Umuhimu wa Kutambua Hali Halisi Wak...

Egypt's Dar Al-Ifta

Umuhimu wa Kutambua Hali Halisi Wakati wa Kutoa Fatwa

Question

Ni upi umuhimu wa kutambua hali halisi wakati wa kutoa fatwa?

Answer

Namshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu. Rehma na amani zimwendee Mtume wake, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya utangulizi huu.

Maana ya fatwa kilugha ni kutoa hukumu ya jambo fulani. Na neno hili katika lugha ya kiarabu ni Jina linalotokana na kitenzi “ aftaa” yaani amefutu au ametoa hukumu.

Na fatwa kisheria ni kumbainishia mtu aliyeuliza hukumu ya kisheria kwa kutumia dalili. Na hili linakusanya uulizaji wa hali halisi ya mambo na mengineyo.(Sharh Almuntahaa, 3/456.  Kampuni ya uchapishaji ya Answar Al Sunna). Na hali halisi inakusudiwa ulimwengu wa vitu, watu, matukio, fikra, na mifumo mbalimbali.

Katika Fiqhi ya Kiislamu, matini zina kikomo na mwisho. Ama matukio hayana kikomo na hayaishi. Kwa kuwa matukio yanategemea utendaji wa mwanadamu usiokwisha mpaka siku ya Kiyama.

Wanachuoni wa madhehebu ya Hanafiy wanaona kuwa matawi ya Fiqhi ya Kiislamu ni milioni moja, laki moja na elfu 75. Kinachokusudiwa katika neno “tawi la Fiqhi” ni sentensi yenye maana ambayo inatokana na kitendo kati ya vitendo vya mwanadamu, halafu kuna hukumu kati ya hukumu za kisheria inaeleza kwamba vitendo hivi ni Mubah au Makruhu au Haramu, au Faradhi au Sunna. Inaeleweka kuwa kiwango hiki kikubwa cha matawi haya na mengineyo kinatokana na vyanzo vikuu vya sheria ikiwemo kutunga sheria. Na asili ya vyanzo hivyo ni Quraani tukufu na Sunna, na viwili hivi ni chimbuko la utungaji wa sheria.

Si haki ya mtu yoyote kutunga sheria kwa kutokuwepo fikra ya kiungu au wanavyuoni wa kidini wanaowatungia sheria watu. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: {Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu} [AL ANAAM 57]. Na hukumu hii ya Mwenyezi Mungu inaweza kuwa imetokana na Quraani au Sunna. Na wanachuoni wote wakubwa ambao tumefikishiwa kauli zao, idadi yao inakaribia madhehebu na maimamu tisini, kama Abu Hanifa, Malik, Shafiy, Ibn Hanbal, Al Hammdiin, Al Sufyaniyiin, Al Awzaiy, na wengine wengi, wanachuoni wote hawa walizitumia matini (aya na hadithi) kwa uelewa wa kina na wa ndani, pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu na kuwa makini kwa ajili ya kutafuta ridhaa ya Mwenyezi Mungu wakati wanapofafanua hukumu ya kisheria. Na kutokana na ufahamu huu, urithi mkubwa wa Fiqhi umekuwa, unaozingatiwa ni hazina kubwa ya utajiri, maji matamu yatiririkayo bila kukatika, na kauli bora ya kuchukuliwa. Na licha hayo, baadhi ya masuala yao yaliathiriwa na hali halisi ya zama zao, na wanavyuoni wa zama hizo wametuamuru kutoyafuata matukio yao na masuala yao, bali lazima tuchukue mifano yao na kuitumia katika hali halisi tuliyonayo sisi. Imamu Al-qirqfi anasema kwa kutumia maneno yenye balagha nzito na yaliyo wazi na yasiyohitaji nyongeza: “Mazoea na matukio ya miamala yanapokuja basi yazingatie, na pale yanapodondoka yadondoshe. Hulazimiki kuyafuata yaliyoandikwa vitabuni katika umri wako wote, bali anapokujia mtu asiyetoka katika eneo lako na akataka umtolee fatwa, basi usimfanye kama ni mtu wa eneo lako, na umwulize juu ya mazoea na matukio ya miamala ya nchi yake, kisha umtolee fatwa bila ya kufuata mazoea na matukio ya miamala ya nchi yako ambayo yamo ndani ya vitabu vyako. Na hii ndiyo haki ya wazi kwa makusudio ya wanavyuoni wa Kiislamu waliotangulia tangu zamani” (Al Furuk, na Al Qirqfi,1/177, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiya)

Maneno hayo yanayotoka kwa Imamu mkubwa mwenye elimu nyingi yametuzindua masuala ya kutambua hali halisi kama ni msingi muhimu miongoni mwa misingi ya kutoa fatwa. Ama kuelekea kwenye vitabu mbalimbali vya Fiqhi na kuchukua hukumu zake za kisheria kutoka katika vitabu hivyo ambavyo vimeathirika na hali halisi pamoja na mazoea na matukio ya miamala maalumu kisha kuhukumu kwayo katika hali halisi nyingine na mazingira tofauti, huu utakuwa ni upotovu wa wazi na ujinga mbaya. Kwa hivyo katika utaratibu wa kutoa fatwa tunapaswa kuvitambua vyanzo na kuvifahamu kwa kina kwa mujibu wa misingi ya lugha, balagha, na sarufi, au kile kinachoitwa kiujumla elimu za ufundi na kutambua hali halisi.

Na tunaposema kutambua hali halisi tunakuwa na maana pana sana, kwani wanavyuoni wa ustaarabu kama vile Malik Ibn Nabiy na wengineo wanajaribu kuidhibiti maana hii, wanasema: Uhalisi wa hali unaweza kugawanywa na kuwa aina za vipengele mbalimbali ambavyo tunavielewa, kwa maana kila kipengele kina njia ya kukitambua, kama ambavyo tunalazimika kuzitambua aina za uhusiano wa pande mbili kati ya aina mbalimbali za vipengele hivi. Vipengele hivyo ni kipengele cha vitu, kipengele cha watu, kipengele cha matukio, kipengele cha fikra . Vipengele hivi vinaunganishwa na kipengele cha mifumo. Wanavyuoni hao hawakuishia hapo tu, bali wameufanya mhimili wa kuutambua mpangilio huu ndiyo utamaduni wenyewe. Kwa mfano mkulima mdogo anatilia umuhimu kipengele cha vitu ambavyo ni shamba lake, mazao yake, nyumba yake, wanyama wake, maradhi yao, na afya yake mkulima.

Na wakati mwingine mkulima huyu anatilia umuhimu vitu vinavyofungamana na vya wengine, kama vile fulani amesafiri, na fulani amenunua nyumba, n.k. Tukifika kwa mtu wa mjini tunakuta kuwa shime yake iko juu kiasi kwani yeye anawajali watu, kisha matukio kama maandamano, uchaguzi, kupanda kwa bei, n.k. Na tukienda katika vyuo vikuu na kumbi za tafiti hapo huanza shime ya kufikiri katika fikra za matukio na namna ya kuyasoma.

Kwa hivyo mufti anapaswa wakati wa kutoa fatwa au kuchagua kauli maalumu avisome vipengele hivi kwa kutumia njia zake tofauti, mahusiano yake ya ana kwa ana, na matokeo ya kutekeleza fatwa hii katika jamii husika. Kwa mfano mtu fulani akiuliza kuhusu hukumu ya kisheria juu ya bidhaa fulani, basi bidhaa hii inaingia katika kipengele cha vitu. Hapo Mufti lazima aelewe habari maalumu ili atoe fatwa kuhusu kitu hicho. Kwa mfano Mufti akiulizwa kuhusu kinywaji cha siki ya tufaha, basi Mufti aulize, nini tatizo lake? Harufu yake? Elementi zake? Matokeo yake? Je ina asidi? Ina mafuta ya nguruwe? Je, aina ya asidi hiyo ni ya ethyli inayosababisha kulewa, au ni ya methyl, na ya kiwango gani? Ili kuelewa yote haya ni lazima kutambua elimu mbalimbali, kama elimu ya kemia, fizikia, uchambuzi wa lishe, tiba, na fiziolojia. Kuelewa mambo hayo na mengineyo kuna faida kubwa kwa mufti ili kutambua athari za elementi hizi juu ya afya ya binadamu, manufaa yake na madhara yake. Kwa hivyo inampasa mufti kuwauliza wajuzi na wahusika wa elimu hizo, kwani mafanikio ya fatwa yake yanategemea kuuliza kwake.

Maelezo hayo yaliyotangulia yanaweza kusemwa pia tunapotendeana na vipengele vya matukio na fikra. Lakini pamoja na hayo mufti anatakikana kuelewa hali halisi ya jamii yake, na kutumia vyanzo vyake na matini zake sawasawa. Vilevile atafute njia nzuri ya kutekeleza matini ya fatwa kwa mujibu wa hali halisi ya jamii yake. “Njia hii lazima ikusanye malengo makuu ya sheria, nayo ni kuhifadhi nafsi, akili, dini, heshima, na mali. Pia mufti lazima afuate msingi wa Ijmaa (maafikiano ya wanavyuoni) na asiende mbali na Ijmaa hii. Vilevile afahamu lugha ya Kiarabu na maana zake. Kwa kuwa vyanzo vya kisheria na matini zake ni kwa lugha ya Kiarabu. Pia mufti lazima azingatie maadili ya ujuzi wa Kiislamu yanayoitwa Akida. Aidha wakati wa kutoa fatwa na kuzingatia hali halisi ni lazima kuchunga misingi ya kifiqhi au misingi ya sheria. Mambo hayo yaliyopita tunapoyazingatia yatakuwa kama daraja linalounganisha kati ya vyanzo na kuelewa hali halisi”. (Al Tareek Ilaa Al Turath. Uk.20, Ch. Nadit Masr).

Kwa mujibu wa yaliyotangulia, hakika mufti kuelewa hali halisi kwa vipengele vyake vinne ni jambo muhimu katika kutoa fatwa.

Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas