Kufuata Madhehebu Manne ya Kifiqhi ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kufuata Madhehebu Manne ya Kifiqhi Na Hukumu ya Kuacha Kuyafuata

Question

Nini hukumu ya kufuata madhehebu ya wanachuoni wanaojitahidi wasiokuwa maimamu wanne mashuhuri ambao ni Abu Hanifa, Malik, Shafii, na Ahmad radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao katika fatwa na utekelezaji wake? Na nini hukumu ya kuacha kufuata tu, na kulingania kwa fiqhi ya dalili?

Answer

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfua, na baada ya hayo:
Madhehebu ya fiqhi manne nayo ni Hanafiya, Malikiya, Shafiiya, na Hanbaliya kwa hakika yamepata nafasi kubwa zaidi kuliko madhehebu mengine, madhehebu haya manne yanashika usukani katika kufuatwa, uandishi, kuboreshwa, uhakiki, upambanuzi, na uainishi na mengineo kiasi ambacho madhehebu mengine ya maimamu wanaojitahidi hayajafikia katika nafasi kama hiyo. Wanachuoni wamefikia kusema kwamba hukumu yoyote inayokwenda kinyume na madhehebu manne haikubaliki. Ibn Najm Al Hanafiy anasema: “Miongoni mwa mambo yasiyotekelezwa hukumu yake ni ile hukumu inayokwenda kinyume na Ijmaa (makubaliano ya wanachuoni wa madhehebu manne), na atakayeacha kuwafuata maimamu wanne inamaanisha ameacha Ijmaa – ijapokuwa kuna hitilafu kati ya wanachuoni. Na hakika imeelezwa wazi katika kitabu cha “Al-Tahriir” kwamba Ijmaa imekubaliana juu ya kutokufanyiwa kazi kwa madhehebu yoyote yanayotofautiana na madhehebu manne, kwa kuwa madhehebu manne yana udhibiti, yameenea sana na wafuasi wake ni wengi. [Al-Ashbaah wa Al-Nadhair, Uk.92, Ch. Dar Al-Kutub Al-Ilmiya].
Na kumtii Allah S.W na Mtume wake S.A.W ni haki iliyo wajibu kwa kila baleghe, mwenye akili na mwenye kuweza. Utekelezaji wa kutii unakuwepo kwanza juu ya kufahamu kilichoamrishwa na kilichokatazwa ili aliyeamrishwa kisheria aweze kutekeleza yaliyo sawa na yatakiwayo. Na ufahamu sahihi unaozingatiwa kisheria unarejea moja kwa moja katika vyanzo vya kisheria vya kiislamu kwa yule aliyefikia daraja ya juu ya kujitahidi (kufahamu fiqhi). Ama asiyeweza kujitahidi na hazijakamilika kwake sharti za jitihada ya kifiqhi na nyenzo zake, basi ni juu yake kumfuata mwingine miongoni mwa wenye elimu, wenye kutoa fatwa, na wanachuoni wenye kujitahidi, na wenye madhehebu ya kifiqhi yenye kufuatwa. Basi jitihada ya kifiqhi katika hali zote ni kiunganishi cha lazima, ni elementi muhimu katika kuzijua hukumu za sheria ya kiislamu, nayo ni fardhi kifaya (kutoshelezena) kwa kuwa waislamu wote wangekalifishwa kuziangalia dalili, kuzifuatilia, kupata uhakika ndani yake, yale yanayokwenda kinyume nazo, na kuondoa yanayopingana nayo kama wafanyavyo wanavyuoni wa fiqhi na wenye kujitahidi, basi ukalifishaji huu ungalikuwa ukalifishaji mzito, na maisha hayawezi kuendelea kwa ukalifishaji huo unapelekea kuzoroteka kwa kazi na uzalishaji, kuvuruga maslahi ya watu na mahusiano yao ya kijamii na mambo yote yanayohusu maisha yao. Na bahari za elimu na jitihada ya kifiqhi ni pana na zenye kina kirefu zisizo na mipaka wala mwisho. Kwa hivyo kuna kauli maarufu zilizoenea kati ya wanachuoni na wanafunzi wao. Miongoni mwa kauli hizo; “ Kwamba elimu haikupi sehemu yake isipokuwa mpaka wewe uipe nafasi yako yote”, na kauli “ Na utumie kalamu mpaka kufa”. Kwa hivyo kubobea katika elimu ya kujitahidi kifiqhi uzito wake ni sawa sawa na kubobea katika elimu za tiba, uhandisi, viwanda, kilimo, biashara, uchumi na nyanja nyingine muhimu zisizokuwa hizo ambazo zinafungamana sana na misingi mikuu mitano, nayo ni: kulinda nafsi, akili, dini, kizazi, na mali. Na kubobea katika jitihada ya kifiqhi ni miongoni mwa sababu za kuilinda dini.
Haingii akilini kisheria wala kimaumbile kuwalazimisha watu baleghe wote wabobee katika nyanja hizi zote kwa ajili ya kuitikia wito wa mahitaji yao ya nyanja hizo. La sivyo ukalifishaji huu utakuwa hautekelezeki. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:{Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila yaliyo sawa na uweza wake} [AL BAQARAH 286]. Na kwa sababu hii imekuwa wajibu kwa baadhi ya waislamu na watu maalumu hasa wanachuoni na watu wa fiqhi kujitahidi katika kutoa fatwa. Ama wengine (watu wa kawaida) wanawajibika kuuliza kwa ajili ya kupata fatwa na kufuata tu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Basi waulizeni wenye kumbukumbu (wanachuoni wa vitabu vya mbinguni) ikiwa nyinyi hamjui} [AN NAHL 43]. Na vilevile Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Wala haiwapasii waislamu kutoka wote (katika miji yao wakaja Madina wakaiwacha miji yao mitupu). Lakini kwa nini halitoki kundi tu katika kila taifa miongoni mwao kujielimisha vyema dini na (kisha wakaja) kuwaonya wenziwao watakapowarudia, ili wapate kujihadharisha (na wao na mabaya)}. [AL TAWBA 122]. Na katika hadithi tukufu kutoka kwa Jabir amesema: "Tulitoka katika safari basi mmoja wetu akapigwa na jiwe likamjeruhi kichwa chake kisha akapatwa na janaba usingizi, akawauliza wenzake akasema: je, mnaona ninaruhusiwa kutayammamu? Wakasema: Hatuoni kwamba wewe unaruhusiwa kutayammamu wakati una uwezo wa kutumia maji, basi yule mtu akaoga na akafa". Tulipomwendea Mtume S.A.W. akaambiwa jambo hilo akasema: “Wamemuua huyo, na wao Mwenyezi Mungu Mtukufu awaue, kwa nini wasiulize kama hawajui? Hakika dawa ya ujinga ni kuuliza”. [Imepokelewa na Abu Dawud]. Hadithi imeonesha kwamba asiyeweza kufahamu kwa nafsi yake hukumu ya sheria ni wajibu juu yake kuuliza wenye ujuzi na waliobobea.
Imamu Abu Bakar Al Jasas amesema katika kitabu chake [Al-Fusul Fil Usuul, Ju.4, Ku. 281-282, Ch.Wizarat Al-Awkaaf Alkuwaytiya]: “Mtu wa kawaida asiyejua hukumu za kisheria akitiwa mtihani katika msiba fulani ni juu yake kuwauliza wenye ujuzi, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu {Basi waulizeni wenye kumbukumbu (wanachuoni wa vitabu vya mbinguni) ikiwa nyinyi hamjui} [AN NAHL 43], na kauli yake {kwa nini halitoki kundi tu katika kila taifa miongoni mwao kujielimisha vyema dini na (kisha wakaja) kuwaonya wenziwao watakapowarudia, ili wapate kujihadharisha (na wao na mabaya)}. [AL TAWBA 122]. Basi Allah S.W. amemuamrisha asiyejua akubali kauli ya mwenye ujuzi wa elimu ya sheria wanapopatwa na misiba. Na kwa ajili hiyo umma umejilazimisha tangu mwanzo wa uislamu, masahaba kisha Taabiyn na mpaka hivi sasa kufuata utaratibu huo. Na watu wa kawaida wanapopatwa na jambo la dini yao yapaswa kuwakimbilia wanachuoni wao. Na inaonesha pia kwamba mtu wa kawaida haiepukani na mtihani wa matukio na awe mwenye kuamrishwa kupuuzia jambo lake, kuacha kuuliza na kuacha jambo lake kama lilivyo kabla ya kutokea, hapana ajifunze mpaka afikie uwezo wa kujitahidi, kisha apite kama inavyopelekea jitihada zake, au amuulize mwingine miongoni mwa wenye ujuzi, kisha aifanyie kazi fatwa yake na ni lazima ikubaliwe fatwa yake. Na haifai kwa asiyejua kupuuzia jambo lililotokea wala kulipa mgongo na kuliacha jambo kama ilivyokuwa kabla ya kutokea, kwani yeye ni mwenye kulazimishwa kulifanyia kazi kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu iliyothabiti kwa matini na kwa dalili. Na kwa kuwa yeye hafahamu uwajibu wa kuacha kwake namna kabla ya kutokea kwake ni kwa sababu ya tofauti za wenye ujuzi. Na kwamba huelekezwa katika kuujua ukweli wake kwa upande wa kulitizama na kutafuta dalili zake na sio ufahamu huu uwe kwa watu wasiojua. Na haijuzu pia kusemwa: ni juu yake ajifunze misingi muhimu na kujitahidi kutoa fatwa na vipimo mpaka afikie kuwa na uwezo wa kugundua dalili mpya kwa kuwa kufanya hivyo hana uwezo nao, na huenda umri wake ukaisha kabla ya kufikia hali hiyo. Na inaweza kuwa mwenye kupata mtihani ni mvulana katika hali ya mwanzo ya kubaleghe kwake, au ni mwanamke aliyeiona damu akatia shaka kwamba ni hedhi au si hedhi, hapo watu hao wawili lazima waulize wanachuoni na ni wajibu wakubali hukumu zao”.
Na wala si wajibu kwa watu wa kawaida kumfuata imamu maalumu wala kujilazimisha na madhehebu yake katika kila matawi yote ya kifiqhi katika kauli iliyo sahihi miongoni mwa kauli za wenye elimu, kama alivyoipitisha kauli hii Annawawey na akasahihisha mwanachuoni Azzarkashey na wengineo kama walivyopita wanachuoni wakubwa. Basi hapana ubaya kumfuata mmoja wa maimamu wanne. Imamu Izzi Al-Dini Ibn Abdusalaam amesema katika kitabu chake “Fatawi”: Inajuzu kumfuata kila mmoja miongoni mwa maimamu wanne radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao. Na inajuzu kwa kila mmoja kumfuata mmoja miongoni mwao katika suala fulani na kumfuata imamu mwengine katika suala jingine. Na wala asichague kufuata mmoja peke yake katika masuala yote. Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi, mwenye hekima, mpole zaidi na mweye rehma zaidi. [Uk. 122, Ch. Dar Al-Maarifa, Beruti].
Mwanachuoni mkubwa Al-Zarkashey alisema katika kitabu chake [Al Bahr Al Muhiit, Ju.8, Ku.374-375, Ch. Dar Al Kutubi]: “Swali: Inajuzu kwa mtu wa kawaida kujilazimisha kumuainisha mmoja katika kumfuata katika kila tukio? Kuna maoni mawili, Alkiya alisema: inamlazimu. Ibn Burhaan alisema: Hapana. Na Annawawey ameunga mkono hilo la mwisho katika kitabu chake [Awail Alkadhaa], nalo ni sahihi. Hakika maswahaba radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao hawakukanusha juu ya watu wengi wa kawaida kuwafuata baadhi yao bila ya masharti. Katika zama za Imamu Malik baadhi ya makhalifa walitaka kuwabeba watu katika maoni ya madhehebu ya Malik basi Imamu Malik akawakataza na akatoa hoja kwamba Mwenyezi Mungu ameieneza elimu katika miji kwa kuwaeneza wanachuoni, kwahiyo hakuona haja ya kuwalazimisha watu kumfuata yeye tu. Ama kuhusu kauli mashuhuri “Hafutu yoyote ilhali Imamu Malik yupo ndani ya mji”. Ibn Al-Munir alisema kuhusu kauli hiyo: mimi nafahamu hivi: asifutu mtu yoyote mpaka Imamu Malik amshuhudie mtu huyo kuwa ana uwezo wa kutoa fatwa. Baadhi ya wafuasi wa Hanbily wakaeleza kuwa hayo ni madhehebu ya Imamu Ahmad, wakati aliposema kuwaambia baadhi ya wafuasi wake: Usiwalazimishe kufuata madhehebu yako watapata taabu, waache watafute ruhusa katika madhehebu mengine. Na akulizwa kuhusu kesi ya talaka akasema: bila shaka inatokea, basi muulizaji akamuuliza: Ikiwa kuna mwanachuoni mwingine atamjibu kwa kutotokea, inajuzu kumfuata? Akasema: ndiyo na akamjulisha kikundi maalumu katika mji wa Rusafa. Akamuuliza: Wakinijibu, inajuzu? Akasema : Ndiyo. Watu wa zamani walikuwa wakiwaiga wanaowataka kabla ya kudhihiri madhehebu manne. Na Mtume S.A.W. amesema: “Mwenyezi Mungu Mtukufu anapenda zichukuliwe ruhusa zake kama anavyopenda zichukuliwe faradhi zake”. Na Al Rafii ameeleza kutoka kwa Abi Al Fathi Al Harawey mmoja wa wafuasi wa Imamu Ahmad, amesema kwamba mwenendo wa wafuasi wetu wengi wanakubaliana kuwa mtu wa kawaida hana madhehebu maalumu”.
Ibn Aabidiin alisema katika maelezo ya kitabu chake [Rad Al Muhtaar, Ju. 4, Uk. 80, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]: “Hatakiwi mtu wa kawaida kufuata madhehebu kwa kuwa kuna kauli mashuhuri; mtu wa kawaida hana madhehebu maalumu, lakini madhehebu yake ni madhehebu ya mufti wake. Na Ibn Aabidiin akatolea sababu katika maelezo ya kitabu chake [Al-Tahrir] ya kwamba kufuata madhehebu inamhusu mtu mwenye aina fulani ya ujuzi, na mwenye mwono maalumu katika madhehebu yenyewe, au kwa mtu aliyesoma sehemu makhsusi katika kitabu kinachofungamana na tawi maalumu katika madhehebu hayo, na ameelewa fatwa na kauli za Imamu wake. Ama wengine waliosema: Mimi ni Hanafiy au Shafiiy hawezi kuwa hivyo kwa maneno tu, kama kauli yake mimi ni mwanafiqhi au mwanasarufi. Na maelezo kamili ya hayo yametangulia katika utangulizi wa ufafanuzi huu. Na imenukuliwa mwanzo wa ufafanuzi wa Al Sharnablali kauli yake [Ju.1, Uk. 75]: Kisha akasema baada ya kutaja maelezo marefu ya matawi ya madhehebu: kwamba inajuzu kutofuata madhehebu maalumu. Na kwa mujibu huo si wajibu kwa mtu kufuata madhehebu fulani na inajuzu kwake kutenda yale yanayopinga madhehebu yake. Bali inajuzu kuyafanyia kazi mambo mawili yenye kupingana katika matukio mawili ambalo moja halina uhusiano na lingine, na hata hawajibiki kubatilisha kazi aliyoifanya kwa kumwiga imamu mwingine kwa kuwa kupitisha kitendo ni kama kupitisha maamuzi ya kadhi (jaji) hayatenguki. Na alisema pia: Ana haki ya kuiga baada ya kutenda; kwa mfano kama anasali akidhani sala hii ni sahihi katika madhehebu yake kisha akaelewa baadaye ni batili katika madhehebu yake, lakini sala hii ni sahihi katika madhehebu mengine basi mtu huyu ana haki ya kuyaiga na anaweza kutosheka kwa iliyotajwa katika Al Bazaziyah: ya kuwa imepokelewa kutoka kwa imamu Abu Yusuf ya kwamba alisali Ijumaa akiwa ameoga akitumia maji ya kisima kisha akaambiwa kuna panya amekufa ndani ya kisima hicho akasema: katika hali kama hiyo tunaweza kuchukua kauli ya madhehebu ya ndugu zetu miongoni mwa watu wa Madinah: Maji yanapofika kipimo cha Kulla mbili hayabebi uchafu (siyo najisi).
Na pia kauli iliyo sahihi ni kwamba haijuzu kwa watu wa kawaida kufuata ruhusa za wenye kujitahidi na kuchukua kauli nyepesi kutoka kila dhehebu katika hali ya kukusudia kuchezea, kudanganya na kutaka kujiepusha na hukumu za kisheria.
Na wanachuoni wametofautiana katika kitendo hicho na ni kwa nani sifa zake, katika kauli zifuatazo:
Kauli ya kwanza Inaharamishwa, na ni muovu mwenye kufanya hivyo. Na kauli hii ameisema Abu Hanifa, Malik, Hanbal na madhehebu ya Imamu Shafi.
Isipokuwa wao yaani Shafi wamesema. Ikiwa kuhama kwake kwenda madhehebu miongoni mwa madhehebu yaliyosajiliwa basi katika hali hii si muovu. Shihab Ramliy ameweka shartii nalo ikiwa kutii kwake kumeyashinda maasi.
Na ikiwa kahama kwenda katika madhehebu yasiyosajiliwa na ikawa katika zama za mwanzo yaani Maswahaba, basi hawi muovu. [Rejea: Rad Al Muhtaar 5/481, na Al Fawakh Al Dawany2/356, Ch. Dar Al Fikr, na Tuhfat Al Muhtaaj 10/112, Ch. Dar Ihyaa Al Turaath Al Arabiy, na Asna Al Mataalib kilichofuatwa na maelezo ya Al Ramly 4/286, Ch. Dar Al Kitaab Al Islaami, na Fatawa Al Ramly 4/378, na Al-Insaaf 12/50, Ch. Dar Ihyaa Al Turaath Al Arabiy].
Makubaliano juu ya jambo hili amechukua zaidi ya mtu mmoja. Na miongoni mwa waliyechukua makubaliano juu ya uovu kwa mwenye kufuata ruhusa kwa matamanio ni Ibn Abdul-Bar na Annafrawy. [Rejea: Jaami Bayaan Al Ilm wa Fadlihi 2/927, Ch. Dar Ibn Al Jawzi, na Al Fawakh Al Dawany 2/356].
Wametoa ushahidi juu ya hilo kwamba haiwi kwa yoyote aamini kitu kilicho wajibu au haramu kisha aamini si wajibu na wala si haramu kwa matamanio yake tu, na haya ni maelezo yake Imamu Ahmad kama alivyotaja Ibn Taimiyah. [Alfatawa Alkubrah 20/220-221]. Kama ilivyo sisi lau tungesema kujuzu kuhama kwa matamanio kwa kuzingatia kwamba yeye amechukua kauli ya baadhi ya wenye kujitahidi ingekuwa kuzuia ni bora.
Ni kwa sababu nafsi inamili kuelekea wito wa raha na kukimbia tabu na majukumu, na hivyo inapelekea kukimbia utekelezaji wa hukumu za sheria mara nyingi. Basi ikawa ni wajibu kumzuia ili kufunga mlango unaopelekea ufisadi.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amekemea kufuata na kushibisha matamanio ya nafsi. Allah S.W amesema: {Hawafuati ila dhana na zinazoyapenda nafsi} [AN NAJM 23]. Na kufuata ruhusa pasina haja au dalili inazingatiwa ni kufuata matamanio yanayopelekea kwenye uovu. Na haya ni maelezo yake Ashatwibiy aliyoyabainisha kwamba hivyo inapelekea "kudharau dini kwa kuwa mazingatio haya ni mfano wa mafuriko yasiyoweza kudhibitika, kwa hivyo nafsi haziwezi kuzuilika na matamanio na wala nafsi hazitokuwa na kikomo" [Al-Muwafaqaat 5/102, Ch. Dar Ibn Afaan]. Aidha kuhama kutoka madhehebu kwenda mengine ni matamanio huenda ikapelekea kauli ya kulinganisha madhehebu kwa njia isiyo sahihi na hivyo kupelekea kuharibu (Ijmaa) Makubaliano ya wanachuoni. [Al Muwafaqaat 5/103].
Na inawezekana kutoa dalili kwa yule aliyesema kwamba hawi muovu akihama kutumia rai miongoni mwa rai za Maswahaba hakika Maswahaba sio kama watu wengine, kwa kuwa wao wana fadhila na uwezo mkubwa usiopatikana kwa wengine, wamemshuhudia Mtume S.A.W. wakaishi katika wahyi na kushushwa Quraani pasina kizuizi baina yao na mjumbe wa Mwenyezi Mungu rehma na amani ziwe juu yake. Ibn Al Qayim anasema akinakili kutoka kwa Shafiy: "Na wao wapo juu yetu kwa kila elimu, jitihada, kumcha Allah, akili, wameipata elimu na kutoa hukumu katika vyanzo vya kisheria. Na rai zao kwetu sisi ni tukufu na bora kwetu kuliko rai zetu mbele ya nafsi zetu" [Iilaam Al Muwaqiiyn 2/150, Ch. Dar Ibn Al Jawzi]. Mtume S.A.W. aliwaombea baadhi yao wapate elimu na uwezo mkubwa wa kuhifadhi na ufahamu.
Na Allah S.W amewatukuza na kiujumla katika Quraani ametuamrisha kuwafuata, na hii ndio inayotupa uaminifu katika kauli zao za hukumu japo zikitofautiana rai zao, na ndio huwa halali kwetu kuchukua moja miongoni mwa hukumu wakati fulani na kuchukua hukumu nyingine wakati mwingine.
Kauli ya pili: Hawi muovu kamwe japo akihama kwa matamanio na kuzifuata ruhusa, nayo ni kauli ya baadhi ya wanachuoni wa madhehebu ya Hanafiy, na kauli hii pia ameisema Ibn Abdu Assalaam na Ibn Abi Huraira miongoni mwa wafuasi wa Shafiy, na Ahmad katika moja ya riwaya mbili aliyenukuu kujuzu kuzifuata ruhusa. Nayo ni lazima kwa madhehebu ya Omar Ibn Abdul-Aziz kiasi cha kujuzisha kuchukua akitakacho katika tofauti za wanachuoni, na akaashiria kwamba tofauti hizo ni neema. Na hii pia ni kauli ya Kasim Ibn Mohammad na Sufian Thauriy. [Fathi Al Kadiir 7/258 na Faidh Al Kadiir 1/209, na Jamii Bayaan Al Ilmi 2/898, na Al Tahbiir 8/4091-4093, na Sharh Al Kawkab Al Muniir 4/578, na Sharh Al Jalaal katika maelezo ya Al Attaar 2/441].
Wakatoa dalili za hadithi, miongoni mwa hizo kauli yake Mtume S.A.W. "Maswahaba wangu ni kama nyota yoyote mtakaemfuata mmeongoka", Na ushahidi hapa ni kwamba kuna uwezekano wa kuchagua miongoni mwa kauli za wanachuoni kwa kuchagua kauli za maswahaba radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao.
Na kutoka kwa Aisha radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: Na alikuwa anapenda waliyofanyiwa urahisi, maana yake Mtume S.A.W. alikuwa anapenda waliyofanyiwa wepesi umma wake. Na Mtume s.a.w ametumwa kwa upole na msamaha, basi hakatazwi yoyote kufuata na kuchukua ruhusa muda wa kuwa katika kuchukua ruhusa ni sehemu ya wepesi kwake.
Na amesema Mtume S.A.W. "Hakika Mwenyezi Mungu anapenda ichukuliwe ruhusa yake kama anavyopenda zichukuliwe faradhi zake" (Imepokewa na Ahmad).
Na ufahamu wa dalili ni kwamba kuchukua kilichokuwa ndani yake wepesi kunapendeza mbele ya Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kuchukua faradhi pia kunapendeza mbele yake.
Hivyo inaonesha kujuzu kuchukua ruhusa, kwa kuwa ni miongoni mwa wepesi ambao anaupenda Mwenyezi Mungu uchukuliwe.
Na kwa upande mwingine yaliyosemwa juu ya ulazima wa kukataza kuhama pasipo na sababu, hivyo ni kuwazuia watu kuzifuata ruhusa.
Yakiondoka makatazo (maana; watu wakiacha kufuata matamanio ya nafsi) hapo inajuzu kufuata ruhusa.
Kama walivyozoea watu tangu zama za Maswahaba mpaka yalipodhihiri madhehebu walikuwa wakiwauliza wanachuoni wenye maoni tofauti pasina kuwakataza. Ni sawa walikuwa wakiuliza kuhusu ruhusa au faradhi.
Al Shaatibiy anasema kwa kuyapa nguvu maoni hayo “Kwa kutumia kipimo cha kiasi: Mwenyezi Mungu ni Mkwasi na Mkarimu, na mwanadamu ni mweye kuhitajia, na ukitokea mgongano baina ya pande mbili, basi kuchukua upande wa Mkwasi ni bora zaidi”. [Al Muwafaqaat, 5/104-105].
Na iliyo sahihi kutokana na kauli mbili hizi kuna ufafanuzi ufuatao: Nayo ni kuwa mwenye kuhama kutoka madhehebu kwenda mengine au kutoka kauli ya mwenye kujitahidi (katika fiqhi) kwenda mwenye kujitahidi mwingine kwa matamanio sio kwa sababu ya kisheria hawi muovu kwa sharti asiwe mwenye kuhama mwanachuoni, na hivyo ni kwa makubaliano ya wanachuoni wa Ussul Al fiqhi, kuwa mwenye kujitahidi akijitahidi na dhana yake ikawa kubwa katika hukumu maalumu haijuzu kumfuata mwingine (Miongoni mwa wanachuoni). Maana yake haijuzu kwake kuhama. [Al Mustaswfa 368, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah, na Al Ihkaam , Lil Aamidiy 4/204, Ch. Al Maktab Al Islaamey, na Kawaatwi Al Adilla, Libn Al-Samaani 2/341, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]. Ama kwa asiye kuwa mwenye kujitahidi (katika fiqhi), watu wamesema kuwa inajuzu na wengine wakasema haijuzu. Al Ghazaliy anasema katika kitabu chake [Mustasfa, Uk. 369] baada ya kutaja tofauti za wanachuoni anasema asiye kuwa mwenye kujitahidi "Hukumu yake ni kuishinda dhana"; maana anaweza kuhama au kutokuhama. Kwa maana kuwa sisi tungesema kujuzu kuhama lingekuwa jambo hilo ni karibu zaidi.
Na tunachoona ni kwamba kuweka kiziwizi na kikomo katika madhehebu manne katika kutoa fatwa na hukumu hakuko katika kila zama au hali, lakini jambo hili litakuwa chini ya amri ya mweye mamlaka, mila na yale wanayoyaridhia watu katika kuhukumiana kwao na kurejelea maswala ya kidini na matatizo yao ya kimaisha. Msingi ni kwamba kila mwenye kujitahidi (katika mambo ya fiqhi) inajuzu kumuiga sawasawa akiwa ni miongoni mwa Masahaba watukufu au Tabiina au maimamu wanne au wengineo, kwa sharti la kuwa yule muigaji awe amepata maarifa ya hukumu za kisheria kwa kusikia moja kwa moja au kupitia watu wakweli waliohifadhi kwake.
Ni wazi kuwa – Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi – kwamba haja ya watu ni kuwepo nidhamu kwenye suala la hukumu na kuziba milango ya kuchezea na ushawishi wa jaji katika kuchagua madhehebu fulani yatakayo kuwa na maslahi kwa upande mmoja wa mgogoro. Hiyo ndiyo iliyokuwa sababu ya msingi ya kushurutishwa Kadhi asiekuwa mwenye kujitahidi kufuata madhehebu maalumu miongoni mwa madhehebu manne yanayofuatwa na yenye kuaminiwa pasina madhehebu mengine ya wenye kujitahidi ambayo wafuasi wake waliyahama. Na kama si hivyo, laiti kama milango ingeachwa wazi kwa kuchagua kiholela kila rai anayoiona Imamu mwenye kujitahidi basi kungeingiwa na shaka na tuhuma kwenye hukumu inayotolewa na kadhi, ugomvi usingeamuliwa wala mambo ya watu yasingetulia, kwa ajili hiyo madhehebu manne yaliyoridhiwa na jamhuri ya waislamu yakawa ndiyo kama mpatanishi wa kila ugomvi.
Pia suala la fatwa, lilipokuwa linahusiana na masuala ya umma na yanaoneshwa katika kundi la umma, na mahitaji ya watu wote ni kuchukua katika dini yao madhehebu ya wanachuoni yaliyoandikwa na yanayotumika na ambayo yamepata bahati ya kutiliwa umuhimu na wanachuoni na wanafunzi, madhehebu manne ndiyo yaliyokuwa mfano wa karibu katika kufikia mahitaji hayo. Madhehebu manne yalianzishiwa vyuo na yakaandikiwa vitabu katika matawi, misingi, kanuni, tafsiri na matabaka, wafuasi wake wakashiriki katika elimu mbalimbali za kiislamu na wakaongoza kuwafundisha watu na kuwaelimisha dini. Kwa sifa hizo ndiyo yakawa chanzo cha imani katika dini, fatwa, na hukumu katika mambo ya watu kwa jumla na mambo maalumu.
Lakini pamoja na yote hayo hakuna dalili yoyote ya kisheria inayowawajibisha watu kufuata haya madhehebu manne hasa katika fatwa, hukumu, au kuyalazimisha kwa nguvu kwa umma na mataifa ya kiislamu, kwa kuwa kanuni ya msingi ni kumfuata kila Imamu mwenye kujitahidi, na katika kutofautiana maimamu kuna fursa na rehma. Panapo kuwa maslahi yenye nguvu au mashaka yanayotakiwa kuondolewa, na linathibiti hilo kwa kutegemea rai ya kifiqhi iliyothibiti na kunasibishwa kwa Imamu mwenye kujitahidi asiekuwa miongoni mwa maimamu wanne wakati huo hakuna kizuwizi cha kuchukua rai hiyo sawasawa ikiwa katika hukumu au fatwa au katika kazi za watu za kila siku. Amesema Sheikh Al Nafarawiy Al Maalikiy katika [Al Fawakiha Al Diwaniy 1/24 Ch. Dar Al Fikr) kwa ujumla ni kwamba yafaa kuamini kuwa wenye kujitahidi wote wapo katika muongozo hata wale waliohamwa katika madhehebu yao, na kujizuia kuwaiga wasiokuwa maimamu wanne ni kwa sababu ya kutohifadhi madhehebu yao, si kunyume na kwamba wote wapo katika kheri na muongozo wa Mwenyezi Mungu na hawapo katika upotovu wa bidaa.
Akasema pia Al Nafarawiy [Al Fawakiha Al Diwaniy 2/356] : “Leo yamepitishwa makubaliano ya waislamu kwamba ni wajibu kumfuata mmoja wa maimamu wanne : Abu Hanifah, Maalik, Shaafii na Ahmad Ibn Hanbal (R.A), na haijuzu kwenda kinyume na madhehebu yao, na hakika imeharamishwa kuwaiga wasiokuwa hao wanne miongoni mwa wenye kujitahidi, japo kuwa kwamba wote wapo katika muongozo lakini ni kutokana na kutohifadhiwa madhehebu yao kwa kufariki watu wake au kutoandikwa”.
Baadhi ya wahakiki wamesema: kauli iliyopitishwa ni kwamba inafaa kuwaiga maimamu wanne, na pia wasio kuwa wao miongoni mwa wanaohifadhiwa madhehebu yao katika maswala hayo na yakaandikwa mpaka yakafahamika masharti yake na mazingatio mengine. Makubaliano yaliyonukuliwa na zaidi ya mmoja kama vile Ibnu Salaah, Imamu Al Haramain na Al Qarrafiy ni kuzuia kumuiga Swahaba kwa kile kilicho kosa sharti katika hayo.
Sheikh Alawiy Ibn Ahmad Al Saqaaf anasema katika [Al Fawaid Al Makkiyah, uk.50]: Madhehebu yanayofuatwa si madhehebu manne tu , bali kuna kundi la wanachuoni madhehebu yao yanayofuatwa pia, kama vile Al Safyaniin, Is-haak Ibn Rahawayhi, Dawud Al Dhaahiry na Al Auzaiyy. Licha ya hayo, kundi la wanachuoni wetu wamesema haifai kuwaiga wasiokuwa maimamu wanne. Dalili yao ni kutokuwa na imani na yale yaliyonasibishwa kwa wenyewe kwa kutokuwepo misingi au Sanadi (mtiririko wa wapokezi) zinazozuia kupotosha au kubadili tofauti na madhehebu manne , hakika maimamu wake walitoa nafsi zao katika kuandika kauli na kubainisha kilichothibiti kwa msemaji wake na kile ambacho hakikuthibiti, watu wake wakaweka usalama wa kila mabadiliko na upotoshaji, wakafahamu sahihi na dhaifu, kwa ajili hiyo amesema zaidi ya mmoja kuhusu Imamu Zaydi Ibn Ally: hakika ni Imamu mwenye heshima na mwenye utambuzi wa juu, na hakika imani ya madhehebu yake iliondoka kutokana na wafuasi wake kutotilia umuhimu wa Sanadi ,madhehebu yake hayakuwa salama, kupotoshwa, kubadilishwa na kunasibshwa na yale asiyoyasema. Madhehebu manne hivi sasa ndiyo mashuhuri na yanafuatwa. Na kila Imamu miongoni mwao alikuwa maarufu katika kundi miongoni mwa makundi ya kiislamu, kiasi ambacho muulizaji hahitaji ufafanuzi wala hakuna tatizo kumuiga asiyekuwa Imamu wa madhehebu yake katika maswala ya upande mmoja, sawa sawa ikiwa kumuiga kwake ni kwa mmoja wa maimamu wanne au wengineo waliohifadhiwa madhehebu yao katika maswala hayo na yakaandikwa mpaka yakafahamika masharti yake na mazingatio mengine, makubaliano yaliyonukuliwa na zaidi ya mmoja juu ya kuzuia kumuiga Swahaba inachukuliwa kwa yale ambayo haikufahamika kunasibishwa kwake miongoni mwa wanaofaa kuwaiga au imefahamika lakini baadhi ya masharti yake hayajulikani.
Inaongezwa katika yaliyopita kuwa, Mufti na Kadhi wanaweza kuwa ni wenye kujitahidi moja kwa moja, wana haki ya kuacha kufuat madhehebu manne ikiwa kama jitihada yake itampelekea kufanya hivyo. Na anaweza kuwa mwenye kujitahidi ambaye jitihada yake imewafikiana na jitihada ya Imamu aliyepita mwenye madhehebu akajinasibisha kwake pia hiyo inafaa. Na anaweza kuwa mwenye kujitahidi katika madhehebu ya Imamu maalumu na akaweza kutohoa juu ya misingi ya Imamu wake. Pia anaweza kwenda kinyume ikiwa kama atazama zaidi katika kufahamu madhehebu ya mwengine na dalili zake mpaka yakawa yana nguvu kuliko fatwa za madhehebu yake. Mufti anaweza kuwa mwenye kujitahidi kwe fatwa yaani mwenye uwezo wa kulinganisha kati ya kauli na aina tofauti katika madhehebu ya Imamu wake, anaweza kumuonesha au kumueleza muulizaji kauli yenye nguvu katika madhehebu yake, na kumuonesha rai za madhehebu mengine yenye kuaminiwa kwa kuyanasibisha kwa watu wake bila kumlazimisha muulizaji kufuata madhehebu maalumu. Pia Mufti anaweza kunukuu madhehebu ya Imamu mwenye kujitahidi madamu amefahamu ukweli wa madhehebu yasiyo ya Imamu wake, na anatakikana kumuelezea muulizaji baada ya kumuulezea madhehebu yake.
Na kutokana na yaliyopita: Mwenye kujitahidi na akaacha kuiga na kuwa mfuasi tu ni jambo linalonahitajika kwa wanavyuoni. Ama mtu wa kawaida anatakiwa amuige mwenye kujitahidi miongoni mwa wanavyuoni wenye kujitahidi, na inajuzu kwenda kinyume na madhehebu manne katika fatwa na kazi ikiwa kama kiongozi hajamshurutisha mufti kufuata madhehebu maalumu katika kutoa fatwa. Na lazima afahamu uhakika wa madhehebu anayoyatumia katika fatwa na kuthibitisha kunasibishwa kwake na mwenye madhehebu miongoni mwa maimamu wenye kujitahidi, kwa sharti la kutotokea uharibifu au usumbufu katika jamii.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Mjuzi zaidi ya wote.
 

Share this:

Related Fatwas