Burashi Iliyotengenezwa kwa Nywele ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Burashi Iliyotengenezwa kwa Nywele za Asili

Question

Ni nini hukumu ya matumizi ya burashi iliyotengenezwa kwa nywele za asili za wanyama?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Kwa mujibu wa makubaliano ya wanachuoni inajuzu kutumia nywele za asili zilizochukuliwa kutoka kwa mnyama ambaye ni tohara, kuchukua huku ni wakati wa uhai wake au baada ya kuchinjwa kisheria, na pia hukumu hii inajumuisha sufi, manyoya na kila aina ya matumizi na kutengeneza vyombo mbalimbali vinavyotokana navyo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na Mwenyezi Mungu amekujaalieni majumba yenu yawe ni maskani yenu, na amekujaalieni kutokana na ngozi za wanyama nyumba mnazo ziona nyepesi wakati wa safari zenu na wakati wa kutua kwenu. Na kutokana na sufi zao na manyoya yao na nywele zao mnafanya fanicha na vifaa ya kutumia kwa muda}[AN-NAHL 80]. Mwenyezi Mungu ametaja hivyo kutukumbusha neema zake, na hiyo inaonesha usafi wa vilivyotajwa, na kujuzu kutengeneza kutokana na sufi, manyoya na nywele tunachotaka kama samani na vitu. Na “vitu” Ni kila kitu anachofaidika nacho mtu kama zana, vyombo na bidhaa. Makubaliano haya ya wanachuoni ameyanukuu Imamu Abu Bakar Ibn Al Mundhir katika kitabu chake [Al-Awsat, 2/273, Dar Taiba], amesema: “Walikubaliana kwamba inajuzu kutumia nywele zao, manyoya yao na sufi zao kama vitachukuliwa kutoka kwa mnyama aliyehai”.
Ama kuhusu nywele za mnyama ambaye ni tohara lakini haliwi awe hai au nyamafu, au analiwa lakini hajachinjwa basi wanachuoni wamehitalifiana. Imamu Shafii amesema kuwa nywele za nyamafu ni najisi isipokuwa baada ya kusafisha ngozi yake kwa kutengenezwa, na pia nywele zilizotengwa za mnyama ambaye hata akiwa hai ni marufuku kuliwa.
Imepokelewa katika “Al Muhadhab” kwa Sheikh Abu Ishaq Al-Shirazi na maelezo yake ya Imam Al-Nawawi kutoka katika vitabu vya wafuasi wa madhehebu ya Al-Shafii [1 / 230-342, Dar Al-Fikr, kwa ufupisho] anasema: Mtunzi wa “Al Muhadhab” anasema: “Kila mnyama anayenajisika kwa kifo, basi nywele zake na sufi zake ni najisi kwa mujibu wa matini ya sheria, kwa sababu ni sehemu inayoshikamana na mnyama kimaumbile, basi hunajisika kwa kifo kama viungo vya mwili. Kadhi Abu Tayib na wengine walisema: "nywele, sufi, manyoya, mifupa, pembe na kwato huhalalika kwa uhai na hunajisika kwa kifo, hii ni rai sahihi kwamba ni najisi..". Na baadhi ya wanavyuoni wamesema kwamba kuna rai mbili kuhusu nywele.
Ya kwanza ni najisi kama tulivyoeleza. Ya pili ni kwamba nywele siyo najisi kwa sababu hazina hisia wala hazipati maumivu, kwa hivyo najisi ya kifo haitaambatana na nywele ... Ikiwa nywele zimekatwa kutoka kwa mnyama basi hutazamwa kama mnyama ni miongoni mwa wanyama wanaoruhusiwa kuliwa, basi nyewele zake hazitakuwa najisi, bali ni safi kwa mujibu wa Quraani na makubaliano ya wanachuoni, kwa sababu kukatwa kwa nywele za mnyama ni kama kumchinja, basi kama akichinjwa mnyama na hakunajisika, basi hali ni hiyo hiyo kama akikatwa nywele zake, ... kipimo cha unajisi wake kama viungo vingine vya mnyama vinavyotengwa katika uhai wake, lakini wanavyuoni walikubaliana juu ya usafi wake; kwa kuwa watu wanahitaji sana mavazi na vifaa vya kutandika ... na kama zimekatwa nywele, sufi na manyoya ya mnyama ambaye hairuhusiwi kuliwa au zimeanguka chini zenyewe au zimenyofoka, basi wanachuoni wetu wamekubaliana kwamba hukumu yake ni kama hukumu ya nywele za mzoga kwa sababu sehemu ni iliyojitenga na mnyama ambaye ana uhai. Kwahiyo tofauti iliyotangulia inakuwa kuhusu nywele za mzoga, na madhehebu yote yanaona kuwa hukumu yake ni unajisi wake kutoka kwa wanyama, na usafi wake kutoka binadamu”.
Na wanachuoni wengi kama wafuasi wa madhehebu ya Imamu Abu Hanifa, Malik na Hanbali wamesema nywele hizo ni tohara. Madhehebu ya Maalik peke yake yamesema nywele za nguruwe na nywele za mbwa ni tohara; kwa sababu kwa maoni yake nywele za wanyama hao ni tohara wanapokuwa hai.
Imamu Abu Bakar Ibn Almundhir katika kitabu chake [Al-awsat, 2/272-274] anasema: “Wanavyuoni wametofautiana kuhusu matumizi ya nywele za nyamafu, sufi zake na mayoya yake, kundi la wanavyuoni waliruhusu matumizi yake yote, na miongoni mwa walioruhusu ni Hasan Al Basri, Muhammad Bin Sirin, naye Hammad Bin Abi Suleiman amesema: "Inajuzu zikisafishwa, na pia Al-Aamash alisema: "Marafiki wa Abdullah wanaamini kwamba kuosha sufi za nyamafu ndio tohara yake, msimamo huu pia ni wa Malik Bin Anas, Laith Bin Saad, Ahmad, na Isaka, na wakasema: "Zisafishwe. Al-Awzaai amesema: manyoya, mishipa, na sufi vyote havina najisi... Wanavyuoni walikubaliana kwamba kondoo au ngamia au ng'ombe akikatwa kiungo hali ya kuwa yu hai, basi kiungo kilichokatwa ni najisi, na wamekubaliana kwamba inajuzu kutumia nywele zake, manyoya yake, na sufi zake kama zitachukuliwa kutoka wanyama hali ya kuwa wa hai, pia walikubaliana kuwa kuna tofauti kati ya viungo na nyewele, sufi na manyoya kwa kutofautiana hali zake, na inaonesha kwamba kinachohitaji kuchinjwa ni ambacho kama hakikuchinjwa kinakuwa haramu, na ambacho hakina haja ya kuchinjwa na wala hakina uhai ndani yake basi ni kisafi, ikiwa vilivyochukuliwa vilichukuliwa kutoka kwao wakiwa hai au baada ya kifo; kwani hawana uhai ndani yake; kwa sababu kama walikuwa na uhai, basi wangekuwa kama viungo vinavyohitaji kuchinjwa, hakuna kitu chochote kibaya kuhusu nywele za mzoga, sufi zake na manyoya yake kwa mujibu ya wanavyuoni wengi, na Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua zaidi ... Na kutoka kwa Abu Wakid Alliythi amesema: Mtume S.A.W amekuja Madina, watu wakawa wanakata nundu za ngamia, na mafuta ya kondoo, Mtume S.A.W. amesema: “Kinachokatwa kutoka kwa mnyama yu hai basi ni maiti” Wanachuoni wamekubaliana kwamba hapakutajwa nywele wala sufi wala manyoya”.
Imamu Al Kamal Bin Al Hamam Al Hanafi katika kitabu cha [Fathu Al Qadeer ala Hidaya, 1/84.85, Ihiyaa Al-Turath.] alipofafanua kauli ya (Al-Hidaya) amesema: “Nywele za nyamafu na mifupa yake ni tohara”: “kila kitu kisichokuwa halali kwa uhai wa (mnyama) miongoni mwa sehemu ya mnyama, kinahukumiwa kuwa kisafi baada ya kifo cha sehemu yake, kama vile nywele, manyoya, mdomo, mfupa, mishipa, na kwato ... hakuna kutofautiana kati ya wenzetu katika hilo, lakini kifo huathiri uchafu katika kile na uhai... na kama uhai haujakihalalisha basi inalazimika hukumu yake kuendelea kuwa na sifa yake iliyozoeleka kutokana na kutokuwepo cha kuiondosha sifa hiyo, na katika Sunna ya Mtume S.A.W. pia kuna ushahidi unaoonesha hivyo kwa ushahidi uliopokelewa katika kauli yake Mtume kuhusu kondoo wa mtumwa wa Maymuna pale alipopita naye akiwa mzoga : "imeharamishwa kuliwa" (ilipokelewa hadithi hii katika sahihi mbili).
Kisha akataja hadithi za Mtume zinazoonesha usafi wa nywele za mzoga, akibainisha sababu ya udhaifu wake na kisha akasema: “.. hadithi hizi kama ni dhaifu basi matini zake ni nzuri, basi iweje wakati miongoni mwazo ni zile zisizoshuka chini ya cheo cha HASAN ina ushahidi wa mwanzo uliopo katika sahihi mbili (Al-Bukhari na Muslim)? ... Na hukumu ya kisheria iliyo thabiti kisheria ni kuwa hali ya uhai wake haiondoki kwa kifo isipokuwa itakapoonekana kisheria kuwa kifo kinaiondoa”.
Katika kitabu “Al Durr Al Mukhtar” moja ya vitabu vya madhehebu ya Hanafi [1 / 205-209 Dar Al-Fikr]: Kuchinja mnyama ni kutoharisha ngozi yake na nyama yake ikiwa ni mnyama anayeliwa, na kama haliwi lakini ni najisi, basi hakuna kinachotoharika kutoka kwake, au ikiwa ngozi yake haiwezekani kusafishwa na kutengenezwa, basi hairuhusiwi pia, kwa sababu ngozi yake katika wakati huu ni kama nyama, laa si hivyo basi ngozi yake inatoharika... (na nyewele za nyamafu) isipokuwa za nguruwe ni safi kwa mujibu wa madhehebu hayo (na mifupa yake na mishipa yake) kwa mujibu wa maoni yaliyo maarufu (na kwato na pembe yake) zisizo na mafuta, na kila kitu kilichokuwa na uhai (isipokuwa kwa kuwa mwilini), nacho ni kila kitu ambacho kikikatwa mnyama hateseki kama manyoya, mdomo na kwato, na sehemu ya tumbo na maziwa kwa mujibu wa maoni yaliyosahihi zaidi. Katika sahihi mbili Mtume S.A.W. amesema kuhusu mbuzi wa Maymuna: (imeharamishwa kuliwa), na katika usimulizo wengine (nyama yake), hii inajulisha kwamba kisichokuwa nyama hakiharamishwi, kwa hivyo sehemu zilizotajwa zimeingia katika uharamu, na kwa sababu kawaida yake kabla ya kifo sehemu hizo si najisi, basi vile vile hazitakuwa najisi baada ya kifo cha mnyama huyo, kwa sababu hali ya kifo haipatikani katika vitu hivyo isipokuwa vinapokuwa mwilini."
Imamu Al Qarafi Al Malikiy katika kitabu cha [Al Dhakhira, 1/183-184, Dar Algharb Al-islamiy] anasema: “Na sufi, manyoya na nywele ni tohara, na Abu Hanifa akakubaliana naye lakini Imamu Shafiy amesitasita katika jambo hilo. Ushahidi wetu kwamba shemu hizo ni safi kabla ya kifo, hivyo zitakuwa safi pia baada ya kifo; kwa mujibu wa msingi wa Al-Istishab katika Fiqhi (nayo ni uthibitisho wa hukumu kutokana na uthibitisho wake katika zama iliyopita, ila ukiwepo ushahidi unaogeuza maeleweno hayo). Na kwa mujibu wa kitabu inapendeza kusafisha, kwa sababu ngozi pengine ikatoa uvundo baada ya kifo. Mwenye kitabu cha Al Turaz anasema: Ibn Al-Muwaz alisema: "kinachonyofolewa kutoka kwa mnyama si safi; kwa sababu kinaambatana na sehemu za nyamafu”.
Muhtasari wa Sheikh Khalil mkuu wa wafuasi waliokuja baadaye wa madhehebu ya Imamu Malik [Uk. 16 Dar Al Hadith], na waliousherehesha kama vile mwanachuoni Al-Muwaq katika ufafanuzi wake unaoitwa [Al-Taji wa Al-Iklil, 1/125-126 Dar Al-Kutub Al-Elmiya.], na mwanachuoni Al Hattab katika ufafanuzi wake unaoitwa [Mawahib Al-Jalil, 1/89 Dar Al-Fikr], na Sheikh Al-Dardeer katika [Al-Sharh Al-Kabir, 1/49 pamoja na Hashiat Al-Desuqi, Dar Al-Fika], na mwanachuoni Sheikh Aleesh [1/45-46, Dar Al-Fikr] kwamba miongoni mwa vitu tohara ni (sufi) ya kondoo na (manyoya) ya ngamia au ya sungura na kadhalika (na manyoya) ambayo yapo karibu na shingo, ambayo inaonekana kama nywele (na nywele) ya wanyama wote (hata nywele za nguruwe) na mbwa, na alieleza sharti ya usafi wa mambo hayo, akasema: (kama yatakatwa) katika uhai na baada ya kifo, hata bila ya kuchinjwa, kwa sababu ni miongoni mwa yasiyohalalishwa na uhai, na yasiyohalalishwa na uhai basi hayanajisiki kwa kifo, na “kwa kukatwa” muradi wake ni kinyume cha kunyofoa, kwahiyo hujumuisha kukatwa na kuondolewa kwa dawa. Kama zitanyofolewa kutoka kwa mnyama aliyechinjwa awe Mubah au Makruhu basi zote ni safi, na kama zikinyofolewa kwa mnyama amabye ana uhai au asiyechinjwa, basi asili yake ambayo inahusiana na sehemu ya ngozi ni najisi, kama ikiondolewa, basi vitu vingine ni safi. Ibn Arafa alisema: nywele, sufi na manyoya zikichukuliwa kutoka sehemu yoyote bila ya kung’olewa kutoka mnyama asiyechinjwa ni tohara, pia nywele za nguruwe na mbwa kwa rai ya madhehebu ya Imamu Malik. Na Ibn Al Qasim Allakhmiy amesema: “Imam Malik ameruhusu kwa ajili ya kushona ngozi”.
Al Bahuti Al Hanbaliy alisema katika [Kashf Alqinaa, 1/56-57 Dar Al-Fikr]: “... (na inachukizwa kushona kwa nywele za nguruwe), kwa sababu ni matumizi ya kitu najisi (na inapasa kuosha kilichoshonwa kwa nywele hizo zikiwa zina unyevu) kutokana na unajisi wake. (Na inaruhusiwa) kutumia (chungio) (kutokana na nywele najisi zilizokauka); kwa sababu najisi haipindukii, kama kupanda nyumbu na punda kunatofautiana matumizi yake katika unyevu ... (na mifupa yake), yaani: nyamafu (na pembe yake, ncha yake, mshipa wake, kwato yake chimbuko la nywele zake) kama zikinyofolewa. (na) chimbuko la (manyoya kama zitanyofolewa wakati wa unyevu au ukavu: ni najisi), kwa sababu ni moja ya sehemu za nyamafu, kwani ni kama sehemu zake zinazobaki, na kwa kuwa chimbuko la nywele na manyoya ni sehemu ya nyama, (na sufi ya nyamafu tohara katika uhai) kama vile kondoo ni safi (na nywele zake, sufi zake na manyoya yake) ni safi (hata kama ni miongoni mwa wanyama wasioliwa kama paka na panya). Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na kutokana na sufi zao na manyoya yao na nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia kwa muda}[AN-Nahl, 80], aya hii dhahiri yake inajumuisha uhai, kifo na manyoya ni kipimo cha vitu hivi vitatu”. Imamu Ibn Qudamah Al Hanbaliy katika kitabu cha [Al Kafi, 1/48-50] amesema: “sufi yake –inakusudiwa ya nyamafu- na nywele zake na manyoya yake ni safi, kwa sababu hazina roho, kwahiyo kifo hakihalalishi; kwa sababu mnyama hateseki kwa kukatwa vitu hivyo, wala hahisi, kwa sababu kama vitu hivyo vina uhai, basi vitakuwa najisi kwa kuenguliwa kutoka kwa mnyama katika uhai wake; Mtume S.A.W anasema: "Kilichokatwa kutoka kwa mnyama hai ni maiti" Imepokelewa na Abu Daoud kwa maana yake. Na hukumu ya nywele za mnyama na manyoya yake kama hukumu yake katika hali ya usafi na hali ya unajisi, ziwe zimeungana au zimetengana katika uhai wa mnyama au kifo chake”.
Aidha miongoni mwa dalili za utohara ni hadithi aliyoipokea Bukhari na Muslim kutoka kwa Ibn Abbas, R.A, amesema, Mtume S.A.W amekuta mbuzi nyamafu, Mtume akasema, S.A.W: " (Je mmefaidika na ngozi yake?) wakasema: ni nyamafu, akasema: (kilichoharamishwa ni kula nyama yake".
Na dalili ya kiakili: asili ya nyamafu ni tohara wakati wa uhai wake, lakini kifo hukifanya kiwe najisi kinachohalalishwa na uhai. Na nywele hazihalalishwi na uhai wala kifo, kwa hiyo kama hakizihalalishi basi ni wajibu kuhukumu kwa kubakia sifa yake ya kisheria kwa sababu hakuna kitu kingine cha kisheria kinaweza kugeuza hukumu hiyo. Asili ya usafi wa nywele za nyamafu ni kwamba kisichohalalishwa na uhai –kwa sababu mnyama hahisi wala hateseki kwa kukatwa nywele- hakipatwi na najisi kwa kifo.
Fatwa teule ni kauli ya wanachuoni wengi, nayo: Inajuzu kutumia burashi iliyotengenezwa kwa nywele za asili za wanyama, sawa awe mnyama anaruhusiwa kuliwa nyama yake kwa makubaliano ya wanachuoni, au mnyama tohara lakini nyama yake hailiwi. Tena inajuzu hata kama nywele zimechukuliwa hali ya kuwa mnyama yu hai au amekufa.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua ziadi ya wote.
 

Share this:

Related Fatwas