Imamu Ghazaly na Maadili na Mweleweko wake.
Question
Imamu Ghazaly ni miongoni mwa wataalamu wakubwa wa kiislamu. Wanaoshughulikia sana kwa masuala ya kimaadili. Je, Maadili yana maana ganikwa Imamu Ghazaly?
Answer
Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
1) Imamu Al-Ghazaly ameielezea dhana yake juu ya Maadili katika kitabu chake: [Ihyaa Ulumu Elden] kwamba: "Maadili ni sura thabiti katika nafasi ya mwanadamu, na matendo yote yanatokana nayo kwa urahisi bila ya haja ya Fikira au kuzingatia sura yake. Inapokiwa umbile hilo huyatoa matendo mema mazuri kwa upande wa kiakili au kisheria, basi umbile hili huitwa Maadili mema, ama umbile hilo likiyatoa matendo mabaya basi matendo haya huitwa Maadili mabaya".
2- Kwa hivyo, sura thabiti ndani ya mwanadamu inahitaji Maadili yaliyo thabiti katika nafsi yake kwa njia ya kutohisi kusitasita hata kidogo, na pia hauwezi kutokea ukatikaji baina ya surah hii thabiti katika nafsi na silka ya mwanadamu inayoafikiana na sura hii. Mwanadamu hasifiki kwa ukarimu au utoaji mali ila ikiwa ukarimu wake huo ni sifa yake ya kudumu. Kwa yule mwanadamu anayetoa mali yake kwa uchache ingawa yeye ana mali nyingi na ana kila sababu ya kumfanya awe mtoaji, basi mtu huyu hasifiwi kwa sifa hii ya ukarimu kutokana na kutokita ukarimu ndani ya nafsi yake.
3- Kisha Al-Ghazaly anaongezea akisema kwamba binadamu hasifiwi kwa tabia fulani iwapo atakuwa katika hali ya kukalifishwa kutenda jambo, au iwapo kuna uzito kwake kulitenda jambo hilo kwa namna ambayo nafsi yake inalazimishwa kulifanya na inasukumwa kulielekea jambo hilo kwa msukumo. Kwa hiyo mtu ambaye anaona ugumu kutoa mali au kujizuia na hasira pale anapokasirika hazingariwi kuwa ni mtoaji au mpole kitabia. Na kwa ajili hii, yeyote anayeifunza nafsi yake uvumilivu na akajaribu kuikinaisha hazingatiwi kuwa yeye ni mvumilivu bali yeye anataka kuwa mvumilivu na ataendelea kuwa na sifa hiyo mpaka pale tabia ya uvumilivu itulizane katika nafsi yake, na wakati huo ndipo atakapo zingatiwa kuwa mvumilivu.
4- Na Imam Al-Ghazaly anaikuta fursa ili kubainisha elementi zinazoyatnegneza Maadili, nazo zinajumuisha utendaji wenyewe wa wazi, na pia utendaji na misukumo ya ndani yake. Na vile vile hukusanya sababu maalumu za utendaji wake na hali anayokuwa nayo mtendaaji wa kitendo hicho.
5- Na elementi hizi ni:
A- Vitendo vizuri au vibaya.
B- Uwezekano wa kuvifanya.
C- Kuvitambua vyema vitendo hivyo.
D- Hali au sura ya nafsi katika kumili upande mmoja kati ya pande hizo mbili, na kuwepo wepesi wa kuvitenda.
6- Ikiwa tabia hutengenezwa na elementi kuu nne kwa pamoja, sisi hatuwezi kufikia matokeo ya hali hii kwamba kuwepo kwa elementi moja au mbili hakutoshi kukifanya kitendo au mwenendo umepanda kufikia ngazi ambayo tunausifia kwamba umekwisha kuwa mwenedo thabiti, na kwamba kikageuka na kuwa kitendo kilichotulia ndani ya nafsi. Kwani tabia sio kitendo tu, kwa sababu baadhi ya mabahili wanaweza wakajitahidi na wakatoa pesa zao kwa ajili ya kujionyesha mbele za watu kwa ajili ya unafiki na umashuhuri tu, na jambo hili kamwe haliwezi kuitwa kuwa ni ukarimu au utoaji. Na kwa upande mwingine, baadhi ya wakarimu wanaweza kushindwa kutoa kwa sababu ya kupungukiwa na mali zao, na hata ikiwa hivyo wataendelea kuitwa wakarimu kwa kuwa sifa hiyo imetulia nyoyoni mwao.
Pia maadili siyo nguvu ambazo zinazomwezesha mtu kutenda au kujiandaa kutenda. Mwanadamu kwa jinsi alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu, ni mwema na Mola amempa nguvu za kutenda wema na uovu. Na kuna uwezekano mtu akauachia uchoyo umtawale, na hapo ndipo unapoonekana mchango wa utashi katika kuzoesha maandalizi haya ambayo yamo ndani ya nafsi ya mwanadamu.
7- Kama kitendo peke yake au maandalizi ya kimaumbile peke yake hayatoshi kumfanya mtu asifike na aina yoyote ya maadili, basi kuujua wema au ubaya hakutoshi kumfanya mtu awe na sifa ya utendaji wema au uovu kwani kujua kitu kunajulikana mara nyingi kuwa hakumili upande wowote. Kwa hivyo mwanadamu anaweza kujua heri lakini kujua kwake heri hiyo hakumfanyia kuwa mtenda heri, na anaweza kujua shari na hii si sharti ya kumfanya mtu awe na sifa ya ubaya. Bali hapana budi kukamilika kwa elementi zote za tabia ili mtu abebe sifa ya tabia fulani.
Na miongoni mwa elementi muhimu kwa upande wa Imamu Al-Ghazali ni lile umbile la kinafsi lenye uimara na ambalo ndilo huzalisha vitendo vya mja. Na elementi ya utambuzi haipungua umuhimu wake katika jambo hilo, kwani utambuzi ndio unaoelekeza utashi na kuisukuma nia hadi kufanya kitendo husika. Elementi hii ndio inayotoa maamuzi ya upeo wa uwezekano wa kitendo kutekelezwa au kutotekelezwa, na huamua sifa za kimaadili ndani yake. Kwa hivyo elementi hii ina sehemu kubwa ya maamuzi katika utendaji wa kitabia.
8- Mtazamo wa Al-Ghazali una sifa ya kipekee juu ya mweleweko wa tabia na uchambuzi wake kwamba ni: mtazamo wenye mpangilio wenye sifa ya kukusanya hauishii katika mtazamo uliyogawanyika gawanyika, bali huangalia fikra mtazamo jumla unaojumuisha sifa zote, ambapo hutokea kupitia elementi za utendaji wa kitabia, kama ambavyo yeye ameuchukulia kuwa ni chanzo cha mazungumzo yake ya tabia kukubali mabadiliko.
9- Pia Imamu Al-Ghazal ametoa mweleweko wa tabia kupitia muono wa chimbuko la Kiislamu unaothibitisha kuwa hapana budi tabia ipimwe kwa kipimo cha sheria na akili, na si akili peke yake kama tunavyoona ifanywavyo na wanafalsafa. Mtazamo huu wa Imamu Al-Ghazal unakwenda sambamba na na msimamo wa kifikra wa wanavyuoni wote, na ambao unajengeka kwa uhusiano kati ya akili na sheria, kwani akili huongozwa na sheria ambayo huifunza yale isiyoweza kuyafikia yenyewe peke yake wakati ambapo sheria hufahamika kwa njia ya akili. Kwa hivyo akili ni kama macho na sheria ni kama mwanga, na wala mwanadamu hawezi kuona isipokuwa kwa kuvitumia vyote viwili, na vinapokuwa pamoja huwa vinakuwa mwangaza juu ya mwangaza.
10- Hapa tunaangalia elementi ya tano ambayo inaweza kuongezwa katika zile elementi alizozitaja Imamu Al-Ghazal nayo ni: kukariri utendaji na kuizoesha nafsi kitendo hicho, kwani mazoea yana athari inayorahisisha kukifanya kitendo hicho kwa namna ambayo hapahitajiki uzingativu mkubwa au juhudi yoyoyte pevu. Kwa hivyo basi, Mazoea ni maumbile ya pili kama wasemavyo wahenga, na kawaida, mazoea au kukariri kariri jambo hulifanya jambo linalozoeleka au kukaririka liwe na uimara katika nafsi ya mtu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi wa wote.
Marejeo:
1. Al-Ghazaly, Ihyaa Ulum Al-Din, (3\ 52-54).
2. Profesa \ Abdulhamid Madkur, Derasaat fi Elm Al-Akhlak, Al-Qaherah, Dar Al-Hanii, 1426H, 2005 KR, (ku, 14-19) kwa ufupi.