Uhalisia wa Uislamu na Mchango wake...

Egypt's Dar Al-Ifta

Uhalisia wa Uislamu na Mchango wake katika Jamii ya Kisasa.

Question

Uhalisia wa Uislamu na Mchango wake katika Jamii ya Kisasa.

Answer

Hii ndio anwani ya Mkutano wa Kiislamu wa Kimataifa ambao uliandaliwa na Taasisi ya "Aalu Bayti" ya fikra ya Kiislamu nchini Jodan katika mjini mkuu Amman kuanzia tarehe 4 - 6 Julai 2005, chini ya usimamizi wa mfalme wa Jodan Abdalla wa pili, ambaye alihudhuria sherehe za ufunguzi wa mkutano huo, na alitoa hotuba maridadi kuhusu maana hii na risala ya Amman ambayo aliwahi kuitoa katika mwezi wa Ramadhani uliopita, akifupisha ndani ya risala hiyo uhalisia wa Uislamu na vizuizi vinavyomkabili mwislamu na njia ya kusahihisha picha yake duniani. Mkutano huo ulihudhuriwa na Mufti wa Misri Dkt. Ali Juma, waziri wa wakfu Dkt. Mahmoud Hamdy Zaqzuq, Dkt. Ahmad Twayyib Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al-azhar, Dkt. Ahmad Kamal Abu Majd makamu mwenyekiti wa Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Misri, na idadi kadhaa ya wanavyuoni wa Misri na nchi za dunia na kutoka madhehebu yote ya kifiqhi.

Zaidi ya tafiti hamsini ziliwasilishwa, na idara ya mkutano iliomba ipatiwe fatwa kadhaa kutoka marejeo ya kidini ya madhehebu ya Kisunna, Kishia na Kiibadhi kutoka pande mbalimbali duniani juu ya maswali tofauti, na majibu yote yakaafikiana kwa kuwa na maana moja; kwani majibu hayo ndiyo utambulisho wa Uislamu ambao ndani yake haukuwa na tofauti yoyote kati ya wenye akili kupitia zama zote, na ambao umekuwa kwa baadhi ya watu ni sehemu ya kutazamwa kwa mujibu wa upeo mpevu wa upande wa hili kundi la kielimu.

1- Fatwa hizo zimeundwa kutoka maswali matatu: Je mfuasi na anayeyatumia madhehebu yoyote kati ya madhehebu manane ya kiislamu ambayo ni: madhehebu ya Hanafiy, Maalikiy, Shafiy, Hanbaliy, Jaafariy, Zaidiy, Ibaadhiy, Dhaahiriy, inajuzu kumzingatia ni mwislamu?
Na jibu lake lilikuwa hivi:


Hakika Uislamu una mzunguko mpana zaidi kuliko matokeo ya akili za wenye kujitahidi, kwani Uislamu unafaa kwa kila wakati, kila sehemu na kwa walimwengu wote katika hali zote, na anayemsadiki Mtume Muhammad S.A.W. basi ni miongoni mwa Umma wa Kujibu, na asiyemsadiki basi yeye ni miongoni mwa Umma wa kulingania.

Na waislamu wa mashariki na magharibi, waliotangulia na waliokuja baadaye, wamekubaliana kuwa mwanachuoni mwenye kujitahidi ni yule ambaye anafuata maneno yake katika kuilingania dini ya Mwenyezi Mungu, na hii inazingatiwa kuwa ni utekelezaji wa masharti ya kujitahidi yaliyowazi katika Elimu ya Misingi ya Fiqhi naye ni katika wataalamu wakuu (wenye ukumbusho), ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika hali yao: “Nasi hatukuwatuma kabla yako ila watu wanaume tuliowapa Wahyi (Ufunuo). Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui”. [AN NAHL 43], na “Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tuliowapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye elimu ikiwanyinyi hamjui.” [AL ANBIYAA 7].

Na baadhi ya masahaba wema R.A, walifikia daraja hiyo, basi waliwafikishia wanafunzi wao ambao ni taabiyna madhehebu yao, na kisha Taabiyna waliwafikishia taabiy taabiyna madhehebu yao na waliokuja baada yao mpaka karne ya kumi na nne Hijriya. Wakadhihiri wenye kujitahidi mpaka idadi yao ikafikia tisini takriban ambao madhehebu yao yalifuatwa na rai zao zikategemewa, halafu madhehebu manane yakaenea na kutufikia sisi kwa mlolongo wa mapokezano pamoja na baadhi ya wanazuoni kuyatumia katika zama mbalimbali kama vile kutohoa dalili zake, kupata uhakika wa nakala zake, na kurekebisha kile ambacho kila madhehebu yamekitumia kama ni dalili kutoka hadithi tukufu ya Mtume S.A.W. au athari zinazotajwa katika chanzo chake, na kutafiti katika maana ya maneno yanayotajwa katika vitabu vya madhehebu hayo ambayo ni: madhehebu ya Hanafiy, Maalikiy, Shafiy, Hanbaliy na huitwa -madhehebu ya Kisunna- na Jaafariy, Zaidiy, Ibaadhiy, Dhaahiriy -madhehebu yasiyo ya Kisunna- Na tofauti baina ya madhehebu hayo ipo katika upande wa yanayodhaniwa na hayakutafautiana katika msingi wa dini ambao unamkufurisha mwenye kuupinga.

Kutokana na hayo, mtu yoyote anayefuata madhehebu yoyote miongoni mwa madhehebu hayo basi yeye ni mwislamu na Uislamu wake ni sahihi. Na jambo hili linaafikiana na amri ya Mwenyezi Mungu kwetu sisi kuwa tushikamane katika kamba yake na tuwe umma mmoja na wala tusitofautiane zikatofautiana nyoyo zetu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto, naye akakuokoeni nalo.

Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni ishara zake ili mpate kuongoka.” [AAL IMRAAN 103], na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: “Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungelitoa vyote viliomo duniani usingeliweza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaunganisha. Hakika yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hekima.” [AL ANFAL 63], na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: “Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote watarudi kwetu.”. [AL ANFAAL 93].

2- Na swali la pili linasema:
Ni ipi mipaka ya kukufurisha katika Uislamu? Na je, inajuzu kuwakufirisha wanaofuata Al Asha'ariyah au Al Sufiyah?

Na jibu lake lilikuwa:
Hakika mwislamu anayetoa shahada mbili kwa ulimi wake hatoki katika dini ya Uislamu isipokuwa akifanya kitu miongoni mwa yanayokufurisha kwa makusudi, kwa kujua na kwa kutaka yeye mwenyewe, kama vile kusema kwake wazi wazi kuwa amekufuru, au akanushe kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, na haki ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake S.A.W., au ukweli wa Quraani Tukufu, na kwamba Quraani si maneno ya Mwenyezi Mungu, au akalisujudia sanamu, au akahalalisha madhambi makubwa kama vile unywaji wa mvinyo, na uzinzi kwa ndugu au uzinzi wa aina yoyote kwa ujumla, na mabalaa mengine ambayo mwislamu yoyoye kati ya watu wa Kibla hawezi kuyatamka.

Na mabwana wa Ashaaira R.A, ni miongoni mwa jamhuri ya wanachuoni wa umma, na wao ndio waliopambana na mambo yenye utata mbele ya makafiri na wengineo, nao ndio waliowajibika kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W katika historia, na yoyote atakayewakufurisha au kuwatia makosani basi huhofiwa katika dini yake, Alhafedh Bin Asaker akasema katika kitabu chake: [Taabiyiyn Kadheb Al Muftariy]: "Ujue - Mwenyezi Mungu aniwafikishe mimi na wewe kwa ridhaa zake na atujaaliye sote tuwe miongoni mwa wenye kumcha kikweli kweli - hakika ni vigumu kuwashinda wanazuoni, na Mwenyezi Mungu Mtukufu huwafedhehesha wale wote wanaozivunja haki za wanazuoni au kuzivuruga elimu zao, na hili jambo linaeleweka wazi kwa watu wote. Na wale wanaowaudhi wanazuoni kwa maneno mabaya au kwa vitendo vya dhuluma au hata kwa kuwatukana basi Mwenyezi Mungu Mtukufu huzifisha nyoyo zao na kuziweka mbali na haki kabla hawajafa."

Basi mtu anayewapaka matope Ashaaira na Wasufi yuko hatarini, na inachelewa kuwa miongoni mwa Khawaarij na Murjifiin ambao Mwenyezi Mungu amewazungumzia katika Quraani Tukufu: “Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitna katika Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.” [AL AHZAAB 60].

3- Ama swali la Tatu lilikuwa linasema: Je, nani anafaa kuzingatiwa ni Mufti katika Uislamu na kwa masharti gani?
Na jibu lake lilikuwa ni:

Mufti ni yule mwenye kujitahidi ambaye watu wa Usuli wamemzungumzia, na mwenye kujitahidi ni yule anayechukua hatua za kujitahidi, nazo ni kufanya juhudi katika ugunduzi wa hukumu za kisheria kutokana na dalili zinazozingatiwa.

Alkhateeb akasimulia katika kitabu chake: [Al Faqiyh wa Al Mutafaqih, 330-331/2] kutoka kwa Imamu Shafiy kauli yake: "Si halali kwa yoyote kutoa fatwa katika dini ya Mwenyezi Mungu isipokuwa mtu mwenye kukijua kitabu cha Mwenyezi Mungu; kwa kujua aya zinazofuta na zinazofutwa, aya za hukumu, aya zenye mshabihiano ndani yake, na tafsiri ya Quraani, kuteremka kwake, Sura za Makka na Madina, na kinachokusudiwa kwayo, na kisha baada ya hayo akawa na ujuzi wa hadithi za Mtume S.A.W, akayajua yaliyomo katika hadithi kama ujuzi wake wa Quraani, awe mjuzi wa lugha, mjuzi wa mashairi, na kila anachokihitaji kwa ajili ya Sunna na Quraani na akatumia vyote hivi kwa uwiano, na akawa msimamizi wa tofauti za wataalamu wa miji mbali mbali, na akawa na uwezo baada ya hayo, na iwapo atakuwa hivi anaweza kuzungumza na kutoa fatwa katika Halali na Haramu, na iwapo hatakuwa hivyo basi hatakiwi kutoa fatwa."

Na inamlazimu mtaalamu huyo ambaye aliijua Quraani Tukufu na elimu zake, Sunna na elimu zake, Kiarabu na elimu zake kufuata mfumo maalum katika kutoa fatwa, na hayo kwa mujibu wa mpangilio wa dalili, basi akiulizwa kuhusu Sala, atafute hukumu yake katika Quraani, asipokuta jibu lake basi katika Sunna, na asipokuta jibu lake basi akisie (Kiasi), mpaka agundue hukumu ambayo moyo wake unatulizana kwayo, na inashurutishwa katika hukumu hiyo isiende kinyume na Ijmaa (mtazamo wa wanachuoni wote).

Na ama dalili zinazotofautiana ndani yake kama vile Istihsaan na sheria za waliokuwa kabla yetu, na iwapo jitihada yake itampelekea katika usahihi wa kitu katika hilo basi atatoa fatwa kwa jitihada hiyo, na iwapo dalili mbali mbali zitakinzana kwake basi atalazimika kutoa fatwa kwa ile iliyokuwa sawa zaidi miongoni mwazo.

Hayo ndiyo madhumuni tuliyoyajibu na tukawafikiana nayo -wanachuoni wa Sunna wakiongozwa na Imamu Mkuu wa Al-azhar, wataalamu wa Shia kama bwana Muhammad Said Alhakiym, sheikh Ishaaq Alfayaadh, na sheikh Bishr Alnajafiy, na mwanachuoni Ayatullah Muhammad Ali Altaskheeriy, na Imamu wa madhehebu ya Kiibaadhiy sheikh Ahmad Bin Hamad Alkhalil Mufti wa Oman, na sheikh Ibrahim Alwaziyr kutoka madhehebu ya Zaidiy nchini Yemen, na taasisi ya Fikhi ya Kiislamu na wengineo.

Huwenda Mwenyezi Mungu akawaongoza vijana katika dini ya haki ambayo alimteremshia Mtume Muhammad S.A.W, na akawasaidia waitumie katika maisha yao.
Marejeo: Kitabu cha: (Simaat Al Asr), cha Dkt. Ali Juma; Mufti wa Misri.
 

Share this:

Related Fatwas