Hukumu ya kuchinja Udh’hiya baada y...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kuchinja Udh’hiya baada ya siku za Tashriiq

Question

Baadhi ya Taasisi za kitaifa na za kiraia zinawawakilisha Waislamu kuchinja Udhiya na kusambaza nyama yake kwa watu masikini wanaostahiki, wakati mwingine idadi ya mifugo watakaochinjwa huwa kubwa sana mpaka muda wa Sikukuu ya Idi na siku tatu za Tashriiq hautoshi, ingawa kuchinja wakati wote wa muda huu, na huenda matayarisho na maandalizi ya kuchinja idadi hiyo ya mifugo yahitaji kuongeza muda zaidi ya siku hizo kwa masilahi yanayozingatiwa; kama vile upatikanaji wa aina maalumu ya mifugo wenye manufaa kwa masikini, au huenda kuongezeka kwa muda wa kuchinja huwa kwa sababu ya nyenzo na vifaa vya shirika maalumu ambalo ni chaguo lililo bora zaidi kwa Taasisi inayosimiamia shughuli hizo, basi je hukumu ya kisharia katika hali hii? Na je, Udh’hiya wanaochinjwa baada ya kupita kwa siku ya Idi na siku tatu za Tashriiq ni halali kisharia? Na je, inawezekana kukubali kauli ya baadhi ya Wanachuoni wa Fiqhi kuwa: kuchinja kunaruhusiwa kuendelea mpaka mwisho wa mwezi wa Dhul-Hijja?

Answer

Udh’hiya ni ibada katika ibada za dini, na Sunna mojawapo Sunna za Sharia ya Kiislamu, na wakati wa kwanza wa kuchinja Udh’hiya ni siku ya kwanza ya siku za kuchinja, na kuendelea kwa wakati wa kuchinja Udh’hiya kutoka siku ya Eid A-Adha hadi mwisho wa mwezi wa Dhul-Hijja ni suala la kuhitilafiana baina ya Wanazuoni, na inaruhusiwa kuchukua kauli ya yule aliyeona kuruhusiwa kuchinja Udh’hiya hadi mwisho wa mwezi wa Dhul-Hijja, hasa kwa Taasisi zilizoaminiwa kununua na kuchinja ikiwa hazikuweza kutoshea kabisa Udh’hiya zote katika wakati wa asili, na bora kwa taasisi hizi kufikia wakati wa asili wa kuchinja ikiwa zimeweza kufanya hivyo.

Maelezo

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu yaliyo thabiti kisharia, ni haramu kuchinja mnyama wa Udh’hiya (sadaka ya Eid el-Adh’ha) kabla ya Alfajiri ya siku ya kuchinja (Yawm An-Nahr). Imamu Ibn Al-Mundhir alieleza kwamba kulikuwa na makubaliano ya Wanazuoni wote juu ya jambo hili. Wakati wa kuchinja unapatikana ndani ya mwezi wa Dhul-Hijjah, na siku ya kuchinja ndiyo mwanzo wa muda wa kuchinja. Baada ya kumalizika kwa mwezi wa Dhul-Hijjah, hakuna tena kuchinja kwa ajili ya Udh’hiya.

Wanazuoni wa Fiqhi walitofautiana kuhusu muda wa mwisho wa kuchinja. Baadhi yao walipanua muda huo, na wengine wakaubana; baadhi walisema ni siku moja tu ya kuchinja, kama alivyoeleza Ibn Sirin. Wengine, kama wafuasi wa Madhehebu ya Imamu Hanafi, Maliki na Hanbali, walisema ni siku ya kuchinja na siku mbili zinazofuata. Wafuasi wa Imamu Shafi walisema ni siku ya kuchinja na siku tatu za tashriiq, kauli ambayo pia ni maarufu miongoni mwa Wanazuoni. Wengine walipanua zaidi muda huo hadi siku sita baada ya kuchinja, kama alivyosema Qatadah, au hadi siku kumi, kama alivyonukuliwa Ibn al-Tin. Wengine, wakiwemo Wanazuoni wengi wa salaf kama Abu Umamah bin Sahl, Sulaiman bin Yasar, Abu Salamah bin Abdurrahman, na Hasan al-Basri, waliruhusu kuchinja hadi mwisho wa mwezi wa Dhul-Hijjah. Kauli hii pia imenukuliwa kutoka kwa al-Nakha’i, Umar bin Abdulaziz, na Qatadah bin Di’amah al-Sadusi, na ndio rai iliyochaguliwa na Imamu Ibn Hazm pamoja na Wanazuoni wa Madhehebu ya Dhahiriyyah.[1]

Kuchukua kauli ya Wanazuoni waliotoa ruhusa ya kuendelea kuchinja hadi mwisho wa mwezi wa Dhul-Hijjah kunaleta unafuu kwa watu, na kunazingatia maslahi ya masikini kwa kuongeza idadi ya wanyama wa Udh’hiya. Ruhusa hii imeripotiwa kutoka kwa Mtume (S.A.W.) na pia imenukuliwa kutokana na matendo ya Maswahaba (R.A.), ambayo yanaonesha kuwa Mtume (S.A.W.) aliyaona na kuyakubali.

Imamu Abu Dawud amepokea Hadithi hii katika Al-Marasil, na Ad-Daraqutni katika As-Sunan, Ibn Hazm katika Al-Muhalla bil-Athar, na Al-Bayhaqi katika As-Sunan Al-Kubra. Wote wameipokea kutoka kwa Abu Salamah bin Abdurrahman na Sulaiman bin Yasar kwamba walipata habari kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alisema: “Udhiya yaani wanachinjwa mpaka mwezi wa Al-Muharran kuonekana kwa yule aliyetaka kusubiri kwa muda huu” (Kuchinja kwa ajili ya Udh’hiya kunaruhusiwa hadi kuonekana kwa mwezi wa Muharram kwa yule anayetaka kuchelewesha kufanya hivyo). Na katika riwaya nyingine iliyotajwa na Imamu Al-Bayhaqi katika Ma’rifat As-Sunan wal-Athar amesema: “Udhiya yaani wanachinjwa mpaka mwezi wa Al-Muharran kuonekana kwa yule aliyetaka kusubiri kwa muda huu” (Sadaka za kuchinja zinaendelea kuruhusiwa hadi mwisho wa mwezi kwa yule anayetaka kuchelewesha). Neno Al-istina’ (الاستيناء) linamaanisha kusubiri kwa utulivu, kutazamia muda ufaao, na kufanya jambo kwa utulivu hadi litimie ipasavyo.

Imepokelewa kutoka kwa Yahya bin Sa‘id kwamba alisema: “Nilisikia Abu Umamah bin Sahl bin Hunayf (R.A.) akisema: “Waislamu walikuwa wananunua mnyama wa kuchinja kwa ajili ya ‘udhiya’, kisha wanamlisha hadi anenepe, halafu wanamchinja baada ya Siku ya Eid hadi mwishoni mwa mwezi wa Dhul-Hijjah.” Riwaya hii imesimuliwa na Al-Bayhaqi katika As-Sunan Al-Kubra, na pia na Abu Nu‘aym bin Al-Haddad [aliyefariki mwaka 517 H] katika Jami‘ As-Sahihayn bi-hadhf Al-Ma‘ad wa At-Turuq. Imamu Al-Bukhari pia aliitaja Hadithi hii kwa yakini katika Sahih yake (kwa namna ya ta‘liq), akizingatia tu kipengele kinachoonesha uhalali wa kunenepesha mnyama wa kuchinja, akisema: “Tulikuwa tukinenepesha wanyama wa kuchinja mjini Madina, na Waislamu walikuwa wakinenepesha (wanyama wao).”

Wanazuoni wa Fiqhi na wafasiri wote wa Sahih Al-Bukhari na vitabu vingine walikubaliana kutumia Hadithi hii kama ushahidi wa uhalali wa kunenepesha mnyama wa Udh’hiya, au kuchagua awe mnene na bora. Kwa mantiki hiyo, inakuwa sahihi pia kutumia sehemu nyingine ya Hadithi hiyo kama hoja ya kuruhusu kuchelewesha kuchinja hadi mwisho wa mwezi wa Dhul-Hijjah. Hii haipingani na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Maswahaba wengi (R.A.) kwamba muda wa kuchinja ni siku ya Nahr (Siku ya Eid) na siku mbili au tatu baada yake; kwa kuwa Hadithi hii imebeba maana ya ruhusa maalumu katika hali za dharura au haja, si kwa utaratibu wa kawaida. Ama kauli ya Maswahaba kuhusu siku tatu, hiyo ndiyo hukumu iliyo thabiti na desturi ya Waislamu katika hali za kawaida. Kuhusu kuruhusu kuchinja hadi mwisho wa Dhul-Hijjah, hilo ni rukhsa (ruhusa ya kisharia) inayolenga kuleta unafuu na wepesi kwa watu.

Jambo hili linaonekana wazi, kwa mfano, kwa mtu ambaye ana mnyama wa Udh’hiya (sadaka ya kuchinja) lakini anasubiri hadi mnyama huyo afikie umri unaokubalika kisheria; au anangoja hadi mnyama awe na nyama ya kutosha, akomaa vizuri, na awe na uzito kamili; au ikiwa mnyama huyo alikuwa akila kinyesi au taka (anayejulikana kama Al-jallālah), basi anachelewesha kuchinja ili amlishe chakula safi na halali mpaka nyama yake iwe tamu na safi. Kwa hali kama hizi, Hadithi zilizotajwa zinathibitisha uhalali wa kupata ruhusa ya kuchelewesha kuchinja pale inapokuwa na haja.

Na katika maana hii ya haja binafsi, inajumuishwa pia haja ya kijamii au ya pamoja—kama vile kuongezeka kwa idadi ya wanyama wa kuchinja, jambo linalosababisha ugumu katika kuwachinja wote kwa wakati mmoja, au changamoto za maandalizi ambazo zinahitaji muda zaidi ili kupata wanyama wazuri na nyama bora. Hata hivyo, ni wajibu kwa Waislamu kujitahidi kadiri ya uwezo wao kuhakikisha kuwa wanachinja ndani ya muda wa asili uliowekwa kisharia, na kuepuka kuchelewesha bila sababu ya msingi.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Haifai kuchinja wanyama wa Udh’hiya kabla ya kuchomoza kwa Alfajiri ya siku ya kuchinja.

Siku ya Nahr ndiyo mwanzo wa muda wa kuchinja, na hakuna kuchinja kwa ajili ya Udh’hiya baada ya kumalizika kwa mwezi wa Dhul-Hijjah.

Inajuzu kufuata kauli ya Wanazuoni wanaoruhusu kuchinja hadi mwisho wa mwezi wa Dhul-Hijjah, kwa kuwa katika hilo kuna urahisisho kwa watu na kuzingatia mahitaji ya baadhi ya taasisi zinazoshughulika na maandalizi ya wanyama wa Udh’hiya.

 

[1] «Al-Hāwī» (15/124, ch. Dar Al-Kutub Al-'Ilmiyyah), «Al-Mughnī» (11/113, ch. Dar Al-Fikr), «'Umdat Al-Qārī» (21/148), «At-Tamhīd» (23/196), na «Al-Istizkār» (15/202).

Share this:

Related Fatwas