Kuhiji kwa Mali ya Haramu

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuhiji kwa Mali ya Haramu

Question

Nina rafiki yangu, asilimia kubwa ya mali yake ameipata kwa kazi za haramu, na nimekuwa nikimsihi na kumpa mawaidha mapaka ametubu kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, na sasa anataka kwenda Hija kwa sehemu ya mali yake hiyo, je, kunajuzu kwake kuhiji kwa Mali ya Haramu?

Answer

Kuhihiji kwa mali ya haramu, Hija ni sahihi na inaondoa ufaradhi wa Hija pamoja na kupata dhambi na kutopata thawabu za Hija, na kunatakiwa kwa Muislamu kuchunga na kuwa makini kutumia mali ya halali katika kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Maelezo

Maandiko matakatifu yamekuja yakiamrisha kula vya halali vilivvyo vizuri kwa njia ya chumo halali, Mwenyezi Mungu Anasema: (Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za Shetani. Hakika yeye ni adui yenu aliye dhahiri)[Al-Baqarah:168].

Pia Sharia tukufu imekataza kuchuma mali kwa njia ya haramu isiyo halali. Kwani njia hiyo ni katika kula mali za watu kwa dhuluma, Mwenyezi Mungu Anasema: (Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe)[An-Nsaai: 29]

Wanazuoni wote wa Madhehbu ya Imamu Hanaf, Malik na Shafi wamekubaliana kwamba mwenye kutekeleza Hija yake iliyokamilika masharti na  nguzo kwa mali ya haramu, ulazima wa Hija unaondoka kwake pamoja na kupata madhambi, wala hapati malipo ya thawabu.

Madhehebu ya Imamu Hanbali wanaeleza kuwa Hija yake haisihi na ni batili, na Fatwa iliyochaguliwa ni: Kusihi Hija kwa mali ya haramu na kuondoka ulazima wa Hija pamoja na kupata dhambi na kutopata thawabu, hii ni Hija isiyokubaliwa[1].

Ama kusihi kwa Hija na kuondoka ulazima wa hija kwa Hija hii, ni kwa mambo mawili:

Kwanza: Kwamba Hija ni matendo maalumu, na katazo la kuhiji kwa mali ya Haramu ni jambo lililo nje ya kitendo cha Hija yenyewe, haingii uharibifu na kubatilika.

Jambo la pili: Inajuzu kukutanika kwa usahihi na uasi kwa kuwa ni mambo kutoka katika nyanja tofauti; kwani Hija ni matendo ya kimwili, na mali huhitajika ili kufanikisha utekelezaji wake. Hivyo basi, mtu akifanya Hija, haidhuru kuwa alitumia njia isiyo halali kuifikia. Mfano wake ni kama mtu aliyesafiri kwa kujihatarisha au kupita njia za hatari kisha akahiji – basi Hija yake inasihi na inamtosheleza.

Ama kutokubaliwa Hija kwa kukosekana sharti lake, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu (Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam kwa kweli. Walipo toa mhanga, ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwingine haukukubaliwa. Akasema: Nitakuuwa. Akasema mwingine: Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu)[Al-Maida: 27]. Na imepokewa Hadithi kutoka wa Abu Hurayra R.A. kwamba Mtume (S.A.W.) amesema: “Enyi watu Hakika Mwenyezi Mungu Anasifika na uzuri, na hakubali isipokuwa kizuri, na hakika Mwenyezi Mungu Amewaamrisha Waumini kile alichowaamrisha Mitume, Akasema: (Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda)[Al-Mmuuminoun: 51].  Na Akasema: (Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni)[Al-Baqarah: 172], kisha akamtaja mtu anasafiri umbali mrefu akiwa na nywele zilizotimka zenye vumbi, ananyanyua mikono yake juu, Ewe Mola, Ewe Mola, na chakula chake ni cha haramu, kinywaji chake ni cha haramu, na nguo zake ni za Haramu na anakula haramu basi vipi itajibiwa dua ya mtu kama huyo?”  imetolewa na Muslim.

Kutoka kwa Abu Hurayrah R.A kwamba Mtume wa Allah (S.A.W) alisema: 

((Mtu anapotoka kwenda kuhiji kwa kutumia mali halali, akaweka mguu wake kwenye mguu wa mnyama wa kupanda, kisha akasema: Labbaika Allahumma Labbaik (Nimeitikia wito wako Ewe Mola), basi mtangazaji kutoka mbinguni humwambia: Umekaribishwa na umebarikiwa, riziki yako ni halali, mnyama wako ni halali, na Hija yako imekubaliwa isiyo na dhambi. 

Lakini akitoka kwa kutumia mali haramu, akaweka mguu wake kwenye mnyama, kisha akasema: Labbaik, mtangazaji kutoka mbinguni humwambia: Hakuna Labbaik wala baraka kwako, riziki yako ni haramu, matumizi yako ni haramu, na hija yako haijakubaliwa.)) 

Imepokewa na At-Tabarani katika “Al-Mu’jam Al-Awsat”

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kuhiji kwa mali ya Haramu, Hija inakuwa sahihi, na ulazima wa Hija unaondoka, ikiwa tu imetosheleza nguzo za Hija na masharti yake.

Kuhiji kwa mali ya Haramu haikubailiwi, na hakuna mgongano kati ya hukumu ya kusihi na kutokubaliwa; kwa sababu athari ya kukubaliwa ipo inafuatana na thawabu, na athari ya kusihi katika kuondoka uhitaji.

 

([1]) Abahr Ar-Raaiq {2/332), Nihaayat Al Muhtaj, (3/255), Al-Insaaf (6/205).

Share this:

Related Fatwas