Dawa za kuongeza nguvu za kiume.

Egypt's Dar Al-Ifta

Dawa za kuongeza nguvu za kiume.

Question

Nini hukumu ya kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kabla ya kuingiliana na mke?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuumba mwanamume na mwanamke, na kila mmoja ana tabia ya kumili kwa mwenzake. Inajulikana kwamba hamu ya kijinsia ni miongoni mwa matamanio yenye nguvu zaidi kwa mnyama, kwa hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu ametunga sheria ya ndoa kupanga uhusiano baina yao ili uwe uhusiano wa kisheria kujiepusha na dhambi na kupata ujira.

Ni wazi kuwa sababu iliyo nguvu zaidi miongoni mwa sababu za ndoa ni kukidhi haja, na hilo ndilo jambo ambalo sheria imelikubali na imelihimiza kulifanya kwa manufaa ya kidunia na ya Akhera yaliyoambatana nalo, kwani linatuliza nafsi na kujiepusha na wakati mgumu. Tena linamfanya mwanandoa ainamishe macho na kuulinda utupu. Na kutoka kwa A’lqama amesema: “Nilikuwa pamoja na Abdullah nikamkuta Uthman akiwa Mina akasema: Ewe Abu Abdul-Rahman! Mimi nina haja nawe, wakakaa faragha, Uthman akasema: Je, Abu Abdul-Rahman wataka tukuozeshe mwanamwali - bikra - atakayekukumbusha vile ulivyozoea? Alipoona kuwa Abdullah hana haja na jambo hilo, akaniashiria, kisha akasema: Ewe A’lqama! Kama utasema hivyo basi Mtume S.A.W. tayari ameshatuambia: Enyi vijana! Awezae miongoni mwenu majukumu ya kuoa aowe kwani inainamisha macho na inalinda utupu na asiyeweza basi afunge kwani kufunga ni ngao (kutamuondolea matamanio)”(Bukhari na Muslim).

Al Nawawiy alisema: “ujue kwamba matamanio ya jimai ni matamanio ambayo Manabii na watu mema waliyapenda; ambapo walisema: yanakuwa na masilahi ya kidini na ya kidunia k.v. kuinamisha macho, kujiepusha na matamanio ya zinaa, kupata watoto ambao wanaweza kuiimarisha dunia na umma uzidi kuwa na idadi nyingi zaidi mpaka siku ya Kiyama, aidha walisema: matamanio mengine yote yanamfanya mtu awe mwenye ugumu wa moyo lakini matamanio ya jimai kinyume cha matamanio mengine kwani yanaleta ulaini wa moyo”[Sharh Al Arobaini Al Nawawiya, Uk. 76, Ch. Al Maktab Al Islamiy].

Naye Mtume S.A.W. aliwahimiza watu wa umati wake kukidhi haja; ambapo alibainisha kwamba mwanamume anapewa ujira juu ya kitendo hicho, katika Sahihi mbili kutoka kwa Abu Dharr ya kwamba Mtume S.A.W. alisema: “Tendo la ndoa la mmoja wenu ni sadaka. Wakasema: Ewe Mtume wa Allah! Mmoja wetu afanye jimai halafu apate ujira? Akasema: akifanya hivyo katika haramu si atapata dhambi? Hali kadhalika akifanya katika halali lazima apate ujira”.

Al Nawawiy alisema: “maneno yake Mtume S.A.W. “Tendo la ndoa la mmoja wenu ni sadaka” ni dalili ya kuwa mambo yanayoruhusika (mubaha) yanaweza kuwa ni ibada kwa mujibu wa nia njema; kuingiliana kunaweza kuwa ibada akiwa mtu ana nia ya kumpa mke haki yake na akae naye kwa wema ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu Ameuamrisha, kuomba kupata mtoto mwema, kujizuia nafsi yake au nafsi ya mke kutokana na kuangalia yaliyoharamishwa au kuwaza yaliyoharamishwa au kukazia nia ya kutaka yaliyoharamishwa. Na pia matakwa mengine mema”[Sharh Muslim, 7/92, ch. Ihiya’ Al Turayh Al Arabiy].

Al Taibiy alisema: “hali kadhalika; juu ya hayo itakuwa kiasi, “akifanya katika halali” na akaacha kuomba haramu ingawa nafsi inaielekea na inapata ladha kufanya zaidi haramu kuliko ya halali; kwani kila jambo jipya lina ladha yake na nafsi inaelekea zaidi kwake na Shetani kwa zamu yake anasaidia nafsi kuipata. “lazima apate ujira” … ujira hapa hautakuwa kwa sababu ya kukidhi haja, bali kwa sababu ya kufanya hilo katika halali kama vile kuwahi kufungua kinywa katika Idi, kula daku na matamanio mengine ya kinafsi ambayo sheria inayakubali, kwa hayo; inasemekana: matamanio yakiafikiana na matakwa binafsi yatakuwa kama samli na asali, na kwa maana kama hiyo Mwenyezi Mungu Amesema: {Na nani aliyepotea zaidi kuliko yule anayefuata matamanio yake pasi na uwongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu}[Al-QASAS, 50]”[Merqat Al Mafateeh, 4/1338, ch. Dar Al Fikr].

Pia ilidhihirika katika Hadithi kadhaa ya kwamba Mtume s.a.w. alikuwa anawaangalia Masahaba wake katika kipengele hiki, ambapo ilitajwa katika Sahihi mbili kutoka kwa Jabir bin Abullahi R.A. alisema: “Nilikuwa pamoja na Mtume S.A.W. katika vita, basi akataja Hadithi; kutoka kwa Mtume S.A.W. aliponiuliza: Jabir umeoa? Nikasema: ndiyo. Akaniuliza: mwanamwali au mjane?. Nikamjibu: mjane. Akaniuliza: kwa nini usioe bikra ukacheza naye, naye akacheza nawe, ukamchekesha naye akakuchekesha? Jabir akasema: nikamwambia: hakika nina ndugu wa kike, ninapenda nimuoe mke atakayewakusanya na kuwachana nywele zao na kuwaelekeza na kuwaongoza. Mtume S.A.W. akasema: wewe ndio unafika kwenu hiyo ukifika fanya bidii (uwe karibu na mkeo) upate mtoto”.

Al Hafez bin Hajar alisema: “maneno yake: “upate mtoto”, Mtume s.a.w. aliyasema kumhimiza kuingiliana na mkewe au kutoacha kuingiliana”[Fat-h Al Bariy, 9/342, ch. Dar Al Maarifa].

Katika Sahihi mbili: “Kutoka kwa Abdullahi bin Amr bin Al-As R.A. alisema: “Mtume wa Allah S.A.W. aliniambia: Ewe Abdallah! Hivi sikuelezwa kuwa unafunga mchana na usiku unasimama kusali? Nikasema: ni kweli ewe Mtume wa Allah! Akasema: usifanye hivyo, funga na kula, na simama (usiku kusali) na ulale; kwani hakika mwili wako una haki juu yako na jicho lako lina haki juu yako, na mkeo ana haki juu yako”.

Katika Sahihi ya Al Bukhari kutoka kwa Abu Juhaifa alisema: “Mtume S.A.W. aliunda udugu baina ya Salman na Abu Al Dardaa, basi Salman alimzuru Abu Al Dardaa akamwona Um Al Dardaa katika hali ngumu, akamwuliza: mbona unaonekana na hali hii? Alisema: ndugu yako Abu Al Dardaa hana haja katika dunia. Akaja Abu Al Dardaa akamtayarishia chakula. Akasema: kula. Akamjibu Salman: Mimi nimefunga. Akasema: sitakula mpaka wewe ule. Alisema: basi akala. Na usiku Abu Al Dardaa alienda ili kusali usiku. Salman alisema: lala! Akalala. Kisha Akaenda tena kusali usiku, akasema: lala! Basi mwishoni mwa usiku Salman alisema: amka sasa! Wakasali pamoja, Salman akamwambia: Mola wako ana haki juu yako, nafsi yako ina haki juu yako, watu wako (mke wako) wana haki juu yako, basi mpe kila mwenye haki haki yake. Baadaye akaenda kwa Mtume S.A.W. kumwambia hayo, Mtume s.a.w. alisema: Salman amesema ukweli”.

Al Hafez bin Hajar alisema: “miongoni mwa faida za Hadithi hii ni uhalali wa mke kuweka mapambo kwa ajili ya mumewe na kuthibitika kwa haki ya mke juu ya mumewe kuhusu kukaa naye kwa wema na pengine inatokana na hayo, haki yake katika kuingiliana kwa maneno yake “watu wako wana haki juu yako” kisha akasema: “uingiliane na mkeo” … ”[Fat-h Al Bariy, 4/211].

Na Mtume S.A.W. aliubainishia umati wake baadhi ya mambo yanayozidisha nguvu ya kufanya tendo la ndoa anayeyataka. Katika Sahihi Muslim kutoka kwa Abu Said Al Khudariy alisema: Mtume s.a.w. alisema: “mmoja wenu anapomuingilia mkewe halafu akataka tena (jimai) basi atie udhu”.

Na katika Hadithi ya Ibn Khuzaima, Ibn Haban na Alhakem: “basi atawadhe kwani udhu unachangamsha wakati wa kurejea”.

Anayeangalia maneno yake: “kwani udhu unachangamsha wakati wa kurejea” yanamaanisha sababu pamoja na kusifu yanayosaidia kumhimiza mtu arudi tena na hiyo ni dalili juu ya uhalali wa kila yaliyopita pamoja na uhalali wa vitu vinavyosaidia katika hayo kama mazoezi, chakula, vinywaji au dawa.

Na Mtume S.A.W. baadhi ya wakati alikuwa akisidisha jimai kama ilivyotajwa katika Sahihi mbili “kutoka kwa Anas R.A. ya kwamba: Mtume S.A.W. alikuwa anazunguka kwa wake zake katika usiku mmoja, hali ya kuwa ana wake tisa”.

Imamu Al Ghazaly katika maelezo yake juu ya manufaa ya ndoa alisema: “faida ya tatu ni kutuliza nafsi pamoja na kupata furaha ya kukaa, kuangalia na kucheza na mke ambapo moyo unapata utulivu pamoja na kuimarika ibada, kwani nafsi inachoka haraka, aidha inataka daima kuwa mbali na haki; na kwa kuwa ni tofauti ya tabia yake basi ikilazimishwa itaenda mbali zaidi na ikionja ladha kwa muda mfupi itaimarika, licha ya kuwa kukaa na mke kunasaidia kuiondoa shida na kunaleta utulivu wa moyo. Hali kadhalika, nafsi za wacha Mugu lazima zipate raha za mubaha, Mwenyezi Mungu Amesema: {(Ili kila mwanamume) apate utulivu kwake(mkewe)}, aidha Aly R.A. alisema: ipumzishemi mioyo saa; kwani ikilazimishwa itaenda mbali”[Ihiya’ Ulum Al Din, 2/30, Ch. Dar Al Maarifa].

Kadhalika inaruhusika kwa mwanamke kufanya hivyo kwa sharti zilizotajwa; maana ana haki ya kufurahia mubaha, aidha ana haki ya kuingiliana na mume wake kama walivyosema wanachuoni wengi, na kwa yaliyotajwa katika Hadithi ya Mtume S.A.W.” Mke wako ana haki juu yako” yanafahamika kuwa ndoa inasaidia kukidhi haja [Rejea: Ibn Qudama, Al-Mughniy, 7/307 & Ibn Taimiya, Maj-mu’ Al Fatawa, 28/383, Maj-ma’ Al Malik Fahd].

Kutokana na yaliyopita; kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kabla ya kuingiliana na mke ni jambo ambalo asili yake mubaha (ruhusa) likiwa halisababishi madhara, kwa hiyo lazima kupata ushauri wa wataalamu wa tiba waliohusika kabla ya kuanza kutumia dawa hizo; kwani zinaweza kusababisha baadhi ya madhara kwa baadhi ya watu kwa sababu ya umri, maradhi au kitu chochote ambacho kinazuia kuzitumia dawa hizo za kuongeza mguvu za kiume, aidha inapendeza kwa yule ambaye hana kizuizi kuzitumia atie nia safi moyoni ili apate ujira kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya yaliyo mubaha. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas