Quraani na Hadithi Hufanya Kazi kwa...

Egypt's Dar Al-Ifta

Quraani na Hadithi Hufanya Kazi kwa Pamoja Quraani Imekamilika na Inafafanuliwa na Sunna

Question

Nini mnasema kuhusu wanaodai inawezekana kutegemea Quraani tu na hakuna haja ya Sunna? Bali wamedai kuwa kuweka kando Sunna kunaondoa hitilafu kati ya Waislamu katika hukumu.

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

Quraani Tukufu ina aya zina maelezo mengi sana, kwa hivyo, ni lazima kuzitekeleza kwa kupitia maelezo yanayozibainisha na yanayozifasiri, na pia zipo aya za kiujumla zinazohitaji kuwekwa wazi kiini chake na kilichojificha, na maelezo hayo na ufafanuzi lazima utoke kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu yeye ndiye ambaye amewakalifisha waja wake, naye ndiye anayejua makusudio ya kitabu chake, hakuna yoyote anayejua zaidi kuliko yeye.

Ufafanuzi huu na maelezo hayo ni Sunna ya Mtume S.A.W iliyoteremshwa kwa ufunuo (Wahyi) au ambayo Mwenyezi Mungu ameyakubali kwa kupitia Mtume, kwa hiyo Mwenyezi Mungu anasema: {Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao} [AN NAHL 44], na Mtume S.A.W, amebainisha hivyo katika kauli yake: "mimi nimepewa hiki kitabu (anakusudia Quraani Tukufu) pamoja na mfano wake (yaani Sunna)". [Imepokelewa na Abu Dawud na wengine].

Imepokelewa na Imamu Malik katika Al-Muwatta, Al-Hakim katika Al-Mustadrak, na Al-Bayhaqiy katika Al-Kubra kutoka kwa Ibn Abbas R.A kwamba Mtume S.A.W alisema: "Nimeacha kwenu kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake mkishikamana nazo haiwezekani kupotea".

Mwenyezi Mungu Mtukufu amemtakasa Mtume wake katika kauli zake na vitendo vyake, kwa kusema: {Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni ufunuo uliofunuliwa} [AN Najm: 3-4].

Haiwezekani kutengana Quraani na Sunna, kwa sababu Sunna ni maelezo ya Quraani , kila kilichofika kwetu kutokana na dini ni kupitia Mtume Muhammad S.A.W na kilichotangulia vyote ni Quraani Tukufu yenyewe, ambayo haikuthibitishwa ila kupitia habari za Mtume, S.A.W

Mtume Muhammad S.A.W amesema kuhusu kuwaumbua wapotevu na waharibifu hawa kama ilivyopokelewa na Abu Dawud, Al-Tirmidhi, na Ibn Majah kwa lafudhi yake kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Inakaribia mtu anakaa juu ya sofa lake husema hadithi miongoni mwa hadithi zangu, akisema: baina yetu na nyinyi ni kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, tuliyoyakuta miongoni mwa mambo ya halali tutayahalalisha, tuliyoyakuta miongoni mwa mambo ya haramu tutayaharamisha, hakika mambo yaliyoharamishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu yanafanana na mambo yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe".

Na miongoni mwa mifano inayoonesha haja ya Quraani kwa Sunna ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na simamisheni Sala, na toeni Zaka} [AL BAQARAH: 43], aya hiyo inafahamika kuwa inafaradhisha Sala na Zaka. Lakini nini uhalisia wa sala iliyofaradhishwa, Sala inasaliwa vipi? wakati gani? idadi yake? na nani anawajibu kusali na mara ngapi inawajibika katika umri?

Nini maana ya Zaka? Nani anawajibika kutoa Zaka? Ni zipi mali zinastahiki kutolewa Zaka? Kiwango chake? Na masharti yake? Ibn Hazm anasema: “Katika Quraani umeona wapi Sala ya Adhuhuri ni rakaa nne, Sala ya Magharibi ni rakaa tatu, mfumo wa kurukuu, jinsi ya kusujudu, jinsi ya kusoma na kutoa salamu, taarifa kuhusu mambo ya kujiepusha nayo wakati wa kufunga, jinsi ya kutoa Zaka ya dhahabu, fedha, kondoo, ngamia, ng'ombe, idadi na kiwango cha Zaka, maelezo ya matendo ya Hija kuanzia wakati wa kusimama Arafah, jinsi ya kusali katika Arafah na Muzdalifah, kutupa Jamaraat, jinsi ya Ihram, na mambo ya kujiepesha katika Ihram, kukata mkono wa mwizi, jinsi ya Unyonyeshaji ulioharamishwa, vyakula vinavyoharamishwa, jinsi ya kuchinja wanyama, adhabu za kisheria, namna gani talaka inatekelezwa, hukumu za mauzo, taarifa ya riba, hukumu, viapo, wakfu, Sadaka na aina nyingine ya Fiqhi?

Hakika katika Quraani kuna aya tukiziacha kama zilivyo hatutajua tuzifanyie kazi vipi? Lakini ni lazima turejee Sunna ya Mtume S.A.W na makubaliano ya wanavyuoni, kwa hivyo ni lazima turejee katika hadithi za Mtume, na kama mtu atasema “hatutachukua ila yanayopatikana katika Quraani tu”, basi yeye ni kafiri kwa mujibu wa makubaliano ya wanavyuoni wote.

Na kama kauli yake hiyo ina ukweli basi angewajibika kusali rakaa moja tu ndani ya wakati baina ya kuchomoza kwa jua mpaka giza la usiku, na rakaa nyingine wakati wa alfajiri, kwa kuwa huo ndio uchache wa Sala, na hakuna zaidi ya hapo, na mtu anayesema hivyo ni kafiri, mshirikina na damu yake na fedha zake ni halali, baadhi ya wanavyuoni wa Rawafidh (kundi miongoni mwa makundi ya Mashia) wamesema hivyo, wanavyuoni wote waliafikiana kwamba hao wamekufuru.

Na Mwenyezi Mungu atupe mafanikio. Na kama mtu hachukui ila waliyoafikiana wanavyuoni wote tu, na anacha waliyotofautiana katika yaliyothibitishwa na kwa aya au hadithi za Mtume, basi yeye ni mwovu kwa mujibu wa makubaliano ya wanavyuoni, kwa hivyo ni lazima tuchukue kwa aya za Quraani na hadithi za Mtume pia”. [Al-Ihkam fi Usuul Al-Ahkam 2/207, Dar Al-Afaaq Al-Jadida - Bairut].

Uhuru wa kufahamu sheria, maelezo yake na hukumu zake zote kutoka Quraani peke yake haiwezekani bila ya kurejea hadithi za Mtume S.A.W., kama itakavyobainishwa katika mifano ijayo, ni lazima tuangalie Sunna iliyoshuka kwa ufunuo au Mtume ameitoa kwa jitihada yake kutoka Quraani na aliyoyakubali Allah S.W. ili tuweze kuelewa makusudio ya Mwenyezi Mungu, na kuzingatia maelezo ya hukumu za Quraani, kwa sababu Sunna ni njia pekee ya kufanya hivyo.

Na laiti kama Sunna si hoja na maelezo ya wazi, basi isingesihi kwa yoyote mwenye kujitihadi kuiangalia, na kuitumia, na asingeelewa yoyote alichokalifishwa –kwahiyo hukumu zisingetekelezeka, na sheria ingebatilika, jambo ambalo wanataka litokee maadui wa Uislamu kwa ajili ya kuangamiza dini.

Ama aya ambazo zinatumiwa kuoneshea kwamba Quraani inajitosheleza na wala haihitajii Sunna ni kutokana na ufahamu mbovu. Aya hizo ni kama vile kauli ya Mwenyezi: Mungu Mtukufu: {Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote} [Al-ANA’AM: 38] kwa maana ya kuwa kitabu ni Quraani, lakini maana ya kitabu katika aya hiyo si Quraani bali ni ubao uliohifadhiwa na Mwenyezi Mungu, ubao uliohifadhiwa ni ule uliozunguka kila kitu, na ambao una maelezo kamili ya viumbe vyote, kama alivyosema Mtume S.A.W., kutoka kwa AL-Tabarani katika kitabu chake: [Al-Mu’jam Al-Kabir], na Al-Baihaqi katika kitabu chake: [Shuab Al-Iman], imepokelewa na Ibn Abbas R.A: "Kalamu imekauka kwa mambo yatakayokuwa katika Siku ya Kiyama".

Ama kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uongofu, na rehma, na bishara kwa Waislamu}. [AN NAHL: 89], Al-Shawkaani alisema katika ufafanuzi wake: “{Na tumekuteremshia Kitabu hiki} yaani, Quraani ... na maana ya kuwa { kinachobainisha kila kitu} kwamba ina maelezo ya hukumu nyingi, na kurejea katika Sunna kuhusu hukumu zinazobaki, na kuwaamuru kumfuata Mtume S.A.W katika mambo yote, na kumtii kama iliyothibitishwa kwa aya za Quraani tukufu, na Mtume S.A.W pia alisema: "Nimepewa Quraani na mfano wake pamoja nayo". [Fathul Qadiir 3/224, Dar Ibn Kathir na Dar Al-Kalim Al-Tayib].

Imamu Fakhru Al-Razi alisema katika maelezo yake [20/258, Dar Ihyaa Al-Turath Al-Arabiy.]: “Wanafiqhi, walisema: Quraani ilibainisha kila kitu, kwa sababu inathibitisha kwamba makubaliano na habari ya mmoja -yaani: Sunna ya Mtume iliyopokelewa na mmoja hadi mwengine- na Kipimo ni hoja, kama ikithibitishwa hukumu moja miongoni mwa hukumu kupitia moja ya misingi hiyo, ilikuwa ni hukumu iliyothibitishwa kwa Quraani .”

Hii inasisitiza maana ya aya {Mwenye kumtii Mtume basi ndio amemtii Mwenyezi Mungu. Na anayekengeuka, basi Sisi hatukukutuma wewe uwe ni mlinzi wao} [AN NISAA 80], na kauli yake: {Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho.} [AL-HASHRI: 7], na kauli yake pia: {Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.} [AAL-IMRAAN: 31].

Ama kuhusu madai yao kwamba kutochukulia Sunna kunaondosha tofauti ya kifiqhi kati ya Waislamu, basi dhana hiyo ni batili; na mfano wa hayo, ni aya ya eda ya mwanamke aliyetalikiwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na wanawake walioachwa wangoje peke yao mpaka tahara (au hedhi) tatu zipite.} [AL-BAQARAH: 228], kama tukiangalia maana ya neno la “AL-Qur’u” tunaona kwamba neno hilo ni miongoni mwa maneno ya tungo tata (yaani neno hilo lina maana zaidi ya moja), bali neno hilo ni miongoni mwa maneno yanayoeleza maana ya kinyume, nalo linamaanisha hedhi na tahara pia, kama tukiuliza hukumu kutoka aya hiyo kwa kupitia lugha, hatutaweza kufanya hivyo, kwa sababu kamusi za kilugha zitatutupa maana mbili zinazopingana, Katika kitabu cha [Al-Misbah Al-Muniir] kwa Al-Fiyumi [uk. 500, Al-Maktaba Al-Elmiya] wakati anapofasiri neno la “AL-Qur’u”: “Wataalamu wa kilugha wanasema kwamba neno hilo linakusudiwa hedhi na tahara pia”.

Kutokana na yaliyotangulia hapo juu, kudai kwamba Quraani inajitosheleza yenyewe bila ya kutegemea Sunna ni madai batili, na kushikilia madai hayo kunasababisha uharibifu wa sheria na hata uharibifu wa dini. Na anayedai kwamba Quraani inajitosheleza yenyewe bila ya kutegemea Sunna huyo anataka kuondosha Sunna na baadae atakuja kutaka iondoshwe Quraan, hapo sasa Quraan itakuwa imeharibiwa haiwezekani kuifahamu wala kuifanyia kazi bila ya maelezo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. Ni lazima kwa kila Mwislamu kuishika dini yake kama ilivyokuja kwake kupitia Mtume S.A.W na Masahaba wake, hadi leo, na kudai huku kwamba Quraani inajitosheleza yenyewe bila ya kutegemea Sunna ni kwenda kinyume na Quraani na mafunzo yake.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi wa wote.
 

Share this:

Related Fatwas