Zawadi ya Mwenye Mali Halali Iliyoc...

Egypt's Dar Al-Ifta

Zawadi ya Mwenye Mali Halali Iliyochanganyika na Haramu

Question

Ni nini Hukumu ya kukubali zawadi ya mwenye mali halali iliyochanganyika na haramu?

Answer

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Wanavyuoni wametofautiana katika hukumu ya kushirikiana na mtu mwenye mali halali iliyochanganywa na haramu, katika kuuza kununua, kukubali zawadi, kula chakula, n.k. Kuna kauli mbili iwapo uharamu wenyewe haupambanuliki:
Kauli ya kwanza: wanavyouni wa madhehebu ya Hanafiy
wanasema ni haramu iwapo mali ya haramu itakuwa nyingi kuliko ya halali. Na Asbagh miongoni mwa wanavyouni wa madhehebu ya Maalikiy anasema, ni haramu moja kwa moja iwapo mali ya haramu ni zaidi ya halali au hapana. Al-Desokiy anasema: "Najua kwamba mwenye mali ambayo sehemu kubwa ya mali hiyo ni halali na sehemu ndogo ya mali hiyo ni haramu, inaruhusiwa kushirikiana naye na kula kitu kutokana na mali yake hiyo kama alivyosema Ibn Al Qaasim, tofauti na Asbagh aliyetaja uharamu wa mali hiyo. Ama mtu ambaye sehemu kubwa ya mali yake ni haramu na sehemu ndogo ni halali, basi madhehebu ya Ibn Al Qaasim yanaona kuwa inachukiza kushirikiana naye na kula kutokana na mali yake hiyo tofauti na Asbagh aliyetaja uharamu wa jambo hilo" [Hashiyat Al Sharhu Al Kabeer 3/277, na rejea. Ghamzu Oyun Al Basair 1/192, Ch. Dar Al Kutub Al-Elmiya).
Dalili ya Asbagh ni kwamba kuchanganya mali ya halali pamoja na ya haramu kunaeneza mali haramu katika mali yote. Na kutokana na hivyo mali hiyo itakuwa haramu, na mwenye mali hiyo analazimika kuitoa sadaka [Rejea: Al Zakhira 13/317, Ch. Dar Al Gharbu Al Islamiy).
Kauli ya pili: Inaruhusiwa pamoja na kutopendeza, na hiyo ni kauli ya wanavyuoni wa madhehebu ya Maalikiy, ikiwa mali ya haramu ni zaidi ya mali ya halali. Na kauli ya wanavyuoni wa madhehebu ya Shafiy na Hanbaliy ni kuwa inaruhusiwa kwa hali zote, ikiwa mali ya haramu ni zaidi ya mali ya halali au chache. Na hiyo ndiyo kauli ya wanavyuoni wa madhehebu ya Hanafiy ikiwa mali halali ni zaidi ya haramu.
Imamu Al Nawawiy anasema: “Dua ya mtu ambaye sehemu kubwa ya mali yake ni haramu, haipendezi kuitikiwa na pia haipendezi kushirikiana naye” [Rawdhatu Al Talibeen 7/337, Ch. Al Maktab Al Islamiy na rejea: Asna Al Mataalib 3/227, Ch. Dar Al Kitaabu Al Islamiy).
Al Suyutiy anasema: “kushirikiana na mtu ambaye sehemu kubwa ya mali yake ni haramu ikiwa uharamu wenyewe haukupambanulika, usahihi wake ni kuwa si haramu, lakini haipendezi kufanya hivyo. Na pia kuhusu kuchukua zawadi ya Sultan ikiwa mali ya haramu ni zaidi ya halali kama ilivyosemwa katika [Sharhu Al Muhadhab] kwamba inajulikana kuwa jambo hilo linachukiza na siyo haramu” [Al Ashabah wa Al Nadhaer Uk.107, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiya).
Al-Mardaawi anasema: “Faida: kuna mitazamo mingi kuhusu ruhusa ya kula mali ya haramu ya mtu…
Mtazamo wa nne: kutoharamishwa kwa vyovyote iwavyo, iwapo sehemu kubwa au ndogo ya mali hiyo itakuwa haramu, lakini tu haipendezi. Na kuchukiza kwake kunazidi na kunapungua kwa mujibu wa ukubwa wa uharamu na uchache wake. Na mtazamo huu umeelezwa katika Al Mughniy, Al Sharhu, Ibn Aqeel katika sehemu zake, Qudama Al Azjiy na wengine. Nasema: huo ndio mtazamo sahihi” [Al Insafu 8/322, Ch. Dar Ihyaa Al Turaath Al Aarabiy.).
Wanaona kwamba inaruhusiwa suala hilo la ushirikiano kwa sababu asili ya mali na kushirikiana kwayo ni halali na kuharimishwa ni jambo la mpito ambalo halithibitiki ila kwa uhakika wake, na kwamba kuna uwezekano pia wa kushirikiana kwa mali ya halali, na hasa kwa kuwa uwazi wake ni kuwa mali ya mtu na haki yake ni kile alichonacho mkononi mwake. [Rejea: Al Mughniy 4/180, Ch. Dar Ihyaa Al-Turaath Al-Aarabiy).
Mtume S.A.W. na masahaba wake walikuwa wakishirikiana na wasio Waislamu na walikuwa wanakubali zawadi zao ingawa watu hao wasio Waislamu walijulikana kwa kutendeana na kushirikiana wao kwa wao kwa mali ya haramu kama vile riba na pato la pombe, ufisadi, masanamu na maovu mengine mengi. Na Mwenyezi Mungu amewaeleza wao kwamba: {Hao ni wasikilizaji kwa ajili ya kusema uwongo, na ni walaji mno vya haramu!} [Al MAIDA 42]. Kuna mtu mmoja alikuja kwa Ibn Masud R.A. akasema: “Nina jirani anakula riba, na bado anaendelea kuniita (nishirikiane nae), Ibn Masud akasema, tabia unayokubaliana nayo ni kwako na dhambi itakuwa juu yake.” [Kitabu cha Abdul Razzaq 8/150, Al Maktab Al Islamiy).
Aidha katika dalili wanayoitegemea katika kuchukiza hali hiyo ni hadithi ya Nu’man bin Bashir R.A.anasema: nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, S.A.W. akisema: (Halali iko wazi na haramu iko wazi, na baina yao ni vitu vyenye shaka ambavyo watu wengi hawajui. Kwa hivyo, yule anayeepuka vyenye shaka anajisafisha nafsi yake kwenye dini yake na heshima yake, lakini yule anayetumbukia katika mambo yenyeshaka, huanguka katika haramu, kama mchunga anayechunga pembezoni mwa mpaka, mara huingia ndani (ya shamba la mtu). Hakika kila mfalme ana mipaka yake, na mipaka ya Allah ni makatazo Yake.) [Imepokelewa na Bukhari na Muslim]. Na mchanganyiko wa mali ya halali pamoja na haramu ni miongoni mwa vitu vyenye shaka ambavyo inapendeza kujikinga navyo.
Na kauli ya kwamba ni haramu inasababisha uzito na ugumu wa maisha kwa Waislamu, na pia inasababisha kufunguliwa kwa mlango wa wasiwasi wa shetani, kugombana na kubadilishana mashtaka kati ya watu, na kauli ya Asbagh ilipingwa na wanavyouni wa madhehebuya Malikiy. Al-Qaraafiy alisema katika “Al-Dhakhira”: “Kauli ya Asbagh ni kali, na msingi wa sheria ni kuzingatiwa kilichoshinda kwa kuwa na wingi zaidi”(13/317). Ibn Al Arabiy anasema: Asili ya yeye kuharamisha mali zote zinazochanganyika halali na haramu ni asili mbaya, kwa sababu uharamu ni sifa inayothibiti kwa mtu mwenye jukumu la kisheria, na wala hauhusiani na mali yenyewe. Mali kama mali haisifiwi ni haramu au halali, bali kitendo cha mtu mwenye jukumu la kisheria ndicho kinachosifiwa kuwa ni halali au haramu.

Kutokana na yaliyotangulia: Inajuzu licha ya kuwa ni Makruhu, kukubali zawadi ya mwenye mali ya halali iliyochanganyika na mali ya haramu, kwa mujibu wa madhehebu ya wanavyuoni wengi. Na hayo ikiwa mtu hatambui uharamu wa mali hiyo, na iwapo atajua uharamu wake basi ni haramu kwake kukubali zawadi ya aina hiyo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi ya wote.
 

Share this:

Related Fatwas