Kutumia akili katika kuthibitisha itikadi
Question
Baadhi ya watu wanawatuhumu watu wa Sunna na Jamaa (Asha’ira na Matrudiya) kwamba walipindukia mipaka ya akili katika elimu ya Tawhiyd (Elimu ya kumpwekesha M/Mungu). Je, tuhuma hii ni kweli?
Answer
Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
Maana ya akili katika lugha ni uwezo wa kufikiri na kuamua kwa busara. Kinyume chake ni upumbavu. Na tunapotumia neno “akili” tunamaanisha kuelewa na kutambua. Al-Raghib alisema katika kitabu chake “Al-Mufradat”, akili ni uwezo wa kukubali ufahamu na ujuzi. Na mtu anayefanya hivyo anaitwa akili pia kwa lugha ya kiarabu, mwenye akili kwa lugha ya kiswahili.
Maana ya akili kwa waarabu ni kinga inayomkinga mwanadamu -baada ya mafanikio na mwongozo wa Mwenyezi Mungu- kutokana na upuuzi, upumbavu, na kuharakisha katika kutekeleza mambo. Kwa kuwa akili inamzidishia mwanadamu uelewa na ufahamu, wakati huo huo akili inamuepusha kutenda makosa na upumbavu.
Al-Mawardy ametoa maana mbali mbali za akili. Na zilizotiliwa mkazo zaidi kati ya hizo ni: Akili ni kuelewa kwa njia za kufahamu uelewa wa lazima. Nazo ni aina mbili. Ya kwanza ni kuelewa kwa hisia. Na ya pili ni zile zilizokuwepo mwanzoni mwa kuumbwa. Ama kuhusu aina ya kwanza mifano yake ni kama kuelewa kwa kutazama kwa macho na kusikia kwa masikio… Na binadamu akielewa vitu kwa kutumia akili kwa aina yoyote ya hisia hizo, huthibiti kwake aina hiyo ya kufahamu. Ama kuhusu aina ya pili, ni kama kuelewa kuwa kitu hakikosi kuwa na sifa ya kuwepo au kutokuwepo. Na kwamba kitu kilichopo hakikosi kuwa ni chenye kuzuka au kuwepo tokea zamani. Vile vile hatuwezi kusema kuwa kitu fulani kipo na hakipo kwa wakati huo huo mmoja. Na kusema kitu kimoja ni kidogo zaidi ya vitu viwili. Aina hii ya kuelewa hupatikana kwa mtu mzima mwenye akili sawa sawa. Kwa hiyo mtu akipata aina hizi mbili za kuelewa basi ni mtu mwenye akili kamili. Hali hii ya mwenye akili kamili ilishabihiana (katika utamaduni wa kiarabu) kwa kufananisha na akili ya ngamia. Kwa sababu akili inamzuia binadamu kufuata matamanio ya nafsi yakiwa ni mabaya. Hali hii ni sawa sawa kama kumfunga ngamia asiende mbali anapoghadhibika. [Adabu Al Dunia wa Al Din . Uk. 19, Ch. Dar Maktabat Al Hayat] .
Wanachuoni wamehitilafiana katika kuainisha mahali pa akili. Imesemwa, mahali pake ni moyoni. Haya ni maoni ya maulamaa wengi wa madhehebu ya Malikiy, Shafiiy, na Hanabil [tazama: Ihkaam Al-Fusuul Uk.71, Ch. Dar Al Gharb Al-Islami, na Al-Muhiyt 1/89, Ch. Wizaarat Al-Awqaaf wa Al-sh’uwn Al Islamiya Al-Kuwait, na A ‘Udda, 1/ 89, na Al-Tamhiid 1 /48, Ch.]
Ama kauli ya pili kuhusu mahali pa akili ni kichwani. Kauli hii imenasibishwa kwa wanachuoni wa madhehebu ya Hanafiy. Al-Baji aliinasibisha kauli hii kwa Imam Abi Hanifa, pia ni kauli maarufu kwa Imam Ahmad [Al-‘Udda, 1/ 89, na Sharh Al- Kawkab Al Muniir, 1/ 84].
Ama kauli ya tatu kuhusu mahali pa akili ni moyoni na ina uhusiano na ubongo. Kauli hii imenasibishwa kwa Abi Al-Hasan Al-Tamimiy na wengine miongoni mwa wafuasi wa Imam Ahmad.
Mwenyezi Mungu aliitukuza akili na akaijaalia kuwa sababu ya Taklifu (mtu kupewa jukumu la kisheria). Imepokelewa na Ali R.A. kwamba mjumbe wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alisema: “Kalamu imenyanyuliwa kwa watatu: Aliyelala mpaka aamke, mtoto mpaka abaleghe na mwendawazimu mpaka awe na akili timamu”. ( Imepokelewa na Al-Termiziy katika kitabu chake).
Na Quraani tukufu imejaa Aya nyingi zilizohimiza kufikiri, kutazama na kuzingatia kwa njia mbali mbali. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Basi atazame binadamu chakula chake. Kwamba sisi tumemwaga maji kwa mmimino. Kisha tukaipasua pasua ardhi mpasuo. Tukaotesha humo nafaka. Na mizabibu na (mimea ya) mboga mboga. Na mizaituni na mitende. Na mabustani yaliyosongamana. Na matunda na (majani ya) malisho (ya wanyama). (Kuwa ni) Manufaa kwenu na wanyama wenu wa mifugo. [ABASA 24-34].
Vile vile Uislamu umeharamisha kuidhuru akili, na ukaharamisha aina zote za ulevi na udhoofishaji wa afya. Allah S.W anasema: {Enyi mlioamini! Hakika ulevi na kamari na (kuabudu) masanamu, na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; (yote hayo) ni uchafu katika amali ya shetani; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu.} [Al-MAIDAH 90]. Kutoka kwa Ummu Salama R.A. alisema: “Mtume S.A.W. alikataza kila chenye kulewesha na kudhoofisha afya”. (Hadithi hii mepokelewa na Ahmad katika Musnad na Abu Daud katika Sunan).
Elimu ya Tawhiyd (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) maana yake ya kilugha ni kukipwekesha kitu. Lakini kisheria maana yake ni: kujua kuwa anayestahiki kuabudiwa ni mmoja, kuuamini upweke wake na kusadikisha uwepo wake, sifa zake na vitendo vyake. Na kwamba hakuna dhati inayofanana na dhati ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na wala dhati yake haikubali kugawanyika, si kivitendo, wala kidhana, wala kwa nguvu. Na kukiri kwamba sifa zake hazifanani na sifa nyingine. Na sifa moja kati ya sifa zake haikubali kuwepo idadi ya sifa hiyo ndani yake, kwa mfano Mwenyezi Mungu Mtukufu akawa na sifa mbili za uwezo zinazofanana, na vitendo vyake havishirikiani na vitendo vingine, maana yeye peke yake ndiye aliyeumba na sio wengine.
Tawhiyd, tunapoitazama kama elimu, inaweza kutusadia kuthibitisha itikadi za dini nyingine kwa hoja za yakini. [Hash’at Al-Baijuriy katika kitabu chake Aljaw-hara, Uk.28, Ch. Daar Al- Salaam].
Kazi ya akili ni kuelewa kiini na sifa ya kilichopo na kufahamu jambo lenyewe kwa mujibu wa uwezo wa binadamu. Sisi tunapotaka kufahamu kuwepo kwa Mwenyezi Mungu tunatumia akili kwa kutia akilini vitu katika ulimwengu wa nje. Ama wajibu wa kumwamini Mwenyezi Mungu kwamba anayeamini atapata thawabu, na asiyeamini atapata adhabu inajulikana kutokana na sheria na sio akili. Na madhehebu ya Asha’ira na watu wengine wanasema kumjua Allah na hukumu nyingine kwao kunawajibika kwa sheria. Maana hakuna hukumu yoyote kabla ya sheria , sawa hukumu hii ni kubwa au ndogo. [Hashiat Al-Baijuriy katika kitabu cha Al- Jawhara, Uk.70].
Wanachuoni wa Sunna hawakutofautiana kuhusu kukiri kwamba akili inaweza kufahamu baadhi ya hukumu za kiitikadi, lakini waliafikiana kwamba hukumu ya Majukumu ya kisheria ya itikadi haiwezi kuthibitishwa ila kwa kunukuliwa kwa hoja za kisheria. Kwa hivyo wanachuoni wa Sunna wanatoa dalili juu ya maswala ya itikadi kwa hoja za akili. Na makusudio ni kuthibitisha ukweli wa masuala hayo na kuafikiana na yaliyotokea katika maisha ya dunia, na sio kuthibitisha hukumu za Majukumu ya kisheria kwa kutumia akili kwa kuwa kuthibitisha Majukumu ya kisheria kuna kuwa kwa sheria.
Baadhi ya wanachuoni wamekosea walipodhani kwamba wanachuoni wa Sunna na Jamaa au Asha’ira na Maturidiya wanatanguliza hoja za akili kabla ya hoja za kunukuliwa (aya za Quraani na hadithi za Mtume). Na watu wengi walipokea madai haya na wakayaeneza. Ilhali madai haya yametokea kutokana na kutofahamu vizuri kauli za wanachuoni. Na inawezekana sababu za madai haya ni kutokana na yaliyotajwa na Imam Al-Razi katika kitabu chake “Asaas Al-Takdiis”, [Uk.220-221, Ch. Maktabat Al- kulliyaat Al- Azhariya]
Jua kwamba dalili imara za kiakili zikitumika kuthibitisha jambo fulani, kisha tukakuta dalili za kunukuliwa (aya za Quraani na hadithi za Mtume) zinapinga na dalili hizo za kiakili, basi katika kesi hii kuna hali nne:
Ya kwanza: kukubali dalili za akili na mantiki. Na hapa inalazimika kuamini vitu viwili vinavyopingana. Na jambo hili ni muhali (haliwezekani).
Ya pili: kutokubali dalili za akili. Na hapa inalazimika kukadhibisha vitu viwili vinavyopingana. na jambo hili pia ni muhali (haliwezekani).
Ya tatu: kukadhibisha dalili za kunukuliwa, na kukadhibisha dalili za kiakili.
Ya nne: kusadikisha dalili za kunukuliwa na kukadhibisha dalili za kiakili. Na jambo hili ni batili, kwa sababu hatuwezi kujua ukweli wa dalili za kunukuliwa ila kwa kutumia dalili za kiakili kuthibitisha nani aliyeumba na sifa zake, na namna ya kuthibitisha kwa dalili za muujiza juu ya ukweli wa Utume wa Muhammad S.A.W.. Na tukiendelea kuzitia kasoro dalili za kiakili, basi akili itakuwa haikubaliki, maana hatuwezi kuthibitisha misingi ya itikadi. Na tukishindwa kuithibitisha misingi hiyo tutahisi kuwa dalili za kunukuliwa hazina faida. Inathibitika kuwa kuitia kasoro dalili ya akili katika kusahihisha dalili za kunukuliwa hupelekea kuzitia kasoro dalili zote mbili za akili na kunukuliwa, na hii pia ni batili.
Na kwa kuwa hali hizo nne zote zimekuwa batili, hatuna budi ila kukubali dalili za wazi za kiakili kwa ajili ya kuthibitisha dalili za kunukuliwa. Kwa kuwa dalili hizi za kunukuliwa zinaweza kusemwa kuwa si sahihi au ni sahihi, isipokuwa makusudio yake si kama inavyofahamika kwa mujibu wa dalili hizo. Kisha tukijuzisha kufasiri kwa akili: tutakuwa tumetumia njia ya nyongeza katika kutoa maelezo zaidi. Na ikiwa kama haikujuzu kufasiri kwa kutumia akili, elimu hiyo tutaiacha kwa Mwenyezi Mungu. Na hiki ndicho kigezo kamili tunachorejelea katika mambo yenye kubabaisha.
Al- Razi alizungumzia njia za kunukuliwa. Na njia hizo si za kunukuliwa kila wakati. Kwa hiyo walichokifanya watu wa Sunna na Jamaa katika mlango huu ni kutekeleza sheria tukufu kuhusu kuitumia akili katika kuelewa uhakika wa ulimwengu na sheria kwa ajili ya kuifikia imani. Na hiyo ndiyo njia iliyonyooka ilivyo na ambayo itatufikisha katika kumjua Mwenyezi Mungu aliyetakasika na aliyetukuka.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi wa yote.