Maada na Jinsi Quraai Tukufu Inavyo...

Egypt's Dar Al-Ifta

Maada na Jinsi Quraai Tukufu Inavyotendeana Nayo

Question

Quraani Tukufu inatendeana vipi na mielekeo ya maada ambayo inatawala baadhi ya jamii na watu?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

• Hakika maada kama alivyobainisha marehemu Muhammad Albahiy mhadhiri wa falsafa ya Kiislamu na mkuu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Al Azhar, ina sifa zake maalumu ambazo zinaweza kuathiri vitendo vya mwanadamu, au tabia za jamii fulani na uhusiano uliopo baina ya watu wake, sifa ambazo hazihusiki na kundi la watu maalumu au rika maalumu. Mtazamo wa maada unapatikana kwa mwanadamu au jamii kwa namna ambayo vitendo vyake vya kimaisha vinaathiriwa na maada hiyo; maana maada inaambatana na ubinafsi, naye mtoto mdogo kwa umbile lake asili anakuwa na tabia hiyo ya ubinafsi na katika wakati huo huo anakuwa na sifa ya maada; kwani fikra zake zinashughulikia zaidi dhati yake; maana fikra zake zinaambatana na vitu vya kuhisika wala haziambatani na vitu vya ulimwengu wa mawazo, na mwanadamu akibaleghe hali ya kuwa ana sifa za ubinafsi na bado anaathirika na vitu vya kuhisika, basi anaweza kuitwa: mwanadamu mwenye tabia ya maada. Yaani anakuwa bado hajapandishwa cheo kutoka katika mzunguko wa utoto wa kibinadamu kwa kipindi cha hali ya juu zaidi, nacho ni kile cha mzunguko wa uangalifu wa kibinadamu. Kwa hiyo, mwenye sifa ya maada anakuwa ni mwenye kutaka kujinufaisha, pia ni mwenye sifa ya ubinafsi, naye ni mwenye kuamini na kuathirika na vitu vya kuhisika pekee, kwani nafsi yake inamili upande wa kuhisika na ubinafsi.

• Wapinzani wa utume wa Nabii Muhammad S.A.W. katika kuomba dalili zinazohisiwa juu ya utume wake walikuwa na sifa ya maada; kwani walikuwa wanaamini vitu vinayohisika na maada tu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na walisema (makafiri wa kiqureshi kumwambia Mtume): Hatuwezi kukuamini mpaka utububujishie (utupitishie) chemchemu katika ardhi (hii yetu ya Makka). Au uwe na bustani ya mitende na mizabibu; kisha ububujishe (upitishe) mito katikati yake kwa mabubujiko makubwa. Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyodai, au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika uso kwa uso. Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upande mbinguni. Na hatutaamini kupanda kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome (Mungu Anamwambia Mtume) Sema: “Subhanallah! (Mola wangu ni Mtakatifu!). Mimi sikuwa ila ni mtu (tu, niliyefanywa) Mtume. ‘Si Malaika wala si Mungu, nitafanya vipi hayo?. Na hapana lililowazuilia watu kuamini uliowajia uwongofu isipokuwa walisema. “Je! Mwenyezi Mungu humtuma binadamu kuwa mjumbe wake}. [Al ISRAA, 90: 94].

• Inatarajiwa katika vipindi vya kukua mwanadamu kama mtu akue taratibu kutoka kipindi cha hali ya utoto mpaka kipindi cha hali ya uangalifu ili atambue hadhi ya wengine na kujitambua yeye mwenyewe. Kuanzia hapa, uhusiano wa ushirikiano unaweza kupatikana; ushirikiano wa mtu na mtu mwengine katika masilahi na kuepusha madhara kutokana na tabia ya kuwatambua wengine na haki zao, pamoja na kunufaishana, kuhisiana na kuepusha madhara. Mwanadamu wakati wa kukua anaanza kutambua maadili na misingi mikuu, ambayo inautawala uhusiano uliopo baina yake na wengine.

• Hali ya mtu mmoja katika suala hilo ni sawa na hali ya jamii; maana kiwango cha utoto wa jamii kinawafanya watu wake wawe na mtindo wa kutafakari kibinafsi, licha ya kuwa mtindo wao wa fikra unaambatana zaidi na jinsi kila mmoja alivyo, yeye kama yeye, licha ya kuwa imani zao zinahusika zaidi na vitu vya kuhisika, yaani maada tu, mpaka jamii ipandishwe cheo pamoja na namna ya fikra zake zikue na wengi wa watu wake waanze kujitafakari wao wenyewe pamoja na haki za wengine. Kwa hali hiyo, jamii inayotawaliwa na mwelekeo wa kibinafsi kwa hali ya maada na ubinafsi inaweza kusifika kuwa ni jamii ya ubinafsi au jamii changa, jamii ya maada au jamii isiyo na ustaarabu.

• Quraani Tukufu imekataza tabia ya ubinafsi. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na kulikuwa kundi jengine nafsi zao zimewashughulisha (hawajijui hawajitambui); wakimdhania Mwenyezi Mungu dhana zisizokuwa ndizo, dhana za ujinga; wakisema. “Ah! Tuna amri sisi katika jambo hili?” sema: “Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu”. Wanaficha katika roho zao (hao wanafiki) wasiyokubainishia. Wanasema: “Tungekuwa na chochote katika jambo hili tusingeuawa hapa”. Sema: “Hata mngalikuwa majumbani mwenu, basi wangalitoka wale walioandikiwa kufa, wakenda mahali pao pa kuangukia wafe. (Amefanya haya Mwenyezi Mungu ili) Ayadhihirishe yaliyomo vifuani mwenu, na Asafishe yaliyo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu Anayajua yaliyomo vifuani”.}[AALI IMRAN, 154].

• Quraani Tukufu katika kukabiliana na mfumo wa maada iliainisha sifa za wenye sifa ya maada wakiwa watu binafsi au jamii kiujumla ambapo Quraani iliiangalia maada kwa makini ili tusije kuangukia ndani yake. Na miongoni mwa sifa maalumu za wafuasi wa maada ni: kutaka dalili zinazoonekana kihisia za maada pamoja na kuacha mambo ya kiakili tu na maadili ya hali ya juu, ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na bila shaka tumewaeleza watu kwa namna nyingi katika hii Quraani kila mfano. Lakini watu wengi wanakataa (kila kitu) isipokuwa kukanusha tu. Na walisema (makafiri wa Kiqureshi kumwambia Mtume): “Hatuwezi kukuamini mpaka utububujishie (utupitishie) chemchemu katika ardhi (hii yetu ya Makka)}. [Al ISRAA 89-90}. Na miongoni mwa sifa zao ni ubinafsi kama Alivyobainisha Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na kulikuwa kundi jengine nafsi zao zimewashughulisha (hawajijui hawajitambui); wakimdhania Mwenyezi Mungu dhana zisizokuwa ndizo, dhana za ujinga}. {AALI IMRAN, 154}. Kujifaharisha, jaha, utajiri na kutoangalia mafukara na wanyonge ni moja ya sifa hizo, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Wakasema: “Je, tukuamini wewe, hali ya kuwa wanyonge ndio wanaokufuata”.} [AS SHUWRAA, 111]. Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Walisema: “Kwa nini Quraani haikuteremshwa juu ya mtu mkubwa katika miji miwili (yetu hii ya Makka na Taif? Kwa nini akapewa maskini huyu)?”}. [AZ ZUKHRUF, 31]. Aidha katika sifa zao zilizojulikana ni kujitia nguvu kwa mali na uwezo wa kimaada, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Wakasema: “Sisi ni wenye nguvu na ni wenye vita vikali; na amri iko kwako, basi tazama ni nini unaamrisha”}. [AN-NAML, 33], pia Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na wakasema: “Sisi tunayo mali nyingi na watoto wengi, wala sisi hatutaadhibiwa}. [SABA, 35], na “Wakasema: {Ni nani aliye na nguvu zaidi kuliko sisi?” Je! Hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu Aliyewaumba wao ni Mwenye nguvu zaidi kuliko wao? Wakawa wanazikanusha Aya zetu}. [FUSALAT, 15]. Aidha miongoni mwa sifa zao ni kibri na uasi, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Ama yule aliyeasi. Na akapenda zaidi, (akayafadhilisha maisha) ya dunia. Basi kwa hakika Jahanamu ndiyo itakayokuwa makazi yake}. [AN-NAZIAT, 37: 39]. Na miongoni mwa sifa zao ni ubakhili, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na wanapoambiwa: “Toeni katika yale aliyokupeni Mwenyezi Mungu” (msaidie masikini) wale waliokufuru huwaambia walioamini. “Je, tuwalishe (tuwaruzuku) ambao Mungu Angependa Angewalishe yeye Mwenyewe? (Lakini Mwenyewe Mwenyezi Mungu Amependa wawe mafakiri, kwa kuwaacha vivyo hivyo bila ya kuwatajirisha). Nyinyi hamumo ila katika upotofu (upotevu) uliyo dhahiri}. [YASIN, 47]. Aidha miongoni mwa sifa zao ni kukanusha kufufuka, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Je! Anakuahidini ya kwamba mtakapokufa na mkawa udongo na mifupa, kuwa mtatolewa, (mtafufuliwa)?}. [AL-MUMINUN, 35].

• Jamii ya maada inaathirika na vishawishi vya vitu vya kuhisika mpaka vinakuwa ndio msingi wa kukubali na kukataa kwa jamii hiyo. Kwa hiyo, mtu anajaribu kuwaathiri wengine kwa alama au umbo la nje bila ya kuangalia undani wake au elimu au utamaduni wake. Aidha mwanamke anashawishi matamanio ya mwanamume kwa mapambo yake siyo kwa kiwango chake cha kiubinadamu. Kwa hiyo, Quraani Tukufu iliainisha mapambo ya wanawake kuwa ni jambo la ujahili wa falsafa ya maada na moja ya sifa za jamii zisizo na ustaarabu kama Alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na kaeni majumbani mwenu, wala msionyeshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionyesha mapambo yao wanawake wa zama za Ujahili (Ujinga, ukafiri)}. [AL-AHZAB, 33]. Aya Tukufu inawataka akina mama wa waumini na wanawake wa Kiislamu kiujumla wajiepushe na mapambo, kwani ni moja ya sifa za kiujahili na hali za maada ambapo jamii kwa hali hizo inasifika kwa kutokuwa na ustaarabu, na watu wake wana mielekeo ya kuangalia vitu vya kuhisika tu. Kwa hiyo, Quraani Tukufu imekosoa sifa hiyo, kwa kuamrisha utiifu na ibada. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na simamisheni Sala na toeni Zaka, na Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Mwenyezi Mungu Anataka kukuondoleeni uchafu, enyi watu wa nyumba (ya Mtume), na (anataka) kukutakaseni kabisa kabisa}. [AL-AHZAB 33]. Aya hiyo imewaamrisha wanawake kusimamisha Sala na kutoa zaka ili washikamane zaidi na maadili na misingi licha ya ibada ambazo zinawaepusha na hali ya ubinafsi na katika wakati huo huo kutohusika na vitu vya kuhisika. Zaka kama ni ibada ambayo inaelekeza ushirikiano na kuacha hali ya ubinafsi, pia kuelekea kwa Mwenyezi Mungu katika Sala ni jambo ambalo haliambatani na vitu vya kuhisika na vya maada.

• Uislamu katika ujumbe na uongofu wake unawapandisha watu cheo kutoka kwenye kipindi cha uchanga wa falsafa ya maada mpaka katika ngazi ya juu zaidi ya maadili bora, na kutoka kwenye kipindi cha mzunguko wa mtu binafsi mpaka katika hali ya ushirikiano wa kibinadamu. Uislamu katika jambo hilo unaepusha uasi wa vitu vya kuhisika na vya kimaada ingawa hauvinyimi kabisa; maana Uislamu unafanya uwiano baina ya maadili ya kiubinadamu kwa upande, na vitu vya maada kwa upande mwengine, kwa hiyo Uislamu hauzuii ladha kiujumla, lakini umekataza kutumia maada kwa uasi, aidha haukatazi uchumi, uwezo wa maada na wa kifedha bali umekataza uchumi ulioabudiwa na watu kama ni mungu, pia Uislamu umekataza uwezo wa kimaada kwa njia ya uadui na uvamiaji.

• Kwa hiyo, Uislamu katika hali ya kukabiliana na maada unayalingania maadili bora ya kibinadamu ili yawepo katika maisha ya watu pia yawe ni sehemu ya uhusiano baina ya watu, aidha Uislamu unalingania mapenzi, ushirikiano na kuhurumiana, na unawataka Waislamu washikamane na uadilifu na kutekeleza majukumu na kufikisha amana za watu, hali kadhalika Uislamu unafadhilisha na unautanguliza wema kwa vitendo na kauli.

• Wito wa Uislamu wa kushikamana na maadili bora zaidi ya kiubinadamu, haumaanishi kuukana upande wa maada katika maisha ya mwanadamu, au kuyazuia manufaa ya maada kiujumla, isipokuwa Uislamu katika suala hilo umeweka mipaka ya kisheria ya kustarehe. Mwenyezi Mungu Mtukufu Alivyosema: {Sema: “Ni nani aliyeharimisha mapambo ya Mwenyezi Mungu ambayo Amewatolea waja wake. Na (nani aliyeharimisha) vitu vizuri katika vyakula?” Sema: “Vitu hivyo vimewahalalikia Waislamu (hapa) katika maisha ya dunia; (na) vitakuwa vyao peke yao siku ya Kiyama”. Namna hivi tunazieleza Aya kwa watu wajuao}. [AL-AARAF, 32]. ulichokikataza Uislamu ni kuchupa mipaka katika kupata ladha ya manufaa ya maada kama Alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi wanadamu! Chukueni mapambo yenu wakati wa kila Sala; na kuleni (vizuri) na kunyweni (vizuri). Lakini msipite kiasi tu. Hakika Yeye (Mwenyezi Mungu) hawapendi wapitao kiasi (wapindukiyao mipaka)}. [AL-AARAF, 31].

• Uislamu hauharamishi kupata ladha ya maada kwa njia za halali, lakini unaharamisha tu machafu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Sema (uwaambie): “Mola wangu Ameharimisha (Haya: Ameharimisha) mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika, na dhambi na kutoka katika taa (ya wakubwa) pasipo haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ambacho hakukiteremshia dalili (ya kusema kishirikishwe naye) na (Ameharimisha) kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua}.[AL AARAF, 33].

• Yoyote anayefahamu ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu anayeishi hapa duniani kuwa ni ujumbe unaoepusha mtu kupata ladha ya manufaa ya maisha ya dunia au kuwa manufaa hayo ni vitu vichafu, basi huyo mtu asikaribiwe, kwani anafahamu kimakosa kinachotakikakana kutoka ujumbe wa Mwenyezi Mungu, nao ni kuepusha uasi kwa hali ya kimaada, aidha kupita mipaka katika kutumia manufaa hayo ya maada; maana jambo linalotakiwa hapa ni kujenga uhusiano baina ya watu, uhusiano uliosimamishwa kwa maadili bora zaidi ya kiubinadamu ili maadili hayo yatangulizwe zaidi ya uhusiano wa kimaada.

• Hakika Uislamu kama unavyokabiliana na maada, aidha unajenga sawa sawa misingi ya jamii ya kibinadamu pamoja na kuweka uhusiano mzuri wa watu wanaoishi katika jamii hiyo. Hapa ni lazima tubainishe kwamba jambo la kujibu shaka kuhusu masuala yanayoambatana na maada, halitakiwi kuchukua nafasi kubwa, kwani juhudi zifanywazo zinatakiwa kuelekezwa kwenye ulinganiaji wa Uislamu pamoja na kubainisha misingi ya jamii ya Kiislamu ambayo inajenga tabia ya kibinadamu.

• Ujumbe wa Kiislamu ni wito, mfumo na jitihada endelevu inayokwenda kwa kukipandisha cheo cha mwanadamu akiwa mtu binafsi au jamii katika nyanja za itikadi na tabia; kumpandisha mtu cheo kinachomfaa awe kama mwanadamu anayeheshimika mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; yaani kumpandisha cheo hadi kufikia kiwango kinachotokana na mfumo wa mfungamano wa watu na msingi wa maadili ya kibinadamu yaliyo bora; msingi usioambatana na ubinafsi au hali ya kutafuta manufaa tu. Na Uislamu katika kukabiliana na falsafa ya maada, unatoa wito wa kuacha tabia na maadili yanayohusiana na falsafa ya maada na kurejea kwa tabia na maadili yanayohusiana na cheo cha mwanadamu mwenye kuheshimika.

Marejeo: Profesa Muhammad Albahiy. Quraani fi Muwajahat Al Madiya, Cairo, Maktabat Wahba, cha 1, 1987, uk. 3: 47.
 

Share this:

Related Fatwas