (Sema: A'udhu billahi minash-shaytanir-rajim), na uteme (puliza hewa) upande wako wa kushoto mara tatu.' (Uthman) akasema: 'Nikafanya hivyo, na Mwenyezi Mungu akaniondolea hali hiyo” Imepokelewa na Muslim.

Wasiwasi wa kutoka upepo (ushuzi) wakati wa Swala: kwa namna kunamfanya anayeswali kuwa na shaka ya kutoka hewa akakata Swala yake.

Tiba yake: Kunapasa kwa mtu kutokata Swala yake mradi tu hajasikia sauti ya upepo huo au harufu yake. Kutoka kwa Abdullah bin Zaid (R.A.) amesema: "Alilalamika kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W). kuhusu mtu ambaye anadhani kuwa amepatwa na kitu (uchafu/hadathi) akiwa ndani ya Sala. Mtume (S.A.W). akasema: 'Asiondoke - au asikatize Swala yake - mpaka asikie sauti au anuse harufu" Imepokelewa na Bukhari.

Hadithi hii inaashiria kuwa twahara ni yakini (uhakika) na haiondoki kwa shaka. Huu ni miongoni mwa wepesi wa Sharia ya Kiislamu, kwani haifai kwa mtu kusalimu amri kwa wasiwasi huo ambao unamfanya aishi katika hali ya mkanganyiko na kuchanganyikiwa katika mambo yake yote.

Wasiwasi unaomjia mtu kumfanya awe na shaka katika itikadi yake na imani yake kwa Mwenyezi Mungu:

Matibabu yake: Ni kwa kumuomba ulinzi Mwenyezi Mungu (A’udhu billahi mina shaytani rajeem) na kuacha kabisa kufikiria wasiwasi huo. Ni lazima mtu ajue kwamba wasiwasi huo haumjii isipokuwa muumini aliyekamilika imani yake; kwani Shetani anataka kumpoteza kwa mawazo hayo anayoyatia moyoni mwake; Kutoka kwa Abu Hurayrah (R.A). Mtume (S.A.W.) amesema: "Shetani humjia mmoja wenu na kusema: Nani aliyeumba hiki? Nani aliyeumba kile? Mpaka hufikia kusema: Nani aliyemuumba Mola wako? Akifikia hapo, basi na amuombe ulinzi Mwenyezi Mungu na aache (asijishughulishe na wazo hilo)." (Imepokelewa na Bukhari).

Imepokewa pia kutoka kwa Abu Hurayrah (R.A).: "Walikuja watu miongoni mwa Masahaba wa Mtume (S.A.W). wakamuuliza: Hakika tunapata ndani ya nafsi zetu mambo ambayo mmoja wetu anaona ni jambo zito sana hata kulitamka. Mtume akasema: Je, mmeliona hilo (mnalihisi)? Wakasema: Ndiyo. Akasema: Hiyo ndiyo imani ya kweli." (Imepokelewa na Muslim).

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

 Katika rehema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwamba hawahesabii (hawaandikii madhambi) kwa wasiwasi unaopita akilini mwao, na huu ni wepesi wa dini ya Kiislamu.

Matibabu ya wasiwasi ni kumuomba ulinzi Mwenyezi Mungu dhidi ya Shetani, kujikinga kwa kusoma Qurani Tukufu (hususan Suratul-Nas), kukithirisha Dhikri, Dua, na kumsalia Mtume (S.A.W).

Kuendelea na Ibada: Mtu anayepata wasiwasi wakati wa kutekeleza ibada fulani, ni lazima akamilishe ibada yake na asijishughulishe na wasiwasi huo.

Share this:

Related Fatwas