Zaka Ya Vito Vya Thamani
Question
Ninamiliki vito kama almasi, yakuti na zumaridi. Je, ninawajibika kuvitolea zaka au hapana?
Answer
Alhamdulilahi, na sala na salamu ziwe juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, ukoo wake, masahaba wake na wafuasi wake. Baada ya utangulizi huo.
Vito ni kila aina ya jiwe lenye thamani ambalo huwa na manufaa kwa mwanadamu [Lisan Al Rab, Ibn Manzour 4/152, Ch. Dar Sader, 6/238].
Na vito vya thamani ni kila aina ya madini na vito vya mawe yenye thamani ambavyo huwa na thamani na manufaa kwa watu wote.
Na vito vya thamani vimegawanyika sehemu mbili, moja: haramu kutumia wanaume kama dhahabu. Na pili ni halali kutumia wanawake kama vile fedha na dhahabu, ama vito kama yakuti, almasi na vito vya aina nyingine ni halali kutumia wanaume na wanawake. Sheikh Dardir anasema katika kitabu chake Al-Sharh Al-Saghir: ”Dhahabu na fedha zenye nakshi, ufinyanzi au kwa sura ya kifungo ni haramu kwa wanaume, na kwa hivyo utumiaji wa vito hivyo ni haramu kwa mwanamume aliebaleghe. Na kwa upande mwingine vito vya dhahabu na fedha haviharamishwi kwa watoto wadogo ambao bado hawajabaleghe na wanawake wote kwa ujumla. Pia vito kama yakuti, lulu na zumaridi ni halali kwa watu wote, wanaume na wanawake”. [Hashiyat Al Sawy Al Sharh Al Saghir 1/62 ch, Dar Al Maaref].
Kwa mujibu wa wanachuoni wa zamani, hakuna Zaka juu ya vito halali kama yakuti na vinginevyo. Imamu Malik katika Al Mowattaa amepokea kutoka kwa ibn Omar: “Hakika yeye aliwavalisha watoto wake wa kike na vijakazi wake dhahabu, na wala hakuvitolea Zaka vito vya dhahabu”. Na Ibn Al-Juwzy amepokea katika kitabu cha [Al-Tahqiq Fi Masael Al Khilaf” kutoka kwa Jabir kwamba Mtume S.A.W anasema :"Hakuna Zaka katika vito vya thamani". Na Abdulrazik amepokea kwamba Ibn Omar alisema: "Hakuna Zaka katika vito".
Na Malik amepokea kwamba: ”Bi Aisha R.A alikuwa akiwatunza wasichana mayatima wa ndugu yake katika nyumba yake na hatoi zaka ya vito vyao”, na AL-darqutny alipokea kutoka kwa Aly Ibn Sulaiman anasema: Nilimuuliza Anas ibn Malik juu ya vito, akasema: ”Havina Zaka”. Na Imamu Shafiy na Al-baihakiy walipokea kutoka kwa Abu Sufyan kutoka kwa Amru ibn Dinar alisema :”Nilimsikia ibn Khaled anamuuliza Jabir ibn Abdullah kuhusu zaka ya vito, Jabir akasema: Hakuna zaka juu yake, na akasema: Hata vikifikia dinari elfu moja? Jabir akasema: Vingi sana”. Na Al Darqutniy amepokea kutoka kwa Asmaa bint Abubakar kuwa aliwavalisha wasichana wake dhahabu, na hakuzitolea Zaka licha ya kukaribia elfu hamsini”. Ibn Abdulhady anasema katika kitabu chake [Al Tanqih]: Al-Athram anasema: Nilimsikia Aba Abdullah Ibn Hanbal akisema: "Watano miongoni mwa Masahaba waliona kuwa hakuna Zaka katika vito vya thamani kama dhahabu, na Masahaba hawa ni Anas Ibn Malik, Jabir, Ibn Omar, Aisha na Asmaa”.
Na kwa kuwa vito vinafananishwa na vitu vinavyotumiwa kwa ajili ya kujinufaisha kwavyo si kwa ajili ya mauzo, kwa hivyo si wajibu kuvitolea Zaka. [Bidayat Al Mujtahed wa Nehayat Al Muqtased 2/12, Ch, Dar Al Hadith].
Al-Dardiyr anasema katika kitabu cha [Al Sharh Al Kabeer]: Hakuna Zaka katika vito vinavyoruhusiwa kuvaliwa”. (Hashiyat Al-Desoqiy, Al Sharh, Al-Kabeer 1/460, Ch. Dar Al Fikr].
Na Al-bajiy anasema katika kitabu cha (Al-Muntaqiy) akifafanua hadithi ya Bi Aisha R.A: "Na kauli yake (Hakuna Zaka katika vito vyao), maana ya maneno haya ni kwamba Bi Aisha hakutoa Zaka katika vito, na hakuliacha jambo hilo la kutoa Zaka ila kwa sababu hakuona wajibu wa kutoa Zaka katika vito. Na dalili yetu ni kwamba vito hapa vinafanana na mavazi yanayotumiwa kwa kuyavaa, kwa hivyo hakuna Zaka juu yake. Na Al Bajiy anasema akifafanua kauli ya Athar Ibn Omar: Na kauli yake: (Kisha havitolewi zaka) inatokana na ilivyotajwa kwamba vito vinavyotumika kwa ajili ya kujinufaisha kwavyo havilipiwi Zaka. Na mtazamo huu ni wa masahaba wa Mtume S.A.W. akiwemo Bi Aisha mke wa Mtume S.A.W., na pia Abdullah ibn Omar ambaye ni ndugu wa Bi Hafsa mke wa Mtume S.A.W, na hukumu ya vito vyake haifichiki kwa Mtume S.A.W, na wala haifichiki kwa Bi Hafsa hukumu ya Zaka ya vito vyake”. (Al-Muntaqiy, Sharh Al Muwatta 2/107, Ch, Dar Al-Kitaab, Al-Islamiy).
Na Al Bahoty Al Hanbaly alisema: ”Hakuna Zaka katika vito vya thamani kama dhahabu na fedha vinavyotumiwa na wanaume na wanawake kwa ajili ya kujinufaisha kwavyo si kwa ajili ya biashara. Iwe ni kwa kutumia au kwa kuazima kwa wengine. Jabir amepokea kwamba Mtume S.A.W anasema: ”Hakuna Zaka katika vito”. Ameipokea Tabarany. Nayo ni kauli ya ibn Omar, Aisha na Asmaa bint Abubakar. Kwa sababu vito vinavyoandaliwa kwa ajili ya kutumiwa ni halali na havina Zaka. Na vito hivyo ni sawa na mavazi na vitu vingine vinavyotumiwa”. (Kashshaf Al-Qinaa 2/235, Ch. Dar Al Fikr).
Kutokana na yaliyotangulia, hakuna Zaka juu ya yakuti, zumaridi na vito vingine vinavyofanana na hivyo miongoni mwa vito vya mawe ya thamani.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi wa yote.