Kuondoa uovu

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuondoa uovu

Question

Sheria inatuamrisha kuondoa uovu, Ni vithibiti gani vinatuelekeza kutambua kitendo fulani ni uovu? Na njia gani na nyenzo gani ni sahihi kutumia katika kuondosha uovu?

Answer

Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata, ama baada ya hayo:

    Al Ragheb Al Asfahaniy amesema: “Uovu ni kila kitendo ambacho akili sahihi zinaweza kutoa hukumu ya kubainisha ubaya wake, au akili zikiacha kukijali, sheria inatoa hukumu ya kubainisha ubaya wake” [Al Mufradat, Uk. 823, Ch. Dar Al Qalam & Dar Al Shamiya, Syria & Beirut]. Al Gasas alisema: “Uovu ni kile kitendo ambacho Mwenyezi Mungu amekikataza” [Ahkam Al Quraan, 2/44, Ch. Dar Al Kutoob Al Elmiya). Naye Al Aluseiy alisema: “Uovu: maasi ambayo sheria imeyakataza” [Roho Al Maaniy, 4/28, Ch. Dar Ihyia’ Al Turath Al Arabiy].

    Basi tukijumuisha maana hizo zote za uovu, tunaweza kusema kwamba: uovu ni kila kitendo ambacho akili sahihi zinatoa hukumu ya kubainisha ubaya wake au sheria inaainisha kwamba ni cha uovu, haramu au kinachukiza, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika kitabu chake: {Na anakataza uchafu na uovu} [AN NAHL, 90].

Al Jerjaaniy amesema: “Kuamrisha mema ni kuongoza kwenye njia zilizonyooka, na kukataza maovu ni kukataza mambo maovu yasiyokubaliwa na sheria. Inasemekana kwamba: kuamrisha mema ni kuongoza kwenye heri, na kukataza maovu ni kukataza shari. Pia inasemekana kwamba: kuamrisha mema ni kuamrisha kila kitendo kinachokubaliwa na Quraani na Sunna, na kukataza mema ni kukataza matamanio ya nafsi na na shahawa zake. Kadhalika inasemekana kwamba: kuamrisha mema ni mtu kufanya yanayomridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa maneno na vitendo, na kukataza maovu ni kukataza yale mambo yasiyokubaliwa na sheria na murua, na hilo ndilo jambo ambalo halifai katika sheria ya Mwenyezi Mungu” [Al Taarifat, 1/54, ch. Dar Al Kitaab Al Arabiy].

Al Asfahaniy anasema: Kuna aina mbili za kubadilisha (kuondosha), moja ni kubadilisha sura ya kitu bila ya kitu chenyewe. Unasema: "nimebadilisha nyumba yangu", yaani nimeijenga katika sura nyengine inatafautiana na ile ya awali. pili ni kubadilisha kitu kwa kitu chengine. Unasema:" Nimebadilisha mtumwa wangu na mnyama wangu", yaani umewabadilisha kwa kuwaleta wengine wapya. (Al Mufradat, uk. 619).

Uovu ambao Umma wa Kiislamu unalazimika kuubadilisha ni ule unaokiuka wazi wazi Quraani na Sunna. Uovu ni kwenda kinyume na yale aliyoamrisha Allah S.W, au kufanya aliyoyakataza, au kuacha kikamilifu aliyoamrisha Allah S.W, au kuzidisha hukumu bila ya kuwepo matini za kisheria, au kupunguza hukumu bila ya udhuru, au kuigeuza au kuibadilisha.

    Ili uovu uwe uovu ni lazima upitishwe na Ijmaa (makubaliano ya wanachuoni) juu ya kuukataza kwa kuwepo dalili imara kutoka Quraani na Sunna. Kukataza uovu hakutakikani kuwe na hitilafu baina ya wanachuoni wanaoaminika ambao ni wahusika na wachamungu. Na ikiwa miongoni mwa mambo ambayo yanatokana na kujitahidi na hitilafu za wanachuoni, basi Umma haulazimiki kuuondoa.

    Kuamrisha mema na kukataza maovu ni faradhi yenye kutosheleza (faradhi kifaya) wakifanya baadhi ya watu, waliobaki hawapati dhambi. Na wakiacha wote kufanya bila ya udhuru au hofu, basi wanapata dhambi.

    Kuwepo kwa maovu katika jamii ni jambo la kawaida, maana hakuna jamii yoyote katika zama yoyote, ambayo haina maovu, lakini ambalo si la kawaida ni pale wanajamii wanaona maovu katika jamii yao na wasifanye haraka kuyabadilisha kwani katika kuyabadilisha, maisha yanaendelea katika njia ambayo Mwenyezi Mungu anaipenda.

    Quraani inausia kukumbusha, kuamrisha mema, kukataza maovu, kuusiana haki na kuusiana kusubiri. Mwenyezi Mungu amesema: {Na kumbusha, kwani hakika ukumbusho (mawaidha) unawafaa waumini.} [ADH DHAARIYAT, 55], pia Allah S.W amesema: {Mmekuwa umma bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza mabaya na mnamwamini Allah.} [AAL IMRAN, 110].

    Aidha, Sunna ya Mtume S.A.W. inatuhimiza kuamrisha mema na kukatza maovu, kama alivyosema Mtume s.a.w.: “….. Kuamrisha mema ni sadaka, na kukataza maovu ni sadaka … ” [Imepokelewa na Imam Muslim katika kitabu chake “Sahihi Muslim” na Abu Dawud katika kitabu chake “Sunan Abu Dawud”].

 Al Nawawiy -Mwenyezi Mungu amrehemu- alisema: “Jua kwamba kuamrisha mema na kukataza maovu ni jambo ambalo limepotezwa kwa kiasi kikubwa katika zama zilizopita, na hakikubaki katika zama hizi isipokuwa ni kidogo tu, nacho ni mlango ulio mkubwa. Uchafu ukienea, adhabu ya Mwenyezi Mungu itamkumba mwema na mwovu, na dhalimu asipozuiliwa kufanya uovu, basi adhabu ya Mwenyezi Mungu huwenda ikawajumuisha watu wote. Mwenyezi Mungu amesema: {Basi wajihadhari wale wanaokaidi amri yake, usije ukawapata msiba au ikawafika adhabu iumizayo} [AN NUR, 63]. Basi mwenye kuyataka maisha ya akhera, na mwenye kuitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu lazima auangalie mlango huo, kwani una faida nyingi ingawa kiasi kikubwa chake kimepotezwa, tena mwenye kuamrisha mema lazima aitakase nia yake na wala asiogope yule anayemkataza kwa ajili ya cheo chake kilicho juu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na bila shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayesaidia dini yake} [AL HAJJ, 40], na amesema: {Na atakayeshikamana na Allah basi kwa yakini ameongozwa kuelekea njia iliyonyooka.} [AALI IMRAN, 101]. Pia amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na wale wanaojitahidi kwa ajili yetu, kwa yakini tunawaongoza kwenye njia zetu} [AL ANKABUUT, 69], pia Allah S.W anasema: {Je, wanadhani watu kwamba wataachwa (bila ya misukosuko kwa kuwa) wanasema: “Tumeamini.” basi ndio wasijaribiwe?. Kwa yakini tuliwajaribu wale wa kabla yao, ili Allah awatambulishe wale waliosadikisha na ili awatambulishe waliokadhibisha.} [AL ANKABUUT, 2:3]. Na jua, ujira unalipwa kwa mujibu wa taabu. Na anayeamrisha mema haifai kuacha kumkataza anayefanya maovu kwa kuwepo urafiki na mapenzi baina yao au kwa ajili ya kutaka sifa. Ni haki yake kumnasihi, kumuongoza katika njia yenye mafanikio ya akhera yake, na amwokoe kutokana na madhara yake. Rafiki wa mtu na mpenzi wake ni yule anayemsaidia mwenzake kukidhi mambo yatakayomfaa katika maisha yake ya akhera, hata ikipunguka hadhi yake katika maisha ya hapa duniani. Na adui yake ni yule anayefanya juhudi ya kuondoka au kupunguka hadhi yake katika maisha ya Akhera, hata akipata hadhi katika maisha ya duniani. Kwa hiyo, Iblisi ni adui yetu. Na Manabii     -sala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwafikie wote- walikuwa vipenzi kwa waumini kwani walifanya juhudi kubwa kufanikisha maslahi yao ya kufuzu maisha ya akhera na kuwaogoza.

 Mwenye kuamrisha mema na kukataza maovu anapaswa awe mpole ili aweze kufikia lengo. Imamu Shafii -Mwenyezi Mungu amrehemu -alisema “Mwenye kumpa mawaidha ndugu yake kwa siri basi amemnasihi na amempamba, na mwenye kumpa mawaidha ndugu yake kwa dhahiri basi amemfedhehesha na amemdhalilisha”. [Sharh Al Nawawiy juu ya Sahihi Muslim, 2/24, Ch. Ihiya’ Al Turaath Al Arabiy, Beirut].

    Na kwa kuwa kuondoa uovu ni jambo adhimu na muhimu katika maisha, basi Mtume S.A.W. alibainisha mfumo wa kuondoa uovu, njia zake na nyenzo zake ili Umma usipotee wakati wa kutekeleza faradhi hii kwa kuelekea njia isiyonyoka.

    Mtume S.A.W. alisema: “Mmoja wenu akiuona uovu basi auondoe kwa mkono wake, na kama hana uwezo wa kuondoa kwa mkono wake basi kwa ulimi wake, na kama hana uwezo wa hivyo, basi achukie kwa moyoni. Na hii ni daraja dhaifu”. (Imepokelewa na Imamu Muslim katika kitabu chake kinachoitwa Sahihi Muslim & Abu Dawud katika Sunan Abu Dawud & Ibn Magah na Annassa’i).

    Imam Al Nawawiy alitaja katika maelezo ya Hadithi hii kwamba, Jaji Ayadh - Mwenyezi Mungu amrehemu -alisema: “Hadithi hii ni nguzo katika sifa ya kubadilisha; mwenye kutaka kuuondoa uovu ana haki ya kuuondoa uovu kwa kila njia anazozimiliki, ikiwa kwa maneno yake au vitendo vyake; basi anaweza kuvunja zana za batili na kumwaga ulevi, pia anaweza kumwamrisha mwengine kufanya hivyo. Anaweza kuchukua vitu vilivyonyang’anywa na kuvirudisha tena kwa wanaovimiliki kihalali kwa mkono wake au kwa kumwamrisha mwengine kufanya hivyo. Licha ya kuwa mwenye kufanya uovu anaweza kuwa hatambui athari ya kosa lake au anaweza kuwa miongoni mwa madhalimu wenye nguvu ambao watu wanaogopa shari zao, na hapa mwenye kutaka kuondoa uovu anaweza kuongea na watu wa namna hii kwa utaratibu. Tena jambo linalopendeza zaidi hapa ni kuwa mtu atakayechaguliwa kujishughulisha kuondoa uovu awe miongoni mwa watu watendao mema na wenye fadhila, na huadhibiwa zaidi yule anayevuka mipaka na kufanya uovu na yule anayepindukia kiasi katika kuambatana na batili. Na huadhibiwa zaidi yule anayevuka mipaka katika kufanya uovu na anayepita kiasi katika kuambatana na batili iwapo akipata adhabu inamsaidia kuacha kufanya uovu, lakini iwapo akipata adhabu anazidi kufanya uovu anaofanya, basi bora aachwe, na mwenye kutaka kuondoa uovu atakuwa hana budi ya kuuondoa uovu wa yule mtu kwa moyo wake kama ilivyotajwa katika Hadithi” [Sharh Al Nawawiy juu ya Sahihi Muslim, 2/25].

    Abu Bakar bin Al Araby alisema katika maelezo yake juu ya Hadithi hiyo: “Katika Hadithi hii tunakuta Mtume S.A.W. kwa namna ngeni ya Fiqhi ya Kiislamu, anaanzia kwa kitendo; yaani kubadilisha uovu kwa kuuondoa kwa mkono na hajaanza kwa kuubadilisha kwa ulimi, Na iwapo mwenye kufanya uovu hajaacha dhambi, basi mwenye kutaka kuondoa uovu atumie mkono wake; maana anakusudia kutenga baina ya uovu na mwenye kuzoea kuufanya, na iwapo mwenye kutaka kuondoa uovu ameshindwa kumfanyia mwenye uovu aache dhambi ila kwa kutumia silaha; basi atakuwa hana budi amwache aendelee na dhambi lake; kwani watu wakipigana kwa silaha itakuwa fitina na matokea yake yatakuwa mabaya zaidi kuliko kuacha kuamrisha mema ila katika hali ya kwamba uovu unazidi kuwa na nguvu; Na iwapo ataona maadui wanapigana, basi ni juu yake kuwatenganisha, kwani akiwaacha, mmoja wao atamwua mwenzake, na hali ya kuwa mtu anaweza kuwatenganisha basi anaruhusika kutoa silaha” [Ahkam Al Quraan, Ibn Al Arabiy, 1/383:384,  Dar Al Kutoob Al Elmiya, Beirut].

    Hadithi hii imetubainishia daraja za kuondoa uovu; mtu akishindwa kutumia njia moja, anaweza kutumia nyingine. Kadhalika imetubainishia zana za kubadilisha kwa mfumo ambao unamfanya mtu hachagui njia moja ila baada ya kushindwa kutekeleza jambo la kuondoa uovu kwa njia ya mwanzo; maana kuondoa uovu kwa mkono kunakuwa kwa yule mwenye mamlaka juu ya mwenye kufanya uovu; mamlaka ya baba juu ya mwanawe, mamlaka ya mume juu ya mkewe, mamlaka ya mchungaji juu ya raia wake. Na katika hali ya baba na mume, wanakuwa na mamlaka ya kuondoa uovu lakini katika mipaka ambayo wakiivuka watakuwa wenye madhambi au wakiivuka mipaka madhara makubwa yatatokea au uovu mkubwa zaidi unatokea. Ama katika hali ya mchungaji, basi anakuwa na mamlaka kamilifu. Al Qurtuby alisema: “Katika kuamrisha mema, watawala wanauondoa uovu kwa mkono, maulamaa wanauondoa uovu kwa ulimi na wale wanyonge -watu wa kawaida- wanauondoa kwa kuchukia moyoni” [Al Jami’ Li Ahkam Al Quran, 4/49, Dar Al Kutoob Al Masriya].

    Katika hatua yoyote ya kuuondoa uovu lazima hekima na busara zitawale ili mtu afanyaye uovu asipate madhara na kutokea uovu zaidi au kutokea fitina itakayosababisha kueneza uovu na baadaye itashindikana kuondoa uovu.

 Kwa hivyo, kuondoa uovu kunakuwa na athari zinazoathiri mtu binafsi au jamii, kwa hiyo jambo la kuondoa uovu halitakuwa sawa ila baada ya kuziangalia vizuri athari na matokeo ya kulifanya juu ya mtu na jamii, pamoja na kuangalia uwiano kati ya kuuondoa uovu na athari za kuuondoa. Kwa hivyo, inawajibika kuwauliza watu wa elimu na hekima; kwani daktari baadhi ya wakati anapendelea kuacha kumtibu mgonjwa akiogopa athari za dawa au operesheni juu ya mgonjwa mpaka hali yake iwe tayari kupokea matibabu bila ya kuwepo athari mbaya. Hali kadhalika, mwenye kuondoa uovu anahitaji hekima kuliko anavyohitajia daktari; kwani daktari akjisahau basi madhara yake ni madogo kuliko akijisahau mwenye kuondoa uovu. Na katika hali hii ya kughafilika hakuna mtu atakaemtuhumu daktari kuzembea, kufanya hiana au kutotekeleza wajibu wake.

    Pia watu wa kawaida hawaruhusiki kuwatuhumu maulamaa wa Umma wakiwa wanausia subira juu ya uovu mpaka mazingira na hali iwe tayari kuondoa uovu, na matokeo ya kubadilisha yawe rahisi kutekelezwa, na hiyo ndiyo inayotokana na maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Waite (watu) katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema} [AN NAHL, 125], na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Sema: “Hii ndiyo njia yangu nalingania kwa Allah kwa ujuzi wa kweli, mimi na anayenifuata. Na Utakasifu ni wa Allaah nami, si miongoni mwa washirikina.} [YUSUF, 108].

    Hekima na ujuzi wa kweli ni mambo yanayosaidia kufaulu katika kutekeleza kuondoa uovu, na hilo ndilo jambo ambalo linamridhisha Mwenyezi Mungu na linawezesha kufanikisha lengo linalotakiwa .

    Kutokana na yaliyopita inabainika kwamba, jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu ni faradhi yenye kutosheleza (faradhi kifaya) wakilifanya baadhi ya watu, waliobaki hawapati dhambi. Na kuondoa uovu kunakuwa kwa daraja tofauti; kuondoa uovu kwa mkono ni kazi ya watawala, kuuondoa kwa ulimi ni kazi ya maulamaa na kuuondoa kwa ulimi kunakuwa kwa watu wa kawaida. Yote haya yafanyike kwa kuchunga hekima na kipimo wakati wa kutekeleza hiyo kazi kuu.

Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas