Kupangusa juu ya Piopio (hogo)

Egypt's Dar Al-Ifta

Kupangusa juu ya Piopio (hogo)

Question

Je, inajuzu kupangusa juu ya piopio (hogo)? Na ikijuzu, basi nini vidhibiti vyake?

Answer

Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W, watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
Piopio (hogo) ni miongoni mwa njia za matibabu inayotumiwa kutibu mifupa inayovunjika nk. Hogo hutumika kuunganishia mifupa ya viungo baada ya kuvunjika. Wanachuoni wanaingiza katika maana ya hogo kila kitu chenye kuganda katika kiungo cha udhu au dawa inayozuia kufika maji ngozini na inayowekwa katika jeraha (kidonda), -kama dawa ya kupaka n.k-. Hii ni kauli ya maulamaa wa madhehebu ya Hanafiy waliotaja maana ya hogo katika [Tanweer Al Absar, na Sharh yake, 1/279, Ch. Dar Al Kotoob Al Elmiya], kuwa ni: "Vijiti (kwa njia ya kizamani) vinavyotumiwa kuunganishia mifupa ya kiungo kilichovunjika kwa kuwekwa juu ya sehemu iliyovunjika ili kuidhibiti isitingishike, (na kitambaa cha kidonda, na mahali pa jeraha).
Hapo zamani, piopio (hogo) lilikuwa katika umbo la mifupa na huwekwa juu ya jeraha ili kuunganisha sehemu iliyovunjika. [Al Musbah Al Muneer, uk, 89, kidahizo cha Jabar (unganisha) Ch. Al Maktabah Al Elmiya]. Baada ya koboreshwa njia za matibabu, watu wengi sasa hawatumii piopio la umbo la mifupa ili kuunganisha kilichovunjika lakini wameamua kuita kila kitu au njia zote zinazotumika kukaza na kuunganisha mifupa iliyovunjika kwa jina la piopio. [Al Mua'jam Al Waseet, uk, 105, Ch. Dar Al Daua]
Wakati fulani, piopio (hogo) linakuwa katika kiungo kinachopaswa kuoshwa kwa ajili ya tohara kutokana na hadathi mbili ili kutekeleza ibada, hapa piopio huwa kizuizi kinachozuia kufika maji katika kiungo hiki, kwani sharti ya tohara ni kufika maji katika kiungo lakini kama piopio (hogo) litaondoshwa basi kutatokea madhara.
Hapo zamani, wanachuoni walizungumzia hukumu ya jambo hili, na waliafikiana juu ya kujuzu kupangusa juu ya piopio (hogo) kama kuna udhuru badala ya kuoga au asili ya kupangusa katika udhu, au kuoga, au kutayammamu. Dalili ya wanachuoni katika hukumu hii ni: Mtume s.a.w alimuamrisha mtu aliyewekewa piopio (hogo) kupangusa juu yake. Kutoka kwa Imamu Ali R.A amesema : Ulivunjika mkono wangu wa kulia siku ya Uhud na bendera ikaanguka kutoka mkononi mwangu, Mtume saw akasema “ iwekeni bendera katika mkono wake wa kushoto, kwani yeye ni mshika bendera yangu duniani na akhera” nikasema: ewe mjumbe wa Allah, nilifanye nini piopio (hogo) (wakati wa tohara na udhu)? Akasema: pangusa juu yake. Ameitoa Al-Bayhaqiy na Ibn Majah.
Mtume s.a.w alimuamrisha bwana wetu Ali R.A kupangusa juu ya piopio (hogo) badala ya kuosha kwa maji. Amri hii ni dalili ya kujuzu kupangusa juu ya hogo.
Mtume S.A.W. aliwalaumu vibaya waliotoa fatwa inayokwenda kinyume na maelezo ya hapo juu(kujuzu kupangusa juu ya hogo), kwani ni madhara kufanya mambo kuwa magumu katika mambo ambayo Allah s.w na Mtume wake wameyarahisisha. Jaber R.A. amepokea kwamba: " Mtu mmoja alipigwa na jiwe likamjeruhi kichwani, halafu akaota (akatokwa na manii usingizini) akawauliza marafiki zake : Je mnaniruhusu kutayammamu? Wakasema hakuna ruhusa hiyo kwani wewe unaweza kukoga kwa maji, basi akakoga na akafa kutokana na maji kumdhuru, Mtume s.a.w akasema: Wamemuua!, Mwenyezi Mungu atawaua. Hivi! Hamuulizi kama jambo hamlijui? Kwa sababu dawa ya mgonjwa ni kuuliza. Ilikuwa inamtosha kutayammamu, na aweke kitambaa juu ya jeraha halafu apanguse juu yake na anakosha kwa maji sehemu nyingine zilizobakia." Ameitoa Abu Dawuud, Al Darqatniy na Al-Bayhaqiy. Katika hadithi hii, Mtume S.A.W. anafafanua wazi uhalali na kujuzu kupangusa juu ya piopio (hogo).
Uhalali wa kupangusa juu ya hogo umethibiti kutoka kwa Ibn Omar R.A na hakuna sahaba yoyote aliyempinga. [Al Sunnan Al Kobra kwa Al-Bayhaqiy, 1/228, Ch. Dar Al Fikr, na Kashaaf Al Ginaa' 1/112, Ch. Dar Al Kotoob Al Elmiya].
Aidha Maimamu wa Taabiiyna wameunga mkono kupangusa juu ya hogo , kama vile Obaid Ibn Omair, Tawuos, Mujahid Bin Jaber, Attaa Bin Abi Rabaah, Al Hassan, Abi Majliz, Ibraheem Al Nakhaiy na Qataadah. [Sunnan Al Bihaiqiy Al Kobra, 1/229].
Dalili za kiakili nazo zinaashiria kujuzu kupangusa juu ya piopio (hogo), kwani haja inalazimisha hivyo, kwa sababu kulivua hogo kuna madhara na usumbufu, Al Merghaniy Al Hanafiy alisema katika [Al Hidaya Sharh Al Bidaya katika sababu ya kujuzu kupangusa piopio (hogo), 1/23, Ch, Dar Al Arabiy]; " Kwa sababu madhara ya kuvua hogo ni makubwa kuliko kuvua khufu, kwahivyo ni bora kupangusa juu ya hogo.".
Na wafuasi wa madhehebu ya kifiqhi wamenukulu uhalali wa kupangusa juu ya piopio (hogo) badala ya kuosha kutoka kwa wanachuoni wa Hanafiy. Katika kitabu cha Tanweer Al Absaar na Sharh yake yamekuja yafuatayo: "(Na hukumu ya kupangusa hogo) ni Vijiti (kwa njia ya kizamani) vinatumiwa kuunganisha mifupa ya kiungo kilichovunjika (na kitambaa cha kidonda, na mahali pa jeraha), basi kupangusa huku kunakuwa ni faradhi" {Al Dur Al Mukhtaar Sharh Tanweer Al Absaar 1/279-280, pamoja na Hashiyat Ibn Abdeen, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiya}.
Madhehebu ya Maalikiy yameunga mkono hayo katika kitabu [Mukhtasar Al Sheikh Khalili] na maelezo yake yalitolewa na Sheikh Al Dardeer: katika (Mlango) wa kupangusa jeraha au hogo wakati wa dharura badala ya kuosha (iwapo mtu ataogopa kuosha jeraha) (kama kutayammamu) au anaogopa kuzidi ugonjwa au kuchelewa kupona (apanguse) mara moja ambapo ndio lazima kwake kama ataogopa kujiangamiza, kuzidi ugonjwa au kupoteza hisia ya kusikia na kuona, (halafu) kama hawezi mwenyewe kupangusa basi litapanguswa hogo lake na mtu mwingine" [Al Sharh Al Kabeer, 1/162-163, Ch. Dar Ihiyaa Al Kotoob Al Arabiya].
Na madhehebu ya Shaafiy yanasema hivyo, lakini walishurutisha kuweka piopio (hogo) baada ya kutwaharisha mahali pake(sehemu iliyovunjika), Abu Ishaq Al Sheraziy alisema: "Ikiwa kiungo cha mtu kilichovunjika kinahitaji kuwekewa piopio (hogo), basi lazima kiungo kiwe tohara kabla ya kuwekwa hogo, basi likiwekwa katika kiungo kilichotwaharishwa halafu akapatwa na hadathi akahofia kulivua au ameliweka bila ya tohara na akahofia kulivua basi anapangusa juu ya hogo. Kwa sababu Mtume s.a.w alimuamrisha Ali bin Abu Talib kufanya hivyo kama khufu, [Al Muhadhab katika Al Furuo', 1/37,Ch. Issa Al Halabiy].
Pia madhehebu ya Hanbaliy yanasema hivyo, kama ilivyokuja katika kitabu [Kashf Al Qinaa', 1/112, Ch. Dar Al Kotoob Al Elmiya]: "Na inajuzu kupangusa juu ya piopio (hogo); nalo ni mbao au mfano wake, kazi yake ni kuunganisha sehemu iliyovunjika au kufunga sehemu yenye jeraha".
Ufuatao ni utaratibu wa kupangusa juu ya piopio:
Kwanza: Ni lazima kupangusa juu ya hogo wakati wa kujitoharisha, ikiwa kuosha kiungo kilichovunjika au jeraha au kukipangusa kunapelekea madhara au mtu anahofia kutokea madhara endapo atalivua hogo. Akiacha kupangusa juu ya hogo basi Sala imebatilika kwa mujibu wa kauli ya Abu Yussuf na Muhammad wanachuoni wa madhehebu ya Hanafiy, pia madhehebu ya Maalikiy, Shaafiy na Hanbali yamesema hivyo. Na kwa Madhehebu ya Abi Hanifa; mtu anayeiacha kupangusa hogo hilo anapata dhambi lakini Sala yake ni sahihi pamoja na kuwajibika kuirudia tena sala hiyo -basi wajibu ni jambo linalowafikiwa na wanavyuoni wa madhehebu ya hanafiy, pamoja na kutofautiana kwao katika maana yake- lakini ikiwa kupaka maji piopio (hogo) kuna madhara ya wazi, basi kupaka maji huko kunaondoshwa ili kuepusha madhara; kwani kuosha huwa kunaondoshwa kwa udhuru, basi kwa hiyo, kupaka maji piopio (hogo) kunaondoshwa pia kutokana na sababu hiyo hiyo. Na ikiwa katika kuosha viungo vyenye afya kuna shaka ya kupatikana madhara kwenye viungo vyenye jeraha, basi kutayammamu ni faradhi wakati huo na kupaka maji kunaondoshwa.
Pili: Wakati wa kupangusa juu ya piopio (hogo) : ni pale mtu aliyepatwa na hadathi anaosha kiungo (badala ya kuosha kwa maji unapangusa) kilichovunjika isipokuwa janaba mtu anapangusa wakati anaoutaka. Hii ni kauli ya madhehebu ya Abu Hanifa, Maalikiy, Ahmad na ni sahihi zaidi katika madhehebu ya Shaafiy. [Asny Al Amatalib kwa Sheikh Zakariya Al Ansariy, 1/82, Ch. Dar Al Kitaab Al Islamiy na Al Majmou' 2/370, Ch. Matabaat Al Manbariya].
Tatu: Haishurutishwi kukusanya uoshaji wa viungo vizima, kupangusa juu ya hogo na kutayammamu kama ilivyo katika madhehebu ya Shaafiy, bali inatosha kuosha na kupangusa tu, lakini inapendeza kukusanya uoshaji wa viungo vizima, kupangusa juu ya hogo na kutayammamu ili kuepuka hitilafu, kwani inapendeza.
Nne: Madhehebu ya Hanafiy na Maalik yanasema ili kupangusa kusihi si lazima kuweka piopio (hogo) hali ya kuwa kuna tohara ya maji. Lengo hapa ni kurahisisha na kuondosha usumbufu. Lakini Shaafiy na Hanbali kwao ni lazima. Ni vizuri kuliweka hogo katika kiungo ambacho kipo tohara ili kuepuka hitilafu.
Imamu Shaafiy katika kauli yake mashuhuri na katika riwaya yake aliyoipokea Imamu Ahmad anashurutisha piopio liwekwe katika kiungo kilisho tohara, mtu akienda kinyume kwa kuliweka hogo bila ya tohara basi ni lazima kulivua kama kulivua huko hakuna madhara, ikiwa kuna madhara hatakikani kulivua na inasihi kupangusa juu yake. [Nehayat Al Muhtaaj kwa Ramliy, 1/269, Ch. Mustafa Al Halabiy].
Tano: Kama mtu hajaweza kupangusa juu ya piopio (hogo), kwa kuwa akipangusa atapata madhara basi inapendeza atayammamu katika kiungo ambacho hajaweza kukipangusa. Hapa unachukua kauli ya walioruhusu kutayammamu katika kiungo ambacho huwezi kupangusa juu yake, nayo ni kauli ya baadhi ya wafuasi wa Imamu Shaafiy aliyoisimulia Al Rafiy kutoka kwa Al Hanattiy kwamba inatosha kutayammamu, na wala piopio halipanguswi kwa maji. Kauli hii pia ameinukulu Sahibu Al Edda, na Al Qadhi Abu Al Ttaib ameichagua. (Al Majmou', 1/326, Ch. Dar Al Fikr]. Hii ni akiba katika mambo ya ibada na kuepuka hitilafu.
Mweye haja ya kufunika kiungo kati ya viungo vya udhu au viungo vya josho (kukoga) basi analazimika kupangusa juu yake anapotaka tohara ikiwa kuondoa kitu kinachofunika kuna madhara na usumbufu, afanye hivi kwa vithibiti vilivyotajwa hapo juu, kama hawezi kupangusa basi amesameheka (hakoshi wala hapangusi), katika hali hii ni vizuri kutayammamu katika sehemu iliyofunikwa ili kuepuka hitilafu. Na akisali katika hali hii halazimiki kurejea tena Sala.
Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas