Kuchelewesha kutoa zaka ya fitri

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuchelewesha kutoa zaka ya fitri

Question

Nini hukumu ya kuchelewa kutoa zaka ya fitri mpaka baada ya sala ya Idi au mchana wake?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Zaka ya fitri ni zaka inayotokana na kumalizika kwa Ramadhan, na ilifaradhishwa katika mwaka wa pili wa Hijra, tena ni zaka ya mwili si zaka ya mali.

Zaka ya fitri ni faradhi ya wajibu. Ibn Omar R.A amepokea kwamba Mtume S.A.W. alifaradhisha zaka ya fitri kutokana na Ramadhan pishi ya tende au ngano juu ya kila mwislamu muungwana au mtumwa na mwanamume au mwanamke. ]Bukhari na Muslim[. Zaka ya fitri ni wajibu juu ya kila mwislamu mtumwa au muungwana, mwanamume au mwanamke na mdogo au mkubwa, kila mmoja aitoe mwenyewe au kwa niaba ya yule anayemchunga, na mke anaitoa mwenyewe au mumewe anamtolea.

Zaka ya fitri inasifiwa kuwa ni njia ya kumsafisha mwenye kufunga Ramadhan kutokana na upuuzi, mazungumzo yasiyo na maana na ni aina ya kuwalisha masikini; Abu Dawud amepokea kutoka kwa Ibn Abass R.A kwamba alisema: Mtume S.A.W. alifaradhisha zaka ya fitri kwa ajili ya kumtakasa mwenye kufunga kutokana na upuuzi na mazungumzo yasiyo na maana, na kuwalisha masikini, mwenye kutoa zaka ya fitri kabla ya sala ya Idi basi zaka inakubaliwa, na mwenye kuitoa baada ya Sala basi hiyo ni sadaka kama sadaka nyingine.

Kuhusu wakati wake; Madhehebu ya Shafiy, Hanbaliy na moja ya rai mashuhuri ya Malik yanasema zaka ya fitri inawajibika kuanzia kuzama kwa jua siku ya mwisho ya Ramadhan, na rai nyingine ya Malik inasema zaka ya fitri inawajibika kuanzia kupambazuka kwa alfajiri ya siku ya Idi [Rejea: Kifayat Al-Taleb Al-Rabaniy na maelezo ya Al-A’dawiy, 1/452 & Mughniy Al-Muhtaj, 1/401 & Kashf Al-Kina’i, 2/251].

Wengi wa Maulamaa wanasema inajuzu kuitoa zaka mpaka kuzama kwa Jua siku ya kwanza ya Idi, na ni Sunna kwao kutoichelewesha kuitoa baada ya sala, na kwao inakatazwa kuichelewesha hadi kumalizika kwa siku ya kwanza ya Idi (ambayo inamalizika kwa kuzama kwa Jua) bila ya kuwepo dharura, na uwajibu wake haufutiki kwa kuichelewesha bali italazimika kulipa.

Abu Alhasan Almalikiy alisema katika kitabu cha [Sharhu Risala, 1/514]: hapati dhambi madamu siku ya Idi haijaisha, lakini akiichelewesha hali ya kuwa ana uwezo wa kuitoa basi atapata dhambi.

Imamu Nawawiy Alshafiy alisema kuhusu zaka ya fitri na kuichelewesha mpaka baada ya sala ya Idi: “Kwa mujibu wa madhehebu yetu mtu akichelewesha zaka mpaka sala ya Idi na akaitoa katika siku hiyo ya Idi basi hapati dhambi na analazimika kuitoa. Lakini akichelewesha mpaka baada ya siku ya Idi basi atapata dhambi pamoja na kulazimika kuitoa, na rai hii aliisema Al-Abdariy kutoka kwa Malik, Abu Hanifa, Allaith na Ahmad” [Sharh Al Muhazab, 6/142, Dar al Fikr].

Al Bahutiy Al Hanbaliy alisema katika kitabu cha [Kashf Alkinaa, 2/252, Dar Al Kutub Al Elmiya]: “akichelewesha (kutoa zaka) mpaka baada ya siku ya Idi basi atapata dhambi kwa kuchelewesha kutekeleza lililo wajibu kutolewa katika wakati wake pia atapata dhambi kwa kutotimiza sharti hiyo, aidha analazimika kuitoa kwani ni ibada ambayo haisamehewi kwa kutotekelezwa katika wakati wake, kama vile ibada ya sala”.

Dalili ya kujuzu kuchelewesha kutoa zaka mpaka mwisho wa siku ya Idi ni yale yaliyopokelewa na Baihaqiy kutoka kwa Abdullah Bin Omar R.A aliposema: Mtume S.A.W. alituamrisha kutoa zaka ya fitri juu ya kila mdogo au mkubwa, muungwana au mtumwa pishi ya tende au ngano. Na alisema tulikuwa tunaamrishwa kuitoa kabla ya Sala ya Idi, Mtume S.A.W aliwaamrisha waigawe baina yao, ambapo alisema: “msiwaache watoke ovyo kutafuta riziki katika siku hii ya Idi”.

Imamu Ibn Qudama alisema katika kitabu cha [Al Mughniy, 3/88:89, Ch. Maktabat Al Kahira] “Inapendeza kuitoa sadaka ya fitri katika siku ya fitri kabla ya sala; kwani Mtume S.A.W. aliamrisha zaka itolewe kabla ya watu kwenda kusali, na akiahirisha mpaka baada ya sala basi atakuwa ameacha fadhila bora; kwani madhumuni ya sadaka ya fitri ni kuwatosheleza wanaohitaji wasitoke ovyo kuomba omba katika siku hii, na sadaka ya fitri ikiahirishwa basi madhumini yake yatakuwa hayajatokea kwa wote. Na waliomili katika kauli hii ni Ataa, Malik, Musa Bin Wirdan, Is-haq na watu wa rai. Naye Al Kadhi alisema: akiitoa (sadaka ya fitri) muda wowote wa siku ya Idi atakuwa hajafanya la Makruhu; kwani jambo la kuwatosheleza wenye kuomba litatokea katika siku hiyo”.

Madhehebu ya Hanafiy yanaona kuwa sadaka ya fitri inakuwa wajibu juu ya kila mwenye wasaa akiwa yuko uhai, alisema katika kitabu cha [Al Durr Al Mukhtaar na maelezo ya Ibn Abdeen, 2/72, Ch. Ihyaa Al Turaath]: “(Inawajibika): Mtume S.A.W. alifaradhisha kutoa zaka ya fitri ingawa mwenye kuikanusha hatahesabika miongoni mwa makafiri (kwa mujibu wa madhehebu yetu) na hiyo ndiyo rai iliyosawa”.

Kiufupi, utoaji wa zaka ya fitri kabla ya sala ya Idi utakuwa bora zaidi, na inasuniwa kutoichelewesha mpaka baada ya sala, lakini ikicheleweshwa mpaka baada ya sala ya siku ya Idi na kabla ya kuzama kwa jua, basi inajuzu kisheria. Ama jambo la kuichelewesha zaka mpaka kumalizika siku ya Idi ni haramu na mwenye kufanya atapata dhambi, ingawa atalazimika kuitoa kwani haisamehewi kwa kutotekelezwa.

 Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas