Kumsalimia anayesoma Qur’ani

Egypt's Dar Al-Ifta

Kumsalimia anayesoma Qur’ani

Question

Ulizuka mjadala  kati ya watu Msikitini kuhusu kumsalimia mtu anayesoma Qur’ani, kwa hivyo tunaomba ufafanuzi wa hukumu ya kisharia ya Kiislamu kuhusu suala hili?

Answer

Kusalimia ni maamkizi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo aliwapa Waislamu, na akawaagiza kusalimiana, na akajaalia kuwa na athari kubwa katika kuimarisha misingi ya mshikamano na upendo katika jamii. Na inafaa kumsalimia msomaji wa Qur’ani Tukufu, na tofauti katika jambo hilo ipo baina ya karaha na kupendeza. Kwa hivyo inafaa kwa mwenye kukalifishwa na sharia kumsalimia au kutomsalimia, na hakuna dhambi kwake wala ubaya, na haijuzu kwa wengine kumkemea, kwa kuzingatia kwamba ni bora kuzingatia hali ya msomaji, iwe amejikita katika kusoma au la, pamoja na kuzingatia hisia zake, ikiwa amehuzunika kwa kutomsalimia au la.

Maelezo

Salamu ni maamkizi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo amewapa Waislamu, na akawaagiza kusalimiana, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka na mema}. [An Nuur 61]. Na kutoka kwa Abdullah bin Amr R.A., kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume (S.A.W.), “Ni kipengele gani cha Uislamu kilicho bora zaidi?” Akasema: “Kuwalisha wenye njaa na kusalimia unaowajua na usiowajua.” (Imepokelewa na Bukhary na Muslim).

Na salamu ina athari kubwa katika kuimarisha misingi ya mshikamano na upendo na kuzoeana katika jamii. Kutoka kwa Abu Hurairah R.A., amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.), amesema: “Hamtaingia Peponi hadi mtakapoamini, na hamtaamini hadi mpendane. Je, niwajulishe kitu ambacho, mkifanya hivyo, mtapendana? Salimianeni .” Imepokelewa na Imamu Muslim katika Sahihi yake.

Wanavyuoni wa Fiqhi wamekubaliana kwa kauli moja kwamba kutoa salamu ni Sunna ya Mtume (S.A.W) iliyothibitishwa, isipokuwa kwamba Wanazuoni wa Fiqhi wa Imamu Hanafi, baadhi ya Maimamu wa Imamu Malik kama vile Ibn Farhun, na kadhalika baadhi ya Maimamu wa Imamu Shafi, kama vile Al-Wahidiy na Al-Adhra’iy, na wafuasi wa Madhehebu ya Imamu Hanbali, wameeleza hali ambapo huchukizwa kwayo kutoa salamu, kwa kuzingatia hali ya mpokeaji (anayesalimiwa) na uwezo wake wa kujibu salamu ili isimsababishie kosa. Walizingatia Miongoni mwa hali hizi, kumsalimia mtu ambaye anashughulika na kusoma Qur’ani Tukufu, kwani hawezi kisharia kujibu salamu.

Wanazuoni wa Madhehebu ya Imamu Malik na Shafi, katika rai zilizopitishwa, wanaona kuwa hakuna karaha kumsalimia anayesoma Qur’ani Tukufu, na kwamba yeye ni kama mtu mwingine yeyote; kwa hivyo, kumsalimia bado kunaruhusiwa kulingana na asili yake ya awali kama kitendo kilichopendekezwa na kupendeza. [1] Kutokana na yaliyo hapo juu tunapata yafuatayo: kwamba suala hili linategemea kuweza, kwa hivyo inaruhusiwa kulifanya kwa rai yeyote kati ya hizi mbili bila tatizo lolote, na hakuna mtu mwenye haki ya kumkosoa mtu mwingine katika hili, kwa kilichopitishwa katika misingi ya Fiqhi; kwamba "Halikemewi walilotofautiana, bali hukemewa walilokubaliana."

Na Maana ya kukemewa ni kumkemea mtu, au kumkataza kufanya jambo kwa sababu ni kinyume na kile mkemeaji anachokiona na kukichagua, au kuhusisha kauli yake kwa maovu katika njia yeyote miongoni mwa njia tatu za kukemea zilizotajwa katika Hadithi - mkono, ulimi, au moyo - kwa lengo la mabadiliko.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kumsalimia mtu anayesoma Qur’ani Tukufu inaruhusiwa, na tofauti katika jambo hilo ipo baina ya karaha na kupendeza. Kwa hivyo inafaa kwa yule mwenye kukalifishwa na Sharia kumsalimia au kutomsalimia, na hakuna dhambi kwake katika hilo na hakuna ubaya, na haijuzu kwa wengine kumkemea, kwa kuzingatia kwamba ni bora kuzingatia hali ya msomaji, iwe amejikita katika kusoma au la, pamoja na kuzingatia hisia zake, ikiwa amehuzunika kwa kutomsalimia au la. Kama ilivyobainishwa hapo juu.

 

[1] - Maratib Al Ijmaa’, (uk. 156, Ch. Dar El Kutub Al Elmeah) na Al Bahr Ar Ra’iq (16/2 Ch. Dar El Kutub Al Elmeah)

Share this:

Related Fatwas