Muislamu kudumu na udhu wake kwa muda wote
Question
Ni ipi hukumu ya kuhifadhi / kudumu na udhu ili Muislamu aendelee kuwa na udhu muda wote?
Answer
Mtu timamu aliyekalifishwa na Sharia kubaki katika hali ya udhu kila wakati ni jambo linalopendeza kisharia. Inapendekezwa kutawadha mara kwa mara na kuudumisha, na kutawadha upya. Hili lina kheri nyingi na humzidishia Muislamu nuru juu ya nuru, ilimradi lisimletee taabu.
Maelezo:
Usafi ni miongoni mwa Sunna za maumbile (fitra). Mwanadamu kwa asili yake hupenda usafi na mambo yanayohusiana nayo na huchukia uchafu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: ((Mambo matano ni katika maumbile (fitra): Usafi, kunyoa nywele maeneo ya siri, kuvyoa nywele za kwapani, kukata kucha, na kupunguza masharubu)).
Hadithi imepokewa na Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Abu Huraira (R.A). Na anayeangalia mambo haya atagundua kwamba yote yanatekeleza usafi na utakaso.
Na kwa kuwa Uislamu ni dini ya maumbile (fitra), imesisitiza juu ya usafi na kudumisha nao, na umeweka wazi kwamba usafi una fadhila kubwa. Hivyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametueleza kwamba Anawapenda wanaojisafisha. Amesema: { Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu na huwapenda wanao jisafisha.} [Al-Baqara: 222].
Kutokana na hayo, Sharia ya Kiislamu imependekeza Muislamu adumishe udhu wake kadri anavyoweza. Imepokelewa kutoka kwa Abdullah bin Amr (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: (Hakuna anayehifadhi udhu ila ni muumini). Hadithi imesimuliwa na Ibn Majah katika Sunan na Imamu Ahmad katika Musnad kutoka kwa Thawban (RA).
Kudumu na udhu ni kwamba mtu aliye timamu atatawadha kila mara unapotoka udhu wake, kama alivyokuwa akifanya Sayyiduna Bilal (R.A). Imepokelewa na Ibn Abi Shaybah katika Musannaf kwamba Mtume (S.A.W) amesema: (Nilisikia sauti ya nyayo mbele yangu Peponi, nikauliza: Nani huyo? Wakasema: Ni Bilal. Akamwambia (Bilal): kwa kitu gani umenitangulia peponi, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sikutokwa na udhu ila isipokuwa nilitawadha tena).
Kudumu na udhu pia ni pamoja na kutawadha mara nyingi hata kama mtu yupo katika hali ya udhu, kwani udhu ni ibada inayojitegemea, kama walivyobainisha Wanazuoni wa fiqhi.
Riwaya ya Al-Bayhaqi katika Shu‘ab Al-Īmān kutoka kwa Anas (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) alisema: Mjumbe wa Mwenyezi Mungu aliniambia: (Ewe mwanangu, ukipata uwezo wa kuwa daima katika udhu, basi fanya hivyo).
"Na maelezo haya kama yanavyoonesha kupendeza mtu kubaki akiwa na udhu wakati wote, pia yanaonesha – kwa ujumla – kupendeleza mtu kuhuisha (kufanya upya) udhu wake hata kama bado ana udhu, na hilo lina maelezo ya kina katika Madhehebu mbalimbali.
Na dalili juu ya hili zimetajwa kwa wingi, miongoni mwazo ni kauli ya Mtume (S.A.W): (Mwenye kutawadha akiwa bado ana udhu, Mwenyezi Mungu humwandikia thawabu kumi) – imepokewa na al-Qasim bin Sallam katika kitabu chake “At-Tahur (Usafi)”.
Na pia miongoni mwa hizo: Hadithi Iliyopokewa na Imamu Ahmad katika ‘Musnad’ yake, kutoka kwa An-Nazzal bin Sabrah (R.A) amesema: “Aliletwa Ali (R.A) na mtungi wa maji akiwa katika sehemu ya wazi, akachota kiganja cha maji, akasukutua, akapandisha maji puani, akapaka uso wake, mikono yake miwili, na kichwa chake; kisha akanywa maji akiwa amesimama. Kisha akasema: Huu ni udhu wa mtu ambaye hajapatwa na Hadathi (yaani hajavunjika udhu), na ndivyo nilivyomuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akifanya.”
Nayo ni ibada hii iliyokuwa miongoni mwa tabia za wema waliotangulia (Salafu Salihina), kwani Al-Qasim bin Sallam alipokea kutoka kwa ‘Abdullah bin Abi Al-Hudhail alisema: {Walikuwa wakipendelea kuukaribisha usiku wakiwa na udhu, kama walivyopendelea kuupokea mchana wakiwa na udhu.”
Mwanadamu kubaki na udhu muda wote kuna faida nyingi sana na fadhila zaidi zikiwemo:
Ikiwemo: Kumlinda mtu na shari ya shetani na hasira. Mtume (S.A.W) amesema: (Hakika hasira zinatokana na shetani, na shetani ameumbwa kwa moto, na moto unazimwa kwa maji. Basi mmoja wenu akikasirika na atie udhu). Amepokea Imamu Ahmad na Abu Dawud. Na kinachokusudiwa kwa udhu wa Sunna wakati wa hasira ni: Udhu kamili kama ule wa Swala, hata kama mtu tayari ana udhu.
Ikiwemo: Sababu ya kuongeza umri na kupendwa na Malaika. Amepokea Imamu Ṭabarani: katika “Al muujam Al-Awswat” na Al-Muujam Asagher” kuwa Mtume (S.A.W) aliwambia bwana wetu Anas (Ewe mwanangu! Fanya udhu kwa ukamilifu, utaongezewa umri wako na Malaika wako watakupenda).
Ikiwemo: Kufutwa kwa madhambi. Mtume (S.A.W) amesema: (pindi Muislamu anapotia udhu, dhambi za masikio yake, macho yake, mikono yake na miguu yake huondoka). Na amesema (S.A.W) (Mwenye kufanya udhu kwa ukamilifu, makosa yake hutoka mwilini mwake hata mpaka kilicho chini ya kucha zake)). Amepokea Muslim:
Ikiwemo: Kubakia na udhu ni sababu ya kukubaliwa kwa dua. Imepokewa na Imamu Ahmad katika ”Musnad” yake, kuwa Mtume (S.A.W) amesema” (hakuna mtu yeyote alalaye na udhu, kisha akamka usiku na kumtaja Mwenyezi Mungu na akaomba mema ya dunia na Akhera – isipokuwa Mwenyezi Mungu humpa). Hadithi ya Al-Barā’ bin ‘Āzib (Bukhari na Muslim): kwamba Mtume (S.A.W) amesema. {Unapolala, tia udhu kama ule wa Swala, kisha jilaze ubavuni upande wa kulia, halafu sema: Ee Mwenyezi Mungu, ninaukabidhi uso wangu Kwako, na nimekabidhi (mambo) yangu Kwako, na nimeuegemeza mgongo wangu Kwako kwa kutarajia na kukuogopa. Hakuna pa kukimbilia wala pa kuokoka isipokuwa Kwako. Nimeamini Kitabu Chako ulichokiteremsha, na Mtume Wako uliyemtuma.' Na yafanye maneno haya yawe ya mwisho utakayosema. Basi ukifa usiku huo, utakufa juu ya fitra. Nikayarudia maneno hayo ili niyakariri, kisha nikasema: "Nimeamini Mtume Wako uliyemtuma." Mtume (S.A.W) akasema: "Sema: Nimeamini Nabii Wako uliyemtuma.").
Ikiwemo: Kwamba udhu unawafanya wale wanaouhifadhi na kuuzidisha kuwa na haki zaidi ya kupata maombezi (shafaa) ya Mtume (S.A.W) na kuwa ni alama atakayotutambua kwayo Mtume (S.A.W) Siku ya Kiyama; kama alivyopokea Ibn Mas‘ud (RA) aliposema: Iliulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, utawatambuaje wale ambao hujawahi kuwaona katika umma wako Siku ya Kiyama? Akasema: (Watakuwa na nyuso zenye kung'aa na miguu na mikono yenye kung'aa kutokana na athari za udhu) Ameipokea Ibn Majah na Ahmad.
Na miongoni mwa faida za kuzidisha udhu(Kutawadha mara kwa mara): Malaika wanamwombea msamaha na kumwombea dua aliye na udhu hata akiwa amelala, katika Hadithi: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: (Mwenye kulala akiwa katika hali ya twahara, hulala pamoja naye Malaika katika nguo yake, na haamki ila Malaika husema: Ee Mwenyezi Mungu msamehe mja wako fulani, kwa hakika amelala katika hali ya twahara)) Ameipokea Ibn Hibban katika “Sahihi” yake na Al-Bayhaqi katika “Shu‘ab Al-Iman”.
Na miongoni mwa fadhila: Kwamba kubaki Muislamu akiwa na udhu kunamfanya awe tayari kukutana na Mwenyezi Mungu iwapo kifo kitamjia ghafla, na huenda akapata daraja ya shahada, kama alivyopokea At-Tabarani katika “Al-Mu‘jam Al-Awsat” na “As-Saghir”: kwamba Mtume (S.A.W) alisema kumwambia Anas (RA): (Ewe mwanangu, ukiweza usilale ila ukiwa na udhu, basi fanya hivyo, kwa hakika mwenye kumjia mauti naye yuko katika hali ya udhu hupewa shahada).
Hivyo basi, mtu kubaki akiwa na udhu muda wote au kurudia udhu juu ya udhu ni miongoni mwa Sunna Tukufu za Mtume (S.A.W) zilizothibiti kwa kauli na vitendo vya Mtume (S.A.W) na Maswahaba zake (R.A).
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Kwamba inasisitizwa kwa Muislamu kuzidisha udhu na kuudumisha, na kuurudia mara kwa mara; kwa kuwa ndani yake kuna kheri nyingi, na Muislamu huongezewa nuru juu ya nuru, mradi jambo hili lisimletee taabu, na ikiwa litamletea taabu basi halipendekezwi.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
