Udhu kwa anayefanya kazi ya rangi na gundi.
Question
Nafanya kazi ya kutengeneza rangi na gundi na vitu vingine vya upakaji wa rangi katika moja ya viwanda, na hivyo vitu huniganda mikononi wakati wa kazi, na huwia vigumu kuondoa kabisa kila wakati wa Swala. Je, udhu wangu unakubalika nikiwa na vitu hivi? Ikijulikana kwamba mara nyingi hufanya tabaka juu ya ngozi.
Answer
Udhu unakubalika ikiwa kuna baadhi ya vitu vilivyoshikamana /vilivyogandia ngozi ya viungo vya twahara kwa wale wanaofanya kazi viwandani na kazi ambazo ni vigumu kujiepusha navyo, na hawalazimiki kujisumbua kuondoa vitu ambavyo ni vigumu kuondoa kila wakati wa Swala.
Maelezo
Sharia Tukufu imehimiza kufanya kazi na kutekeleza kwa ustadi, na imewapa heshima kubwa wamiliki wa kazi, ikafanya mwenye kufanya kazi inayomletea riziki yake na kutosheleza haja zake kuwa bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko yule anayejiweka katika kushughulika na ibada za Sunna huku akiacha wengine wafanye kazi ili wamlishe na wamlee. Mwenyezi Mungu amesema: {Na sema: Fanyeni kazi, basi Mwenyezi Mungu ataona kazi yenu, na Mtume wake na Waumini} [Tawba: 105].
Na kutoka kwa Abu Hurayrah (R.A) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: (Kuchukua mmoja wenu kuni mgongoni mwake ni bora kwake kuliko kuomba kwa mtu, akampa au akamnyima).
Na kutoka kwa Al-Miqdam (R.A) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: (Hakula yeyote chakula bora kuliko kula kwa kazi ya mikono yake, na hakika Nabii wa Mwenyezi Mungu Daud (R.A) alikuwa anakula kwa kazi ya mikono yake)). amezipokea Al-Bukhari katika «Sahihi».
Na inachukuliwa kutokana na Hadithi: Kwamba Muislamu kula kwa kazi ya mikono yake kwa juhudi yake ni bora kwake kuliko kuvunja nafsi kwa udhalili wa kuomba, na kwa kuwa ndani yake kuna kufikisha manufaa kwa mwenye kufanya kazi na kwa wengine, na kwa kusalimika na uvivu unaopelekea mambo yasiyo na maana.
Na kutoka kwa Ibrahimu At-Taymi kwamba alisema: «Masihi Isa bin Maryam (R.A) alikutana na mtu, akamwambia: Unafanya nini? Akasema: Najishughulisha na ibada. Akasema: Nani anakulisha? Akasema: Ndugu yangu. Akasema: Ndugu yako ni mwenye ibada zaidi yako».
Na kutoka kwa Muslim bin Yasaar (R.A): ((Kwamba kundi la Al-Ash’ariyina walikuwa safarini, waliporudi wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hatukuona yeyote baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) bora kuliko fulani; anafunga mchana, na tunaposhuka anakaa akiswali mpaka tunaposafiri. Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akasema: Ni nani anayemhudumia, au kumtosheleza, au kumfanyia kazi? Wakasema: Sisi. Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akasema: Ninyi ndio wenye kuabudu zaidi kuliko yeye)). Hadithi hizi zimetolewa na Ad-Dinawari katika «Al-Mujalasa wa Jawahir Al-‘Ilm».
Na miongoni mwa kutukuza kwa Sharia Tukufu thamani ya kazi katika maisha ya watu na jamii ni kwamba imeifanya kuwa miongoni mwa sababu zinazojuzu kwa ajili yake kupunguziwa au kurahisishiwa katika utekelezaji wa baadhi ya ibada, ikiwa itatokea mgongano kati ya mtu kufanya kazi yake ambayo hana budi kuifanya ili kupata riziki yake, na utekelezaji wa ibada kwa namna yake ya asili ilivyoamrishwa, kwa namna ambayo kumkalifisha nayo kwa njia hiyo kunamletea mashaka makubwa, au kumlazimu kuacha kazi yake na huenda kukampelekea kukosa riziki yake na ya wale anaowahudumia katika familia yake, basi inajuzu wakati huo kwake kuitekeleza kwa namna inayomuondolea uzito na mashaka, na kumwezesha pamoja na hivyo kuendelea kufanya kazi yake na kupata riziki yake; kwa kutekeleza kauli ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: {Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake} [Al-Baqara: 286], na kauli yake Mtukufu: {Wala hakuweka juu yenu katika dini uzito} [Al-Hajj: 78]. Na alivyopokea Abu Hurayrah (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) amesema: (Nikikuamrisheni jambo basi fanyeni kadiri ya uwezo wenu)) Wamepokea (Al-Bukhari na Muslim), ambapo dalili hizi kwa ujumla wake zimebainisha kwamba «Mashaka huleta wepesi», na kwamba «Kilichowezekana hakidondoki kwa kisichowezekana», na kwamba «Udhuru unaathiri kwa kupunguza katika ibada».
Na masharti ya Wanazuoni ili kusihi udhu ni kufikika maji katika ngozi yote ya viungo vyote vya udhu, na hili ndilo asili linalomlazimu mwenye kutawadha iwapo hana udhuru unaomzuia kufanya hivyo[1].
Ama iwapo kuna udhuru kwa kinyume cha hilo: kama mtu akifanya kazi ambayo haiwezekani kwake kujiepusha na kinachogusa ngozi yake miongoni mwa vifaa vinavyotumika humo ambavyo vinakuwa kizuizi cha kufika maji kwenye sehemu vilipogusa katika ngozi, kama vile vifaa vya rangi na gundi na mfano wa hayo, kiasi cha kuwa ni vigumu kwake kuondoa kinachoganda mwilini mwake katika kila udhu, ama kwa sababu ya ufinyu wa muda huku kazi ikiwa lazima, au kwa ugumu wa kuviondosha, basi husamehewa kiwango hicho ambacho maji hayakufika, na kufikishwa maji juu ya kizuizi hicho huchukua nafasi ya kufikishwa juu ya vilivyomo nyuma yake katika viungo vya udhu, kwa sababu ya kuthibitika udhuru na ulazima wa kwamba haja ya mtu kwa kazi yake ni miongoni mwa mambo asiyoweza kuyaepuka, na kwamba haiwezekani kwake kujiepusha na hili, na hilo kwake ni miongoni mwa mambo yanayoenea sana kwa watu, na imekwisha bainika kuwa « "Kile ambacho balaa lake lmeenea, hukumu yake huwa nyepesi." », na kwamba «kuenea kwa balaa huondoa mashaka» na «kila kisichowezekana kuepukika, wala haiwezekani kujiepusha nacho basi huondolewa uzingativu wake».
Na maelezo ya Wanazuoni wa Madhehebu manne yameafikiana kwamba husamehewa kwa wafanya kazi kile kinachoweza kugusa viungo vya udhu miongoni mwa vizuizi vinavyozuia maji kufika kwenye ngozi wakati wa kutawadha, ambavyo ni vigumu kwao kujiepusha navyo, kama matope yanayompata mkulima anayefanya kazi ya kilimo, na wino unaompata mwandishi kwa sababu ya ulazima wa kazi yake ya uandishi, na rangi kwa anayefanya kazi ya kupaka rangi na mfano wa hayo ambacho ni kigumu kujiepusha nacho, na kigumu pia kukiondoa kwa kila udhu.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Wanazuoni wameweka sharti la kusihi kwa tohara kuwa maji yafike kwenye ngozi yote ya viungo vyote vya udhu, na hilo ni katika hali ya kutokuwa na udhuru.
Twahara inasihi ikiwa kuna baadhi ya vitu vilivyoshikamana / kugandia na ngozi ya viungo vya udhu kwa wenye majukumu na kazi ambazo ni vigumu kwao kujiepusha navyo, wala hawalazimiki kuondoa vilivyo vigumu kuondoa kwa kila sala.
[1] "Kitabu Marāqī al-Falāḥ cha al-‘Allāmah ash-Shurunbulālī Hanafiy (ukurasa wa 30, chapa ya Al-Maktaba al-‘Asriyya), na Sharḥ al-Kabīr cha al-‘Allāmah ad-Dardīr, Mālikiy (juzuu ya 1, ukurasa wa 87, chapa ya Dār al-Fikr).
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
