uda wa Kukaa Itikafu

Egypt's Dar Al-Ifta

uda wa Kukaa Itikafu

Question

Muda gani kisheria unazingatiwa ni muda wa Itikafu ambapo mtu akikaa msikitini kwa nia ya Itikafu anaitwa ni mtu aliyekaa Itikafu na huandikiwa thawabu za ibada hiyo?

Answer

Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimfikie Mtume Muhammad s.a.w, watu wake, Masahaba wake na waliomfuata, ama baada ya hayo:

Itikafu ni ibada ya Sunna na ni miongoni mwa sheria za mbinguni za kale kabla ya Uislamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa itikafu misikitini}[AL BAQARAH, 187], pia Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na tulimwusia Ibrahimu na Ismaili (tukawaambia): “Itakaseni (isafisheni) nyumba yangu kwa ajili ya wale wanaoizunguka kwa ajili ya kutufu na wanaokaa hapo na (kwa ajili ya) wanaorukuu na kusujudu hapo pia”} [AL BAQARAH, 120]. Aidha ilipokelewa katika Sahihi mbili (Bukhari na Muslim) kutoka kwa Bi. Aisha R.A. alisema: “Ilikuwa desturi ya Mtume S.A.W. kukaa itikafu katika siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhani hadi Mwenyezi Mungu alipomfisha. Baada yake wakeze waliendelea kukaa itikafu”.

Itikafu kilugha: ni neno la Kiarabu lenye maana ya “kukaa kwa muda”, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Ni nini masanamu haya mnayakalia wakati wote “kuyaabudu”}[AL-ANBIYAA, 52], aidha lina maana ya “kizuizi”; Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na wakawazuilia wale wanyama (mliowachukua kwa ajili ya kuchinjwa) wasifike mahala pake} [AL-FAT-H, 25]. Pia Itikafu maana yake ni kuzuia nafsi isifanye baadhi ya vitendo vya kawaida [Al Fayoumi, Al Musbah Al Munir, 2/424, Ch. Al Mak-taba Al Elmiya]. Mwanachuoni Sheikh Ibn Al Athir alisema katika kitabu chake [Al Nihaya fi gharib Al Hadith wa Al Athar, 3/284, Ch. Al Mak-taba Al Elmiya]: imetajwa mara kwa mara neno la “Itikafu” na kukaa … neno hilo lina maana ya kukaa pahala maalumu, na neno la Kiarabu “Mu’takif”; mtendaji wa ibada ya Itikafu.

Itikafu kisheria: kukaa faragha msikitini kwa nia maalumu; nia ya kutimiza ibada ya Itikafu [Tazama: Bijirmi, 2/591, cha. Al Mak-taba Al Islamiya & Fat-h Al Qadeer, 2/305, Ch. Ihiya’ Al Turath & Al Fatawa Al Hindiya, 1/211 & Al Mughniy, 3/186, Ch. Mak-tabat Misr & Al Sharh Al Saghir, 1/725, Ch. Dar Al Ma’arif]

Maana halisi ya neno “Itikafu” inaashiria “kukaa pahala kwa muda mfupi au mrefu”, na neno hilo “Itikafu” lilitajwa katika matini ya kisheria bila sharti; kwa maana neno hilo likitajwa katika matini ya kisheria linamaanisha “kukaa faragha misikitini” moja kwa moja bila ya kuwa na sharti ya muda, kwa hiyo “Ibada ya Itikafu” inamaanisha kukaa misikitini kwa muda wowote ukiwa mfupi au mrefu. Naye Mwanachuoni Ibn Al Hamam alisema katika kitabu chake [Fat-h Al Qadeer, 2/392, Ch. Dar Al Fikr): “Ibada ya Itikafu kisheria haiwekewi sharti ya muda, tofauti na faradhi ya Saumu; kwani muda wowote wa kukaa faragha msikitini kwa nia ya Itikafu unakuwa Itikafu”.

Ibn Hazm alisema katika kitabu cha [Al Mahali 3/411-412, Ch. Dar Al Fikr]: neno “Itikafu” katika lugha ya Kiarabu linamaanisha “kukaa”, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Ni nini masanamu haya mnayakalia wakati wote “kuyaabudu”} [AL-ANBIYAA, 52]; yaani wanaoyakalia wakiyaabudia. Kwa hiyo, muda wowote wa kukaa faragha katika nyumba ya Mwenyezi Mungu ni Itikafu bila ya kuwa na sharti ya muda; kwani Quraani na Sunna za Mtume S.A.W. hazikuainisha idadi ya masaa wala muda maalumu.

Hali ya kukaa faragha ikipatikana, basi maana ya Itikafu na ukweli wake wa kilugha inatimia. Ama maana yake ya kisheria inatimia kwa kuwepo hali ya “kukaa” pamoja na kupatikana sharti na nguzo zake za kisheria pamoja na kutokuwepo vizuizi vya kisheria.

Mwanachuoni Al Zarkashiy alisema katika [Al Bahr Al Muheet, 5/8, Ch. Dar Al Kotubiy]: “Ujue kwamba taarifa ikitolewa bila ya vizuizi, basi haiwekewi sharti”.

Maana halisi ya neno “Itikafu”; yaani kukaa faragha haiashirii muda maalumu, lakini inamaanisha kukaa tu, ama kitendo cha kupita msikitini hakimaanishi kukaa faragha; kwani mwenye janaba anaruhusiwa kisheria kupita tu msikitini bila ya kukaa, kwa hiyo jambo la kupita msikitini si kukaa wala Itikafu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Enyi mlioamini! Msikaribie Sala, hali mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema, wala hali mna janaba -isipokuwa mmo safarini- mpaka mkoge}[AN NISAA, 43].

Na Imamu Al Tabariy alitilia uzito zaidi tafsiri ya Aya hiyo kwa maana; msikaribie msikitini, kwani ilipokelewa athari za masahaba na waja wema waliotangulia zinazofasiri kupita njia kwa mwenye janaba kuwa ni kupita msikiti kwa dharura. Ibn Abbas alisema: {wala hali mna janaba –isipokuwa mmo safarini} [AN NISAA, 43]; usikaribie msikiti ukiwa na janaba isipokuwa katika hali ya kuwa hakuna njia nyingine, unapita tu bila ya kukaa msikitini [Imamu Al Tabariy, Tafsir Jami’ Al Bayan, 8/382, Ch. Muasasat Al Risala].

Kutokana na yaliyopita, itikafu haisihi kisheria ila kwa kukaa msikitini kwa nia ya kumtii Mwenyezi Mungu na kwa kufanya ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama rukuu au sijda moja kwa utulivu. Kwa hiyo, muda unaosihi kisheria kwa itikafu lazima uzidi kiwango cha rakaa au sijda moja kwa utulivu. Imamu Al Nawawiy alisema katika [Al Rawdh, 2/391, Ch. Al Mak-tab Al Islamiy]: “Ili itikafu isihi kisheria, lazima izidi kiwango cha kutimiza sala kwa utulivu ili ipate sifa na maana ya kukaa”.

Imamu Al Haramayn alisema katika kitabu cha [Nihayat Al Mat-lab, 4/82, Ch. Dar Al Minhaj]: “Jambo la kukaa sharti yake ni kupatikana utulivu wa rukuu na sijda ili ipatikane maana ya itikafu inayokusudiwa, na yule anayefanya hilo anaweza kusifiwa kuwa ni mwenye kukaa”.

Imepokelewa katika Sunna na athari za masahaba yanayoashiria kwamba hakuna sharti ya muda maalumu katika kusihi kwa Itikafu; maana Mtume S.A.W. alikuwa anakaa Itikafu yeye na wakeze katika siku kumi za mwisho za Ramadhani, pia ilipokelewa katika Bukhari ya kwamba Mtume S.A.W. alikiri Itikafu ya usiku mmoja kwa Omar Bin Al Khataab ili atimize nadhiri yake ambayo aliiweka kabla ya kusilimu. Zaidi ya hayo, Mtume S.A.W. alimwamuru atekeleze nadhiri yake kama ilivyotajwa katika Sahihi mbili kutoka kwa Ibn Al Khataab R.A. alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu katika siku za Jahiliya niliweka nadhiri ya kukaa Itikafu usiku mmoja katika Msikiti Mtukufu, basi Mtume S.A.W. alimwambia: tekeleza nadhiri yako. Akakaa Itikafu ya usiku mmoja”.

Al Hafiz Bin Hajar alisema katika kitabu cha [Fat-h Al Bariy, 4/274-275, Ch.. Dar Al Maarifa]: “Hiyo inaonesha kwamba hajazidisha kitu katika nadhiri yake, na kwamba Itikafu si sharti iambatane na Saumu, pia Itikafu haiwekewi sharti ya muda maalumu, na katika Hadithi hiyo anajibiwa anayesema kuwa Itikafu lazima isipungue siku kumi au zaidi ya siku moja”.

Imamu Al Nawawiy alisema katika kitabu cha [Sharh Sahih Muslim, 11/124, Ch.. Dar Ihiyaa Al Turath Al Arabiy]: “Hadithi hiyo ina dalili juu ya ukweli wa madhehebu ya Imamu Shafiy na waliomfuata katika kusihi Itikafu ya usiku kama inavyosihi mchana ikiwa kwa usiku mmoja au zaidi au chini ya hayo. Dalili inayothibitisha maana hiyo ni Hadithi ya Omar R.A. na ndiyo madhehebu ya Imamu Shafiy, Al Hassan Al Basriy, Abu Thur, Abu Dawud, Ibn Mundhir na riwaya iliyo sahihi zaidi kutoka kwa Imamu Ahmad. Na Ibn Mundhir alisema Hadithi hiyo ilipokelewa na Aly na Ibn Masoud”.

Ilipokelewa kutoka kwa baadhi ya Masahaba wenye heshima kuhusu kukaa faragha msikitini “Itikafu” kwa muda wa saa moja kama ilivyopokelewa na Abdu-el-Razaq katika chake [4/346, Ch. Al Mak-tab Al Islamiy] akisema: “Nilikuwa nakaa faragha msikitini kwa muda wa saa moja, na nilikuwa nafanya hivyo kwa nia ya Itikafu”.

Saa katika maana ya kifiqhi kama wanavyoielewa wanachuoni ni sehemu mojawapo ya wakati nayo ni saa ya kilugha, na wanachuoni hawakusudii saa ya kifalaki ambayo ni sehemu mojawapo ya sehemu ya saa ishirini na nne za mchana na usiku [Rejea: Al Durr Al Mukh-tar, 2/444 pamoja na maelezo ya Ibn Abedin, Ch. Dar Al Fikr & Zubaydiy, Taj Al Arus, 21/241, Ch. Dar Al Hidaya].

Al Fayoumi alisema katika kitabu cha [Al Musbah Al Munir, 1/295, Al Mak-taba Al Elmiya]: “Waarabu wakisema “saa” wanakusudia sehemu ya wakati hata ikiwa muda mfupi. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Kila umma una muda wake. Unapofika muda wao hawakawii saa moja wala hawatangulii} [YUNUS, 49]”.

Kutokana na yaliyopita: kukaa faragha msikitini ni sharti ya kusihi itikafu kisheria, na huo ni mtazamo ulio sahihi zaidi kama walivyoona Maulamaa wengi. Ama muda unaotakiwa kusihi itikafu, basi hauna mipaka maalumu kwa ufupi wake au urefu wake isipokuwa sharti ya kupatikana utulivu unaozidi utulivu wa rukuu.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi ya wote.
 

Share this:

Related Fatwas